Sunday 24 September 2017

KIONGOZI WA WAISMAILIA AGA KHAN KATIKA TANGANYIKA YA KIKOLONI



Sheikh Matimbwa,

Tumekushukuru kwa kutuwekea, ''clip,'' adhim ya Aga Khan alipokuja Tanganyika mwaka 1956.

Nimeingia maktaba ili nai nichangie kitu katika mambo ambayo Waismailia, yaani Aga Khan walifanya katika kusaidia Waislam wa Tanganyika.

Al Jamiatul Islamiyya Muslim School 

Katika miaka ya 1930s Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika walikuwa wanajenga shule ambayo sote tunaijua lakini hela zilikuwa tatizo jengo likawa limechukua muda mrefu kukamilika.

Sababu ya kujenga shule hii ni kuwa wazee wetu na wao walitaka wawe na mahali pa kuwasomesha watoto wao kuepuka vijana wao kubatizwa katika shule ambazo serikali ya kikoloni iliziweka mikononi kwa kanisa.

Kleist akiwa kiongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika alitambua mapema sana kuwa tatizo kubwa lililokuwa likiwakabili Waislam ilikuwa ni kukosa elimu ambayo serikali ya kikoloni iliwaachia wamishionari waisimamie.

Si kama Waislam hawakuwa wanatambua faida ya elimu kwa watoto wao. Wazazi wengi walichelea kuwapeleka  watoto wao shule kwa sababu wamishionari walichukua fursa hiyo kuwabatiza. Kuliko kwa watoto wao kutolewa katika Uislam na kuwa murtad, wazazi wengi waliamua kuisamehe elimu yenyewe kabisa.

Kleist aliona kuwa ufunguo wa tatizo hilo kwa Waislam ilikuwa ni kuanzisha shule zao wenyewe ambazo zitasomesha Qur’an pamoja na masomo mengine.

Wakati ule, na hata hivi sasa, Qur’an ilikuwa ikisomeshwa kwa mtindo wa asili ambapo mwanafunzi anakaa chini sakafuni mbele ya maalim akiwa na ubao wake na juzuu.

Katika madras kuchapa viboko, kwa jina maarufu mkambaa, ndiyo ulikuwa mtindo wa kusomeshea. Kleist hakuona sababu kwa nini Qur’an nayo isisomeshwe kama elimu nyingine, wanafunzi wakiwa madarasani wakikaa katika madawati.

Alilitoa wazo hili kwa rafiki zake akashauri madras ipanuliwe ili masomo mengine yasomeshwe pamoja na Uislam.

Ushauri huu ulijadiliwa kati ya Kleist, Ali Kiro, Maalim Popa Saleh na Shariff Salim. Wakitambua kazi kubwa iliyokuwa ikiwakabili, waliamua waanze hiyo shule kwa kidogo kidogo kwa awamu. Nyumba itakayokuwa shule ya muda ilitafutwa na wanafunzi wakaanza kusoma.

Kati ya walimu wa mwanzo wa shule hiyo walikuwa Mzee Ali Comorian na Sheikh Abdallah Idd Chaurembo ambao walikuwa kati ya wasomi wa Kiislam waliokuwa wakiheshimika.

Wazazi wa Kiislam waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe.

Al Jamiatul Islamiyya ikawa inapita nyumba hadi nyumba ikusanya michango kutoka kwa Waislam.

Bahati nzuri mwaka wa 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu ujenzi wa shule ile.

Katika hafla ile mtoto aliysoma risala kwa Aga Khan alikuwa Abdul Sykes akiwa na umri wa miaka 12.

Marehemu Kanyama Chiume amenihadithia kuwa wakati huu alipofika Aga Khan Tanganyika yeye alikuwa anasoma Shule ya Kitchwele na alikuwa katika bendi ya shule iliyompokea yeye akipiga, ‘’triangle,’’ na alinieleza kuwa picha yake yeye akipiga, ‘’triangle,’’ ilitokea katika gazeti.

Aga Khan alitoa fedha na shule ikajengwa New Street si mbali sana na ilipokuwa ofisi ya African Association.

Kleist akawa katika kamati ya ujenzi akikagua kazi hadi ujenzi ulipokamilika. Hii ni moja kati ya shule za mwanzo kujengwa na Waislam wa Tanganyika. Jengo la Al Jamiatul Islamiyya lipo limesimama hadi leo kama ushahidi na kumbukumbu za juhudi za Waislam katika kujiletea maendeleo yao.

Serikali katika kuthamini mchango wa Kleist katika kupeleka mbele elimu kwa ajili ya watoto wa Kiislam ikamchagua kuwa katika Provincial Education Committee of Tanganyika Education. Mwanae Abdulwahid na yeye vilevile akaja kuwa katika Aga Khan Education Committee.

Halikadhalika walimu wawili wa Al Jamiatul Islamiyya walipewa nafasi muhimu katika siasa na uongozi wa nchi. na Sheikh Juma Mwindadi alifanywa mjumbe katika Baraza la Mji wa Dar es Salaam.

Mwaka 1956 Aga Khan alipotembelea Tanganyika Waismailia walimnunulia Mercedes Benz 280S yenye usajili DSQ 666 na hii ndiyo alikuwa akitembeanayo mjini Dar es Salaam.

Mwaka wa 1959 Waismailia waliamua kuiuza gari hii lakini hawakutaka inunuliwe na Muismailia ila inunuliwe na mtu yoyote mwenye hadhi katika jamii ya Watanganyika nje yao.

Gari hii aliuziwa Abdul Sykes na alikaanayo hadi alipofariki 1968.

No comments: