Saturday 30 December 2017

TUNAYOJIFUNZA KUTOKA KWA SHEIKH AHMED ISLAM NA RAMADHANI K. DAU


TUNAYOJIFUNZA KUTOKA KWA SHEIKH AHMED ISLAM
Ramadhani K. Dau


Sheikh Ahmed Islam

Kufuatia msiba wa mzee wetu Sheikh Ahmed Islam, niliandika taazia kuelezea wasifu wake na mchango mkubwa alioutoa kuwaendeleza Waislamu na hasa kazi kubwa aliyoifanya kuwainua viijana wa Kiislamu kielimu.  Baada ya kuandika taazia hiyo, nimekuwa nikipokea maoni mengi sana kutoka watu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Wengi wao wametoa ushuhuda wa namna ambavyo wao binafsi walivyosaidiwa na marehemu Mzee Islam. Wengi zaidi wameonesha hamasa ya kutaka kuiga mfano wa Mzee Islam japo kwa uchache.

Kama nilivyoandika kwenye taazia, kifo ni faradhi na kila mmoja wetu ataonja umauti. Mzee Islam amekamilisha faradhi hii. Lakini pamoja na kuondoka kwake, ametuachia darsa na changamoto kubwa. Yapo mengi sana ya kujifunza kutoka kwake. Kutokana na umri tuliokuwa nao, ni dhahiri kuwa baadhi yetu hatutoweza kudumisha sunna ya kufunga Jumatatu na Alhamisi na kuanza kuswali Tahajud kwa zaidi ya miaka 60 kama alivyofanya Mzee Islam kwa sababu umri umeshatutupa mkono. Lakini hata kwa upande wa vijana, ni dhahiri pia kutokana na harakati za kupambana na maisha, wengi wao wataona ni uzito mkubwa kufanya hivyo kwa muda wa uhai wao, japo  hawajui urefu wa muda uliobaki.

Kama nilivyosema awali, marehemu Mzee Islam amefanya mengi na yapo mambo mengi ya kumuiga kila mtu kwa nafasi yake. Iwapo hayo ya kufunga Jumatatu, Alhamisi na kuswali Tahajud hatuyawezi, basi hakuna hata jema moja la marehemu Mzee Islam ambalo tunaweza kuiga na kulidumisha? Kwa mfano, kwa kuwa Mzee Islam ametumia muda mwingi wa uhai wake kusaidia vijana wa Kiislamu kupata elimu, hivi sisi tuliobaki (na hasa wale walionufaika na juhudi zake) hatuwezi kuanzisha taasisi (Ahmed Islam Foundation? --- AHIFO) na kujilazimisha kuchangia angalau shs. 10,000.00 kwa mwezi (au zaidi kulingana na uwezo wa mtu) kwa ajili ya kusaidia kusomesha mayatima au wanafunzi wasio na uwezo? Kuna njia bora ya kumuenzi Mzee Islam zaidi ya kudumisha mambo ambayo ameyasimamia?

Iwapo watapatikana watu 1,000 ambao watachangia shs. 10,000.00 kwa mwezi, taasisi itakusanya shs. 120 million kwa mwaka, fedha ambazo zinaweza kusomesha wanafunzi zaidi 100 kwa mwaka kwa kiwango cha Chuo Kikuu. Najua wapo watakaosema kuwa uzoefu unaonesha kuwa taasisi zilizoanzishwa kwa utaratibu kama huu wa kuenzi mazuri yaliyoachwa na marehemu hazikuwa na mafanikio. Mfano ni Sheikh Kassim Juma Foundation, Abubakar Tambaza Foundation nk. Kwa upande mmoja kuna ukweli kwenye kauli hii. Lakini zipo taasisi ambazo zilianzishwa kwa malengo kama haya na zimepata mafanikio makubwa sana. Mfano mzuri ni Hassan Maajar Trust.

Hii ni taasisi ambayo ilianzishwa tarehe 11 Julai 2011 kufuatia kifo cha ajali ya gari cha kijana Hassan Majaar kilichotokea tarehe 11 Novemba 2006 Mbabane Swaziland. Wakati wa kifo chake, Hassan alikuwa na miaka 18 na alikuwa anapenda sana kufundisha michezo mashuleni kwa vijana wasiojiweza.  Kutokana na sababu hiyo, wazazi wake waliamua kuanzisha taasisi ya kufadhili madawati, vitabu, kompyuta nk. Hadi sasa Taasisi ya Hassan Maajar imeshanunua na kusambaza madawati zaidi ya 9,000 kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya 30,000 kwenye mikoa 10. Lengo lao ni kununua madawati 3 milioni. Iwapo familia ya Bibi na Bwana  Maajar wameweza kufanya mambo makubwa kama haya tena kwa muda mfupi, naamini kabisa familia ya Mzee Islam ambayo inajumuisha wale wote walionufaika na jitihada zake wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi.

Wengi walioguswa na taazia wamenitumia ujumbe wa simu kuonesha hamasa zao na kusema wanatamani wafanye angalau 10% ya aliyoyafanya Mzee Islam. Hii ni ishara nzuri. Lakini hamasa na kutamani peke yake havitoshi. Wakati umefika tuzibadilishe hamasa zetu ziwe ni vitendo. Marehemu Mzee Ahmed Islam alikuwa anaswali Tahajud kila siku kwa zaidi ya miaka 60. Alikuwa anafunga mara mbili kila wiki kwa zaidi ya miaka 60. Kwa sababu mbalimbali nilizozieleza hapo juu inaelekea wengi wetu hatuwezi kufikia daraja hiyo. Lakini hivi kweli wengi wetu hatuwezi kuchangia shs. 10,000.00 kwa mwezi? (si kwa kila siku au kila wiki kama alivyokuwa akifanya Mzee Islam).

Nawaomba wale wote walioguswa na taazia hii, waweke nia na wawe tayari kuchangia angalau shs 10,000.00 kwa mwezi ili kuendeleza mazuri aliyoyasimamia mzee wetu Ahmed Islam wakati wote wa uhai wake.  Ili kulipa msukumo jambo hili, namwomba Mhe Dr. Hussein Mwinyi kwa upande wa wanaume na Dr. Mashavu kwa upande wa wanawake washirikiane na watoto wa Mzee Islam katika kulianzisha na kulisimamia jambo hili jema. Hii itakuwa ni sadaqa nzuri ya kumtolea mzee wetu. Kwa upande mwingine kuanzishwa kwa taasisi hii kutatoa fursa kwa watu wengi kupata fadhila za kusaidia mayatima na masikini.

No comments: