BURIANI ALHAJ SHEIKH
AHMED ISLAM
Ramadhani K. Dau
![]() |
Kulia: Sheikh Ahmed Islam, Ahmed Rashad na Prof. haroub Othman Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam uzinduzi wa safari ya Jeddad kwa Shirika la Ndege la Tanzania 7 August 1997 |
Ilikuwa siku ya
Jumamosi tarehe 23 Disemba 2017, majira ya saa 5 usiku kwa saa za Malaysia
nilipopata ujumbe mfupi wa sms kutoka kwa Sheikh Issa Othman, maarufu Mufti wa
London, Imam wa Masjid Maamur ukiniarifu msiba wa mzee wetu Sheikh Ahmed Islam.
Ujumbe wake ulikuwa mfupi sana: “Mzee
wetu Ahmed Islam amefariki sasa hivi. Maiti inaletwa msikitini hivi sasa.
Maziko kesho In Shaa Allah. Innallillahi Wainnaillahi Raajiuun”.
Mara tu baada ya
kupata taarifa hiyo na baada ya kumtakia maghfira mzee wetu, nikajua kuwa kwa
mara nyingine tena umeniangukia wajibu wa kuandika taazia ya mtu ambaye
namfahamu, namheshimu na alikuwa na ukaribu sana na mimi. Nimeshawahi kuandika
huko nyuma kuwa kuandika taazia ni jambo zito na gumu sana. Kila niandikapo
hutamani sana taazia hiyo iwe ndiyo ya mwisho. Lakini kwa mipango Yake Mwenyezi
Mungu, najikuta nashindwa kukwepa wajibu huo. Hata hivyo, mara hii nilidhani
ningeweza kuukwepa wajibu huo kwa kumuomba rafiki yangu na ndugu yangu
mwanahistoria maarufu Sheikh Mohamed Said aandike taazia hiyo nami nilikuwa
tayari kumpa maelezo yoyote ambayo yangemsaidia katika uandishi wake. Pamoja ya
kuwa alikubali kuifanya kazi hiyo, Mohamed alisisitiza kuwa lazima na mimi
niandike. Kwa jinsi ya msisitizo aliouweka Sheikh Mohamed, nimejikuta kwa mara
nyingine tena nalazimika kuandika taazia
hii huku nikiwa na moyo wa huzuni sana kwa kuondokewa na mzee wangu ambaye
alikuwa mithili ya baba yangu mzazi.
Marehemu mzee Ahmed
Islam ana mambo mengi na sura nyingi. Wapo wanaomfahamu kama ni miongoni mwa
wazee maarufu na kiongozi katika jamii ya Waislamu, wapo wanaomfahamu kama
mtaalamu wa masuala ya Rasilimali Watu (Human Resources) na wapo wanaomfahamu
mzee Ahmed Islam kama mwana michezo mahiri.
Marehemu Mzee Ahmed
Ijhad Islam alizaliwa Zanzibar tarehe 22 Disemba 1930 akiwa ni mtoto pekee wa
Sheikh Ijhad Islam na bibi yetu Bi Maryam Mussa. Kwa bahati mbaya, mzee Ijhad
Islam alifariki wakati mzee Ahmed akiwa mdogo na hivyo akalelewa na mama yake.
Baada ya msiba huo, bibi yetu Bi Maryam aliolewa na kupata mtoto mmoja wa kike
ambaye jina lake ni Zerah.
Baada ya kumaliza
masomo yake ya msingi na Sekondari kwenye Government
School (sasa Ben Bella) Zanzibar mwaka 1948, ilipofika mwaka 1957 marehemu
mzee Ahmed Islam alikwenda Cornwall, Uingereza kuchukua masomo katika fani ya
Mawasiliano yaani Telecommunications. Wakati huo alikuwa ameajiriwa na kampuni
ya Cable and Wireless (C&W) ambako alikuwa Meneja Msaidizi (Assistant
Manager). Kampuni hii ilikuwa ndiyo kampuni kubwa ya mawasiliano Afrika
Mashariki. Baada ya kurudi masomoni, marehemu aliendelea na kazi yake na baada
ya kampuni ya C&W kumezwa na Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki
(East African Post and Telecommunication), Mzee Islam akahamia Dar es Salaam
mwaka 1970.
Akiwa Dar es Salaam Mzee
Islam alifanyakazi katika Shirika hilo na baada ya mgawanyiko yakaundwa
Mashirika mawili tofauti; Shirika la Posta (TPC) na Shirika la Simu (TTCL).
Marehemu mzee Islam alihamishiwa TTCL hadi alipostaafu mwaka 1986 akiwa katika
nafasi ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu yaani Director of Manpower. Baada ya kustaafu, marehemu alifanyakazi
Ubalozi wa Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu. Wakati wa uhai wake, Mzee
Islam amefanya mengi katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi wa dini,
ujenzi wa nchi, uendelezaji wa michezo na utoaji nasaha kwa taasisi na vijana
mbalimbali katika masuala ya ndoa na kujiendeleza kwenye elimu ya juu.
Kwa upande wa dini,
marehemu ametoa mchango mkubwa sana. Miongoni mwa matunda ya kazi yake ni
usimamizi wa ujenzi wa Masjid Maamur iliyopo Upanga, Dar es Salaam. Kwa
wanaokumbuka vizuri jiografia ya Upanga, kabla 1987 pale palipojengwa Masjid
Maamur hapakuwa na msikiti. Lakini kwa kushirikiana na wazee wenziwe marehemu Mzee
Islam aliweza kusimama kidete katika kusimamia ujenzi wa Masjid. Si wengi
wanaofahamu kuwa ujenzi wa Masjid Maamur ulianza na msukusuko mkubwa kwa sababu
kulikuwa na mwanajeshi ambaye alikuwa amepanga kwenye nyumba ya jirani ambayo
ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Mwanajeshi yule alikuwa anatumia kiwanja cha
msikiti kufugia mifugo na kulima mboga. Historia ya kiwanja kile ni kuwa pale
palikuwa makaburi ya ukoo wa Tambaza toka zamani sana. Siku moja marehemu Mzee
Islam alikwenda kwenye kiwanja kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa msikiti.
Yule mwanajeshi hakutaka msikiti ujengwe pale pamoja ya kuwa kiwanja hicho
kilikuwa mali halali ya Msikiti. Wakati ule ukoo wa Tambaza walikuwa wamekitoa
kiwanja kile wakfu pajengwe msikiti na Meya Kitwana Kondo alikuwa amesaidia
pakubwa kufanikisha hilo. Hivyo basi yule mwanajeshi akatoka na bastola na
kutaka kumshambulia Mzee Islam kwa risasi.
Marehemu Mzee Islam hakuogopa. Badala yake alimwambia yule mwanajeshi
afyatue risasi haraka ili amfungulie njia ya kwenda peponi. Mwanajeshi akabaki ameduwaa na hatimaye
akaondoka. Baada ya hapo ujenzi ukaendelea kwa amani na yule mwanajeshi
akahamishiwa Songea. Ilipofika mwaka 2013, marehemu Mzee Islam pia alichangia
kwa kiasi kikubwa usimamizi wa ukarabati mkubwa wa msikiti huo kwa ufadhili
mkubwa wa kampuni ya Oil Com.
![]() |
Kushoto: Abdallah Kassim, Himid Ashraf, Sheikh Aboud Maalim, Sheikh Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafr wa Tanzania, Sheikh Ahmed Islam |
Mbali na Masjid
Maamur, marehemu Mzee Islam pia alitoa mchango mkubwa sana katika ujenzi wa
Masjid Ngazija hapa Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya sana tokea ukoloni hadi
leo, katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Central Business District), hakuna
msikiti wowote mkubwa wala mdogo zaidi ya msikiti wa Ngazija. Lakini msikiti
huo ambao ulijengwa wakati wa ukoloni ulikuwa ni mdogo sana kiasi cha kutokidhi
mahitaji ya Waumini. Hivyo basi kwa kushirikiana na viongozi wengine kama vile
marehemu Sheikh Aboud Maalim, marehemu Profesa Haroub Othman Miraji, Sheikh
Saidi Kassim, Habibu Nuru, AbdulHamid Mhoma na wengineo, marehemu mzee Islam
alishiriki kusimamia ujenzi wa msikiti mpya wa Ngazija ambao kwa sasa una
ghorofa tatu na ndiyo msikiti pekee uliopo Dar
es Salaam Central Business District. Pamoja na usimamizi wa ujenzi wa
misikiti, Mzee Islam ameandika vitabu mbali mbali vya dua na nyiradi na alikuwa
mmoja wa wasimamizi wa uradi wa kila wiki Masjid Ngazija na Masjid Rawdha.
Kulia: Dr. Gharib Bilal Makamu wa Rais Zanzibar Mstaafu, Sheikh Saleh, Sheikh Ahmed Islam na Sheikh Zubeir Yahya Imam Mkuu wa Msikiti wa Mtoro wakiwa Masjid Ngazija |
Mchango wa marehemu Mzee
Islam katika kuwaendeleza vijana wa Kiislamu kielimu ni mkubwa bila kifani.
Nina hakika si watu wengi wanaofahamu kuwa mzee Ahmed Islam ndiye ambaye
aliyefanikisha kupatikana kwa kiwanja ambacho kwa sasa imejengwa shule ya
Sekondari ya Al Haramain jijini Dar es Salaam. Naishauri BAKWATA ambayo ndiyo
Wamiliki wa Shule ya AlHaramain wathamini mchango wa Mzee Ahmed Islam kwa
kulipa jina lake moja ya madarasa au kumbi za shule. Aidha Mzee Islam alikuwa
mstari wa mbele kwenye Taasisi ya Tanzania
Muslim Solidarity Trust Fund katika kusimamia nafasi za masomo za vijana wa
Kiislamu wanaokwenda kusoma Uturuki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya
Kiislam (Islamic Development Bank) iliyopo Jeddah, Saudi Arabia. Chini ya
ufadhili huo, kwa karibu miaka 30 sasa Benki hiyo imekuwa ikifadhili vijana wa
Kiislamu 15 kwenda kusoma masomo ya Uhandisi (Engineering) na Utabibu
(Medicine) kwenye Vyuo Vikuu nchini Uturuki. Miongoni mwa watu walionufaika na
mpango huu ni Dr. Hussein Mwinyi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Dr. Asante Rabi Kighoma Malima wa Chuo Kikuu cha Northeastern Marekani, Dr.
Mashavu, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, Dr. Munawwara Kaguta daktari
wa hospitali ya Aga Khan na wengine wengi.
Moja ya mafanikio
makubwa ya jitahada za marehemu Mzee Islam ni uvumbuzi ambao ulifanywa mwezi
Agosti 2014 na Dr. Asante Rabi Kighoma Malima ambaye alivumbua kifaa cha kuweza
kubaini maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na saratani (cancer) yakiwa katika
hatua za awali kabisa. Kutokana na uvumbuzi wa kifaa hicho ambacho amekiita Biolom, Dr. Malima alipewa tuzo na
Gavana wa jimbo la Massachusetts, Bwana Deval Patrick. Haya ni matunda ya mzee
wetu Ahmed Islam ambayo yameiletea sifa kubwa sana nchi yetu katika ulimwengu
wa Sayansi na Teknolojia. Aidha mwaka 2002, mzee Islam aliishawishi Taasisi ya Muslim Aid ya London kuja kujenga
maabara tatu za kisasa katika shule ya Sekondari ya Twayyibat iliyopo Temeke
Dar es Salaam. Katika kipindi hicho hicho, kwa kupitia Muslim Aid, Mzee Islam
pia alifanikisha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule ya Sekondari ya
Sotele, Kisiju Mkoa wa Pwani. Harakati za marehemu Mzee Islam kuwasaidia vijana
katika kutafuta elimu hazikuanzia Dar es Salaam. Wakati akiwa Zanzibar,
marehemu alikuwa akiwahimiza sana vijana kusoma na yeye binafsi alikuwa
akijitolea kuwapa vijana mafunzo ya ziada (tuition)
usiku kwa kutumia taa za kibatari/koroboi. Abdallah Mbamba aliyekuwa Radio ya
Umoja wa Mataifa, New York na sasa anaishi Oman anakumbuka sana mafunzo haya ya
ziada kuanzia darasa la sita hadi la nane kabla ya Mapinduzi masomo ambayo
yalimsaidia yeye na wenzake wengi kufaulu vyema mitihani yao.
![]() |
Kulia Sheikh Ahmed Islam na Dr Dau Minna katika safari ya Umrah August 1997 |
Marehemu Mzee Islam
alikuwa Mcha Mungu sana. Pamoja na kuwa na umri mkubwa wa miaka 87 na kuandamwa
na maradhi ya miguu, kamwe hakuacha kuswali swala zote katika msikiti Maamur.
Siku zote alikuwa wa kwanza kuingia msikitini na kuswali kwenye kiti msitari wa
mbele. Hata wakati alipopata maradhi ambayo yalihitimisha safari yake hapa
duniani, hakuacha kwenda kuswali msikitini. Wiki tatu kabla ya kufikwa na
umauti, kwa muda wa siku mbili mfululuzo alikuwa hawezi kula vizuri na matokeo
yake akawa hana nguvu. Hata hivyo ilipofika siku ya Ijumaa akataka lazima aende
msikitini. Watoto wake walimsihi sana lakini hakukubali. Ikabidi abebwe
apelekwe Masjid Maamur kwa ajili ya swala ya Ijumaa na hiyo ndio ikawa Ijumaa
yake ya mwisho kuswali msikitini. Ijumaa iliyofuata wazee wa Masjid Maamur
pamoja na watoto wake wakamsihi sana awe anaswali nyumbani. Ikabidi akubali kwa
shingo upande kwani hakuwa na njia nyingine ya kwenda msikitini isipokuwa kwa
kubebwa na wabebaji ndio hao waliomtaka aswali nyumbani.
Mwaka 1997,
nilibahatika kusafiri kwenda Umra na marehemu Mzee Islam wakati Shirika la
Ndege la Tanzania (ATC) lilipofanya safari yake ya kwanza kwenda Jeddah, Saudi
Arabia. Katika safari yetu walikuwepo marehemu mzee Ahmed Rashad Ali, marehemu
Siraju Juma Kaboyonga na mkewe marehemu Jaji Madina Muro, marehemu Prof. Haroub
Othman, marehemu Balozi Selemani Hemedi, Dr. Idris Rashid, Jenerali Ulimwengu,
mama Fatma Maghimbi, Mhe Hamad Rashid, Hamza Aziz, Yahya Sinani na mwanahistoria
Sheikh Mohamed Saidi na wengineo. Wengi walimshuhudia takriban kwa siku zote
tulizokuwa safarini, marehemu Mzee Islam alikuwa anaamka usiku kufanya ibada.
Iko siku tukiwa Makka baada ya tawafu Mzee Islam kundi kubwa likiwa nyuma yake
alisimama kuomba dua mbele ya Kaaba hadi akatokwa na machozi.
Jambo hili la kuswali
Tahajud limethibitishwa na mmoja kati ya watoto wake ambaye alizaliwa mwaka
1961. Anasema yeye amemshuhudia baba yake akiswali Tahajud kila siku tokea apate fahamu. Inasemekana alianza utaratibu huu wa
kuswali usiku kuanzia mwaka 1951 na hakuacha kisimamo cha usiku mpaka maradhi
yalipomzidi mwishoni mwa mwaka huu. Siri nyingine aliyokuwa nayo marehemu Mzee
Islam ni kudumisha sunna ya kufunga siku za Jumatatu na Alhamisi. Kwa mujibu wa
maelezo ya mwanawe, amemuona baba yake akifunga sunna hii tokea yeye alipokuwa
mdogo.
