Utangulizi
Imekuwa jambo la kawaida kwa Maalim Seif kutukanwa a kukebehiwa katika mitandao ya kijamii na watu ambao wanafahamika. Binafsi siku za mwanzo nilijaribu kuwa naandika nasaha kujaribu kuwafahamisha wahusika wa kejeli na matusi kuwa huyu wanaemvunjia heshima ni kiongozi mkubwa katika nchi yetu lakini ilibidi niache kwa kuona kuwa hawakuwa tayari kunisikiliza na zaidi matusi na kejeli zikizidi. Lakini kinachonistaajabisha vipi vyombo husika kuwa kimya.
MS
Kuna wakati sasa
inakaribia miaka 20 watu fulani walinifikiria kuwa nina, ‘’ujuzi,’’ ambao
ungekuwa na manufaa katika taifa letu na baadhi ya watu hao ni wakubwa wakataka
nikautumie, ‘’ujuzi,’’ huo wangu katika ofisi kubwa sana ya serikali.
Kipindi hiki ni kile
kipindi ambacho palikuwa na malalamiko mengi kuwa kuna upogo mkubwa katika
kushika madaraka katika serikali kuwa jamii moja fulani imeachiwa kuhodhi
serikali nami nilikuwa mmoja wa watu wenye fikra hizo.
Katika walikuwa wametumwa
kunishawishi nikubali ombi hili la kwenda kuitumikia serikali yetu ni mwalimu
wangu wa Chuo Kikuu ambae yeye tayari alikuwa serikalini na ameshika nafasi
kubwa.
Lakini ukweli ni kuwa
hii kwangu mie lilikuwa, ombi la pili, ombi
la kwanza lilikuwa niingizwe chamani
kabisa.
Kweli nilistaajabu kwa
mtu mdogo kama mie kuonekana kuwa naweza kuwa na manufaa katika utendaji wa ufanisi
katika nchi yangu.
Hili pendekezo la utumishi
chamani nilimwambia mjumbe na sahib yangu aliyenifuata kuwa akili yangu jinsi
ilivyo sitaweza kukamilisha majukumu nitakayopewa kwa ufanisi na kubwa
nililohofia ni kuwa vipi nitawatazama ndugu zangu machoni?
Nitaingia msikiti gani
kuswali bila kuingiwa na simanzi?
Huu ndiyo ukawa mwisho
wa jambo lenyewe.
Hili la pili sikuweza
kukataa hapo kwa hapo kwa sababu fulani fulani kwa hiyo nilipeleka hadi CV
yangu.
Lakini katika nafsi
yangu niliamini kabisa kuwa hili haliwezi kuwa kwani mimi nimefika mbali sana
na kukanyaga ardhi ambayo wengi kabla yangu na wajuzi kunishinda hawakuthubutu
kutia mguu wao.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa
baada ya muda siku moja nikapigiwa simu ya dharura nikiendesha gari nikaambiwa
haraka nirudi ofisini kwangu nitume tena ile CV yangu mara moja kwani ile ya
kwanza haionekani.
Nilitii.
Lakini nilijuwa kuwa
hili haliwezekani na kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Bahati nzuri au mbaya
hata kama yangefanikiwa sidhani kama ningedumu kazini.
Allah hakunijaaliwa
ustahamilivu kuacha kusema kile ninachoakiamini kuwa kweli.
Wazee wangu wawili Allah
awarehemu, Ally Sykes na Kitwana Kondo wote wakinipenda na wote walipatapo
kunambia kwa huruma sana kuwa nitakufa masikini na Mzee Ally alikwenda mbali
zaidi alinambia, ‘’Mohamed utakufa masikini kama baba yako Allah kakujaalia
vipaji lakini umeshindwa kuvitumia…’’
Bwana Ally alipomaliza
kusema maneno haya akaniuliza umri wangu. Nilikuwa na miaka 40.
Ally Sykes akatingisha
kichwa kwa masikitiko.
Mzee Kondo yeye
alinifananisha na wenzangu wa rika langu na wengine ni marafiki zangu
akamwambia mkewe, ‘’Mwanangu huyu ndiye pekee dunia yake haikumkalia vizuri.’’
Nimeleta utangulizi huu
kwa kuona imewekwa picha hapa ikimkebehi mmoja wa viongozi wa nchi yetu.
Nimeona na mie nichangie
katika hiyo picha lakini kwa kuweka staha kuwa iko siku iliwekwa picha mfano wa
hii lakini mimi nilipochangia nikaonywa kuwa nisifanye hivyo nami nikatii na
kuomba radhi nikasema kwa kuwa nimeona picha hiyo imewekwa mwekaji na kaandika
maneno hakukemewa nikadhani inaruhusiwa.
Mradi kumbe ni makosa naomba
radhi mnisamehe.
Sasa katika hili lililo
mezani wengi wameona hiyo picha lakini wamekaa kimya kwa nini mimi?
Lugha ya sasa unaweza
kusema kwanini ‘’nimewashwa?’’
Rejea katika utangulizi
wangu jibu liko hapo.
Bibi zangu wake zangu
mabinti Farijala wakisema, ‘’Masikini mume wetu Mohamed, ule ‘’wazimu,’’ wote
wa babu yake Mzee Popo wanae wote umewaruka umekuja kumvaa mjukuu wake.’’
Mie huwaambia watu kuwa
Wamanyema wote wewe tuchungiuze tuna wazimu kidogo.
Baba Juma atanisaidia
kusadikisha.
No comments:
Post a Comment