Marehemu Suleiman Al Shukaili na Mohammed Ghassani |
Mauti ewe mauti, ukija kama hujaja
Huwa waja katikati, ya maisha yetu waja
Katikati ya wakati, na kati ya zetu haja
Na hata tukikutaja, wewe khabari hupati
Huwa waja katikati, ya maisha yetu waja
Katikati ya wakati, na kati ya zetu haja
Na hata tukikutaja, wewe khabari hupati
Nimepokea habari ya Kaka yangu, Mzee wangu, Muhisani wangu,
Sheikh Suleiman Al Shukaili, kuitikia wito wa Aitaye
akalazimika kuitikwa. Asubuhi hii karudi kwa Mola wake. Allah Ampokee ilhali
keshamsamehe makosa yake na aifanye pepo iwe nyumba yake. Amin Yaa Rabb.
Mtoto wake, Immu ShkellĂ˝, alinitumia picha hii hapa akaniuliza
ikiwa nimepata habari ya msiba. Nikamuuliza wa nani, akaniambia wa huyo
uliyenaye pichani. Ni takribani dakika 40 sasa, nami najiona kama siamini.
Kwa hakika, Oman imeondokewa, lakini imeondokewa pia Zanzibar.
Imeondokewa Pandani, ambako anajulikana kama Maalim Suleiman Shkeli. Hadithi
yake ya maisha yaliyokuja kuwa ya rubani na mwanaanga wa Oman mwenye mafanikio
makubwa ilianzia kijiji hiki ambacho mimi pia ninatokea.
Taswira ya kijiji hiki, hata harufu ya udongo wake, ninaamini
ameondoka nayo kwenda nayo kwa Muumba wake. Alikuwa kila mara ananisimulia
maisha yake ya huko, na hata alipokuwa akirudi kwa likizo kuwasalimia wazee,
ndugu na jamaa, alikuwa akinisimulia anavyoumizwa na hali duni ya maisha.
Kila wakati, licha ya kuwa kwake mtu mwenye mafanikio makubwa
kwa kila hali nchini Oman, roho yake iliishi Pandani. Mule mule mikarafuuni,
minazini, miembeni, mifuuni, mibungoni, na alikuwa haoni tabu kukiri hivyo.
Huyu ni mtu aliyeathirika sana na kulikozikwa kitovu chake.
Ni Pandani ndiko alikoanza kazi ya ualimu wakati mimi ndio
kwanza nazaliwa, na baadaye akahajiri kuenda Oman, ambako alisomea urubani na
kupanda cheo hadi kuwa mmoja wa marubani wa ndege za Mfalme Qaboos bin Said Al
Said. Akastaafu kwa heshima zote za kijeshi kama mwanaanga bingwa na mtaalamu.
Kisha akaendelea na shughuli zake za maisha. Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa
mkulima, kazi aliyoiinukia kwenye mabonde ya Msaani na Kijipu na Bibi Wa Tele.
Alinisimulia haya yote wakati nilipokutana naye mwaka jana miezi
kama hii nyumbani kwake, alikonialika rasmi.
Ukiangalia masafa baina yangu na yeye, unaweza kudhani kuwa
palikuwa na ukuta mkubwa baina yetu. Kwa vyovyote, mimi nilikuwa mdogo sana
kwake kwa kila jambo - umri, elimu, uzoefu, uwezo, haiba, na yote mengine. Mimi
nilikulia na kucheza na ndugu zake wawili wa mwisho - Hafidh na Ahmed.
Lakini masafa haya hayakuwa kitu kwake. Alikuwa mtu wa
kujishusha sana sana. Tangu aliponifahamu kupitia hapa ukurasa wa Facebook,
basi alinikurubisha kwake kwa hali na mali, kwa mawaidha na nasaha, na hata kwa
matani pia, kama vile tuko rika moja.
Alinialika mara kadhaa kwenda Oman kumtembelea, nami nikawa
sijapata wasaa, hadi mwaka jana nilipopata nafasi ya kwenda kuwasilisha mada
kuhusu Mchango wa Waomani kwenye Fasihi ya Kiswahili, naye alipofahamu kuwa
ningelikuwa na safari ya huko, akaniambia kuwa nisingeruhusiwa kuondoka bila
kufika kwake. Na ikawa hivyo, akanialika kwanza kwenye klabu yao ya wanajeshi
wa anga kwa chakula cha usiku, lakini akaona haitoshi. Siku nyengine akanialika
nyumbani kwake mchana mzima.
Nakumbuka takrima kubwa aliyonikirimu mimi na familia yangu.
Hata baada ya kurudi hapa Ujerumani, tukaendelea kuwasiliana. Mara ya mwisho
ikiwa ni siku tatu nyuma, ambapo alinijulisha kupitia kwa swahibu yetu wa
pamoja kuwa angekuwa na safari ya China. Na ni China, ambako roho yake asubuhi
hii imetenganishwa na kiwiliwili, akirudi kwa Mola wake.
Nimeanza andiko hili kwa ushairi. Ni kwa kuwa Maalim Suleiman
alikuwa shabiki mkubwa wa ushairi. Vitabu vyangu vyote vya ushairi aliviagizia
na nilipokwenda Oman nikamkuta tayari anavyo. Wakati mwengine alikuwa
akiniandikia ujumbe kwa kutumia beti zangu mwenyewe, au kujibizana nami kwa
beti za kishairi. Kwa hivyo, kadiri ya alivyokuwa Muomani na Mwarabu, huyu pia
alikuwa Mswahili na Mzanzibari. Na utambulisho huu ulikuwa umemganda nyama na
mfupa.
Ubeti huu nimaliziao hatausoma, kitabu changu kijacho, Mfalme
Yuko Uchi hatakipata, lakini wacha kauli yangu hii kwake ibakie:
Kake Selemani, moyo wanipwita
Kun'kwenda Sini, tiba kutafuta
Na kumbe Manani, ndiyo akikwita
Nawe kushamuitika!
Kun'kwenda Sini, tiba kutafuta
Na kumbe Manani, ndiyo akikwita
Nawe kushamuitika!
Kwa idhini yake Allah, awe amekuridhia amali zake zote za kheri,
na akuweke kwenye kundi la waja wake wema peponi!
Innalillah wainna ilayhir raajiun!
Mohammed
Ghassani
12 Aprili 2018
Bonn, Ujerumani
12 Aprili 2018
Bonn, Ujerumani
No comments:
Post a Comment