SHEIKH AHMED ISLAM (1930
– 2017)
KIONGOZI SHIRIKA LA
UMMA, SHEIKH, BABA WA VIJANA NA MWALIMU
Sheikh Ahmed Islam akiwa Masjid Ngazija akiongoza shughuli |
Allah ana njia za ajabu sana za kukutanisha waja wake
na kutokana na kusubihana huko mengi yakapatikana. Ilikuwa mwaka wa 1972 niko
ndani ya basi la KAMATA (Kampuni ya Mabasi Tanzania) natokea Nairobi likizo.
Basi limesimama Korogwe kupakia abiria. Katika basi lile akaingia kijana
mtanashati umri wangu karibia miaka 20 akaniuliza kama pale pembeni yangu kiti
kile ni wazi ili akae. Nilimfahamisha kuwa kiti ni kitupu. Akakaa na mara akaja
mtu mzima dirishani wakawa wanaagana. Yule alikuwa ni baba yake na
amemsindikiza. Huyu kijana jina lake ni Charles James Bossa. Bossa kuanzia siku
ile ndani ya lile basi akawa rafiki-ndugu hadi hii leo ninavyoandika. Bossa
alikuwa amemaliza shule na alikuwa anakwenda Dar es Salaam kufanya
‘’interview,’’ ya kazi Posta. Bossa aliajiriwa na Posta na akafanya kazi hadi
alipostaafu miaka michache iliyopita.
Katika taazia hii ya mzee wetu Sheikh Ahmed Islam
Bossa amekuwa na msaada mkubwa kwangu kwa kunieleza mengi ya Sheikh Islam kwani
alifanyakazi katika Idara ya Rasilimali watu ambayo Sheikh Islam alikuwa
mkurugenzi wake na ameshuhudia mengi katika utu, huruma na ukarimu wake kwa
wafanyakazi. Sasa ndiyo nami nakumbuka
kuwa katika mazungumzo yetu miaka ile sasa zaidi ya miaka 40, jina la Mzee
Ahmed Islam likawa halipungui mdomoni kwake akimtaja kwa sifa nzuri na za
kupendeza za ukarimu na huruma kwa vijana waliokuwa katika idara tofauti za
shirika lile. Kabla sijanyanyua kalamu
kuandika taazia hii nilimpigia simu Bossa kumpa pole kwa msiba wa mzee wake.
Bossa alinistaajabisha kwani alilokujanalo sikuwa nalijua. Baada ya kupokea
mkono wangu wa taazia akanambia, ‘’Mimi nilikuwako mazishini na nikamkumbuka na
mama yetu kwani hata mama tulimzika katika makaburi yale pale pale tulipomzika
Mzee Islam.’’ Nikamuuliza, ‘’Kwani ulikuwa ukimfahamu mkewe? Jibu likaja,
‘’Sana, wakati Mzee Islam alipokuwa mkurugenzi wetu mara kwa mara alikuwa baada
ya kazi jioni akituchukua katika gari yake tukienda nyumbani kwake pale Upanga
kunywa chai na sambusa, bajia na vitu vingi vya tunu na hapo ndipo tulipojuana
na mama. Walikuwa watu karimu mno.’’
Ilibidi nishushe pumzi. Mkurugenzi mzima anajishusha
chini kiasi kile cha kuwachukua wafanyakazi walio chini sana kwake kuwaleta
nyumbani kunywa nao chai. ‘’Sheikh Islam tukizungumzanae sana na alitusogeza karibu
sana na yeye. Sisi alitufanya kama wanae. Hata nakumbuka siku moja katulueleza
jinsi alivyonunua ile nyumba yake. Anasema yeye akifanyakazi Cable and
Wireless, Zanzibar na baada ya kampuni ile kuvunjwa na kuingizwa katika Shirika
la Posta la Afrika ya Mashariki, alipopewa mafao yake yeye alitumia fedha zile
kununua nyumba ile Upanga kwa shs: 54,000.00 kwa wakati ule. Sina la kukueleza
ndugu yangu Mzee Islam kawanusuru wengi katika kazi. Yeye alikuwa mzito sana wa
kuandika barua za karipio kali na kuadhibu. Kawaida yake alikuwa akifanya
nasaha na kutoa msamaha kisha akimweleza muhusika njia ya kulipa msamaha ni
kwake kuwa mfanyakazi mwema kwa faida yake mwenyewe na familia yake na kwa
shirika na nchi iliyompa fursa ya kazi ili aendeshe maisha yake bila tabu.’’
Nilikuwa kimya siwezi hata kutia neno ila kumuitika
rafiki yangu Bossa ili ajue simu haija katika na mimi namsikiliza kwa
makini. ‘’Mzee Islam alikuwa kama mlezi wetu, baba yetu akiuzuia mkono wake kuadhibu.
Kuna mwenzetu alikuwa afukuzwe kazi kama si Mzee Islam kumsaidia kisha
kumkalisha kitako. Ile kesi ilikuwa ya mtu kupewa ‘’summary dismissal,'' na yeye
alilijua hilo kwani aliondoka kazini akabaki nyumbani kusubiri kufukuzwa kazi.’’
Mzee Islam aliagiza aitwe aje kazini. Mzee Islam alimsamehe baada ya kumpa
nasaha. Huyu jamaa hivi sasa amestaafu kwa salama akiwa mfanyakazi wa Shirika
la Posta. Haya yalinitosha sikua na haja ya zaidi. Maisha yake mwenyewe Sheikh
Islam yalikuwa mfano tosha kwa wale aliokuwa akiwaongoza. Hakuna haja ya
kumfananisha na wakurugenzi wengi tuliopata kuwajua na pengine kufanyanao kazi
kwani hawastahili wala hawana hadhi hata ya kuwekwa kwenye mizani moja na
Sheikh Islam.
![]() |
Wafanyakazi mafundi wa mawasiliano ya simu kutoka Shirika la Posta Tanzania waliopelekwa Zimbabwe kwa juhudi za Sheikh Ahmed Islam wakiwa na Mwandishi (aliyevaa miwani) mjini Harare March 1993 |
Baada
ya Cable & Wireless kampuni ya Uingereza kufunga shughuli zake ndiyo ikawa
Extelcomms chini ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na ilipovunjika jumuia Extelcomms
ikaunganishwa na Posta na kuwa Tanzania Posts & Telecommunications
Corporation. Mwaka wa 1993 zikagawanyika kuwa TTCL na TPC. Jumuia ya Afrika ya Mashariki ilipovunjika mwaka wa
1977 Sheikh Islam akiwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Posta alifanya kazi kubwa
ya kuwakaribisha nyumbani wafanyakazi wa iliyokuwa East African Posts and
Telecommunication wengi wao wakiwa wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi Kenya
na Uganda. Hawa walirudi nyumbani wakiwa na hofu kubwa ya hali yao ya baadae
nchini Tanzania. Huu ulikuwa wakati hali ya uchumi Tanzania ilikuwa ngumu sana.
Sheikh Islam aliwatia moyo na kuwatuliza akiwaambia hakuna shida ya kudumu
daima. Zimbabwe ilipopata uhuru wake mwaka wa 1980 Wazungu waliondoka kwa wingi
na pakawa na shida ya wataalamu wa simu nchini. Sheikh Islam alisaidia sana
akishirikiana na serikali katika katika kuchagua mafundi wa simu ambao
walikwenda Zimbabwe kusaidia kuweka mambo ya mawasiliano sawa. Mafundi hawa
kutoka Tanzania wengine wao wakiwa bado vijana wadogo baadae walihamia Botswana
na nchi nyingine za Kusini ya Afrika katika kutafuta maslahi zaidi. Katika vijana waliopelekwa Zimbabwe na Sheikh Islam ni rafiki yangu Erick Mpwagi ambae baadae alihamia Marekani.
Mimi binafsi kumbukumbu yangu ambayo itabaki katika
fikra yangu ni uradi wa kila Alkhamis Msikiti Ngazija ambapo yeye na Sheikh
Aboud Maalim walikuwa hawakosi na kwa hakika ndiyo waliokuwa wakituongoza.
Kadri ya kukumbuka kwangu huu uradi umekuwa ukisomwa hapo msikitini miaka na
miaka na uliwakutanisha vijana na wazee hapo msikitini kutoka sehemu tofauti za
mji wa Dar es Salaam. Uradi huu mbali ya kumtukuza Allah, ulikuwa sababu kubwa ya
kujenga udugu na mapenzi baina ya wengi kwani nawafahamu hii leo watu ambao
nisingefahamiana kwa kiasi cha undani huu uliopo baina yetu kama si ule uradi.
Kwa hakika kwa sisi ambao wakati ule tulikuwa vijana sana si jelebi, kababu na
samabusa ndizo zilizokuwa zikitupeleka katika uradi, hapana. Uradi ule
ulitunufaisha zaidi ya hapo. Labda kama si uaradi huu wengi tusingeingiliana na
Sheikh Islam na watu wengine kwa kiasi cha kuwa na mapenzi ya kiasi kilichokuja
kujengeka.
Nafasi yangu kubwa ya kumjua Sheikh Islam kwa karibu
zaidi ilikuja mwaka 1997 tulipokwenda sote Umrah na ndege ya kwanza ya Shirikia
la Ndege la Tanzania ilipofanya safari yake ya kwanza kwenda Jeddah, Saudi
Arabia. Namshukuru Allah kuwa si tu kuwa nilipata kuwa karibu yake tukiwa
safarini, bali tulikuwa sote katika dhifa tuliyoandaliwa Al Harithy Hotel, moja
ya hoteli mashuhuri Jeddah na vilevile mimi na Dr. Dau tulilala ubavuni kwake
katika nyumba ya Tanzania Haj Trust ambako baadhi yetu tulifikia. Si haya tu
bali Sheikh Islam alituongoza Makka katika Umrah na baada ya kumaliza alisimama
mbele ya Kaaba akaomba dua hadi machozi yakammwagika. Sote tuna machozi lakini
tabu kutoka kwa ugumu wa nyoyo zetu.
Baada ya kufanya Umrah baadhi yetu tulikwenda Madina
kumzuru Mtume SAW Sheikh Islam akituongoza. Nakumbuka tukiwa Madina asubuhi
baada ya kusali Fajri Masjid Nabawy Sheikh Islam, Balozi Ramadhani Dau
na mimi tulikwenda nje si mbali na msikiti kulikuwa na kiosi kinauza chai ya mkono
mmoja. Basi wakati tunakunywa chai sikumbuki nani alianza kusoma kasda maarufu,
‘’Twala Al Badru,’’ ninachokumbuka ni kuwa asubuhi ile ilikuwa njema sana
kwangu mimi na Dr. Dau kwani Sheikh Islam na yule mwenye kile kibanda wakawa kama vile wako
kwenye ‘’duet,’’ wanapokezana kusoma, mmoja akimaliza ubeti mwenzake anapokea.
Walipomaliza kasda hii wakaingia katika kasda nyingine, ‘’Yarabibi Mustafa…’’
Binafsi kasda hizi zilinikumbusha mbali sana Moshi kwa Mwalimu Juma aliyekuwa
akitusomesha watoto Qur’an Msikiti wa Ijumaa, Mtaa Chini. Miaka mingi sana sasa
nikiwa mtu mzima nilionana na Maalim Juma pale pale msikitini na nyuma tu ya
pale walipokaa ndipo aliponishikisha alif kwa kijiti. Maalim Juma alikuwa amekaa
na wazee wenzake. Maalim Juma hakunikumbuka kwani ilikuwa zaidi ya miaka 40
imepita. Mwenzake mmoja anaenifahamu akamwambia, ‘’Sheikh Juma lisikutishe lile
gari lake pale huyu mtoto umemsomesha hapa.’’ Nikizisikiliza hizi kasida mbele
ya Msikiti wa Mtume SAW nilikuwakumbuka waalimu wangu wote, Maalim Badi na Maalim
Mussa wote weshatangulia mbele ya haki.
