Saturday, 14 April 2018

JUMA MWAPACHU ANAZUNGUMZA KUHUSU HISTORIA YA UHURU


Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na
Juma Volta Mwapachu
Utangulizi

Juma Mwapachu alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Nansio, Ukerewe wakati Abdul Sykes na Ali Mwinyi Tambwe walipokwenda Nansio mwaka wa 1953 kumuona baba yake, Hamza Kibwana Mwapachu kuhusu uchaguzi wa TAA wa mwaka huo uliokuwa ufanyike miezi michache mbele. 

Abdul Sykes alikuwa anataka kauli ya mwisho kutoka kwa Mwapachu kuhusu Nyerere kuwa ndiyo Hamza hajabadili fikra yake na anamtaka Abdul ampishe Nyerere katika nafasi ya urais wa TAA? 

Hamza Mwapachu alirejea katika fikra yake na akamueleza Abdul kuwa Nyerere achukue nafasi ya urais na mwaka ujao, 1954 iundwe TANU. Juma Mwapachu kashuhudia haya kwa macho yake hakuhadithiwa. 

Juma Mwapachu kasoma niliyoandika kuhusu historia ya TANU na hayo hapo chini ndiyo maneno aliyoniandikia:

''Mohamed naafiki kabisa na maelezo yako.


Ndugu Msekwa hajaandika historia ya ukweli kuhusu vuguvugu la siasa za kugombea uhuru kuelekea uundwaji wa TANU.

Historia haifutiki wala kupinduliwa.
Hivi tatizo ni nini hasa kutoa maelezo ya ukweli?

Dr Kyeruzi alinipa nakala ya makala ya kitabu chake ' The Muhaya Doctor' baada ya kunitumia salaams kupitia kwa kaka yangu Harith Bakari kuniita niende kumuona nyumbani kwake Bukoba.

Nilikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo akitaka nimsaidie kuchapisha kitabu chake.

Nisiseme zaidi.

Muhimu ni sura moja ya kitabu hicho ikifafanua historia ya kukuzwa kwa uongozi wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mapambano yalishika moto kuanzia 1949 mjini Dar-es-Salaam. Dr. Kyeruzi ameandika kwa makini historia hiyo.

Wewe Mohamed ni mkweli katika kunukuu historia sahihi.

Ajabu kwangu Mwalimu Nyerere naye hakutaka kuandika kuhusu historia hii, kwa mfano, Nyerere baada tu ya harusi yake Butiama alipitia Mwanza na kuonana na rafiki yake, Hamza Mwapachu ambaye alisafiri toka Ukerewe kuonana na Kambarage kwa mara ya kwanza baada ya kurejea kutoka Scotland masomoni.

Chief Abdallah Fundikira pia alikutana na Nyerere wakati huo.
Mazungumzo yao yalikuwa kumshawishi Nyerere kuongoza vita ya uhuru.

Wakati huo Edward Twinning alikuwa bado hajapiga marufuku watumishi wa serikali kujihusisha na siasa.

Lakini Twinning alitambua kwa haraka kwamba sera yake ya kuwapeleka uhamishoni mbali na Dar es Salaam wakina Hamza Mwapachu na Dr. Kyeruzi na hata Ally Sykes ilikuwa inashindwa kuzima uongozi wa siasa.

Hivi Msekwa hajui historia hii?
Na kwanini Nyerere hakutaka kuandika historia hii?

Katika mahojiano ambayo Nyerere kaweza kuongelea kuingia kwake katika siasa nasikitika kusema kwamba maelezo yake huwa mepesi au kijuujuu.

Nyerere alinipenda kama mwanawe hivyo siwezi kumlaumu.
Lakini hawa wengine kama Msekwa lazima tuwakosoe.

Wasipinde historia ya vita vya uhuru.

Nasikitika sana kwamba Hamza Mwapachu na Abdul Sykes walifariki mapema mno baada ya uhuru.

Hawa marafiki kama ndugu walikuwa hazina ya jinsi Tanganyika ilivyojiandaa na kujenga misingi ya vita vya huru.''


No comments: