Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi
Baraka)
Sehemu ya (2)
Na Ben Rijal
Katika makala haya ya leo
yatamuangalia Sayyid Omar Abdalla katika kuendelea kusoma na kazi alizozifanya
alipokuwa bado yupo Zanzibar, sio kitu cha kawaida katika Wasomi wengi wa
Kiislamu kwenda nazo sambamba elimu ya dunia na elimu ya dini. Sayyid Omar
Abdalla alielimika na elimu zote mbili hizo aidha alikuwa akijisomea vitabu
mbalimbali na majarida katika kuendeleza uwezo wake kielimu.
Katika makala ya wiki iliopita
nilianza kwa kunukuu misitari miwili mitatu ya Kiengereza kwa yule aliojuwana
na Sayyid Omar Abdalla na leo aidha nitaanza hivyo hivyo na mistari miwili
mitatu alioyaandika yeye mwenye Sayyid Omar Abdalla.
Dear Mr. Harvey, I have just
received your circular in connection with Religious Teaching in School. Thank
you very much. During the last vacation I resumed my discussion with the Chief
Kadhi and at the end we arrived to a definite conclusion which I am sure you
would like to hear. Since the beginning of the term I have been trying to come and
see you at your office but in vain, as I am very busy throughout the week
including Saturday. Could you kindly therefore fix me up on any one convenient
Sunday so that I might come to see you in your home? Your sincerely, Omar
Abdalla (Kumbukumbu ZNA AD 3/8).
Tafsiri ya juu juu kutokana na Faili lake lenye nambari ZNA 3/8 akimuandikia Mkurugenzi wa elimu Mr. Harvey
akimwambia, “Nashukuu kuwa nimepata
chapisho ulionitumia kuhusu usomeshwaji wa masomo ya dini katika maskuli.
Katika mapumziko yangu bada ya mhula wa masomo
nilishafanya mazungumzo juu ya masaala hayo na Kadhi Mkuu ambaye
tulifikia makubaliano, imani yangu kuwa
wewe Mkurugenzi wa Elimu utapenda kusikia juu ya mazungumzo hayo. Nilijitahidi
kupiga hodi kwenye ofisi yako pasi mafanikio, ikiwa na mie nimebanwa na
mashughuli kwa wiki nzima pamoja na Ijumamosi yake, nitaomba uitenge siku ya
Ijumapili tuweze kuonana. Wako mtiifu.
Omar Abdalla.”
Nitapenda kugusia jambo mmoja muhimu
sana ambalo katika utawala wa Muiengereza uliweza kusaidia sana katika uwekaji
wa kumbukumbu. Ilikuwa Maofisa wote wa Serikali wakitakiwa taarifa zao
kuhifadhiwa katika mafaili maalumu kisha kuwekwa kwenye ofisi ya nyaraka
(Archives).
Ilikuwa ofisa yoyote akipandishwa
cheo, akiongezwa mshahara, akipata uhamisho barua atakayopewa lazima ikawekwe
kwenye faili lake huko ofisi ya nyaraka na mpelekaji wa taarifa hizo ni tarishi
ambaye kila mtu akimjua kama ni tarishi au kwajina hilo la zama hizo akiitwa
Ofisi boi, kwani akivaa shati na surula ya khaki na baskeli yake nyekundu.
Ofisi boi akijivunia kazi hio kwani
ilikuwa siku hizo ukiwa mfanya kazi wa Serikali basi maisha yako utayaweza
kutokana na mshahara unaolipwa. Taarifa nyingi za waliopita tunaweza kuzipata
kwa njia hio ambazo kwa leo ni kitu kigumu kuweza kuzipata taarifa za wafanya
kazi mbalimbali.
Aidha katika sehemu hio ya
kumbukumbu utaweza kupata taarifa za kila aina, hata zile za magazeti yaliopita
ambayo kila nakala iliokuwa ikitolewa hupelekwa hapo na kuwekwa.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na
Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani
Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi
kusoma Makerere College huku anasomesha, alikuwa ansubiri nafasi ya kwenda
kuongeza masomo kwa hamu huko nchi za nje, kama nilivyokwisha kueleza
kabla kuwa Sayyid Omar alikuwa kati ya
wanafunzi wa mwanzo kusoma masomo ya Sekondari viiswani Zanzibar aidha alikuwa
kati ya wanafunzi wa mwanzo wa kwenda kusoma masomo ya juu katika Chuo cha
Makerere.
Ilipofika mwaka wa 1951 Sayyid Omar
Abdalla na Abdalla Jahadhmi walikuwa wanafunzi wawili waliopata fursa ya kwenda
Uiengereza kwa masomo ya juu. Sayyid Omar Abdalla alikwenda chuo cha SOAS
kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini pamoja na Kiarabu.
Kuna mapendekezo mengi ambayo
watawala wa Kiengereza walikuwa wakijadiliana katika uongozi wa elimu pamoja na
mahusiano ya mambo ya nje juu ya kumsomesha Sayyid Omar Abdalla ili aweze kuja
kuwa Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Kiislamu ambacho kilikuwa katika katika
mataarisho ya kufunguliwa mwisho wa miaka ya 40.
Sayyid Omar Abdalla alikuwa
akitamani kwenda kusoma nchi za Kiarabu lakini fursa ilipomuangukia ya kusoma
Uiengereza kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini ngazi ya Shahada ya Diploma
hakusita akakubali, huku akijuwa kuwa atakuwa na pengo katika kuzungumza
Kiarabu, ingawa akizungumza Kiarabu lakini sivyo namna alivyokuwa akitamani
mwenyewe kukimudu hicho Kiarabu. Wengi wa watu wa visiwani siku hizo katika
maisha yao ya kujifunza Msikitini tangu utotoni hadi utuzimani mwao walikuwa
wakizungumza Kiarabu lakini wenyewe wakikiita Kiarabu cha Msikitini.
Ahlil Darsa wa Msikiti wa Ijumaa
mdogo
Alipokuwa anafanya masomo yake hayo
hapo Uiengereza alipewa magwiji wawili ambao kazi yao ilikuwa kuhakikisha
analifikia lengo lilokusudiwa, akisimamiwa na mjuzi wa elimu ya Ulinganisho wa
dini David Cowan (al Dundawi) na R. B. Serjeant inagawa msimamizi mwengine
alimkataa kumsimamia na kujiunga na chuo hicho alikuwa ni J.N.D Anderson.
Akiwa anasoma huko Uingereza alikuwa
akiwasiliana na wanafunzi wa maeneo mbalimbali kuweza kupata kwenda
kujiendeleza bada ya kukamilsiha masomo yake na khasa alilenga kuweza kupata
fursa ya kwenda kujiendeleza katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu.
Ilipofika mwaka wa 1953 akiwa bado
yupo Uiengereza alifanya safari ya kwenda Marekani na kuhudhuria mafunzo ya
nyakati za kiangazi, masomo ya muda mfupi, huku akiwa amefanya aridhilhali ya
kupata kwenda kusoma masomo ya Kiarabu.
Hakuchoka kuandika na kuwataka
Waiengereza wamlipie masomo yake katika nchi za Kiarabu kitu ambacho katika
siku zake za utuzimani bada ya kuondoka Zanzibar hakuwa ni mtu wa kushikilia
jambo analolitaka ila akipenda kuona ajiachie na aone upepo utavyomchukua
utakavyo.
Akiwa bado yupo huko Uiengereza na kiu chake
kutaka kujiendeleza masomo yake katika nchi za Kiarabu, hakuona tabu kukamata
kalamu na kuandikia Wizara ya elimu, aliandika lugha nzito yenye ufasaha na
unapoisoma barua hii utaona namna alivyokuwa akikimudu Kiengereza.
Sayyid Umar bin Sumayt na Sayyid Omar Abdalla |
“Sir, you may be pleased to hear
that I have done well in my examination, and next year I hope to complete my
course. I must thank the government for affording me the unique opportunity,
being the first and the only student in the course. I am becoming a learned
man. But you will agree that however high the standard of knowledge I get here, I shall not be
really competent to hold any post involving the use of Arabic or Islamic law
unless I spend some time in a country where Arabic is the language, and where
Islam form the background of the people. Here, there is no proper atmosphere.
My stay in Arabia will be a shield against those who criticize my coming to
London. It will give me a greater confidence, and I confess that I shall not
completely qualified for a responsible position without actual living in
Arabia” (kumbukumbu ANA AB 86/47, barua alioiandika tarehe 30.6.1953)
Kwa kifupi aliandika barua kusema
kuwa amemaliza masomo yake na amefanya vizuri ni vyema sasa wakampatia fursa ya
kwenda kuongeza msomo yake katika nchi za Kiarabu, kufanya hivyo kutawafunga
midomo wale watakao bwabwaja kuwa elimu yake kaipata Ulaya, ila tu kukosa
kwenda kufanya mafunzo katika nchi za Kiarabu zenye utamaduni wa Kiislamu basi
hatokuwa na uwezo wa kukamata nyadhifa kubwa za kitaaluma.
Katika mwaka wa 1954 Sayyid Omar
Abdalla aliandika barua ya kukumbusha azma yake ya kupata fursa ya kuendelea
kusoma katika nchi za Kiarabu na Kiislamu na alitaka kuwa akiwa anarudi kutoka
Uiengereza apewe ruksa ya kwenda Kuhiji Makka kisha apite Hadharmout huko Yemen
akae kidogo ajifunze kwa Kiarabu masomo aliokwisha kuyasoma kisha ndio arudi
nyumbani, alikubaliwa hilo na safari yake alilipiwa na Serikali.
Kuna kumbukumbu ambayo sijaipata
lakini niliisikia kuwa alipokwenda Makka na kupita Hadahrmout alichelewa kwa
siku 2 kurudi Zanzibar kwahio alikatwa mshahara wa siku 2 lakini hapo hapo
kutokana na kufanya vizuri masomo yake alipandishwa cheo na kupatiwa nyongeza
ya mshahara.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na
Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani
|
Fatwana
na mie katika makala inayofwata kumuangalia Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi
masomoni kazi zake na kuhama Zanzibar kuhamia visiwa vya Comoro.
No comments:
Post a Comment