Utangulizi
![]() |
Mh. Zitto Kabwe |
Mh. Zitto
Kabwe ndiyo sasa nimejua kuwa ni mgonjwa na anahitaji kuaguliwa ila maradhi
yanayomsibu ni maradhi mazuri kila mtu amuombe Mola amjaalie na sababu ni kuwa kwa
kawaida maradhi hufifilisha mwili lakini maradhi haya badala ya kuchosha mwili
hayo huujenga mwili ukawa imara na siha nzuri hasa ubongo. Mh. Zitto ni msomaji wa
vitabu wa sifa. Mwaka jana aliweka orodha ya vitabu alivyosoma mwaka mzima.
Nilimuonea wivu sana lakini ni ule wivu mzuri wa mimi kutamani niwe kama yeye
si ule wa hasad wa kutaka neema ile ya usomaji imuodokee hata kama mimi sitoipata.
Hii ni roho mbaya.
Leo
mmoja wa marafiki wa Mh. Zitto kwa kuwa anajua mimi ni mpenzi wa vitabu ingawa
si msomaji wa kiwango cha Mh. Zitto kanirushia makala aliyoandika Mh. Zitto (ambayo
ndiyo hiyo hapo chini) kunionyesha orodha ya vitabu alilvyosoma rafiki yetu
katika miezi kumi na mbili iliyopita. Nimeogopa sana nikajiambia huyu Zitto ni ‘’Jamal al Layl,’’ mkeshaji, akisoma usiku kutafuta elimu. Hii imenifanya nielewe kwa nini
Bunge hukaa wima, likasimama na kutulia tuli kama maji mtungini wakati Mh.
Zitto anachangia hoja yoyote Bungeni. Hakika akili mtu huzaliwanazo lakini
kusoma kunaongeza sana maarifa.
Nimemtia
Mh. Zitto katika orodha yangu ya watu nikiwausudu sana miaka na miaka kwa ajili
ya maktaba zao na mapenzi yao ya vitabu na nitawataja lau si kwa mpangilio wa
uzito wao. Naijua Maktaba ya Abdilatif Abdallah maktaba yake nimeiona London na
Humburg, Mashaallah siwezi kuihadithia yataka mtu aishuhudie kwa jicho lake
mwenyewe. Naijua maktaba ya Juma Mwapachu ingawa miaka mingi sijaoina na ya Walter
Bgoya. Ukifika nyumbani kwa watu hawa unaweza kuonekana huna adabu jinsi
utakavyokuwa unachakura vitabu safu na safu ukutani badala ya kutulia kweye
kochi kama mgeni na hutoweza kuvimaliza vitabu hivi.
Napenda
kuhitimisha kwa kusema kuwa zamani kidogo Juma Mwapachu alipata kuniambia kuwa
Maktaba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyoko Butiama ni ya kipekee.
Itapendeza sana kama waheshimiwa wetu In Shaa Allah na wao watapata ugonjwa huu
wa kupenda kusoma kama Mh. Zitto Kabwe Mbunge wa Kigoma, Mjini.
MS
Vitabu Nilivyosoma Mwaka 2017
Niliuanza
mwaka kwa matumaini makubwa kuhusu usomaji wa vitabu. Mwezi februari Prof.
Karim Hirji alinipa zawadi ya vitabu 11 na mimi mwenyewe nilinunua vitabu 12,
lakini sikuweza kusoma vyote kutokana na ama kununua vitabu vipya kila
ninaposafiri ama kuingiliwa na shuguli nyengine. Mwaka 2017 nimesoma vitabu 36
tu na vitabu viwili navisoma kwa pamoja kumalizia mwaka.
Wakati
mwaka 2016 nilisoma vitabu vingi kuhusu udikteta na hususan namna udikteta
mamboleo unavyotekelezwa nchini Urusi mwaka huu nilijikita sana katika kupanua
wigo wa uelewa kuhusu itikadi ya Ujamaa. Kwamba mwaka 2017 ni miaka 50 ya
Azimio la Arusha kulichangia sana kutoka vitabu vingi vinavyohusu Ujamaa au
Wajamaa.
Mwaka
2016 nilisoma riwaya nyingi kuliko mwaka huu ingawa nimeendelea na kazi za
Mankel na Grisham, pia nimesoma kazi za Ally Saleh ( moja nimeorodhesha na
nyengine sijaorodhesha maana bado najisomea au nazirudia kuelewa muktadha wake).
Orodha
yangu ya mwaka huu ni hii pamoja na maelezo kidogo.
