SHAJARA YA MWANA MZIZIMA
Zuberi
Mwinshehe Manga Mtemvu
Na Alhaji
Abdallah Tambaza
KAMWE asikuongopee mtu kwamba, eti
utaweza kuwa umeelezea kikamilifu harakati za kuikomboa nchi ya Tanganyika
kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza kama humtaji, humjui, au hukusikia chochote kuhusu
simulizi za mwanamajumui huyo wa Kiafrika aliyetokea kupendwa hapa kwetu.
Jina lake akiitwa Zuberi Mwinshehe
Manga Mtemvu. Alikuwa gwiji wa siasa za hapa kwetu aliyeupenda, kuupigania na
kujivunia Uafrika wake vilivyo, hata ikabidi kukosana na kuachana na wenzake
kwenye harakati na mapambano yakiwa ndio kwanza yanapamba moto; akiwamo hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Zuberi Mtemvu, alikuwamo kwenye siasa
za enzi za AA, TAA na TANU siku nyingi nyuma kabla Nyerere wa Butiama hajaja
Pugu Sekondari kufundisha. Mtemvu, si tu alikuwa rafiki mkubwa wa wanaharakati
wengine wa siasa za nchi hii—akina Sykes, Tewa, Dossa Aziz na nduguze Ramadhan
na Hamza, Iddi Simba na Ngombale Mwiru—lakini alicheza na kusoma pamoja na
kundi hilo kutoka maeneo ya Gerezani mjini Dar es Salaam.
Kundi hilo lote, pamoja na baba mzazi
wa mwandishi huyu, hayati Mzee Mohammed Saleh Tambaza, walisoma pamoja pale Al
Jamiatul Islamiya fi Tanganyika kwa elimu ya madrassa halafu wakaenda pamoja shule
za Mchikichini na Kitchwele wakati huo kwa elimu hiyo iitwayo ya ‘Kizungu’.
Wakati TANU ilipoanzishwa 1954, Mzee
Mtemvu alikuwa katibu mkuu wake wa mwanzo na Mzee John Rupia akawa makamu
mwenyekiti na mwenyekiti akawa Julius Kambarage Nyerere, msomi na mtoto wa
chifu kutoka Butiama.
Nyerere, Mtemvu, Bibi Titi na John
Rupia walizunguka nchi nzima hii ya Tanganyika kuelezea na kuhamasisha umma
kujiunga katika mapambano haya mazito ya kuutokomeza ukoloni nchini mwetu. Kila
walipoenda wasemaji wakubwa wakawa ni Nyerere, Mtemvu na Bibi Titi Mohammed,
mwanamke pekee aliyejitoa mhanga kipindi hicho.
Kulia Zuberi Mtemvu, Julius Nyerere na John Rupia nyuma ni vijana wa Bantu Group walinzi wa viongozi wa TANU na wahamasishaji |
Msomaji, kumbuka kwamba wengi wa
wananchi wakati huo tayari walikuwa wamekwisha kukata tamaa kwamba kamwe
haitofika wakati eti mtu mweusi ndiye atakayekuwa kiongozi mkuu na Waafrika
sisi kushika hatamu za kuongoza mambo mengine tupendavyo; kwa maana ya kwamba
hali itabadilika na sisi kuchupa kutoka daraja la sifuri mpaka la mwanzo tukiwa
juu ya Wahindi, Waarabu na Wazungu.
Kwa ufasaha na weledi mkubwa kabisa,
Nyerere na wenzake waliwaeleza watu kwamba hiyo pia maana ni kwamba maeneo ya
kuishi na nyumba za kuishi pia zitabadilika pale utukufu utakapotujia sisi na
unyonge kutoweka—tutahamia magorofani kwa Wahindi na Oysterbay kwa Wazungu.
Watu wakafurahia sana ndoto hiyo na
hivyo kuingia na kukikubali ‘chama cha tano’ (kilivyojulikana wakati huo)
makundi kwa makundi wakiwamo wazee, vikongwe, vijana na wanawake pia. Kila
walipoenda walipokewa vyema na Bibi Titi ndiye aliyekuwa kivutio kikubwa;
kwamba lilikuwa ni jambo la kushangaza kuona mwanamke mno akiweza kupanda juu
ya jukwaa na kuhutubia kwa kiwango kile na kuwashawishi wanawake wenziwe
kujiunga na ‘uamsho ule mkuu.’
Mnamo miaka ya kuelekea kupatikana
uhuru wetu, watawala wa Kingereza, walitengeneza mpango wa kufuatwa katika
upigaji kura za kuchagua Wabunge na Rais wa nchi. Mpango huo ulioitwa wa ‘Kura
Tatu’ haukukifurahisha hata kidogo chama cha TANU, kwa sababu ulipangwa kwamba
kila mtu apige kura tatu atake asitake; yaani moja umchague mgombea Mzungu;
nyengine mchague
Muhindi; na ya tatu mchague Mwafrika.
Ilipangwa hivyo kwa sababu ilikuwa
dhahiri kwamba chama cha TANU na Waafrika wangezoa viti vyote vya uwakilishi.
TANU na watu wake hawakupenda ujanja huo utumike, hivyo kikatishia kususia
uchaguzi wote kama utaendeshwa namna hiyo.
Nyerere, kwa upande wake akawa ameona
mbali kwamba wakisusa itakuwa ni hasara kwao, hivyo ni bora kushiriki hivyo
hivyo na kuwachagua hao Wazungu na Wahindi. Hali hiyo ikapelekea mvutano na
mgawanyiko mkubwa ndani ya TANU baina ya wanaotaka na wasiotaka kushiriki
uchaguzi ule.
Mmoja wa watu ambaye hakukubali hilo
alikuwa ni Katibu Mkuu wa chama cha TANU Zubeir Mtemvu. Yeye Mtemvu, hakuona
mantiki ya kuchagua mtu yeyote asiye Mwafrika ukizingatia kwamba wao
hawakupenda hata kidogo kuishi na sisi kwa njia ya usawa. Mtemvu na Nyerere
wakawa mbalimbali kwa hilo. Potelea mbali, hata mimi ningemuunga mkono Mtemvu,
nikizingatia kwamba hawa jamaa hata kwenye biashara zao ukitaka kumlipa pesa,
basi walikupa kopo utumbukize hiyo pesa ili tu msigusane mikono na wewe ‘mchafu.’
Sasa nimchague kwa lipi.
TANU ikaenda Tabora kufanya mkutano
wake mkuu na moja ya ajenda ilikuwa kujadili na kutoa maamuzi kama washiriki au
wasishiriki uchaguzi ule. Nyerere, kwa kumhofia Mtemvu, kwamba anaweza akawa na
ushawishi mkubwa kwenye hilo, akambakisha ofisini Dar es Salaam ili aratibu
mambo mengine muhimu ya chama wakati huo.
Walipofika Tabora, Mwalimu akampanga
mjumbe kutoka Tanga, Mwalimu Kihere aje kuzungumzia umuhimu wa kushiriki na
hasara za kususia uchaguzi ule. Mwalimu Kihere akaifanya kazi hiyo kwa ustadi
mkubwa sana, na pale kura zilipopigwa upande wa Nyerere ukaibuka kidedea.
Akiwa ofisini Dar es Salaam, Mtemvu
alitumiwa taarifa kwamba atangaze kuwa chama cha TANU kitashiriki Uchaguzi wa Kura
Tatu. Mtemvu alichukizwa sana na hilo, hivyo akatuma ujumbe kwamba yeye
anajiuzulu kutoka chama hicho na kwamba atatangaza kuanzisha chama chake
mwenyewe.
Aliita waandishi na akatangaza kwamba
kufuatia maamuzi ya Tabora, yeye hayumo tena TANU na kwamba ameanzisha chama
kipya kilichojulikana kama Congress Party, kwa malengo yaleyale ya kupambana na
utawala dhalimu wa Malkia wa Kiingereza mpaka atoe uhuru wetu.
Mtemvu, alikuwa hodari wa kuzungumza
na kushawishi umma. Chama cha Congress kikavuma na kupata wafuasi wengi hasa
kwenye maeneo ya Bukoba, Tabora na Mwanza kama takwimu za matokeo ya Uchaguzi
Mkuu zilivyoonyesha.
Makao makuu yake yalikuwa pale Mtaa
wa Nyamwezi na Faru alipochukuwa ghorofa nzima ya nchini kwenye nyumba
iliyojengwa na Mzee Nassor Kiruka na sasa inamilikiwa na familia ya marehemu
Mzee Masha, kada wa CCM kutoka Mwanza.
Mzee Mtemvu, aliyeng’oka na wanachama
wengine shupavu wa TANU, akiwamo Said Chamwenyewe, Emmanuel Makaidi, Kassanga
Tumbo, alikuwa tishio kwa Nyerere na TANU yake ingawa si kwa kiasi kikubwa,
maana Nyerere na Bibi Titi, hiyo ilikuwa ni habari nyengine kabisa.
Chama cha Congress na Mtemvu ikawa
ndio habari ya mjini. Alitembelea nchi nyingi duniani kwa mialiko ya vyama
rafiki, hasa nchi zilizokuwa na siasa za mrengo wa kushoto. Amehutubia mikutano
mingi ya kisiasa hapa kwetu na kwingineko duniani kuelezea kiu na kilio cha Watanganyika
kutaka kujitawala wenyewe.
Kama walivyokuwa wakiitwa TANU
linapokuja suala la kukutana na mawaziri mbalimbali wa serikali ya kikoloni ya
Kingereza, na Mtemvu na Congress pia walipata nafasi hiyo hiyo kuelezea azma ya
kuwa na serikali huru. Sasa vipi leo sisi tumsahau mtu wa namna hiyo?
Aliyewakabili bila woga kwa niaba yetu Wazungu wale wafuga masharubu?
Nilimfahamu kwa kiasi fulani Mzee
Mtemvu kwa kuelezewa kwenye mazungumzo nyumbani tukiwa na babangu mzazi. Baba
akiishi kwao Upanga alikozaliwa na Mtemvu kwao kukiwa Gerezani. Baadaye
wakakutana tena chuoni na shuleni.
Abdul Mtemvu, ni mdogo wa mwisho wa
Mzee Zubeir Mtemvu. Kiumri, Abdul alikuwa kijana mdogo sana anayeweza kuzaliwa
na Zuberi Mtemvu. Comrade Abdul na mimi tulisoma pamoja hapa kwetu Dar es
Salaam kuanzia shule ya msingi pale Kitchwele Middle School na baadaye
Sekondari ya Mtakatifu Joseph pale Forodhani.
Nyumba yao ilikuwa barabarani pale
Mtaa wa Kitchwele na hivyo wakati wa
kutoka shuleni nilipitia kwao mara kwa mara nikiongozana na Abdul kupata maji
baridi ambayo wakati huo yalikuwa ni kitu adimu sana maana sisi wa daraja la
tatu majumbani kwetu ilikuwa inatamba mitungi na kata zake. Hiyo ilikuwa ni
fursa ya kumwona kwa karibu zaidi Mzee Mtemvu mwenyewe katika mazingira ya
kinyumbani akiwa ametulia na gari yake TZM 1 ikiwa imepakiwa barazani.
Hapa mjini, aliendesha siasa zake
kistaarabu sana akiranda kwa miguu huku na huku akiwa amevalia nguo rasmi za ‘migolole’
ya kisiasa ya kutoka Afrika Magharibi hasa kule Nigeria na Ghana, na usinga
wake mkononi akisalimiana na kuongea na watu mbalimbali kuelezea mipango yake
ya kujitawala wenyewe nchini.
Wakati mwengine alionekana akiwa
amepiga suti zake nyembamba mwilini akiwa ndani ya gari lake zuri la kipekee,
nadhani ilikuwa Ford Cortina hivi, yenye namba spesheli za usajili – TZM 1. T
ikiwa na maana ya nchi yake Tanganyika; Z jina lake Zubeir; na M ni Mtemvu.
Hivyo ndivyo alivyokuwa akiwakoga
watu Mtemvu na Cortina yake mpya.
Sasa wewe Mtanzania wa leo kwa nini
basi usimtaje, usimjue, usimuenzi na kumtukuza mtu huyu shupavu ambaye alifanya
kazi ileile kama Nyerere – kuelezea dunia – kwamba umefika wakati tupate uhuru
wetu. Je, unafikiri madhumuni ya chama chake yalikuwa nini kama si hayo hayo?
Nyerere na TANU walishinda tu kwenye
sanduku la kura wakapata ridhaa ya kuunda serikali, lakini hawa wengine nao
wanastahili heshima kutoka kwetu. Hivi huoni kwamba kwenye uchaguzi ambao
Zuberi Mtemvu alitokea wa pili, kama angeshinda yeye ndiye angekuwa rais wetu
wa kwanza? Basi hujiulizi kwa nini watu wa Kanda ya Ziwa wakati ule wawe
wamekipa kura nyingi chama cha Congress na Mtemvu?
Tubadilikeni jamani tutoe haki
inapostahili; tuwe tunaelezana haya yanayohusu huko nyuma tulikotoka tulikuwaje;
na kina nani hasa waliotufikisha hapa leo tunajivuna.
Simu:0715808864
No comments:
Post a Comment