Friday 29 September 2017

TAAZIA: ALI JUMA SLEIMAN MHANGA WA MAZOMBIE NA JR. FARREL



Ali Juma Sleiman
Wamemuua mzee wa watu Ali Juma Sleiman bila ya sababu yoyote zaidi tu ya hasad, chuki na ubaya ulio ndani ya nafsi zao. Mzee huyu ni mtu mzima, kosa lake kubwa ni CUF. Wamemdhulumu roho yake kwa mateso, uonevu na unyama usiomithilika. Anakwenda kwa mola wake akiwa na masikitiko ya dhulma si ya mali pekee bali uhai wake, dhamana yake ya kusimamia famili yake na dhima yake ya kusimama na lililo na uhalali.

Wamemdhulumu maisha yake akiwa na majeraha ya vipigo, maumivu ya roho, nafsi na kiwiliwili kibichi kinachotangulia kwa Muumba wake kwa sababu ya uonevu. Mzee huyu ameacha famili, leo wanaamka wakiwa na sanda mkononi ya kuenda kumsitiri mzee wao aliefariki kwa sababu ya dhulma ya wababe dhidi yake na chaguo lake la nani wa kumuongoza katika utaratibu tuliojipangia.

Mzee huyu anakoshwa mwili wake, akimwagiwa maji ya kutoka utosini mpaka vidoleni, bado akivuja damu ya vipigo alivyovipata. Maji yanakosha michibuko ya marungu aliopigwa miguuni ili anapofika kwa aliemuumba awe msafi, akiyakabili maisha yake mapya ya akhera kwa sababu ya wababe na dhulma waliomfanyia. Anakafiniwa na kuvikwa sanda yake, na kusaliwa na jamii ya waislam, masheikh na wanazuoni ambao kila mmoja anajuwa dhulma iliomfika, dhulma iliopevuka ya kumpotezea maisha yake.

Tuna mlolongo wa viongozi wa imani, walioapa kusimama na haki lakini kimnya kwa unyama unaofanyika. Wameamua kusema na nyoyo zao tu na kuacha nafsi zikielemewa na ukubwa wa matukio yaliokosa chembe ya uungwana lakini hakuna wa kukemea. Wanatembea wakitikisa vichwa vyao tu lakini mdomo umebana barabara, hutalisikia la kupinga dhulma hizi zinazofanyika kula kukicha.

Wamemuua akiwa na kauli yake, akisimulia yaliomsibu kichwa chini, mtu mzima alievunjiwa heshima na vijana waliokuzwa katika uislam na waliofunzwa kusimama na wema na ihsan ambao wengine anaweza hata kuwazaa. Anaondoka duniani akiwa amefunga macho lakini taswira ya mwisho ya uhai wake ikiwa ni vishindo, khofu, maumivu, majeraha na istifham ya kuiona roho yake ikimtoka kwa jinsi nguvu kubwa zilivyotumika kumdhuru na kumdhulumu haki yake ya kuishi.

Wafikirie watoto wake, mke wake, wajukuu zake, jamaa zake, dada zake na kaka zake. Wafikirie wale wa karibu watakaoingia kaburini kumsitiri mzee wao wakijuwa kuwa kilichofanyika dhidi ya mzee wao kimekosa utu na kupitiliza mipaka yote ya ubinaadam. Ghafla aliekuwa akiitwa baba sasa marehem kwa sababu ya wababe wanaofugwa wakilishwa na kuvishwa ili kuonea masikini na wanyonge wengine waliomkataa kiongozi asiewafaa.

Waliokuwa wakimtegemea wanaamka sio na simanzi za kumpoteza mpendwa wao tu bali mtafaruk wa mawazo ya maisha baada ya madhila haya yaliopoteza roho ya kipenzi chao. Anabebwa katika safari yake ya mwisho, huku "Laa Ilaha Illa Llah" zikisomwa vifuani vya wenye dukuduku la uonevu, wanaotazamana wakifikiri nao khatima zao dhidi ya madhalimu walio na utayari wa kutoa roho tena kwa ukatili mkubwa wa vipigo kwa wanyonge wasio na nguvu.

Yaliomfika huyu mzee ni sehemu ya maisha ya kawaida kwa wapinzani visiwani na bara kwa sasa. Vipigo kama hivi viko katika kila shehia zetu, na unaweza kukuta kuwa vimewagusa wazanzibari wengi kutokana na ukaribu wetu. Ukandamizaji unaofanyika dhidi ya wapinzani hausemeki na leo hii tumempoteza mzee wetu kwa sababu tu ya ubaya wa wachache waliokosa utu. Wanaojiita waungwana wamebeba kejeli kwa suti ya rangi ipi na ukubwa gani, huku jahazi wakilitoboa kwa makusudi wakifikiri litazama upande mmoja tu.

Mwenyezi Mungu akupokea mzee wetu ukiwa shahid wa kisimama na lililo na uhalali. Akupokee kwa rehma zake na kukuepusha na kila adhabu huku akikusamehe makosa yako yote. Uzindukane ukiwa katika utulivu wa nafsi, katika kaburi lako lililojaa nuru na malaika wema wawe ndio sehemu ya mapokezo yako katika safari yako hii ya milele.

Mwenyezi Mungu akujaalie safari hii iwe ni safari ya kheri kwako, ilio na maisha mema katika pepo yake iliojaa waja wema waliosimama katika ukweli, ihsan na haki. Mwenyezi Mungu awape subra familia yako na kila alieguswa katika mtihani huu wenye machungu yasio mithilika. 

Allahuma ghfirlahu, warhamhu waskanahu filjana. 
Allahuma Ameen.

No comments: