BURIANI
KOMREDI KINGUNGE MSOMI WA TANU ULIYELISOMESHA TAIFA
KIZAZI KILICHOANDALIWA
KUONGOZA NCHI YETU
Nilikutana na Mzee Kingunge Ngombale - Mwiru Bungeni mwaka
2005, mimi nikiwa Mbunge wa kuchaguliwa kutoka Kigoma Kaskazini na yeye akiwa
Mbunge wa kuteuliwa na Rais. Tulipoanza Bunge la 9 Mzee wetu huyu ambaye sasa
ametangulia mbele ya haki alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano ya
Jamii na Siasa. Baadaye alipumzishwa na kuendelea kuwa Mbunge wa kawaida.
Sikuwa na ukaribu naye, japo tulikuwa tuna ukaribu kifikra,
kwa maana ya itikadi ya Ujamaa. Sikuwa nakunywa naye kahawa kama ilivyokuwa kwa
Mzee Prof. Philemon Sarungi au Marehemu Jackson Makweta. Lakini tulikuwa
tunasalimiana kwa bashasha na akipenda ukorofi wangu Bungeni. Baadaye nilijifunza kuwa naye alikuwa mkorofi
sana enzi za ujana wake.
Siku moja mwaka 2009 kulikuwa na mzozo Bungeni kuhusu mjadala
wa Mahakama ya Kadhi. Wabunge Waislam wakiongozwa na Mohamed Misanga wakiitaka
na Wabunge Wakristo wakiongozwa na Godfrey Zambi wakiipinga. Lugha zilizokuwa
zikitumika zilikuwa za mgawanyiko mno na Bunge lilikuwa mubashara kwenye
runinga. Nikaogopa sana namna viongozi wanaongea lugha za kugawa wananchi
kidini. Nikasimama kuongea. Nikafoka sana kuhusu lugha tunazotumia kujenga hoja
bila kujali madhara yake kwa raia wetu. Pia nikawalaumu Wabunge wakongwe kwa
kukaa kimya bila kukemea. Mjadala ukabadilika na kuwa wa staha.
Tulipotoka nje ya Bunge nikakutana na Ezekiel Kamwaga,
mwandishi wa habari ambaye enzi hizo hakuwa mwandamizi. Ezekiel akaniambia, “Nimemhoji
Mzee Kingunge kuhusu lawama zako kwao. Ameniambia wewe umechelewa sana
kuzaliwa. Ulipaswa kuzaliwa wakati wa Mwalimu Nyerere. Una maoni?” Nikamjibu
Kamwaga kuwa wazee waliniudhi kukaa kwao kimya. Hata hivyo nimefarijika sana
kuwa Mzee alikuwa ananisikiliza. Tangu siku hiyo kila nilipokutana na Mzee
Kingunge nilikuwa nataniana naye kuhusu ‘intervention’ ile bungeni.
Nimekuwa na kawaida ya kuandika ‘’obituary,’’ (tanzia) kila
mtu wa karibu yangu ama mtu ninayemheshimu anapofariki. Wakati mwengine huwa
napata tabu sana kuandika kutokana na ukaribu ama uzito wa mtu mwenyewe. Tangu
asubuhi jana nilipoletewa ujumbe wa simu kuwa Mzee Kingunge hatunaye nimekuwa
natafakari kuwa naandika nini kuhusu jabali hili la siasa za nchi yetu?
Naandika nini kuhusu kizazi cha dhahabu cha wanasiasa wazalendo wa nchi yetu?
Naandika nini kuhusu ‘ideologue’ wetu huyu ambaye hajaweza kuzibwa nafasi yake
na yeyote?
Ni kama vile mtu anayetaka kuandika kuhusu maisha ya Komredi
Marcelino Dos Santos wa FRELIMO. Ni kazi ngumu zaidi kwa sisi ambao hatukuwa na
ukaribu mkubwa sana na mzee huyu. Hata hivyo, nimeona lazima nimuage Komredi
Kingunge kwa namna ninayoweza, nayo ni kueleza kizazi cha sasa ni nani Kingunge
Ngombale Mwiru, na ni kwa nini nchi yetu ilikuwa na raia huyu?
Maisha ya Komredi Kingunge ni taswira ya historia ya chama
kilichotukomboa kutoka makucha ya ukoloni mkongwe. Mwaka 1957 ilikuwa dhahiri
kwa chama cha TANU kuwa punde tu, miaka michache mbele, uhuru wa Tanganyika
ungepatikana, hamasa ya wananchi ilikuwa juu mno, na uungwaji mkono wa TANU
ulikuwa mkubwa nchi nzima. Katika wakati husika viongozi wenye maono wa TANU
wakaamua kuliandaa taifa na kukiandaa chama chao kuendesha nchi.
Changamoto kubwa katika wakati husika ilikuwa ni rasilimali
watu, wasomi wachache wa Kiafrika ambao pia walikuwa viongozi wa TANU
hawakutosha kushika nafasi zote muhimu za kuliongoza taifa. Hivyo haja ya
kusomesha wasomi wa Kitanganyika kwa ajili ya kusaidia kuliongoza taifa mara
baada ya uhuru ikaibuka. Rais wa 19 wa Liberia, ndugu William Vacanarat
Shadrach Tubman na chama chake cha True Whig Party (TWP) wakawa kimbilio la
TANU, Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere, akiomba nafasi za masomo ya elimu
ya juu (skolashipu) kwaajili ya vijana wa Tanganyika.
Komredi Kingunge alikuwa mtu wa tano kupata skolashipu hizo, mwaka
1958. Awali, mwaka 1957, Mzee Muharram Macatta Mwinyimtwana na Balozi Paul
Malyago Rupia walikuwa ndio kundi la kwanza la wanafunzi kupata skolashipu za
kwenda kusoma elimu ya juu kupitia Chama cha Ukombozi cha TANU, katika Chuo
Kikuu cha Cuttington, Suacoco, Maili 120 Kaskazini ya mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Muharram na Paul walikuwa watoto wa wafadhili wa chama cha TANU, Mzee Macatta
Mwinyimtwana wa Ngamiani Tanga, na Mzee Paul Rupia wa Misheni Kota Ilala, Dar es Salaam.
Kundi la pili lilihusisha wanafunzi watatu, ambao pia
walikuwa ni wafanyakazi wa kujitolea katika makao makuu ya TANU, hao ni Komredi
Kingunge, Mzee Ghysla Mapunda, aliyekuwa waziri wakati wa Mwalimu Nyerere,
pamoja Shaaban Nyelwa Kissenge, ambao wao walikwenda masomoni mwaka 1958.
Kundi la tatu lilikuwa kubwa zaidi, likihusisha idadi ya watu
zaidi ya kumi, lilikwenda masomoni mwaka 1959. Kundi hili likiwahusisha ndugu
Amani Samuel Mshote, Dakta John Peter Kasiga, ndugu Martin Kayuza, Chifu
Nhindilo Humbi Ziota, Dkt Kassim Guluri, ndugu Charles Buzuka, Dkt William
Kimweri Madundo, Dkt Mbaga, ndugu Joshua Mpogolo, ndugu Mjabuzi, pamoja na
ndugu Edmund Luganga. Hivyo kufanya jumla ya watu wote waliopelekwa masomoni na
TANU kufikia 16, katika kipindi kifupi cha kati ya mwaka 1957 - 1961. Wote hawa
kwa nyakati tofauti tofauti walishika dhamana mbalimbali ndani ya nchi yetu.
Jambo hili la TANU kuandaa vijana wa kuendesha nchi ni
historia muhimu ya taifa letu, inajenga msingi wa namna vyama vya siasa vya
wakati wa ukombozi vilivyojikita katika ujenzi wa nchi. Kwa Zanzibar, chama cha
Umma Party nacho kilifanya jambo hili la kuwaandaa vijana, kwa kuwatafutia
mafunzo kutoka sehemu mbalimbali, ulimwenguni, kuanzia Cuba, Ujerumani, USSR
mpaka Misri. Hivyo vijana wa kizazi cha awali cha Tanzania, kina Komredi
Kingunge na Dkt Salim Ahmed Salim, walipikwa na kuandaliwa vyema kuja
kuliongoza taifa na vyama vyao, jambo ambalo vyama vya siasa vya sasa havifanyi
kabisa.
Taswira kuu ya Mzee Kingunge ni kuwa alikuwa ni tanuri la
kupika fikra zilizozaa sera na maamuzi ya nchi yetu. Ramani ya Maendeleo ya
nchi yetu Tanzania, kwa miongo mitatu ya mwanzoni ilichorwa kwa kutumia nyaraka
tatu; Azimio la Arusha, Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 na Mwongozo wa CCM wa
mwaka 1981. Nimechungulia nyaraka zangu ili kusoma muhtasari wa Mkutano wa
Halmashauri Kuu ya TANU ya Januari, 1967 iliyopitisha Azimio, na sikuona jina
la Komredi Kingunge. Mkutano huu ndio uliiweka nchi yetu kwenye ramani ya nchi
za kijamaa. Mzee Kingunge hakuwamo kwenye ule mkutano wa Arusha. Hata hivyo huwezi
kuzungumzia utekelezaji wa azimio hilo bila kutaja miongozo niliyotaja hapo juu
ambayo aliindika yeye. Kwa hiyo miaka minne mara tu baada ya kutangazwa kwa
Azimio la Arusha unaanza kumwona gwiji la itikadi “The Ideologue” Kingunge
Ngombale Mwiru.
Juzi niliona taarifa kutoka Davos, Uswizi, ambapo mkutano wa
mabepari wa dunia hufanyika. Taarifa ile ilisema Tanzania ndio nchi inayoongoza
Afrika kwa kuwa na uchumi jumuifu (inclusive economy). Kwa watu wa fikra fupi
walikimbilia kusambaza habari hizi bila kuzipa muktadha wake stahili. Muktadha
wake ni Azimio la Arusha la 1967. Hili ndio lilikataa unyonyaji na kujenga
uchumi usio na matabaka (inequality).
Katika kitabu kilichopewa jina ‘Miongozo Miwili: Kupaa na Kutunguliwa
kwa Azimio la Arusha’
(https://www.udsm.ac.tz/sites/default/files/Miongozo_bk.pdf), kilichochapishwa
na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kingunge
anaeleza kwa ufasaha namna Mwongozo wa 1971 ulivyobuniwa na kutekelezwa.
Nanukuu:
“Mwongozo wa TANU wa 1971 ulitolewa na
kutangazwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU ya dharura mwanzoni mwa mwezi wa
Februari, Dar es Salaam. Mwezi wa Januari mwaka 1971 Jeshi la Uganda chini ya
Iddi Amin Dada, liliangusha serikali ya Rais Milton Obote na kutwaa madaraka.
Kufika Agosti kitendo cha uchokozi kisicho cha kawaida kilitokea, kikosi cha
Jeshi la Iddi Amin kilikivamia kikosi cha doria cha polisi wa Tanzania mpakani
Mutukula na kumteka nyara Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na kumtoroshea
Uganda”.
[Kamanda huyu aliyeuwawa hatimaye aliitwa Hans Pope, baba
mzazi wa huyu Hans Pope wa Simba Sports Club inayoifunga funga Yanga kila
wakikutana].
“Kitendo hiki cha uhasama kutoka kwa
nchi jirani kilihitaji kupatiwa jibu la haraka na la kimkakati. Ndipo
nilipoitwa Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais, Ndugu Rashid Mfaume Kawawa,
ambaye nilimkuta na Meja Hashim Iddi Mbita (wakati ule Katibu Mtendaji Mkuu wa
TANU). Ndugu Kawawa alinieleza kwa kifupi kuwa Mwalimu alimwagiza aniarifu kuwa
ameamua mimi niongoze timu ya viongozi wa vijana kadhaa wa TYL (TANU Youth
League) kwenda Mkoa wa Ziwa Magharibi kufanya kazi ya kuhamasisha wananchi
kisiasa na kiulinzi na usalama ili waweze kukabiliana ipasavyo na chokochoko
zozote zile kutoka nchi jirani.
Pamoja na kukubali jukumu nililopewa
na kuahidi kuanza maandalizi mara moja, nilitoa rai kwa Makamu wa Pili wa Rais
kwamba kwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi kutoka Uganda ni sehemu tu ya tishio
kwa taifa, maana kuna tishio kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Kusini, la majeshi ya
Wareno, na uhasama wa Wareno, pamoja na wa dola za Afrika ya Kusini na Rhodesia
(sasa Zimbabwe) ingekuwa busara kuitisha kikao cha NEC kutafakari juu ya ulinzi
na usalama wa Taifa. Ndugu Kawawa alikubaliana na pendekezo langu na palepale
aliondoka akifuatana na ndugu Hashim Mbita, kwenda kuonana na Mwalimu Ikulu.
Walirejea baada ya nusu saa na kunitaarifu kuwa Mwalimu amekubali pendekezo
nililolitoa na tayari ameagiza NEC iitishwe kwa dharura.”
Mwisho wa kunukuu.
Komredi Kingunge sio tu alipokea kazi na kuitekeleza kwa
utii, bali pia alishauri kuipanua na kuipa baraka ya vikao vya Chama. Hebu
fikiria, unaitwa na Kawawa unapewa kazi aliyoagizwa na Nyerere halafu wewe
mpewa kazi unashauri kwanza nini kifanyike. Sio tu ni ujasiri bali ni kujiamini
kulikopita kiasi cha kawaida. Hebu fikiria leo unaitwa na Rais kupewa kazi
halafu unajifanya kujua, Eti itisha Halmashauri Kuu kwanza, thubutu. Kingunge
ni darasa tosha la wanasiasa wa sasa.
Kwa taarifa tu kwa Vijana ni kwamba moja ya zao lililodumu la
mwongozo wa mwaka 1971 ni Jeshi la Mgambo. Ilipotokea vita dhidi ya nduli Idi
Amini, wanamgambo walioandaliwa kutokana na mwongozo wa mwaka 1971 walipigana
bega kwa bega na wanajeshi wengine na kumshinda adui. Ukiona mwanamgambo popote
ni alama ya fikra za Mzee Kingunge tunayemzika siku ya jumatatu ya Februari 5,
2017 siku ambayo kilizaliwa chama ambacho yeye ni miongoni mwa waasisi wake.
Kwa hakika nchi yetu inaweza kumuenzi mzee wetu huyu kwa kuanzisha Kingunge
Brigade ndani ya Jeshi la Mgambo ili vizazi na vizazi wajue wazo hili lilitoka
kwa nani.
Kingunge Ngombale Mwiru na Kitwana Selemani Kondo |
Lakini pia mwongozo wa mwaka 1971 ulisisitiza sana suala la maendeleo
ya watu. Jambo ambalo ni mwafaka wakati huu kuliko wakati mwengine wowote ule katika
nchi yetu. Mwongozo ulisema:
“Kwa hiyo katika kufikiria maendeleo ya taifa
letu na katika kupanga mipango ya maendeleo wakati wote mkazo mkubwa uwekwe
kwenye maendeleo ya WATU na sio ya vitu... [W]atu wenyewe lazima washiriki
katika kufikiria, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo yao.”
Hii ni kauli inayoishi na kudumu milele. Hupimi maendeleo ya taifa
kwa madaraja, ndege, wala njia za reli, bali kwa namna ambavyo watu wa taifa
hilo wameelimika na kuwa na afya tele inayowpa uwezo wa kuzalisha mali na
kuongeza utajiri wa nchi.
Dhana hii ya ‘Maendeleo ya Watu’ Mzee Kingunge aliiamini
mpaka mwisho wa uhai wake. Nakumbuka wakati wa mijadala ya Bunge Maalumu la
Katiba aliamsha mjadala mzito juu ya jambo hilo, na aliandika eneo maalumu la
Uchumi ili kutoa ‘Dira ya namna Uchumi wa Taifa letu unapaswa kuwa.’ Eneo hili
limewekwa kama sehemu ya tatu ya Katiba Pendekezwa, likijikita katika kuelezea
namna dola inavyopaswa kuwa wakala wa ukombozi wa wananchi.
Miaka 10 baadaye mwongozo wa mwaka 1981 ulitangazwa, ambao
pia ni zao la fikra za Komredi Kingunge. Katika kitabu cha Miongozo Miwili hilo
pia limeelezwa vizuri na Kingunge mwenyewe. Nanukuu:
“Mwongozo wa 1981, kama ulivyokuwa mwongozo wa
TANU wa 1971, ulikuwa ni mwendelezo wa fikra na matarajio ya Ujamaa na
Kujitegemea uliotangazwa na Azimio la Arusha. Mwongozo huu ni matokeo ya mila
iliyokuwa imejengwa ndani ya Chama ya kutumia vikao vikuu vyake, hususan NEC,
kujadili na kuchambua masuala mazito ya nchi, ya siasa, uchumi na jamii, na
kuyatolea maelekezo ya kisera, kiufafanuzi na kiutekelezaji.
Wakati Mwongozo wa TANU wa 1971
ulijielekeza kwenye mapambano dhidi ya Ukoloni, Ukoloni-Mamboleo na Ubeberu ili
kufanikisha Ukombozi wa Afrika na wa Mwafrika na kuweka mkakati wa ulinzi na
usalama wa umma ili nchi iwe na uwezo wa kukabiliana na uvamizi wowote kutoka
kwa ubeberu au na vibaraka vyake, Mwongozo wa 1981 umejikita katika kufanya
uchambuzi kosoa wa kina na mpana juu ya hali ya kisiasa na kiuchumi iliyokuwepo
nchini, hali ya maendeleo ya demokrasia nchini na ndani ya chama, n.k., na
kutoa mapendekezo ya kuimarisha na kupanua demokrasia katika Chama na nchi.”
Mwisho wa kunukuu.
Jambo kubwa tunalojifunza hapa ni Chama cha siasa kuwa chombo
cha mijadala na maamuzi ya watu badala ya kuwa chombo cha kupitisha amri za
wakubwa. Kwamba chama kinaweza kufanya uchambuzi kosoa ili kujikosoa. Na kwamba
vikao vikuu vya chama vinapaswa kuwa na ajenda ya kudumu ya kujadili hali ya
uchumi na siasa ya nchi. Sisi ACT Wazalendo tuliiga jambo hili, ndio maana
katika kila kikao kikuu cha chama chetu, ni lazima tujadili hali ya nchi
(Kiuchumi na Kisiasa) na kutoa taarifa ya mwingozo wa kisera kwa chama.
Jambo hilo ni muhimu sana, hasa katika zama za sasa ambapo
hata kukosoa ni dhambi, na vikao vya vyama hukaa kwa dakika masaa machache sana
kupokea amri tu za wakuu wa vyama hivyo. Kwa vyovyote vile vyama vya namna hiyo
vinahesabu siku zake. Ni vema kutumia siku za kuomboleza kifo cha Komredi
Kingunge kujitafakari kama tunafuata misingi ya mwongozo wa mwaka 1981 kuhusu
uchambuzi kosoa ili kujenga msingi madhubuti wa ujenzi wa vyama vyetu vya
siasa, pamoja na kupanua demokrasia nchini.
Mzee Kingunge ametuachia usia kwenye andiko lake nililonukuu
sana kwenye makala haya. Mwenyewe ameziita changamoto na ninaomba niziweke kama
alivyoziweka yeye:
- Unapoisoma miongozo hii miwili, wa
TANU wa 1971 na wa 1981, huwezi kukosa kubaini kuwa fikra, nadharia na tafakuri
kubwa zilitumika katika utunzi wake. Haya ni matokeo ya viongozi wa chama
wanapokaa pamoja na kufikiri pamoja. Hii ni aina mojawapo ya uhai wa chama
iliyo muhimu sana kwa uhai wa jumla wa chama cha siasa.
- Je, mila hii iliyokuwa imejengeka
huko nyuma CCM ya sasa inaiendeleza? Je Vyama vingine vya siasa nchini
vinajaribu kujenga tabia ya viongozi wake kuketi pamoja na kufikiri pamoja na
kuchambua pamoja hali ya nchi yetu na namna vitakavyozikabili changamoto
mbalimbali?
- Huu umaskini wetu wa sasa wa
falsafa unaotuathiri vibaya unatokana na nini?
Mzee Kingunge alikuwa mtu mwenye kusimamia anayoyaamini,
amefariki dunia akiwa ameondoka katika Chama chake alichoshiriki kukiasisi.
Tunaambiwa kuwa hakujiunga na chama kingine cha siasa, ingawa alitoa msaada kwa
chama kilichokuwa kinapingana na chama chake. Hili laweza kubakia kuwa jambo la
mjadala mkali katika miaka inayokuja. Inawezekana mjadala huo ukafunika kabisa
mchango wake kwenye ujenzi wa taifa letu. Hatuwezi kukwepa hilo kuwa mjadala
Lakini tunaweza kukwepa kulikuza na kulifanya lifunike mambo makubwa
aliyoyafanya kwa nchi yetu.
Sina hakika kama Komredi Kingunge aliandika kitabu kuhusu
maisha yake. Hii ni changamoto kubwa kwa Viongozi wetu wengi. Hawapendi
kuandika na hivyo kuondoka duniani na MAARIFA yao bila kuyarithisha kwa vizazi
vya mbele yao. Kuna mambo mengi ambayo vizazi vingependa kujifunza kutoka kwa
watu kama Kingunge Ngombale Mwiru lakini kwa sababu hatuandiki, basi vizazi
vinaikosa hiyo fursa.
Kwa mfano, miaka ya 1970 Komredi Kingunge alikuwa ni Mkuu wa
Mkoa, Katibu wa TANU wa Mkoa, na hivyo kuwa pia mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, aligombana na Mzee Kawawa kuhusu kwenda kinyume na
msimamo wa Serikali Bungeni ilhali yeye ni Mkuu wa Mkoa wa Serikali hiyo hiyo,
kwa jambo la Serikali ambalo yeye hakukubaliana nalo. Mwalimu Nyerere
alimfukuza kazi Kingunge.
Habari hii haijaweza kuelezwa kwa namna ambayo itakaa kwenye
vichwa vya Vijana kama funzo la kuwa na msimamo. Mzee Kingunge hakujali cheo
chake, alisimamia kile alichokiamini bila kujali cheo chake. Alifukuzwa kazi
Lakini baadaye alirudi, na kuwa mjumbe wa kamati iliyoandika katiba ya
kuunganisha vyama vya ASP na TANU. Aliheshimiwa kwa msimamo wake. Jambo hili
hulioni kwa wanasiasa wa sasa. Limefanywa kuwa gumu zaidi pia kutokana na uongozi
wa sasa pia ambao ni wa kiimla na hauruhusu mawazo pinga.
Tabia ya kuwa msimamo Kingunge ameiishi maisha yake yote,
tangu chuo kikuu kule Liberia. Katika kundi la wanafunzi wale 16, ni kuwa ni
kundi la kwanza tu, wazee wetu Muharram Mwinyimtwana tu na Paul Rupia, ndio
waliomaliza masomo yao mwaka 1960, wanafunzi 13 waliobaki chini ya Uongozi wa
Komredi Kingunge walifukuzwa chuo wakitetea uonevu dhidi ya wanafunzi wenzao,
jambo lililozusha vurugu kubwa hapo Chuo Kikuu cha Cuttington, na hivyo
wanafunzi hao kuhamishiwa Dakar, Senegal, na kisha kuendelea na masomo katika
nchi za USSR.
Ningefurahi kusoma visa vyote hivi kutoka kwenye kitabu cha
Komredi Kingunge mwenyewe. Natarajia kuwa ameacha mahala hazina ya maandiko ya
historia hii muhimu kwa taifa, na kuwa watafiti na wanazuoni wataweza kuiweka
hazina hiyo kwenye kitabu. Kwa hakika nchi yetu imepoteza Jabali la Siasa.
Profesa Issa Shivji amejitahidi kumweka wazi Mzee Kingunge kwenye maongezi yao
yaliyochapishwa kwenye jarida la Nyerere Chair miaka tisa iliyopita. Maongezi
haya (https://issabinmariam.files.wordpress.com/2018/02/mazungumzo-kati-ya-ngombalemwiru-na-issa-shivji-2009.pdf
) yanatosha kuanzia kuandika kitabu cha Kingunge.
Nawasihi watu wote msome
maongezi yale. Yamesheheni historia ya nchi yetu ndani ya historia ya Mzee
Ngombale.
Buriani Mzee Kingunge Ngombale - Mwiru. Ulisomeshwa na TANU
nawe ukalisomesha Taifa. Uliandaliwa kuongoza Taifa letu, umetuongoza vema.
Pumzika kwa Amani Komredi.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Februari 3, 2018
No comments:
Post a Comment