Friday, 2 February 2018

TAAZIA: COMRADE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU (1930 - 2018) NA JUMA VOLTER MWAPACHU


TAAZIA: COMRADE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU
NA JUMA VOLTER MWAPACHU

Kaitan Maurus Ngombsle

Leo alfajiri nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha ndugu yetu Kingunge Ngombale Mwiru. Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake ambayo ni wiki chache tu tarehe 4 Januari, kilifiwa na mama yao, Peras Ngombale Mwiru, mke wa Ngombale Mwiru.

Tanzania nzima bila kujali misimamo ya siasa haina budi kuwa na majonzi mazito kwa kuondokewa na Comrade Ngombale Mwiru. Alikuwa shujaa wa siasa tangu TANU hadi kifo chake.

Nilimfahamu kwa karibu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Youth League, Chuo Kikuu, Dar-es-Salaam kwa kipindi 1967/68. Yeye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa TANU Youth League, Makao Makuu. Joseph Nyerere alikuwa Katibu Mkuu na Moses Nnauye alikuwa Katibu Mkuu Msaidizi.

Nilibahatika nami kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU Youth League. Tangu kipindi hicho Ngombale ananiona Comrade. Hata siku ile ya sala ya kumuaga mama Peras pale St Peters Church aliponiona akitoa smile kubwa alinipa mkono akiniita 'Comrade.’

Mwaka 1991 Ngombale alichaguliwa na CCM kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kupendekeza Sera na Mwelekeo wa Chama na nchi katika miaka ya 90. Mimi, Iddi Simba na Reginald Mengi tuliteuliwa kuwa wanakamati. Report yetu iliyokubaliwa kwa kishindo na Mkutano Mkuu wa CCM hapo 1992 baada ya kuwasilishwa na Ngombale kwa fasaha kubwa ndiyo iliyojenga misingi ya mageuzi ya uchumi nchini.

Wakati wa kazi hiyo Ngombale akawa karibu sana nami akitambua kwamba nilikuwa pia mjumbe wa Tume ya Nyalali kuhusu Chama Kimoja au tuingie kwenye Vyama Vingi. Comrade Ngombale alikuwa rafiki wa karibu sana wa Professor Ahmed Mohiddin, Mkenya aliyependwa sana na Mwalimu Nyerere kutokana na maandiko yake kuhusu ujamaa.
Mohiddin ana undugu na familia ya mke wangu. Sote tuliyokuwa karibu ya Ngombale tulimuita Susilov kutokana na kuwa 'ideologue' wa TANU na CCM.

Susilov alikuwa ideologue wa Soviet Union Communist Party. 

Tanzania imempoteza jabari wa siasa. Kwangu nimempoteza Mwalimu na rafiki. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
Amin.

No comments: