Friday, 13 April 2018

JANUARY MAKAMBA NA HISTORIA YA MWALIMU NYERERE NA TANU

Ibrahim Kaduma akizungumza katika kongamano la Mwalimu Nyerere
Mwalimu Nyerere Memorial Academy
Mwalimu Nyerere Memorial Academy zamani ikijulikana kama Chuo Cha Kivukoni jana tarehe 13 April 2018 ilifanya kongamano la kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Hapo chini ni maneno niliyoandikiwa na mmoja wa wasomaji wangu:

‘’Nimeangalia, nimemsikia mgeni rasmi January Makamba akizungumzia umuhimu wa vijana kuwa na maarifa mengi badala ya taarifa, ametolea mfano wa Mwalim Nyerere kuwa alikuwa na maarifa ndio maana alipokuja Dar es Salaam "WAZEE WAKAMPA UENYEKITI WA TANU" awaongoze. Japo hakuwataja ila natumai alikuwa anawarejelea akina Sykes, Takadir nakadhalika.’’


Baraza la Wazee wa TANU

Mimi niliandika maneno hayo hapo chini kumjibu kueleza historia ya TANU kama niijuavyo na kama nilivyoelezwa na wenyewe waasisi wa TANU:

Nyerere hakupokelewa na wazee. TAA kuanzia 1950 ilishikwa na vijana wa Makerere na vijana wenyeji wa mji chini ya Abdul Sykes. Kulikuwa na madaktari watano ndani ya TAA: Dr. Joseph Mutahangarwa, Dr. Michael Lugazia, Dr. Luciano Tsere, Dr. Vedasto Kyaruzi na Dr. Wilbard Mwanjisi. Hawa wakaungana na kundi la watoto wa mjini: Abdul na Ally Sykes, Steven Mhando, Dossa Aziz na Hamza Mwapachu.

Katika kundi hili kukawa na ‘’inner circle,’’ hawa ni Abdul na Ally, Dossa na Mwapachu. Muongeze na John Rupia. Mkutano wa kumuingiza Mwalimu Nyerere katika uongozi wa TAA ulifanyika nyumbani kwa Mwapachu Nansio, Ukerewe kati ya Mwapachu, Ali Mwinyi Tambwe na Abdul. Hii ilikuwa mwaka wa 1953.

Hawa ndiyo waliomtia Nyerere katika siasa za Dar es Salaam.

Wazee walikuja baadae TANU tayari imeshaasisiwa na hapa ndipo unamkuta Sheikh Hassan bin Ameir. Yeye na Sheikh Said Chaurembo ambao walikuwa ndani ya TAA Political Subcommittee na wakijua mpango wa kuunda TANU toka 1950 wala hawamjui Mwalimu Nyerere...hiki ndicho kipande kinachokwepwa kuelezwa siku zote katika historia ya TANU na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Sasa hili ndilo linalowatisha baadhi ya watu toka mwaka wa 1961 Tanganyika ilipopata uhuru kwa maana kuwa, ikiwa historia ni hii kama nilivyoeleza hapo juu, TANU haiwezi kuwa iliasisiwa na Mwalimu Nyerere mwaka wa 1954, kwani "blue print" ya TANU ilikuwa kwa kina Sykes kwa miaka mingi.

Umuhimu wa kuwa na sifa ya uasisi wa wa TANU umuhimu wake ni kuwa na TANU ni "the ultimate prize."

Yule atakae kuwa ndiye muasisi wa TANU nchi hii haiwezi kumsahau maisha.

Historia hii ya TANU baada ya kusoma kitabu cha maisha ya Abdul Sykes ilimpa tabu sana Prof. Haroub Othman kiasi alimkabili Mwalimu Nyerere kutaka ukweli wa historia ya TANU pamoja na mambo mengine.

Msomaji anaweza kuingia hapo chini kusoma na kuona vipi historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika inavyowababaisha wanasiasa:
http://www.mohammedsaid.com/2016/03/pius-msekwa-na-historia-ya-kupigania.html

No comments: