Thursday, 28 December 2017

USHUHUDA WA KWELI KUHUSU WEMA WA SHEIKH AHMED ISLAM NA KALEZI HEMEDI


Sheikh Ahmed Islam 

Ushuhuda wa kweli👇

Innaa lillaah wainnaa ilayhi raajiuun

Abul Fatma... huo ni msiba mkubwa sana, kwa kweli tumefiwa na mzee mchamungu.

Mimi Kalezi Hemedi, nilipata bahati ya kumjua, na ninadiriki kusema alichokisema Dr Dau ni ukweli mtupu.

Hapa nina uchungu mkubwa sana, Mzee Islam katutoka...? 
Alhamdulillah... ninawajibika kesho kwenda Dar inshaallah.

Nitoe ushuhuda kidogo katika kutilia nguvu alichosema Balozi Ramadhani... 
Binafsi (Kalezi Hemedi) na haya ni ya kweli na Allah anashuhudia na wala si kutafuta fakhari...

Mwaka 2008 nilijiunga na Chuo Kikuu Mzumbe, nilikaa wiki mbili bila kufanya usajili kwa kuwa Uongozi wa Chuo walitoa sharti la kila mwanafunzi alipe nusu ya ada ndiyo aweze kusajiliwa.

Kwa kuwa tulijua kuwa HESLB wangetoa majina ya Wanafunzi waliopata Mkopo mapema, na kwa kuwa tulijua tuna dhamana ya mkopo wengi katika wanafunzi tulitumai tusingepoteza nafasi za masomo kwa kutotimiza sharti la chuo

Ajabu, wale wanafunzi ambao wazazi wao waliweza kulipa nusu ya ada walisajiliwa na Bodi ya Mikopo walikuwa na utaratibu wa release majina ya wanafaika wa mikopo punde tu baada ya kupata uthibitisho kutoka vyuoni kuwa wanafunzi husika walikamilisha usajili.

Hapo ili nilazimu nirudi Dar nikamuone mshauri wangu mkubwa wa masuala yangu ya maisha (Marehemu Sheikh Idd Hussein Nyamweru Ndola wa Mwananyamala) ambae baadae aliniridhia nimuoe bint yake na kuwa mkwe wangu.

Nilivyofika kwa Sheikh Idd nikamuhadithia na akaingia ndani akanipa shs. laki moja, kisha akanambia... ''Nenda Bandarini, katika Kampuni ya Fast Ferries kamtafute mtu anaitwa Kassim Kombo, ukimuona mhadithie majambo yako halafu mwambie nimeagizwa na Sheikh Idd nije nikueleze haya.''

Ada kwa fani niliyokuwa nachukua kama sikosei ilikuwa ni Tshs 800,000/= kipindi hicho, na nusu yake ilikuwa ni Tshs 400,000/= kwa hiyo ile laki alonipa Sheikh Idd ilikuwa haitoshi.

Baada ya kumueleza Sheikh Kassim Kombo haja yangu, alifurahi na kunipa nasaha nyingi, akaendelea..."Kwa uharaka wa jambo lako... ntakuelekeza sehemu mbili... hii moja naamini watakuwa na maswali mengi sana na huenda wasikusaidie ila hii nyingine naamini kwa msaada wa Allah patapatikana faraja ila vyovyote vile iwavyo akikuuliza nani kakuelekeza... jitahidi usinitaje." Mwisho wa kumnukuu.

Moja ni taasisi na siwezi itaja, nilikwenda na yaliyotokea ni kama yalivyoelezwa na Sheikh Kassim Kombo na mahala pengine ndio kwa huyu mzee wetu Sheikh Islam.

Alhamdulillah, nilifika Masjid Maamur, ilikuwa ni wakati wa adhuhr, kwa bahati mbaya nilichelewa jamaa na kumkosa lakini akapatika kijana mhudumu wa Msikiti akanipeleka, nikakutana nae na kumueleza haja yangu.

Allah Akbar Allahu Akbar, huyu mzee alikuwa mtu, sijui nimuelezeje, ''any way,'' alinambia niende kesho yake na nilifanya hivyo, na akanipa shs.  300,000/= nikarudi chuo na kuendelea na masomo.

Kwa ambao tulikuwa Mzumbe miaka ile mtakumbuka kuna kijana wa Mzumbe Secondary, alikuwa ni yatima na alipata maradhi ya nyonga, sie kipindi tunashtakiwa tatizo lake kama Viongozi wa Waislam tulichangishana lakini fedha iliyopatikana haikutosha (nadhani Brother Hashim Majaba unamkumbuka).

Basi kwa wajihi niliomuona nao Mzee Islam nilipata nguvu ya kumpeleka yule kijana, lakini kama binadamu niliishia kwenye njia ya mlango wa kuingilia mtaa wake na kumwelekeza aende nami asinitaje.

Alhamdulillah alikwenda, na si tu alimsaidia bali alimtafutia Dr. Bingwa wa Muhimbili na akampeleka na Mzee Issa akawa anasimamia matibabu yake.

Yule kijana sijui sasa hivi yupo wapi ila alifaulu kusomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam....

Jambo la ajabu ambalo nilikuwa nikiliona kwa yule mzee, maana nyumbani kwake nilikuwa naenda mara kwa mara kumsalimia... ni Upanga tena Dar, jiko lipo karibu na sebule kiasi ukiingia nyumbani kwake unaanza jikoni lakini sebule haina joto, halafu kuna harufu nzuri sana, sana, sana, kiasi nilikuwa naamini huenda pailikuwa pakiwashwa ubani lakini ule wa ajabu.

اللهم قدس روحه و ضريحه برضوان
الَّلهُمَّ بَدِّلْهُ دَارًا خَيْرًا من دَارِهِ وَ اَهلاً خيرا مِنْ اَهْلِه اٰمِيْن


No comments: