Thursday, 25 January 2018

CAPTAIN MALIK ''ENCYCLOPEDIA'' YA HISTORIA YA MPIRA

Captain Malik

Jina lake ni Captain Malik. Captain Malik ni mtu maarufu sana kwa watu wa Dar es Salaam hasa wa kizazi cha miaka ya 1950 nyuma kidogo na mbele kidogo ya hapo. Captain Malik sasa anaweza kuwa anakaribia miaka 80 na kupita kidogo. Captain Malik yuko katika orodha yangu ya watu ambao nimefahamiana nao na wamenishangaza kwa akili zao nyingi walizojaaiwa na Allah kiasi kuwa unapozungumza nao haukuchukui muda kutambua kuwa huyu si mtu wa kawaida ambae unaekutana nae Karikaoo kila uchao. Mara moja akili yako inatambua kuwa huyu ni mtu mwenye kipaji ambacho si cha kawaida.

Katika orodha hii yangu nitawataja wachache na nawataja kwa kuwa tayari wameshatangulia mbele ya haki – Peter Colmore, Jim Bailey, hawa ni Wazungu Colmore ni Mkenya mwenye asili ya Uingereza, na Bailey ni Kaburu wa Afrika Kusini na mwingine ni Sheikh Ali Muhsin Barwani, Mzanzibari. Kaka yangu Captain Malik yuko ndani ya orodha yangu hii.

Captain Malik katika ujana wake miaka ya mwishoni 1950 na kuanzia 1960 alikuwa akicheza mpira Young Africans ya Dar es Salaam akiwa nahodha na hapo ndipo alipopata jina lake hili la ‘’Captain,’’ ambalo limemganda hadi leo. Captain Malik ananiitikadi mimi kama mdogo wake nami siku zote amekuwa kaka yangu na kwa kweli si mimi tu, sisi wengi tuliokulia Kariakoo tunamuheshimu Captain Malik kama kaka yetu.

Jana nimemkuta Capatain Malik katika kizingiti cha Msikiti wa Manyema baada ya Sala ya Alasiri anavaa viatu aondoke. Baada ya mazungumzo nikamuomba nimpige picha na akanikubalia na ndiyo hiyo picha hapo juu. Captain Malik Allah amempa kile Wazungu wanakiita, ‘’Photographic Memory,’’ yaani kipaji cha kukumbuka kwa usahihi kabisa kila kile ambacho jicho lake limeona kuanzia tarehe, majina, mahali na yote yaliyokuwapo kwa wakati ule.

Kushoto Athmani Kilambo katika utu uzima 2010 na Abubakar Shariff mchezaji
wa  Cosmopilitan

Athmani Kilambo alikuwa mchezaji wa Yanga na pia timu ya taifa ya miaka ya mwanzoni 1960 akicheza nafasi yoyote ya ulinzi na alitokea Bagamoyo akiwa kijana mdogo labda miaka 20 hivi. Captain Malik ndiye aliyempokea Yanga na kumkabidhi jezi kucheza mechi yake ya kwanza Ilala Stadium. Huu ukaja kupelekea usuhuba mkubwa baina yao uliodumu nusu karne hadi alipokufa Kilambo. Mimi nimemfahamu Kilambo tayari keshakuwa mchezaji maarufu kabisa akijulikana ndani na nje ya Tanganyika wakati ule, mchezaji mwenye umbo kubwa lakini mwepesi na hodari wa ‘’sliding tackles,’ kiasi akiwamudu vilivyo wachezaji wakali wa enzi zile. Kilambo alipatapo kunambia siku moja kuwa yeye wagomvi wake walikuwa wachezaji wa Kenya hasa Wajaluo kwa kuwa wakitumia nguvu sana katika uchezaji wao. Kilambo anasema Kocha wao wa timu ya taifa ya Tanganyika Myugoslavia Celebic akijua mchezo wa Kenya wa kutumia nguvu  na alikuwa katika Gossage Cup akimpanga Kilambo beki wa kulia na Mohamed Chuma beki wa kushoto na hawa wote walikuwa, ‘’hard tacklers,’’ wana uwezo mkubwa sana wa kupambanisha chuma kwa chuma. Kilambo anasema washambuliaji wa Kenya wakiwaogopa sana wao.

TIMU YA BANDARI 1960s MWISHONI
Nyuma waliosimama kulia Maulidi Dilunga, Hassan Gobbos, Athmani Kilambo, Kitwana Manara, Abdulrahman Lukongo,
Kitenge ''Askari'' Baraka, Joseph Anthony.
Waliochutama kulia Mohamed Chuma, (pass), Jamil ''Denis Law,'' (pass), Mbaraka Salum, Abdulrahman ''Bwana Fedha'' Juma (pass) Mohamed Msomali

Turudi kwa Captain Malik.

Captain Malik siku moja kaanichekesha sana kiasi cha kutokwa na machozi. Anasema siku hizo Kilambo mgeni Dar es Salaam na Yanga bado hajawa, ‘’senior player,’’ bahati mbaya timu imeingia uwanjani Ilala Stadium yeye kachelewa na alipofika lango kuu askari wakakataa kumpitisha ingawa aliwaambia kuwa yeye ni mchezaji wa Yanga. Ikabidi Captain Malik afatwe ndani ili aje langu kuu kumtambua Kilambo na kumuingiza ndani awahi kuvaa jezi na kuingia uwanjani. Captain Malik anasema kamkuta Kilambo nje pembeni katoa macho kajikunyata hajui nini la kufanya.

Captain Malik ni ‘’Encyclopedia,’’ ya historia ya mpira Afrika ya Mashariki na hasa Tanzania. Ana hazina kubwa sana ya historia na matokeo muhimu ya mchezo huu ndani ya Yanga, Simba wakati ule ikiitwa Sunderland, Cosmopolitan na club ndogo za mjini kama African Temeke Good Hope, Liverpool, Kahe Republic, Rover Fire na nyingine nyingi za mitaani. Itafaa sana kama Tanzania Football Federation (TFF) watatafuta muda wazungumze na Captain Malik wapate historia za viongozi wa mpira waliopita kama marehemu Kitwana Ibrahim kiongozi wa Yanga maarufu sana Kondo Kipata, Patron wa Simba Habib Segumba akijulikana kama ‘’Underline,’’ au manahodha waliopita wa timu ya taifa kama Captain Ayub Mohamed, au ‘’strikers’’ wa kutisha kama Yusuf Mwamba au wachezaji waliocheza timu ya taifa katika umri mdogo sana kama Hemed Mzee, mchawi wa chenga, Mbwana Abushiri akijulikana kama ‘’Director,’’ wapigaji penalty na ‘’free kicks,’’kama Hemed Seif waliokuwa wakiogopewa, magolikipa hodari wa ‘’diving,’’ kama Kitwana ‘’Popat’’ kabla hajaacha kuecheza golini na kwenda kucheza mbele na kuwa mshambuliaji hodari. 




Captain Malik ataeleza vipi Kitwana alipomkosesha goli la wazi Enos Bondo katika mechi ya Tanganyika na Kenya Kombe la Gossage pale Kitwana alipochomoka golini wakati Enos Bondo keshawatoka mabeki wote anakabilina na goli na Kitwana akaruka juu na kuangukia kwenye miguu ya Bondo na kuokoa hatari ile na Kitwana Popat akatolewa nje kwa machela ameuia bega vibayasana. Picha hii Kitwana yuko hewani ilipigwa na ikatoka katika magazeti yote. Ilikuwa picha nzuri sana ya ‘’action.’’ Captain Malik anayajua yote haya na katika uhodari wake atakupangia timu yote ya Kenya na Tanganyika kutoka kichwani. TFF mtafuteni Captain Malik atawarithisha hazina yake na faida kubwa sana ya kumbukumbu itahifadhiwa.

Timu ya Tanganyika iliyochukua Kombe la Gossage 1965 waliochutma kulia ni Kitwana ''Popat'' Manara, Sembwana, Mohamed Chuma, Abeid Maulid, Mbaraka Salum, Abdallah Aziz
Nyuma waliosimama kulia Kitwana Ibrahim, Hemed Seif, Sharif Salim (Captain), Mwalimu Julius Nyerere, Kocha Celebic, Hamisi Kilomoni
Mstari wa nyuma ya Mwalimu Nyerere kulia Mathias Kissa, mwisho kushoto Mohamed Msomali, Emil Kondo, John Limo, Abdulrahman Lukongo, Hamisi Fikirini na Rashid Seif mdogo wake Hemed Seif

Hemed Seif katika utu uzima 2007

Captain Malik ana mengi katika suala la uchawi katika mpira na ''politics,'' za kupata wachezaji wazuri katika enzi zao, ‘’Benchi la Ufundi,’’ na atakupa na majina ya mafundi wenyewe na walikokuwa wakiwatoa na nini walikuwa wakifanya. Captain Malik atakupa na majina ya vijana waliokuwa wakitumwa kufanikisha mambo haya kabla ya mechi kubwa ya Simba na Yanga labda jana yake usiku wa kuamkia mechi na siku ya mechi wakati timu zinajitayarisha kuingia uwanjani. Miaka ile Kariakoo walikuwa wakiishi wenyewe wenyeji, bado hawajahama kuyapisha maghorofa. Siku ya meshi ya Yanga na Simba pale Mnadani. Mtaa wa Mafia na Msimbazi washabiki wa timu hizi watawasha vitezo na kuchoma ubani toka asubuhi na bendera zinakuwa zimepandisshwa za yanga na Simba zikipigwa na moshi wa ubani. Hali ya mji inakuwa imebadilika toka asubuhi washabiki wa Mnadani wanashambuliana kwa maneno makali makali ya kuvunjana nguvu kuwa nani atatoka mshindi jioni ile. Wkati ule mechi hizi zinachezwa Ilala Stadium. Kwa leo ukitazama unajiuliza watu wailiweza vipi kuenea uwanja mdogo kama ule. Captain Malik kayashuhudia haya yote kwa macho yake na si kama mchezea pembeni.  

Katika ''politics'' za kuwaleta wachezaji utastaajabu kujua kuwa Yanga walikuwa na mapenzi makubwa na baadhi ya wachezaji wa Sunderland wakitana sana kuwachukua kuja kuongeza nguvu Yanga. Viongozi wa Yanga na baadhi ya wachezaji wakimtaka sana wawapate Hamisi Kibunzi siku zile akijulikana kama, ''Mapafu ya Mbwa,'' kwa ile stamina yake ya kupanda kushambulia na kurejea nyuma kulihami goli na wampate pia Arthur Mambeta. Lakini Yanga walikuwa kila wakiwapima wanaona kuwa Hamisi na Arthur walikuwa na mapenzi makubwa na Sunderland wasingeweza kucheza vizuri katika jezi ya Yanga. Hiki ndicho kipindi labda Yanga wakageuza macho yao kuelekeza Morogoro na kuwachkua akina Gibson Sembuli, Juma Matokeo na wengineo. 

Mimi namjua vizuri Captain Malik na TFF haitajuta kumtafuta kwa mazungumzo.

Nyongeza kutoka kwa Sharif Mohamed Yahya:
[8:25 PM, 1/25/2018] Shariff Mohamed Yahy: Samahani!
Timu hiyo ya Gossage ni ya mwaka 1965, ambayo ndiyo alocheza Rashid Seif, kijana mdogo wa Primary School wakati huo.

Mashindano yalikuwa Kampala.

Alobeba kombe ni Sharif Salim (capt).

Nakumbuka hivyo kwani mwaka huo,  1965, ndio Tanga ilichukua Taifa Cup kwa mara ya kwanza nami nilkuwamo kwenye kikosi hicho.

Mwaka 1964 Dsm, Tanganyika ilichukua pia, Captain akiwa ni Mbwana Abushiri.
1963 Gossage Nairobi alipoumizwa Kitwana na Enos Bondo, aliechukua nafasi ni Wingi Mzenga (Tanga) ambae alikuwa kwenye Timu ya Taifa tangu 1959.

Ni majuzi baada ya kifo cha Omar Kapera, na kusikia Sunday Manara yu mgonjwa nilizungumza na Kitwana.


Alifurahi sana nilipomwambia mwaka ule 1965, mwandishi wa Nation, Poly Fernandes, aliandika: "Tanganyika itachukua tena kombe, kwa sababu kipa wao ni Kitwana Ramadhani, ili umfunge itabidi upige kwenye mstari wa goli, jambo ambalo haliwezekani kutokana na ngome imara ya Tanganyika, na kupiga nje ya box itachukua karne moja kumfunga Kitwana".


No comments: