Friday, 2 February 2018

SHEBE MPIGA PICHA WA KWANZA WA TANU NA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE


Shebe

Picha hiyo hapo juu ya Mzee Shebe nimeiona leo asubuhi tarehe 2 Februari, 2018 baada ya kuwekwa FB na Adarsh Nayar mpiga picha maarufu.

Nasikitika kusema kuwa sijui mengi kuhusu Mzee Shebe ila kuwa alinipiga picha yangu ya kwanza hiyo hapo chini mwaka wa 1953 nikiwa na umri wa mwaka mmoja.

Picha hii kwa miaka mingi ilikuwa ikining’inia katika ukuta wa chumba cha mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed toka mimi napata fahamu ya utambuzi.

Katika miaka yangu ya utoto picha hii haikunihangaisha hadi nilipofika umri mkubwa na mimi kuwa na wanangu ndipo nilipoanza kuingalia kwa undani zaidi picha ile.

Lakini sikupatapo kutaka kujua ni nani alipiga picha yangu.
Siku moja nilimtembelea mama yangu Bi. Mwanaisha na nikamuuliza nani alinipiga picha ile.

Mama yangu akanambia kuwa picha ile anilipiga Mzee Shebe Mtaa wa Livingstone na Kipata ambako yeye alikuwa akiishi na mkabala wa nyumba  yake ndipo Mzee Shehe alipokuwa na studio yake.

Mama akaendelea kunihadithia akisema kuwa iko siku Mzee Shebe alikuja nyumbani kuniangalia.

Mama anasema Mzee Shebe akiniita mimi rafiki yake.
Akamwambia mama kuwa amekuja kunichukua akanipige picha pale kwenye studio yake.

Picha ndiyo hii ambayo sasa inafika umri wa miaka 66.
Pale ilipokuwa studio ya Mzee Shebe hatua chache ilikuwa Kirk Street (Sasa Mtaa wa Lindi).

Mtaa wa Kirk Street kulikuwa na nyumba moja ya ukoo wa Sykes akiishi mama yao Abdul, Ally na Abbas Sykes, Bi. Mluguru bint Mussa.

Hii nyumba ina historia kubwa katika uhuru wa Tanganyika.
Miaka ya mwanzo ya TANU Nyerere alikuwa hapungui nyumba hii akifuatana na Abdul Sykes.

Bi. Mluguru alikuwa na nyumba nyingine Kipata Street kona na New Street (Sasa Lumumba Avenue) ambapo serikali ilijenga Cooperative Building miaka ya mwanzo ya 1960.

Serikali ilipotaka kununua nyumba zile ili ijenge Cooperative Building ambayo imeanza Kipata hadi Somali Street Mwalimu Nyerere alimwandikia Bi. Mluguru barua kumwomba akubali kuuza nyumba yake hiyo kwa serikali.

Nyumba hizi zilikuwa zikitazama Uwanja wa Mnazi Mmoja na ukivuka Somali Street kulikuwa na kiwanja cha TANU ambacho baadae TANU ilijenga jengo la Elimu ya Watu Wazima na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kilianzia hapo.

Kirk Street akiishi Ramadhani Mashado Plantan mmoja wa wanachama wa African Association toka miaka ya 1930 na nyuma ya Kirk Street ulikuwa Somali Street alikokuwa akiishi Zuberi Mtemvu na Omari Londo wote hawa wanachama shupavu wa TANU.

Nyuma ya studio ya Mzee Shebe ulikuwa Kipata Street mtaa ambao alikuwa akiishi Ally Sykes. Kwa ufupi ni kuwa hii Gerezani kama mitaa ile iliyokuwa sehemu ilivyokuwa ikifahamika, ilikuwa sehemu inawaka moto kwa siasa za kudai uhuru.

Baadhi ya mikutano ya TANU ya miaka ile ya 1954/55 ilikuwa ikifanyika kiwanja cha Kidongo Chekundu kilichokuwa kinatazamana na Kiungani Street.

Mzee Shebe alikuwa mpiga picha maarufu katika mitaa yote ile na bila shaka hili ndilo liliomfanya yeye atokee na kuwa mpiga picha wa kwanza wa TANU na  Baba wa Taifa Mwalimu 
Julius Nyerere siasa za kudai uhuru wa Tanganyika zilipoanza 1954.

Kulikuwa na kijana mmoja sote tumeajiriwa na Bandari jina lake Shebe.
Siku moja nikamuuliza nani baba yake.

Katika mazungumzo akanambia kuwa baba yake alikuwa na studio Mtaa wa Livingstone katika miaka ya 1950. Hakika nilipata mshtuko.

Nikamwambia basi baba yake ingawa simkumbuki kwa sura kwa kuwa nilikuwa mtoto amenipiga picha ambayo ninayo mpaka sasa.

Nikamuuliza tena kama anamjua Masad Shebe.
Akanambia huyo ni dada yake.

Hii ilikuwa miaka ya 1980 na Masaad alikuwa akikaa Mtaa wa Livingstone na Mkunguni na akifanyakazi Air Tanzania.

Hivi sasa Masad ni Meneja wa Air Tanzania Zanzibar.

Nikazungumza Mengi na Shebe na yeye kwa kujua mapenzi yangu katika historia akanifanyia photocopy za picha nyingi sana alizopiga baba yake katika miaka ya 1950.

Bahati mbaya siku zile ‘’digital,’’ ilikuwa bado.
Hazina hii aliyoacha Mzee Shebe nimeihifadhi kama ilivyo katika Maktaba yangu.

Mwandishi, 1953
Picha aliyopigwa na Mzee Shebe

No comments: