Thursday 5 October 2017

ALLY KLEIST SYKES NA KENNETH DAVID KAUNDA 1953

Utangulizi
Barua hiyo hapo chini kutoka Ikulu inasema kuwa uhusiano wa Zambia na Tanzania ulianzishwa na Baba wa Taifa. 

Ningependa kwa faida ya historia ya taifa letu lau kwa mukthasari ninyanyambue yale niliyokutananayo katika Nyaraka za Sykes wakati natafiti maisha ya Abdul Sykes ili niweke wazi chanzo cha uhusiano wa Tanganyika (Tanzania) na Northern Rhodesia (Zambia) wakati wa harakati za Afrika kudai uhuru wake katika miaka ya 1950. 

Uhusino wa Tanzania na Zambia rekodi za kihistoria zinaonyesha ulianza mwaka wa 1953 wakati Ally Sykes alipoanza kuandikiana barua na Kenneth Kaunda akiwa kiongozi wa Pan African National Congress.
Hayo hapo chini ni kutoka katika kitabu cha Maisha ya Abdul Sykes:

Kulia: Abdul na Ally Sykes 1942 wakiwa katika King's African Rifles Vita Kuu ya
Pili ya Dunia (1938 - 1945) Burrma Infantry


‘’Abdulwahid alipoanza shughuli zake za siasa na Chama cha Makuli, Ally alianza siasa kama alivyoanza kaka yake na chama cha wafanyakazi - Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA). Madai ya kisiasa katika TAGSA ndiyo yaliompa Ally umaarufu katika TAA na ni mchanganyo wa harakati zote mbili kupitia uongozi wa Ally ndiyo uliyoifanya TAA kujulikana na kutambuliwa nje ya mipaka ya Tanganyika kama chama cha ukombozi. Kutokana na sababu hii wanahistoria wanahitaji vilevile kutafiti kidogo kuhusu Ally Sykes na ni kwa kupitia kwake sehemu ya mapambano ya uhuru wa Tanganyika na maisha ya awali ya Nyerere katika siasa yanaweza kuelezwa. Vilevile ni kwa kupitia kwa Ally Sykes historia inaweza kufahamu namna Nyerere alivyoweza kupanda hadi kwenye madaraka na kuongoza moja ya vyama vya siasa vilivyokuwa na nguvu na mshikamano mzuri sana katika Afrika. Halikadhalika kupitia kwa Ally Sykes mtafiti anakutana na wazalendo wengine wa Tanganyika kama Dennis Pombeah, Dr William Mwanjisi, Dr Michael Lugazia, Rashid Kawawa na wengine wengi.  Hivyo hivyo kupitia kwa kaka yake mtu hukutana na watu mashuhuri kama Mwapachu, Nyerere na Kenyatta, kwa kupitia kwa Ally Sykes vilevile mtu anatambulishwa kwa wazalendo wengine wa Afrika kama Tom Mboya na Kenneth Kaunda.

Kenneth David Kaunda na Dr. Martin Luther King


Mwaka wa 1953 Harry Nkumbula alikuwa amechaguliwa rais wa ANC na Kenneth Kaunda aliteuliwa Katibu Mwenezi wa Jimbo la Kaskazini. Mwezi Agosti Kaunda akawa Katibu Mkuu wa ANC. Haukupita muda Kaunda akaanza kupeleka barua Nairobi, Dar es Salaam na Johannesburg akiitikia rai ya Kenya African Union na South African ANC kuwa ëLusaka inapasa kuwa mahali pa kukutana wazalendo kutoka nchi zilizo Kusini mwa Sahara.íUjumbe wa watu watatu wa TAA ulialikwa na Katibu Mkuu wa African Congress ya Northern Rhodesia, Kenneth Kaunda, kuhudhuria mkutano wa Pan African Congress (ANC) mjini Lusaka. Mwezi wa Novemba Ally Sykes alipokea barua kutoka kwa Kaunda akimwalika kuhudhuria mkutano huo. Wakati ule ANC ilikuwa na manungíuniko kadhaa dhidi ya Waingereza na ilikuwa imeamua katika mapambamo yake kutumia njia za amani ambayo katika barua ambayo Kaunda alimpelekea Ally Sykes aliielezea njia hizo za amani kama hivi, ‘’Hutashirikiana na mtu yoyote katika shauri lolote litakalokuwa na madhara kwa maslahi ya Waafrika.’’ (Nyaraka kutoka kwa Kenneth Kaunda kujua kwa Ally Sykes: ANC Circular No. B.1/54 Sykes' Papers).
 Hii ilikuwa mwaka wa 1953.

Miezi ya mwisho ya mwaka 1953 uongozi wa TAA makao makuu ulikuwa na shughuli nyingi. Ujumbe wa watu watatu wa TAA ulialikwa na Katibu Mkuu wa African Congress ya Northern Rhodesia, Kenneth Kaunda, kuhudhuria mkutano Pan African Congress (ANC) mjini Lusaka. Mwezi wa Novemba Ally Sykes alipokea barua kutoka kwa Kaunda akimwalika kuhudhuria mkutano huo.

(Angalia Fergus Macpherson, Kenneth Kaunda of Zambia, Lusaka, 1974 uk. 430. Maelezo mengine ya ziada kutoka kwa Ally Sykes).

Kitu ambacho huwasisitizia wana-historia wa hapa nyumbani ni kuwa wasiiogope historia ya TANU na historia ya uhuru wa Tanganyika wawe na ujasiri wa kuitafiti historia hii kabla ya Baba wa Taifa hajapandishwa katika jukwaa la TANU Viwanja Vya Mnazi Mmoja 1954 kuwahutubia wananchi akitanguliwa na Sheikh Suleiman Takadir kama mtambulishaji na muhamasishaji umma. 

Kuna mengi wanakosa kwa kuwapuuza hawa wazee wetu.


Baba wa Taifa akiwa na Sheikh Suleiman Takadir Viwanja Vya Mnazi Mmoja. Wengine ni Bi. Titi Mohamed, Rajab Diwani, Clement Mohamed Mtamila, Mama Maria Nyerere...picha hii alinipatia Jim Bailey rafiki yake Ally Sykes aliyekuwa mmiliki wa gazeti la Drum.

Si kweli kuwa uhusiano huu wa Tanganyika (Tanzania) na Zambia aliuanza na Baba wa Taifa. Ulikuwapo hata kabla ya TANU kuundwa 1954. 

No comments: