Hamza Aziz alikuwa mzee wangu na rafiki pia.
Nilipokuwa Tanga akinipigia simu kunisalimia tu na mwisho huishia kunipa mwaliko
nende kwake nikja Dar es Salaam.
Nyumba yake ilikuwa baharini kabisa na kule ufukweni
alijenga kibanda cha makuti kwa ajili ya kupumzika na kupunga upepo.
Hapa ndipo ilipokuwa barza yetu tukikaa muda mrefu
sisi wawili tu tukizungumza.
Kwa hakika yalikuwa mazungumzo lakini mzungumzaji
khasa alikuwa yeye mimi nilikuwa msikilizaji na wakati mwingine muulizaji
maswali.
Nilikuwa wakati mwingine nikumvurumishia maswali
mazito. Basi yeye atacheka kisha ataniambia, ‘’Mohamed unajua mimi nina umri wa
miaka 74 nimekula kiapo kutunza siri wakijua nimesema watanifunga mimi.’’
Juu ya haya yote Hamza Aziz alikuwa mwingi kazi ya
polisi alianza toka akiwa kijana mdogo wakati wa ukoloni hadi kufikia kuwa
Inspector General of Police (IGP).
Wakati mwingine nilikuwa nikiwasindikiza watu
waliokuwa wakitaka kuja kumuona Hamza Aziz kwa hili ama lile.
Nakumbuka Mzee Kanyama Chiume ni mmoja wa watu ambao
nilipata kukaanae pamoja na Hamza Aziz katika kile kibanda cha makuti ufukweni
Katika kibanda hiki siku moja Hamza Aziz alinihadithia
maisha yake ya utotoni katika miaka ya 1940 na kazi aliyopewa na baba yake ya
kupeleka karabai katika misikiti yote ya Karikaoo.
Miaka ile misikiti ilikuwa haina umeme. Hamza Aziz.
Hamza Aziz alinieleza kuwa baba yake siku alipofariki mwaka wa 1951, gazeti la
Tanganyika Standard lilitangaza kifo chake kwa kusema kuwa, ‘’Mjenzi wa
misikiti amefariki.’’
Hamza Aziz akanambia kuwa karibu misikiti yote ya Dar
es Salaam iliyojengwa mwanzo wa miaka ya 1900 alijenga baba yake kwani baba
yake alikuwa ‘’Building Contractor,’’ yaani mjenzi wa majumba.
Kwa ajili ya mapenzi haya ya baba yake katika dini
Hamza Aziz alikabidhiwa na baba yake Aziz Ali jukumu la kuweka taa katika
misikiti yote ya Kariakoo kuanzia sala ya Maghrib.
Hamza Aziz alikuwa akiziwasha karabai nyumbani kwao
kisha kuzipeleka misikitini na ikimalizika sala ya Isha anazipitia kuzirejesha
nyumbani kwa ajili ya kuziwekea mafuta na kuziwasha siku ya pili zipelekwe tena
misikitini.
Hii ndiyo iliyokuwa kazi yake na hii ndiyo ilikuwa hali
ya misikiti ya Kariakoo nyakati zile.
Nakumubuka msikiti wa Manyema wa zamani ambao
ulijengwa mwaka wa 1912 ukiwa na kisima cha kuteka maji.
Msikiti wa Badawy Kisutu ulikuwa msikiti mdogo ingawa
ulikuwa na historia kubwa sana kati ya misikiti yote ya Dar es Salaam.
Hapo palikuwa moja ya misikiti ambayo Sheikh Hassan
bin Ameir alikuwa akisomesha darsa zake za tafsir ya Qur’an na akisomesha
masheikh na wanafunzi wengine wadogo, masheikh vijana wanaoinukia.
Darsa nyingine alikuwa akisomesha Sheikh Hassan bin
Ameir ni Msikiti Ngazija, msikiti uliokuwa mjini kabisa.
Huu msikiti wa Ngazija ndiyo nadhani ulikuwa kati ya misikiti
midogo sana Dar es Salaam ingawa kwa pale ulipojengwa usingeweza kuitwa
msikiti uliokuwa Kariakoo.
Ukija msikiti wa Kiblatein uliokuwa Mtaa wa Aggrey
wakati ule (sasa Mtaa wa Max Mbwana), Msikti wa Makonde, Shadhuly yote ilikuwa
midogo ambayo kufikia miaka ya 1970 ikawa haitoshi tena kuchukua umma wa
Waislam wa Dar es Salaam si sala ya Ijumaa wala ya Eid na ukiondoa hayo hata
huduma nyingine zilikuwa hazikidhi haja tena.
Msikiti mkongwe kupita yote Kariakoo ni Msikiti wa
Kisutu ulio na umri wa zaidi ya miaka 150.
Msikiti huu sasa unajulikana kama Msikiti wa
Mwinyikheri Akida.
Huu ulibaki kwa muda mrefu kama ulivyokuwa ulipojengwa
na ni mmoja katika ya misikiti miwili ambayo ilichelewa sana kujengwa upya, huo
na Msikiti wa Makonde.
Mwalimu wangu wa historia ya mji wa Dar es Salaam na watu
wake Sheikh Ali Abbas alipata kunambia kuwa ikiwa nataka kuona misikiti ilivyokuwa
katika miaka ya 1950 nende kusali Msikiti wa Makonde.
Hamza Aziz hii yote ilikuwa misikiti yake akiingia na
kutoka katika utoto wake na ikamfanya ajulikane sana ukiachilia mbali kuwa
alikuwa mtoto wa Aziz Ali, Mwafrika tajiri na maarufu mjini Dar es Salaam.
Kuanzia miaka ya 1970 misikiti mingi ya Kariakoo
ilianza kufanyiwa matengenezo na mingine kuvunjwa kabisa na kujengwa upya na
kufanywa ya gorofa mbili hadi tatu.
Hii ilitokana si zaidi ya uchakavu wa misikiti yenyewe
bali hii misikiti ilikuja kuwa midogo haitoshi na siku za Ijumaa ikawa watu
wanaswali nje juani kwa kutandika majamvi na kufunga barabara na mitaa.
Ikiwa mvua inanyesha hali ilikuwa ngumu sana kwa
Waislam na hii ilikuwa adha kubwa.
Lakini ukweli pia ni kuwa misikiti ile ilipitwa na
wakati kwa mbali sana.
Imekuwa kawaida siku hizi hapa msikitini petu kusali
kiza kwa huku kukatika umeme kwa mara kwa mara kiasi tumeamua kununua taa ya
chemli ambayo tunaiweka mbele kibla tunapokuwa hatuna umeme.
Ninapoangalia ile hali ya kiza ndani ya msikiti wakati
tunaswali huwa inanijia picha vipi misikiti ya zamani ilivyokuwa hapa Dar es
Salaam wakati umeme ulipokuwa bado.
Hapo ndipo huwa namkumbuka marehemu Hamza Aziz na
karabai zake.
No comments:
Post a Comment