Mzee Islam alikuwa
mtu wa watu na alikuwa mwepesi sana wa kusaidia watu wenye matatizo. Aidha mzee
Islam alikuwa anapenda sana kusuluhisha watu. Milango ya nyumba yake ilikuwa
wazi saa zote ambapo watu wa rika zote walikuwa wanaenda kila siku kutaka misaada
au ushauri. Mzee Islam alikuwa jeshi la
mtu mmoja na alikuwa zaidi ya Taasisi. Hapa ntasimulia matukio matatu kati ya matukio mengi sana ambayo yanaonesha ukarimu
na utayari wa marehemu katika kusaidia watu. Siku moja mama mmoja kutoka mkoa
wa Kilimanjaro alikwenda nyumbani kwa Mzee Islam akiwa na watoto wa kike watatu
ambao wote walikuwa yatima. Baada ya kueleza matatizo yake na ugumu wa maisha
ya kulea wale mayatima, marehemu Mzee Islam akamshauri wale watoto wabaki kwake
na yeye atachukua jukumu la kuwalea na kuwasomesha. Yule mama akakubali rai
ile. Hivi niandikavyo Taazia hii, mtoto mmoja amemaliza masomo ya Shahada ya Kwanza
katika Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa sasa
anafanyakazi Tanga. Mwingine amemaliza Shahada ya Uzamili katika fani ya
Uthamini vifaa vya ujenzi (Masters Degree in Quantity Survey) kwenye Chuo Kikuu
cha Ardhi, Dar es Salaam. Na wa mwisho hivi sasa anachukua Stashahada (Diploma)
ya Uhasibu.
Tukio la pili lilitokea mwaka 1991 wakati kijana
mmoja alipokwenda nyumbani kwa Mzee Ahmed Islam kumuomba msaada wa kwenda
masomoni Ujerumani. Kama ilivyo kawaida yake, Mzee Islam hakusita na alisimamia
uchangishaji wa fedha kwa ajili ya safari masomo ya kijana huyo. Leo hii,
kijana huyo ni Daktari Bingwa nchini Ujerumani. Mifano kama hii ipo mingi na
nafasi haitoshi kuisimulia yote.
Tukio la tatu lilitokea mwaka 2008 na linamhusu
kijana ambaye alikuwa na tatizo la ada ya kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kijana
yule alihitaji nusu ya ada (shs. 400,000) ili asajiliwe na Chuo. Baada ya
kuhangaika sana alipata shs. 100,000. Hatimaye kuna mtu alimwelekeza kwa Mzee
Ahmed Islam. Alipofika nyumbani kwake na kueleza shida yake, mzee Islam
akamwomba arudi siku ya pili. Naam, aliporudi siku ya pili alimpa shs. 300,000
na yule kijana akarudi chuoni kuendelea na masomo. Kana kwamba haitoshi, wakati
yule kijana yupo masomoni, kuna mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mzumbe
ambaye ni yatima alikuwa na tatizo sugu la nyonga. Kwa kuona hali yake ilivyo,
yule kijana wa Chuo Kikuu akamchukua mgonjwa hadi nyumbani kwa mzee Ahmed
Islam. Kwa kuwa uso umeumbwa na aibu, yule kijana akabaki barabarani na
akamuelekeza mgonjwa nyumba anayokaa mzee Islam. Marehemu alimtafuta daktari
bingwa wa kumshughulikia yule yatima hadi akapona. Hivi sasa yule yatima ni mhandisi
baada ya kuhitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa upande wa
michezo, Mzee Islam hakuwa nyuma. Wakati wa uhai wake, alikuwa mchezaji mzuri
wa mpira wa miguu kiasi cha kuitwa mchawi wa mchezo huo. Alipokuwa Zanzibar
alicheza timu ya Vikokotoni na timu ya Taifa ya Zanzibar. Akiwa mchezaji wa
timu ya Taifa ya Zanzibar, Mzee Islam alishiriki katika mashindano kadhaa
ikiwemo mashindano maarufu ya kombe la Gossage akicheza namba 10. Mwaka 1952
timu ya Taifa ya Zanzibar ilifika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika
Nairobi Kenya na kushika nafasi ya pili baada ya kuzifunga timu za Tanganyika
na Uganda. Pamoja wachezaji wengine, timu ya Zanzibar iliwakilishwa na marehemu
Mzee Ahmed Islam, marehemu Mzee Abdul Majham Omar, Mzee Mwinyi (Mpiringo), Seif
Rashid na Maulid Mohamed (Machaprala). Pamoja na umahiri wake wa kucheza mpira
wa miguu, Mzee Islam alikuwa mchezaji hodari wa Kriket na mpira wa magongo
(hockey). Kama ilivyo kwenye mpira wa miguu, marehemu Mzee Islam alichezea timu
za Taifa za Zanzibar kwenye Kriket na Hockey.
Wakati wa uhai wake, Mzee
Islam alikuwa mzungumzaji wangu sana sio tu kwenye masuala ya jamii lakini pia
masuala ya michezo. Mimi na marehemu tulikuwa tunakubaliana kwenye mambo mengi
sana isipokuwa mambo mawili ambayo tulikubaliana kutokubaliana. Kwanza kwenye
upenzi wa mpira kwa timu za hapa nyumbani
marehemu mzee Islam alikuwa mpenzi mkubwa wa Yanga wakati mimi ni mpenzi
wa Taifa Stars. Kwa upande wa timu za nje ya nchi, Mzee Islam alikuwa anaipenda
sana Manchester United. Bahati mbaya sikuwahi kumuuliza sababu ya yeye kuipenda
Manchester United. Kama sababu ni kutembelea jiji la Manchester wakati
alipokuwa masomoni Uingereza, basi nilitarajia angeipenda Manchester City kwa
sababu klabu hiyo ndiYo ipo katika jiji la Manchester wakati timu ya Manchester
United ipo shamba kabisa kwenye kitongoji kidogo kinachoitwa Old Trafford. Kwa
hapa nyumbani, kitongoji cha Old Trafford mfano wake ni kama vile Dar es Salaam
na Ruvu Darajani pale panapouzwa samaki wakavu au mbele kidogo kwenye kijiji
cha Vigwaza. Wenyewe Waingereza wanasema, ‘’There
is only one team in Manchester,’’ (Manchester kuna timu moja tu) ambayo ni
Manchester City. Pia wanao msemo wao unaosema, ‘’There is only one football team in London; the Gunners!’’ (London
kuna timu moja tu ya mpira wa miguu; washika Bunduki). Najua Balozi Saleh
Tambwe na Balozi Juma Mwapachu watalipinga hili. Lakini haya si maneno yangu.
Niliwahi kuandika
mapema mwaka huu kuwa kutokana na vifo vilivyoongozana vya wazee wa Dar es Salaam,
jiji letu limebaki kuwa na ukiwa. Mwaka huu tumeshuhudia kuondokewa kwa Kamanda
Dr. Mohamed Chiko, Mzee Iddi Sungura, Mzee Issa Ausi (Smart Boy), Ali Bob, Mzee
Kitwana Selemani Kondo, Balozi Abdul Karim Omar Mtiro (Cisco), Kleist Abdul
Wahid Sykes na sasa Mzee Ahmed Islam. Jiji la Dar es Salaam limegubikwa na
huzuni kubwa. Lakini kwa sababu kifo ni faradhi hatuna budi tuikubali hali
hiyo.
![]() |
Kulia: Sheikh Ahmed Islam, Mussa Sykes na Dr. Ramadhani Dau Jeddah katika safari ya Umrah wakipata kifungua kinywa |
Mzee Islam
ametangulia lakini ameacha simulizi ambazo zitazungumzwa kwa miaka mingi sana
baada ya yeye kuondoka. Wakati wa uhai wake, marehemu Mzee Islam na mama yetu
Bi Rukia Ahmed Iddi ambaye alifariki 1989 walijaaliwa kupata watoto sita ambao
ni Islam, Biubwa, Mohamed (maarufu Eddy), AbdulRahman, Abubakar na Mussa.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu Amrithishe mzee wetu Ahmed Islam Jannat Firdous kama
Alivyosema Mwenyewe kwenye Quran Sura 23 Aya 1-11 pale Alipozitaja sifa za watu
wema kisha Akamalizia kwa kusema Atawarithisha Firdous na wataishi humo milele.
Pia tunamwomba Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema na Atukutanishe na
mzee wetu Ahmed Islam kwenye Firdous. Aaamiin.
No comments:
Post a Comment