Sheikh Islam katika utu uzima wake akiwa kachoka na
anatembea kwa shida hakuacha kuhudhuria shughuli zote alizokuwa akishiriki
wakati ana nguvu zake. Sasa ndiyo naanza kuelewa kwa nini kila alipokuwa kakaa
na nalitumia neno hilo kwa maana yake halisi. Sheikh Islam alikuwa akija
mazikoni Makaburi ya Kisutu atakaa kwenye mabenchi yale ya saruji pale karibu
na lango la kuingilia. Hapo atakuwa anapokea mikono ya wakubwa na wadogo
wanaokuja kumlaki. Hali ni hivyo hivyo akiwa kakaa kwenye kiti chake upande wa
kulia Msikiti wa Maamur. Kila aingiae atakwenda kumsalimu Sheikh Islam kiasi
mimi wakati mwingine nikimuonea tabu kuwa mbona hawa watu hawamwachi Sheikh
Islam akapumzika kila dakika kafika mtu. Lakini hii ndiyo ilikuwa namna ya watu
kuonyesha heshima na mapenzi yao kwake. Sheikh Islam alibeba mambo mengi ya
watu mabegani kwake bila kuona wala kuhisi tabu.
Kama alivyowalea wafanyakazi chini yake aliokuwa
akiwaongoza wengi wao vijana wa kike na wa kiume hivyo hivyo ndivyo alivyowalea
vijana katika jamii. Sheikh Islam katatua migogoro mingi ya kifamilia na
kasaidia vijana wengi kupata kazi na wengine kusoma ndani na nje ya nchi na
wengine kuoa na kuolewa. Hapa nitakielza kisa kimoja. Kisa cha mwenzetu mmoja
ambae alitaka kuposa katika moja ya koo za Dar es Salaam lakini palikuwa na
vikwazo kadhaa ambavyo vilikuwa kwanza viondolewe na wazazi wa pande zote mbili
ili posa ipelekwe na baadae wazee watoe idhini ya ndoa. Hofu ilikuwa ni wapi
mambo yaanze na ugumu ulikuwa hapo kuwa jambo lenyewe likikosewa kwenye hatua
za awali huenda likavurugika kabisa. Kwa kawaida wazazi wa binti huwa hawataki
kabisa kuonyesha kuwa wao ni wahitaji wa mtoto wao kupata mume. Kwa ajili hii
husubiri wafatwe kwa taadhima zote zikiwa zimezingatiwa. Ndugu yangu alikuwa
amezama kwenye lindi la mapenzi hajui afanye nini avuke kizingiti kilichokuwapo.
Sote tukimjua Sheikh Islam heshima yake katika familia
zetu. Wazee wetu wakimuheshimu Sheikh Islam mwisho wa staha. Huyu ndugu yangu
akaenda kwa Sheikh Islam nyumbani kwake kueleza kuwa anataka kuoa lakini pana
ugumu. Nilivyokuwa namfahamu Sheikh Islam sina wasiwasi wowote kuwa ndugu yangu
kwanza alipokelewa kwa utulivu wa hali ya juu na akamsikiliza na kumuuliza
maswali khasa kutaka kuipata yakini ya jambo lenyewe. Ndugu yangu yeye alikuwa kaweka
uzito juu ya kuwa wazazi wa pande zote mbili wamekuwa wagumu. Sheikh Islam yeye
akawa anamtuliza kwa kumwambia kuwa jambo la ibada haliwezi kuwa gumu kwa
yeyote amuogopae Allah labda kama halitofanikiwa ni kwa qadar ya Allah mwenyewe
hataki.
Sheikh Islam alikuwa anajua kuziweka heshima za watu
na alikuwa mtu wa kujishusha sana hakuwa yule mtu wa makuu wa kunyanyua simu
akazungumza na mtu kwa mbali. Baba wa Bwana Harusi mtarajiwa alipofatwa juu na
mama kuambiwa kuwa Sheikh Islam amekuja yuko chini alishtuka. Mzee, baba wa
Bwana Harusi mtarajiwa alishtuka. Sheikh Islam kugonga mlango wa nyumba yoyote
Dar es Salaam kuja kuwaona wenye nyumba ile ni heshima ya pekee isiyo kifani.
Huyu ni mcha Mungu mtu muungwana, kipenzi cha watu. Haraka mzee kashuka chini
akiziruka ngazi mbili mbili tayari tabasamu kubwa limetanda uso mzima kumlaki
Sheikh Islam. Baada ya kumkaribisha na kukaa na kahawa kuwekwa wakawa
wanaulizana hali. Huyu mzee wetu mtu mkubwa sana na Maa Shaa Allah ni mtu wa
kujiweza sana lakini yeye alikuwa anajua ndani ya dhati ya nafsi yake kuwa
nyumba yake Allah kaikumbuka kwa kumleta Sheikh Ahmed Islam. Hili kwake ilikuwa
ni baraka kubwa isiyo na mfano.
Sheikh Islam alianza mazungumzo kwa kusoma aya ya
Qur’an mnasaba na lile aliloendea. Kisha akamgusia vipi wazazi wanakasirishwa
na watoto kiasi watoto wanakuwa na uoga hata wa kuwaendea wazazi wao.
Akamwambia mzee wetu, ‘’Mtoto kaja kwangu kwa kuwa ana hofu kubwa ndani ya
nafsi yake juu ya Allah na wewe baba yake. Anajua kuwa bila ya radhi yenu yeye
hana kitu mbele ya Allah. Apate radhi yenu nyinyi wazazi wake ndipo yeye
atakuwa na mafanikio hapa duniani na kesho akhera.’’ Sheikh Islam alikuwa mtu
fasaha sana labda kwa ile hifdh yake kubwa ya Qur’an na nyuradi chungu mzima.
Kufika hapo akataka kujua tatizo nini kiasi posa isipelekwe nyumba ile na
kijana wao akaoa. Sheikh Ahmed Islam akaelezwa na bahati nzuri maelezo ya mzee
yalikuwa sawasawa na yale aliyopewa na Bwana Harusi mtarajiwa. Kikao
kikamalizwa kwa mzee kumshukuru sana Sheikh Islam na kumwambia kuwa wao
hawatakuwa na pingamizi madam yeye analisimamia jambo lile.
Mimi ni mmoja wa walioshudia harusi nyumbani kwa Bi.
Harusi, Sheikh Islam akiwa kakaa ubavu kwa ubavu na baba wa Bwana Harusi. Bwana
Harusi alikuwa kapendeza, sura inang’ara kwa tabasamu na furaha. Ndoa hii
imetoa mtoto ambae hiVi sasa kila siku baada ya kutoka shule anachukua mfuko
wake ambao ndani kuna juzuu yake anakwenda kusoma Qur’an chuo cha jirani na
nyumbani kwao. Kila siku ya Eid huyu mtoto na baba yake wanakuja kusali Eid Maamur
na baada ya sala watapita kwa Sheikh Ahmed Islam kumwamkia. Mtoto akiwa hajui kama
si juhudi za huyu mzee aliye mbele yake labda asingelizaliwa na baba yake huyu. Huu ni mfano mmoja katika mingi kwa yake
aliyofanya marehemu Sheikh Islam. Katika
uhai wake Sheikh Islam wanasema waliokuwa karibu yake kuwa alipeleka posa 200
na zote zilikubaliwa isipokuwa moja. Rafiki yangu Charles James Bossa anasema Sheikh Islam
hakuacha kumshinikiza kufunga ndoa hadi alipooa. Kwa maneno yake anasema,
‘’Mzee Islam kwetu sisi tuliokuwa tukifanyakazi Posta alikuwa baba na rafiki.
Huenda ni haya malezi ya Sheikh Islam kuwa sababu ya rafiki yangu kwenda kusoma Chuo
Cha Mzumbe na kisha kupata mafunzo zaidi Uingereza.
![]() |
Kulia: Sheikh Ahmed Islam, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Sheikh Aboud Maalim, Himid Ashraf na Said Kassim |
Hakika ni tabu sana kumwandika Sheikh Ahmed Islam bila
ya kumtaja rafiki yake kipenzi Sheikh Aboud Maalim. Wawili hawa walikuwa
mithili ya ambari na zinduna. Muda mwingi sana walikuwa pamoja na walifanya
mengi katika kuusukuma mbele Uislam. Kama alivyokuwa Sheikh Islam, Sheikh Aboud
Maalim alikuwa mzee wangu na mtu wangu wa karibu. Inawezekana pengine bila ya
wao wenyewe kufahamu, mapenzi baina yao na mapenzi yao kwa watu wengine
walijenga kundi kubwa la watu ambao wote kwa umoja wao wakiwapenda na
kuwaangalia kama viongozi katika jamii. Nakumbuka mmoja katika watu ambao
walikuwa katika kundi hili ni marehemu Kiaratu Hussein. Sheikh Islam alipofiwa
na mkewe msiba ule uliwapiga wengi waliokuwa karibu na yeye na Kiaratu
aliathirika sana. Tukawa tukizungumza ananifahamisha vipi Sheikh Islam alivyokuwa
mwenye huzuni kwa msiba ule na namna gani Sheikh Aboud Maalim alivyokuwa
akimfariji kila alipokuwa kamuona kakaa msikitini kajiinamia. Kiaratu
akiniambia kuwa kuwa Sheikh Aboud alikuwa akimshika akimpigapiga na kumwambia,
‘’Ahmed stahamilili mshukuru Allah…’’ Hawa walikuwa watu waliopendana kwa ajili
ya Allah na kwangu mimi nilijifunza kitu kingine kuwa watu wema, wema wao
huambukiza wale waliowazunguka hadi watoto wadogo.
Kiaratu alikuwa na mwanae akiitwa Hussein. Miaka ile
alikuwa mtoto mdogo wa shule ya msingi na kila mwezi wa Ramadhani alikuwa
akifuatana na baba yake pale msikitini Maamur. Kiaratu yeye ndiye alikuwa
akituongoza kwenye Sala ya Tarweh kwa nyuradi na kwa hakika Tarweh ya Maamur
ilikuwa ikipendeza. Mwanae Kiaratu Hussein nikimuona akiswali safu za nyuma na
watoto wenzake kati yao ni Mohamed Bakashmar mtoto wa Ahmed Rashad na Mohamed mwingine
mtoto wa Dr. Amza Mahunda. Hawa watoto wote walikuwa wakija pale msikitini
wamefuatana na baba zao. Baada ya sala hawa watoto watakwenda kumwamkia Sheikh
Islam na yeye atawashika mikono na kichwa bila shaka akiwaombea dua. Miaka
ikaenda na Kiaratu akatangulia mbele ya haki. Ramadhani ilipofika nikawa
naiambia nafsi yangu kuwa Ramadhani hii Tarweh itapooza bila ya sauti ya
Kiaratu pale mbele. Nilipata mshtuko mkubwa sana usio na kifani. Mara baada ya
kumaliza Sala ya Isha na suna nikamuona Hussein, mtoto wa Kiaratu kanyanyuka
kasimama mbele ameikabili kibla analeta nyuradi alizokuwa anasoma marehemu baba
yake. Kilichotufurahisha wengi naamini si tu kumuona mtoto kashika nafasi ya
baba yake katika jambo kubwa la ibada bali na kule pia alivyoshabihiana na baba
yake kwa sauti na zile ‘’gestures,’’ alipokuwa anasoma. Safu ya mbele pale
namuona kasimama Sheikh Islam na safu yake maarufu iliyozoeleka pale Maamur.
Nikaiuliza nafsi yangu, ‘’Huyu Hussein, huyu mtoto lini kapewa haya mafunzo?
Sikutaabika sana kuona ushawishi wa Sheikh Islam na dua zake kwa hawa watoto
waliokuwa wakisali pale na baba zao.
Kipo kisa kingine cha Mohamed mtoto wa Ahmed
Rashad. Kama mwenzake siku zote alikuwa kwenye jicho la Sheikh Islam pale
msikitini. Siku moja Sheikh Islam alikuwa anasafiri na kulikuwa na uradi
ukisomwa pale msikitini katika baadhi ya siku. Sheikh Islam akamwambia Mohamed
kuwa yeye atakuwa anaongoza kusoma uradi ule hadi yeye atakaporejea.
Akamkabidhi Mohamed kitabu cha uradi ule. Mohamed aliongoza uradi ule hadi siku
Sheikh Islam aliporudi. Aliporudi ilipofika wakati wa uradi ule Mohamed akampa
kitabu Sheikh Islam na yeye akawa kimya. Sheikh Islam akamwambia Mohamed
aendelee kusoma uradi ule. Bila kufungua kitabu Mohamed akaanza kusoma ule
uradi ghibu. Baba yake Ahmed Rashad na Sheikh Ahmed Islam wanamtazama na
kumsikiliza. Nitahitimisha kipande hiki kwa kumweleza Mohamed mwingie, mtoto wa
Dr.Mahunda. Katika maziko ya Sheikh Islam nikamuuliza Dr. Mahunda Mohamed
yuko wapi nilikuwa sijamuona muda. Dr. Mahunda akanambia baada ya kumaliza chuo
kikuu Uingereza Mohamed kenda India kusoma shahada ya pili.
Haya ndiyo matunda ya Sheikh Islam na ndiyo wanafunzi
wake ambao ambao nimewaona kwa macho yangu mwenyewe akiwalea pale msikitini
wakiwa watoto wadogo wakiswali safu za watoto nyuma ya msikiti wakati wakubwa
wanasali. Leo ni vijana wakubwa na ndiyo hawa nawaandika hapa. Hussein Kiaratu
yuko Uingereza anasoma, Mohamed Bakashmar, mtoto wa Ahmed Rashad ni Ph D
Political Science anafundisha katika moja ya vyuo vikuu Malaysia na kaoa Mmalay
na ana watoto na Mohamed Mahunda yuko India In Shaa Allah anafanya shahada ya
pili. Haya ndiyo matunda ya uongozi wa Sheikh Islam. Hakuwa mfano kwa vijana
peke yao bali hata kwa watoto wadogo ambao kwa wakati ule walipokuwa wadogo
huenda baadhi yetu walipochokozana safu za nyuma wakati tunasali walitukera.
Lakini babu yao Sheikh Ahmed Islam baada ya sala akiwashika vichwa na kuwaombea
dua Allah awaongoze watie furaha kwenye nyoyo za wazazi wao na ndani ya nyoyo
za umma.
Hatutaweza kummaliza Sheikh Ahmed Islam. Sheikh Islam alikuwa
mtu wa pekee. Tunaomba Allah amsamehe dhabi zake na amweke mahali pema peponi.
Amin.
No comments:
Post a Comment