Mwanasiasa
Mjamaa wa Uingereza Jeremy Corbyn alinivutia mno mwaka 2017 na kuanza kusoma
vitabu vilivyomwandika ili kumwelewa zaidi na kuelewa namna alivyofanikiwa
kukichukua na kukiongoza Chama cha Labour cha Uingereza. Nilibahatika kukutana
naye na tangu mwezi Februari amekuwa ni rafiki mkubwa sana. Kuwa na Mjamaa kama
Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani kwenye nchi ya Magharibi, nchi ya G8 ni
jambo kushangaza kidogo kwa dunia ya sasa ambayo kuna watu wanamini kuwa Ujamaa
hauna nafasi tena. Nilimsoma sana Corbyn na pia Mjamaa mwengine Bernie Sanders
wa Marekani. Hii ilinifanya nisome kitabu kingine kuhusu namna siasa
zinavyobadilika kabisa katika nchi za Magharibi na kupelekea watu wenye
misimamo mikali ya kulia na kushoto kuibuka. Emanuel Macron ambaye sasa ni Rais
wa Ufaransa alishangaza dunia mwaka 2017. Hilo ndio kundi la vitabu 6 vya
vyanzo.
1.
Jeremy Corbyn: Accidental Hero
W
Stephen Gilbert
2. The
Candidate: Jeremy Corbyn’s improbable path to power
Alex
Nunns
3.
Corbyn: The strange rebirth of radical politics
Richard
Seymour
4. Our
Revolution
Bernie
Sanders
5. The
rise of the Outsiders: How mainstream politics lost its way
Steve
Richards
6. The
French exception: Emmanuel Macron-the estra ordinary rise and risk
Adam
Plowright
Mwaka
2017 nilitumia muda mwingi kuelewa vizuri itikadi ninayoamini ya Ujamaa. Hivyo
nilisoma vitabu kuhusu baadhi ya watu walioandika kuhusu au kujenga Ujamaa
nyakati mbalimbali na sehemu mbalibali za dunia. Vitabu 10 vifuatavyo vinahusu
Ujamaa na wajamaa. Katika kundi hili napendekeza kitabu cha Yanis Varoufakis
kuhusu historia ya ubepari kwa watu wanaotaka kuelewa mfumo wa uchumi wa soko
unavyofanya kazi.
7. Rosa
Luxembourg or: The Price of Freedom
Jorn
Schuetrumpf
8. My
Life
Fidel
Castro with Ignacio Ramonet
9.
October: The story of the Russian Revolution
China
Mieville
10.
Marx’s Capital
Ben
Fine and Alfredo Saad-Filho
11. 75
Years of the Communist Party of Vietnam
12.
Liberalism and its discontents: Social Movements in West Africa b
Ndongo
Samba (Ed)
13.
Talking to my daughter about Economy: A brief history of capitalism
Yanis
Varoufakis
14. The
enduring relevance of How Europe Underdeveloped Africa
Karim
Hirji
15. The
contradictions of Capital in the Twenty-First Century
Jeremy
S and Nicole R
16.
Social Security works
Nancy
Altman and Eric Kingson
17. 23
Things They Don’t Tell You about Capitalism
Ha-Joon
Chang
Afrika
ya Kusini bado inapiga hatua katika ukombozi wa kweli baada ya kuondoa ubaguzi
wa rangi. Miaka 5 ya Nelson Mandela kama Rais inakuonyesha Madiba mwenye
madaraka na namna aliyatumia kuanza kusuka jamii mpya. Suala la uteuzi wa
mrithi wake ambalo limeendelea kuwa gumzo kwa miongo miwili nimeelezwa vizuri
kwenye kitabu cha Dare not linger na baadhi ya maelezo yanafanana kidogo na
maelezo ya kwenye kitabu cha Ramaphosa hapa. Ni kweli Mandela alimtaka
Ramaphosa kuwa mrithi wake lakini alishauriwa tofauti na Rais mstaafu Kaunda na
Rais mstaafu Nyerere kwamba Thabo Mbeki ndiye chaguo lao na Mandela akatii
ushauri wa wenzake. Mambo ya sasa ya Afrika Kusini hasa kuhusu ufisadi na
uongozi mbovu yanatia simanzi sana. Vitabu 5 vifuatavyo vinahusu Afrika Kusini na
baadhi ya watu wake muhimu kwenye siasa za ukombozi na siasa za sasa.
18.
Dare Not Linger: The Presidential Years
Nelson
Mandela and Mandla Langa
19. A
Simple Man: Kasrils and the Zuma enigma
Ronnie
Kasrils
20. The
President’s keepers: Those keeping Zuma in power and out of prison
Jacques
Pauw
21.
Ramaphosa: The Man who would be King
Ray
Hartley
22.
Woman in the wings: Nkosazana D Zuma and the race for the presidency
Carien
du Plessis
Nimekuwa
mfuatiliaji wa masuala ya mfumo wa kodi za kimataifa na namna baadhi ya nchi za
visiwa zikiitwa Tax Havens zinavyotumika kuficha fedha chafu zinazotokana na
ukwepaji wa kodi. Naheshimu kazi za waandishi wa habari za uchunguzi na Wabunge
wenzangu katika kufichua namna dunia inaibiwa nan chi zinazoendelea kupoteza
matrilioni ya fedha. Afrika peke yake inapoteza USD 50 bilioni kila mwaka
kutokana na mfumo fyongo wa kodi za kimataifa. Vitabu hivi 2 vimenisaidia sana
kuuelewa mfumo wa kodi za kimataifa na namna mabunge yanaweza kubomoa mfumo wa
kinyonyaji unaonufaisha matajiri wachache.
23. The
Panama Papers: Breaking the story of how the rich and powerful hide their money
Bastian
Obermayer and Fredrik Obermaier
24.
Called to Account: How corporate bad behavior and government waste combine to
cost us millions
Margaret
Hodge
Napenda
historia ya Afrika. Sikuwa nimemwelewa vizuri zaidi Mfalme Haile Selasie kama
anavyoelezwa na Asfa. Kitabu changu cha mwaka 2017 ni Zanzibar Uhuru maana
kimeleeza miezi ya mwanzo ya Uhuru wa Zanzibar na Mapinduzi na maisha ya
baadaye kwa namna ambayo inaeleweka na kuondoa kabisa propaganda tulizolishwa
mashuleni kuhusu Uhuru wa Zanzibar na Mapinduzi.
25.
King of Kings: The triumph and tragedy of Emperor Haile Selasie of Ethiopia
Asfa-Wossen
Asserte
26.
Zanzibar Uhuru: A Revolution, two women and the challenge of survival
Anne M
Chappel
Ndugu
yangu Rakesh Rajani alinitambulisha kwa mwandishi Coates na nimejikuta ninasoma
kila kazi yake. Mjadala wa mahusiano ya watu weusi na nchi ya Marekani bado
mbichi kabisa.
27. We
were Eight Years in Power: An American tragedy
Ta-Nehisi
Coates
28.
Between the world and me
Ta-Nehisi
Coates
Bado
naendelea kujifunza namna nchi zinatoa watu wake kwenye dimbwi la umasikini.
Vile vile kuna haja ya kuelewa upya kabisa mfumo wa uchumi tofauti na nadharia
tunazosoma darasani. Vitabu hivi viwili vinaweza kukupa maarifa mapya kabisa
namna uchumi unaweza kutumikia watu badala ya watu kutumikia uchumi.
29. How
China escaped poverty trap
Yuen
Yuen Ang
30.
Doughnut Economics: Seven Ways to think like 21st-century Economist
Kate
Raworth
Naendelea
kujifunza namna miji inaendeshwa ili kupata maarifa ya kutekeleza katika Mji wa
Kigoma Ujiji ambapo tunajitahidi kujenga Manispaa ya Kijamaa katika nchi ambayo
zimetupilia mbali sera za kijamaa na ukombozi wa mtu wa chini kabisa.
31.
View from the city hall: reflections on governing Cape Town
Patricia
De Lille and Craig Kesson
32.
Taken for a ride: grounding neo liberalism, precarious labour, public transport
in an African Metropolis
Matteo
Rizzo
Nimefurahi
kusoma kazi za Ally Saleh na nimeendelea kusoma riwaya za magwiji. Ally Saleh
amechangia kuelewa muktadha wa kizanzibari katika maandiko yake. Jumba Maro
ambayo sijaiorodhesha hapa na la kuvunda zinaeleza maisha ya Wazanzibari na
harakati zao kwa lugha nyepesi ya kifasihi. The Roaster Bar kinafurahisha na
kufundisha kuhusu maisha ya vijana wanasheria kwenye vyuo hewa vya sheria na
changamoto za mfumo wa uhamiaji na utoaji haki huko Marekani. Riwaya ni
Therapy.
33.
After the fire
Henning
Mankell
34.
Rogue Lawyer
John
Grisham
35. The
Roaster Bar
John
Grisham
36. La Kuvunda
Ally
Saleh
Nina
maliza mwaka na vitabu 2, Zeitoun cha Dave Eggers kuhusu hadithi ya familia
moja ilivyofanya kazi ya kupigwa mfano kuhusu kimbunga cha Katrina huko New
Orleans Marekani. Kitabu cha Pili ni The Feast of the Goat cha Mario Vargos
Llosa kuhusu udikteta wa Rafael Trujillo wa nchi ya Dominican Republic
ulivyoleta vita ya wenyewe kwa wenyewe na umwagaji mkubwa wa damu za raia wasio
na hatia.
Sikufikia
idadi ya vitabu vya mwaka 2016 lakini nimeongeza maarifa hususan kwenye eneo la
misingi ya itikadi ya Ujamaa. Haukuwa mwaka mbaya kwenye usomaji, nilipata muda
wa kutosha ingawa kuna vitabu sikumaliza au sikuvianza kabisa. Nimetimiza miaka
5 sasa natoa orodha kila mwezi Disemba na kupitia kwayo nimevutia watu wengi
kupenda kusoma. Mungu akitupa uhai nitaendelea kuwatajia vitabu vyangu kila
mwaka na pia tunaweza kujadili baadhi yake kwa pamoja.
Nawatakia
kheri ya mwaka mpya 2018 na mungu awasaidie kumaliza kwa amani mwaka 2017.
Zitto
Kabwe, Mb
Kigoma
Mjini
Kushoto: Mh. Zitto Kabwe na Mwandishi |
![]() |
Kulia: Abdilatif Abdalla na Juma Mwapachu wakiwa New Africa Hotel katika uzinduzi wa kitabu, ''Nyerere: The Early Years,'' kilichoandikwa na Thomas Molony |
No comments:
Post a Comment