Shajara ya Mwanamzizima
Bibi Titi Mohammed
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Bi. Titi Mohamed na Julius Nyerere Siku ya Uhuru |
KATIKA safu hii ya Shajara ya Mwanamzizima,
Jumatatu iliyopita tulimwangalia hayati Mzee Mshume Kiyate, na namna Bwana
Mkubwa yule alivyouhangaikia kuutafuta uhuru wa nchi hii mpaka ulipopatikana.
Tuliona pia, jinsi taifa hili na watu wake wasivyo na utu, kwani Bwana Mkubwa
yule mwisho wake alikufa akiwa hana msaada wowote kutoka kwenye chama
alichokiasisi— TANU –na nchi yake aliyoipigania Tanganyika (sasa Tanzania).
Leo hii, shajara inamwangazia mwanaharakati
mwengine machachari, Bibi Titi Mohammed, ambaye amefanya mengi; ambayo ni
vigumu kuyapima kwa mizani yeyote ile. Alijipambanua kama mwanamke shujaa, shupavu,
mwenye haiba, bashasha na weledi mkubwa katika uwanja wa siasa. Sifa zake
zilienea si katika Tanganyika peke yake, bali Afrika Mashariki yote na nje ya
hapo.
Habari zinasema, baada ya kujiunga kwake na
chama cha Tanu, hayati Bibi Titi, ndiye mtu aliyewaingiza watu wengi katika
TANU kupita mtu yeyote akiwamo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“…hakuna hata mtu mmoja Tanganyika
nzima, mbali na Nyerere mwenyewe, aliyeweza kuifanya TANU kuwa maarufu kama
Bibi Titi Mohammed…’’angalia Mohammed Said uk. 208, kitabu kinachoelezea Maisha
na Nyakati cha Abdulwahid Sykes, kinachosambazwa na Ibn Hazm Media Center, Dar
es Salaam.
Moja ya mambo yaliyochangia kupeleka mbele
chama cha TANU ni kule kuingizwa vikundi vya ngoma vya lelemama ambavyo vilikuwa
na wafuasi na wapenzi wengi mjini Dsm. Akishirikiana kwa karibu na Bi. Hawa
Maftah, aliyekuwa kiongozi mkuu wa
Lelemama mjini hapa, Bibi Titi alileta hamasa na msisimko mpya katika jitihada
za kumkomboa mtu mweusi na ukoloni. Nyimbo za Lelemama zikaanza kuimbwa kwa
wingi na hivyo kunogesha harakati zile kwa kiwango kikubwa kabisa.
Moja ya nyimbo hizo, ni ule uliokuwa mashuhuri
aliotungiwa mahsusi Mwalimu Nyerere, uliokuwa ukiimbwa na wapiga ngoma wa Lelemama
kila mara Nyerere, alipokuwa akitaka kuanza kutoa hotuba zake za kudai uhuru,
na watu wote wakiuimba kwa sauti ya pamoja kama wimbo wa taifa vile:
‘Muheshimiwa nakupenda sana, Wallah sina
mwinginewe, Insha Allah Mungu yupo Tanganyika tutajitawala’
Sifa za Bibi Titi zilivuka mipaka na kufika
Kenya ambako kulikuwa na vuguvugu kubwa pia la kudai uhuru. Watu wa Kenya
waliomba kupelekewa Bibi Titi akahamasishe na kwao pia, pale Kiongozi mmoja wa
KAU kule Mombasa, Ronald Ngala alipomtaka aende huko.
Kule nchini Kenya, hasa Mombasa, watu wa Kenya
walishangazwa sana kumwona mwanamke mno, akiwa kijana na mrembo pia, akiwa
katika hadhira kubwa kama ile akaweza kuleta msisimko mko uliopelekea makundi
kwa makundi ya wanawake nchini humo kutoka majumbani mwao kuhudhuria na kuunga
mkono jitihada za kulikomboa taifa lao kutoka mikononi mwa Waingereza.
Bibi Titi, hakuishia hapo. Alitumwa Zanzibar pia
wakati wa Utawala wa Sultan Jamshiid, yeye na mwanasiasa mwengine, Saadan Abdul
Kandoro, kwenda kuhutubia kule nako; maana mwamko wa wanawake kule Unguja ulikuwa
mdogo kutokana na misingi na maadili ya mafundisho ya Kiislamu inayozuia
mwanamke kujichanganya na wanaume.
Mwanasiasa machachari wa wakati huo kule
Zanzibar, Comrade Abdulrahman Babu, aliiponda sana ziara ile ya Bibi Titi na
kukiita kitendo kile cha kumsimamisha mwanamke kuhutubia mkutano pale kwao
Zanzibar, kuwa ni cha kipuuzi na kihuni na kwamba kinaonyesha ni kwa kiasi gani
mwanamke asivyokuwa na thamani huku Tanganyika. Zile zilikuwa siasa za vyama
vingi ambapo Babu pengine alihofia
pengine chama chake kingepoteza mwelekeo baada ya ujio wa Bibi Titi.
Bibi Titi Mohammed, alizaliwa Dar es Salaam na
kupata elimu yake ya madrassa na baadaye kusoma shule mpaka Darasa la IV tu;
kama ambavyo wakoloni walivyotaka, ili mtu mweusi aje kusaidiasaidia tu katika
kuhesabu magunia na maboksi kwenye magodauni na viwandani—elimu kwa shughuli
nyingine yeyote kwetu ilizuiwa au ilikuwa kiduchu sana, isipokuwa kwa watu
wachache tu, hasa watoto wa machifu waliokuwa wakitayarishwa kuja kuwa viongozi.
Madhila na misukosuko ya kutawaliwa si rahisi
kuifahamu vizuri kwa kuhadithiwa na mtu kama hivi nifanyavyo mimi. Ni lazima
uwe umeiishi ndani yake ndipo utakapoyahisi machungu yake. Mbali ya kuwekwa
katika madaraja ya chini kwa ajili ya kupokea huduma mbalimbali—watu weusi
tukawa wa mwisho— lakini pia kwenye kazi za maofisini na majumbani
tulinyanyaswa sana; kitu ambacho kiliwaibua watu kama Bibi Titi kuja kupambana
na kuitokomeza dhuluma ile.
Majumbani kwa wahindi, ambako hapa kwetu Dsm
watu wengi walikuwa wakifanya kazi za ‘uboi’, palikuwa hakuna msalie mtume! Ukiwa
mtumishi pale utaendeshwa na kuzungushwa kama pia (pia ni kitufe fulani ambacho
huchezea watoto ambacho huzunguka namna feni lizungukavyo).
Kwa mfano, mama wa Kihindi akitaka kukutuma
atakupigia kelele nyingi ovyo ovyo bila adabu: ‘Asumani safisha matoto tumbo har..sha; kabla
hujamaliza vizuri atakuita tena: ‘wee asumani angalia machuzi chemka jikoni;
baba naye atakuita hapo hapo, ‘asumani guo kwisha fua wee! Mwingine tena atakuita
‘asumani gapi pilipili weka dani ya boga! Ili mradi kichwa kitakuzunguka hata
usijue la kufanya! Kama vile hiyo haitoshi, utaliona babu la Kihindi linatema
mate na makohozi ya ‘matambuu’ mekundu kwenye sakafu makusudi, halafu linakupigia
wewe kelele ukayasafishe; tena kwa deki.
Wakati wa ‘msosi’ ukifika, chakula kile cha
kihindi, ambacho kwa kawaida huwa
kinanukia na kutamanisha sana; na wewe
ndiye umefanya kazi ya kukipika, huruhusiwa kukigusa! Ikifika saa ya
kula wewe utoke nje ukatafute wapi utapata kitu chochote kinachofanana na wewe
ule.
Pale maeneo ya Faya, Kariakoo, zamani pakiitwa
Mwembetogwa. Akina mama walikuwa wakileta machupa kwa machupa ya togwa lilotengenezwa
kwa mtama mahala hapo. Mwembetogwa ndio mahala ambapo ‘maboi wa majumbani’ kwa
wahindi kutoka majumba ya karibu pale
Upanga, walikokuwa wanakuja kunywa togwa ili kushitua matumbo yao. Muhindi
hana habari na wewe kabisa—atapiga biriani na pilau mbele yako kwa raha zake.
‘Mazungu’
nayo ndiyo mabwana wakubwa; kosa kidogo utasikia unaitwa bomani kwa Bwana DC au
Bwana PC ukaadhibiwe. Ukitoka huko, baba mtu mzima unayeheshimika nyumbani kwa
wanao na wajukuu zako, utakuwa umechezea bakora matakoni, na hivyo kuwa kituko
katika jamii kwenye vilabu vya pombe na vijiweni kwenye kahawa na bao. Fimbo
iliyokuwa ikitumika kupigia Waafrika ni henzerani, ambayo huumiza sana kwani
ina manundu manundu yaliyochongoka!
Kwenye ‘mashule’ yetu huko nako vilikuwa
vinatambezwa viboko kama nini sijui. Ingawa walimu wale walikuwa ni Waafrika
wenzetu, lakini suala la viboko walilitilia maanani sana kwa sababu ya kutaka
kumfurahisha Mzungu Mtawala kwamba wao walikuwa wanatekeleza sera ipasavyo.
Shule ya Msingi Mnazi Mmoja jijini Dsm, ndiko
mwandishi huyu alikosoma mnamo mwaka 1958-1961. Shule ilikuwa imefunguliwa
mwaka mmoja tu uliopita (1957) ili kuipunguzia mzigo Shule ya Mchikichini
ambayo ilikuwa inasomesha watu weusi Dsm nzima. Pale shuleni walimu walikuwa
wakali kama pilipili wakipenda sana kuchapa viboko kwa kosa lolote lile hata la
kipuuzi tu.
Mwalimu Mkuu wakati ule alikuwa Mwalimu Iddi
Rajabu na walimu wengine waliokuwapo ambao wakipiga watoto ovyo ni Mwalimu
Shaaban Mahanyu, Ramadhani Akilimali Kayombo, Justin Daudi, Mwalimu Nuru na
Kupia Abdallah. Pamoja na elimu nzuri waliyotupatia, lakini hili la kuchapwa
bila huruma ilikuwa ni ujinga wa kikoloni tu. Nasema hivyo kwa sababu shule za
wahindi/wazungu hawakupigwa namna yeyote ile. Wahindi, wakati sisi tukienda
shule bila viatu, huku tukiambukizana magonjwa chooni, wao walivaa viatu vizuri
na mashati mepesi yanayongara (Waafrika walivishwa magwanda magumu juu na
chini).
Nakumbuka kama vile imetokea jana, kwa watoto
wote wa shule za Dar es Salaam (wa kiafrika), walikuja kuvalishwa viatu katika
sherehe za uhuru, Desemba 9, 1961 na muasia mmoja aliyekuwa tajiri akijulikana
kwa jina la Habib Punja. Habib Punja alimiliki majumba mengi ya ghorofa mjini
hapa wakati wa ukoloni ambayo yalikuja kutaifishwa na kufanywa mali ya umma wakati
wa Azimio la Arusha. Punja pia alitoa lunch boxes kwa watoto wote waliokuwa
wakishiriki michezo ya halaiki kwa kusherehekea uhuru tokea siku za mafunzo na
‘rehersals’ (majaribio), mpaka kwenye kilele chenyewe cha maadhimisho.
Msomaji, sasa baada ya uhuru kupatikana
‘mwanamke yule wa shoka’ aliyejitolea muhanga kwa kuwaacha watoto wake bila
huduma ya mama na mumewe bila mke wa kumpikia ugali; akawa anazunguka kila
pembe ya nchi yetu hii kubwa, kuhamasisha umoja na mshikamano; saa zote akiwa
na Nyerere ubavuni mwake wakifanya kazi moja hiyohiyo, awe si lolote si
chochote! Haiyumkiniki hata kidogo.
Ndani ya Bibi Titi, nawaona wanawake wengine
mashuhuri waliojijengea majina duniani kama vile Hannan Ashrawi Msemaji Mkuu wa
PLO; Winnie Mandela wa ANC, Afrika Kusini aliyepata umaarufu na kuenziwa
duniani kwa kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini; hayati Wangari Maathai
wa Kenya, mwanamke wa kwanza Mwafrika kupata tuzo kubwa mbalimbali ikiwamo ya
Nobeli; Mama Indira Gandhi wa India na Golda Mair wa Israel ambao kwa nyakati
tofauti walikuwa mawaziri wakuu wa nchi zao.
Ushupavu na ujasiri wa Bibi Titi, naufananisha
pia na watu kama Dk Martin Luther King Jr na Malik el Shabazz (Malcom X) wa
Marekani, ambao waliuawa kikatili si kwa sababu nyengine, bali ni kule kujitoa
kwao kupigania haki na usawa kwa wanyonge nchini mwao. Nauona pia kwa Mmarekani
mwengine mweusi Angela Davis wa Black Panther group iliyokuwa ikipigania
kuondoa kwa nguvu ubaguzi wa rangi nchini Amerika. Bibi Titi anaweza
kufananishwa pia na Mama Mayya Angelou wa kule Marekani pia; msanii na
mwanafalsafa aliyetumia vyema maarifa yake na kukemea vikali ubaguzi kwa
misingi ya rangi ya mtu.
Mama huyu, ambaye jina lake ni Titi,
likimaanisha ‘ziwa la nyonyo’ kutoka kwa mama, linashabihiana sana na vitendo
vyake alivyotufanyia Watanganyika wenzake katika enzi zile za ukatili na
unyanyasaji wa kikoloni. Sote tumenyonya titi lile la bibi yule na leo tuna
nguvu kubwa ya kutembea kifua mbele hapa kwetu.
Maisha na matendo ya Bi. Mkubwa Titi Mohammed,
yanafanana na mwanamke mwengine mpigania haki za binadamu, Rosa Parks, aliyegoma kumpisha
kiti mzungu kule Montgomery, Alabama, Marekani, wakati ule wa sera za kibaguzi,
ambapo ndani ya basi lolote la abiria kuna sehemu za mbele ni lazima wakae
wazungu halafu nyuma ndiyo wakae weusi.
Sasa inapotokea viti vya Wazungu kule mbele
vikajaa; basi viti vinavyofuata vya watu weusi lazima wanyanyuke wawapishe Wazungu
wakae hapo na wenyewe wasimame. Siku hiyo ya siku, Rosa Parks, akiwa amechoka
katokea kazini taabani, aligoma kumpisha mzungu kiti.
Dereva aliripoti tukio polisi na Rosa Parks
alikamatwa na kutiwa hatiani kwenye tukio la kihistoria ambalo alifunguliwa
mashitaka mahakamani. Hukumu ikaja mnamo Novemba 23 1953 kwamba ubaguzi ndani
ya mabasi ni kinyume na katiba (unconstitutional) na ule ukawa ndio mwisho wa
ubaguzi ule wa kijinga ndani ya mabasi Marekani nzima.
Sasa kutokana na kadhia ile, Mama Rosa Parks ametukuzwa kabla na baada ya
kifo chake kule Marekani kwa kuitwa Mama wa Haki za Binadamu na kuna siku
maalumu kule Montgomery, Alabama, California na miji mingi mengine,
inasherehekewa kama Rosa Parks Day ili kukumbuka mchango ule mkubwa alioutoa
kwa wenziwe.
Wanawake wa Tanzania mko wapi sasa? Fanyeji jambo katika hili la Bibi
Titi, maana huyu ndiye muasisi na mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Wanawake
Tanganyika (UWT) ulipoanzishwa mwaka 1963. Kama hamkumuenzi wenyewe msitegemee
wanaume kama watafanya kazi hiyo kamwe, pamoja na kwamba titi la Mama Titi, tumenyonya
sote!
Bi. Titi na Rais Ali Hassan Mwinyi |
No comments:
Post a Comment