Yusuf Chembera Akiwa Mayor wa Lindi Town Council |
SHUKRANI
Ninatoa
shukrani kwa waasisi wa walioleta mabadiliko ya siasa katika sehemu za kusini
ya Tanganyika, Said Alley Mwalimu, Mohamed Ali Abdallah ‘’Makarios,’’ wote
wawili wanatoka Mikindani; na kwa Salum Mpunga na Yusufu Chembera kutoka Lindi.
Wote hawa sasa ni marehemu. Watu hawa wamenisaidia sana kwa kunieleza maisha
yao katika siasa wakati wa ukoloni katika majimbo ya kusini.
SALUM
MPUNGA NA YUSUF CHEMBERA
MARAFIKI
WAASISI WA TANU LINDI
Vita
vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza
Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa
kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana
bega kwa bega na dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi
ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislam wengi na vita
vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni
Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa
kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji
Maji. Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama
vita dhidi ya Ukristo. Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani
walifanya fisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha
kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao
walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina
yoyote ya kupinga ukoloni.
Kufuatia
historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya
utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipumbazwa kiasi
kiasi kwamba waliogopa siasa. Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali
za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo
kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na
Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na
serikali katili na ya kidhalimu ya Wajerumani. Vuguvugu la siasa kama
ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo
ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo
katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama
harakati nyingine za Waislam zilizowa zinakuja tena kwa mara ya pili kuvuruga
amani na utulivu. TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa
wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na
Wajerumani.
TANU
ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa zilipokuwa zikipanda pole
pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za Tanganyika, Jimbo la
Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi
katika zama za kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao,
daraja yao katika jamii na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale
mjini, walikuwa na nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya
TAA, uongozi wa TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU. Mtu wa kwanza
kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi yaliyokuwa yakitokea Tanganyika
na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah
Juma Makopa, kijana kutoka Tanga akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi.
Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANU mjini
Dar es Salaam na aliwashauri waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa
moja kwa moja na Mnonji, Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama
wengine wa TAA.
Chama
cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho
kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini
kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi,
Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea.
Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea
Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka 34 na
Mpunga alikuwa kijana wa miaka 27. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya
msingi na Mpunga alikuwa amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi
katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori
aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga
juu ya uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU
lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe
lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa
akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi
na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya
kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe
wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha
kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata
takriban wanachama kumi na tano walioridhia kujiandikisha kama wanachama
waasisi wa TANU.
Baada
ya kuandikisha wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare
Centre ambako ndiko alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa
ufupi wale wanachama wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya
cha siasa. Mkutano huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera
na Faraj ili kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini
Tanganyika. Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza
wakati kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima
ilikuwa ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale
vijana watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima
isajiliwe mjini Lindi.
Uchaguzi
ulifanyika na Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc
Kenzie, alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na
Idd Toto walichaguliwa wajumbe wa kamati. Ahmed Seif alikuwa kijana ambaye
ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba ya
uongozi. TANU mjini Lindi ilimwajiri ili
kukiandaa chama kiweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hassan Mohamed Kinyozi
aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa
kwanza wa TANU waliokuwa wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa
miongoni mwa wafanyakazi wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule.
Mnonji alitoa nyumba yake katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU
Jimbo la Kusini. Baada tu ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu,
kiongozi wa Lindi Dockworkers’ Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo
hili, kwa TANU lilikuwa la kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkers’ Union ilikuwa na wananchama wengi na hatua ile
iliongezea TANU nguvu.
Baada
ya muda mfupi tu toka kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa
mwaka 1955 ulifuatia. Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao
makuu ya TANU mjini Dar es Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano
huo na kukutana na Julius Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar
es Salaam. Mpunga, mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjawale
waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini. Halmashauri
ya TANU ya Lindi iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa makao makuu
ili Julius Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na wananchi na
kufanya kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na propaganda dhidi ya
TANU zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda.
Mponda akitumia uhusiano wake na serikali ya kikoloni na nafasi yake
kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala; na vilevile akitumia
ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa ambao bila shaka yoyote lilikuwa serikali
ndani ya serikali kule kusini, alikuwa ameanza kampeni yake ya kuipinga TANU.
Hili lilikuwa likiathiri msukumo wa uanachama. Mponda alikuwa mmoja wa wajumbe
waliotumwa na Gavana Twining kwenda Umoja wa Mataifa Februari, 1955 kwa niaba
ya serikali ya kikoloni kwenda kuipinga. Uongozi wa TANU huko Lindi ulitaka
Nyerere aende kupambana na Mponda akiwa katika uwanja wake mwenyewe, ndani
kabisa ya ngome ya Ukristo wa Kikatoliki katika Tanganyika.
Mkutano
mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es
Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye
tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma
Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha. Baada ya mkutano, wakati wajumbe
wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia
nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman
Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na
wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu
hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za
Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa
Tanganyika wasijihusishe na ‘’wafanya fujo wanaotaka kuzusha vurugu.’’ Twining
alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka
uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na
Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana
kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni
za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.
Wakati
huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye
ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki
zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU.
Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa
ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako
kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo
kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali
Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada
ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha
safari ya Nyerere. Ziara ya Nyerere
ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za
kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa
masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi
Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa
wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.
Nyerere
na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji
kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa
moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale
wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita,
hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya
TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori,
alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere
apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea
kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu
kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada
ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake
ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya
Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin
Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si
kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa
sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU
kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere
aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.
Kanisa
Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya
Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna
mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye
viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa
Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi
katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa
miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa
Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika
uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala
hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala
mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo
yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala
hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa
Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize
Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.
Jumapili
hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na
walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa
hii ‘’maalum’’ ilidumu katika fikra za
wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo
liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii
huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku
akiwa amesimamiwa na Waislam.
DC
mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa
amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi
uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda
kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja
ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana
Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere
alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika
historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali
pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine
wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili
kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari
waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa
TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai
uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba
ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi
kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.
Tangu
mwaka 1954 tetesi za chama cha siasa kilichoanzishwa Dar es Salaam kupigania
uhuru zilikuwa zimepenya na kufika Mikindani, mji mdogo kusini mwa Lindi. Huko
Mikindani kama ilivyokuwa mjini Lindi, harakati za utaifa zilianzia kwa wakazi
wa mjini, Wamakonde wengi wao wakiwa Waislam. Kinyume na imani ya watu wengi
kuwa Wamakonde ni wapagani, Wamakonde pekee waliokuwa si Waislam walikuwa wale
waliokuja kutoka Msumbiji, koloni la Wareno. Hawa ni Wamakonde waliovuka mto
Ruvuma kuingia Tanganyika kutafuta kazi katika mashamba ya mkonge kama manamba.
Uislamu ulikuwa umeimarika Kilwa na sehemu nyingine za pwani kwa zaidi ya miaka
elfu moja. Wamakonde wasio Waislam wanaweza kutambulika kwa chale walizochanja
katika nyuso zao na ndonya kwa wanawake wao. Wamakonde wa Tanganyika kutoka
Lindi, Mikindani na Mtwara katika mwambao wa ukanda wa pwani wa kusini ni
kabila la Waislam wengi. Wamakonde Wakristo wanatoka katika maeneo
yanayozunguka Masasi ambayo hadi sasa ni eneo la Wamishonari. Wamishonari wa
UMCA waliingia Masasi, nchi inayokaliwa na Wamakua na Wamakonde katika mwaka
1876.
Mikindani
haikuwa kama Lindi. Lindi ilikuwa kituo cha biashara na utawala wa kikoloni
katika Jimbo la Kusini. Lindi ilikuwa na uwanja wa gofu, sinema na kilabu
mahususi kwa Wazungu ambayo hakuna Mwafrika au Mhindi aliyekanyaga hapo bila
sababu ya maana. Lindi ilikuwa na barabara za lami na mitaa yake iliwashwa taa
usiku kuondoa giza. Kadhalika mji ulikuwa na idadi ya kutosha ya Waafrika
waliokuwa katika utumishi wa serikali. Wakati huo Lindi ilikuwa manispaa
iliyokuwa ikikua na yenye shughuli nyingi. Ikilinganishwa na Lindi Mikindani
ilikuwa kijiji kikubwa cha uvuvi kisichokuwa na mambo ya mjini na wakazi wake
bado walitumia taa za kandili. Si watu wengi waliokuwa wakihamia Mikindani
kutoka sehemu nyingine kuja kutafuta kazi. Uhamiaji wa watu kutoka sehemu
nyingine kuja mjini Mikindani ulikuwa katika kiwango cha chini sana. Watu pekee
waliokuja Mikindani walikuwa Wamakonde kutoka Newala na Masasi ndani ya
Tanganyika na wale kutoka upande wa pili wa mpaka toka Msumbiji. Hawa walikuja
kufanya kazi katika mashamba ya mkonge yaliyokuwa yakimilikiwa na ukoo wa
Karimjee. Hawa Wamakonde wahamiaji walikuwa wakidharauliwa na wenyeji na kwa
ajili hii Wamakonde wakiwa hawana dini walijitenga na wenyeji. Hakukuwa na
maingiliano baina ya Wamakonde kutoka koloni la Wareno la Msumbiji na Wamakonde
Waislam wa Tanganyika. Wakiwa mbali na nyumbani ambako maisha chiini ya Wareno
yalikuwa magumu sana hawa Wamakonde waliangukia chini ya ulezi wa Kanisa.
Ili
kuepuka mgongano na Waislam wamishonari walikuwa wamejenga kanisa kubwa sana
juu ya kilele cha mlima maili chache toka Mikindani sehemu moja ikijulikana
kama Mchuchu. Karibu na kanisa walikuwa
wamejenga shule ambayo Alfred Omari alikuwa akifundisha. Baba yake Alfred
alikuwa Mmakua Muislam lakini mwanae alibatizwa kwa ajili ya kupata elimu.
Inasemekana Mwafrika wa kwanza kusoma shule ya misheni kule kusini alikuwa
Charles Suleiman. Huyu alikuwa kijana wa Kiislamu aliyebatizwa na wamishonari.
Alikuja kuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu ualimu katika miaka ya mwishoni ya 1800.
Mbali
na changamoto hii kwa Uislamu kutoka kwa wamishonari, Mikindani ilibakia kuwa
chemchemu ya elimu ya Kiislamu. Mikindani ilijivunia mchanganyiko wa wanachuoni
wenye sifa kubwa ndani na nje ya Tanganyika. Elimu ya dini ya Kiislamu
ilifundishwa Mikindani na Sheikh
Suleiman bin Said na mdogo wake Ali, Wagunya kutoka Mombasa; Kenya; Sheikh
Saleh Maondoa kutoka visiwa vya Comoro; Sheikh Hassan bin Hassan Mchendange,
Mmakonde kutoka Mikindani; Sheikh Ahmed Mohamed Ghazal, Mwarabu kutoka Mombasa;
Sheikh Abdallah wa Mwalimu; Mohamed bin Abdallah na Sheikh Fumai bin Silim,
Mmakonde wa Mikindani. Kutokana na hawa usufi uliota mizizi na tariqa za
Kadiria na Shadhly zilidumu katika sehemu zote za Waislam huko kusini. Kadiri
miaka ilivyopita wenyeji wa sehemu zile za kusini, Wamakonde, nao wakaipata
elimu hii ya Kiislam kutoka kwa wageni na mabadiliko haya yalikuja kukutana na
kuibuka kwa harakati za kudai uhuru mara baada ya Vita Kuu ya Pili.
Wanachuoni
wa Kiislamu mjini Mikindani hawakuwa wakipendeza machoni mwa Waingereza kama
vile walivyokuwa hawapendezi kwa Wajerumani. Mbali na chuki dhidi ya utawala wa
kikoloni kufuatia Vita Vya Maji Maji, Waislam walikuwa na chuki zao binafsi
dhidi ya Waingereza kutokana na amri waliyotoa ya kumfukuza mwanachuoni
mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Abdallah wa Mwalimu. Sheikh Abdallah aligombana
na Waingereza juu ya jambo la akida na uadilifu. Sheikh Abdallah alikuwa liwali
akihukumu kwa mujibu wa sharia za Kiislam pale Mikindani. Katika wadhifa huu,
afisa wa kikoloni aliamuamuru kutekeleza wajibu ambao Sheikh Abdallah
aliuchukulia kuwa ulimvunjia hadhi yake, heshima na itibari kwa Uislamu. Sheikh
Abdallah, kutokana na ugomvi huu, alihamishiwa Kondoa Irangi, sehemu yenye
Waislam watupu katika Tanganyika, jimbo la kati. Sheikh Abdallah aliishi Kondo
Irangi katika miaka yake ya mwisho na kufariki huko. Waislam mjini Mikindani
hawakuweza kuwasamehe Waingereza wala kusahau ule udhalimu dhidi ya Sheikh
Abdallah. Mwanae, Sheikh Mohamed bin Abdallah wa Mwalimu aliitwa kutoka Lindi
kuja kuongoza Tariqa ya Kadiria mjini Mikindani baada ya kifo cha baba yake.
Mohamed bin Abdallah, alisoma elimu ya Kiislamu mjini Kondoa. Mjini Lindi
alianzisha zawiyya, akahuisha Tariqa ya Kadiria na akawa na madras yake
mwenyewe. Alipofariki Sheikh Suleiman bin Said na mdogo wake, Mikindani,
nyumbani kwa Sheikh Abdallah wa Mwalimu kukawa hakuma khalifa wa kuongoza
tariqa. Hatua ya Sheikh Mohamed kuja Mikindani ilisadifiana na kuibuka kwa
TANU. Sheikh Mohamed akiwa khalifa wa Kadiria na murid wake ndiyo walikuwa watu
wa kwanza kujiunga na TANU pale Mikindani.
Tukio
dogo la kiburi cha askari mpumbavu wa mkoloni ndiko kulisababisha watu wa Mikindani
wafungue tawi la TANU. Askari mmoja mpita njia aliingia katika ubishi na kijana
mmoja wa pale mjini, akiitwa Hassan Masudi Vuni. Akitumia mamlaka yake ya
kukamata mhalifu, askari huyo alimpiga Vuni kwa kumuonea. Miongoni mwa
watazamaji wa tukio hilo alikuwa Rashid Ali. Rashid Ali alikwenda kusimulia
tukio hili kwa Mohamed Ali Abdallah. Alipokuwa akisimulia mkasa ule, pamoja
naye alikuwa Suleiman Hassan Msepele. Walipokuwa wakijadiliana Msepele alitamka
kwamba tukio kama hilo kamwe lisingeweza kutokea Dar es Salaam kwa sababu
Mwafrika mmoja kwa jina lake Julius Nyerere alikuwa ameanzisha chama cha siasa
kupigania uhuru. Rashid Ali na Mohamed Ali Abdallah walitamani kujua mengi
zaidi kuhusu Mwafrika huyu aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nyerere na chama
chake cha siasa, lakini Msepele hakuwa na mengi ya kueleza kuhusu Nyerere na
chama chake. Kwa hiyo basi, hawa watu watatu waliamua kumtuma mtu Dar es Salaam
kupata habari zaidi kuhusu chama hicho. Mohamed Ali aliandika barua na kumpa
Msham Awadh na Ali Muhidin kumpelekea Nyerere. Ndani ya barua hiyo Mohamed Ali
alimweleza Nyerere kwamba ukoloni ulikuwa bughudha kubwa katika Jimbo la
Kusini, na wangependa kufungua tawi la TANU mjini Mikindani ili kupigania
uhuru.
Mwaka
1955 Mohamed Ali alikuwa na umri wa miaka 45. Alikuwa hana elimu kama elimu
inavyojulikana kwa kuwa hakusoma shule yoyote. Alipokuwa kijana mdogo baba yake
alimpeleka Zanzibar kusoma elimu ya dini. Wakati huo Zanzibar ilikuwa ndiyo
kitovu cha elimu ya Kiislamu. Huko Zanzibar kijana Mohamed Ali alisoma kwa
Sheikh Mohamed L’ Khamus. Kisha aliendelea na masomo yake mjini Dar es Salaam
kwa Sheikh Wazir bin Said, mwanafunzi wa Sheikh maarufu sana na aliyekuwa
khalifa wa Tariqa ya Askariyya, Sheikh Idrissa bin Saad. Baada ya kumaliza masomo
yake mjini Dar es Salaam alisafiri hadi Belgian Congo na halafu alirudi Ujiji
nchini Tanganyika kufanya biashara ndogo ndogo. Katika mwaka 1947 alirudi Lindi
na kutoka hapo alikwenda Mikindani na kuwa fundi cherahani.
Msham
Awadh alikuwa akijulikana Lindi nzima na Mikindani kwa sababu ya biashara yake.
Mshama Awadh alikuwa alikuwa muuza uzuri, yaani vitu vya urembo kama vile
uturi, dalia, marashi, rangi na manukato mengine kwa wanawake wa hii miji
miwili. Alikuwa akiuza bidhaa zake kikapuni akipita nyumba hadi nyumba. Hawa
walikuwa ndiyo aina ya watu walioanzisha na kuongoza harakati za kumaliza
utawala wa kikoloni. Hawakuwa wajuzi wa lugha ya Kiingereza wala hawakuwa na
ujuzi wa maisha ya ulimwengu wa kimagharibi kama walivyokuwa baadhi ya Waafrika
wengine waliyopata elimu ya kimagharibi. Msham Awadh na Ali Muhidin walikwenda
hadi Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Rupia, Chamwenye, Kambona na Dossa
katika makao makuu ya TANU, New Street. Msham Awadh na Ali Muhidin walipewa
kadi za TANU na wakaambiwa wafungue tawi Mikindani. Wakati Msham Awadh na Ali
Muhidin wakiwa njiani kwenda Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Mohamed Ali
alisafiri kwenda Lindi kukutana na Mnonji na kumweleza kuwa Mikindani walikuwa
wamekusudia kufungua tawi la TANU. Mnonji alimpa kadi Mohamed Ali na akawa
mwanachama na akamwambia arudi Mikindani na kuanza kufanya kampeni kwa nguvu
kwa ajili ya TANU na awafahamishe watu kuwa Nyerere yupo njiani kuja Jimbo la
Kusini.
Julius
Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi
siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote
waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza
Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo,
aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na
ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na
ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka
yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi
aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa mwa
karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi
la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua
mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo.
Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya
Waingereza. Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza
waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo
ilibidi itaifishwe. Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye
kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.
Utawala
wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati
ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu
cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika
majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.
Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka
alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam.
Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake. Nyumba hiyo
ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi,
usiku Nyerere aliitisha mkutano na wanachama kama thelathini hivi walihudhuria.
Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali
ya siasa kwa ujumla mjini Dar es Salaam. Nyerere aliwahakikishia waskilizaji
wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika
uhai wao.
Siku
iliyofuatia mkutano wa hadhara ulifanyika mjini Mikindani mahali palipojulikana
kama Jangwani, karibu na ufuko wa Bahari ya Hindi. Mkutano huu uliohudhuriwa na
watu wengi na uliendelea bila mushkeli wowote ukitoa kitendo kidogo
kilichofanywa na mwalimu mmoja wa shule, Abdulrahman Muhibu aliyekuwa amelewa.
Muhibu alikuwa ametoka kunywa pombe na alipita karibu na uwanja wa mkutano
ambapo Nyerere alikuwa akihutubia. Katika hali yake ya ulevi alimpigia kelele
Nyerere akamwita muongo. Huenda Muhibu alikuwa akifahamu vyema ujumbe wa Nyerere,
na akiwa vile alivyokuwa, mtumishi wa serikali na mlevi, aliona wazo la mwalimu
wa shule Mwafrika kama yeye kuwaongoza watu hadi uhuru upatikane ni jambo
lisilowezekana. Kwa haraka Muhibu alikamatwa na watu na ilikuwa karibu wamtie
adabu ndipo Nyerere alipoingilia na hivyo kumnusuru.
Jioni
hiyo baada ya mkutano Nyerere na ujumbe wake waliondoka kwenda Newala, kwenye
ngome ya Yustino Mponda. Mponda alikuwa mmoja wa wale wajumbe wa Baraza la
Kutunga Sheria waliosafirishwa na Gavana hadi Umoja wa Mataifa, New York,
kumpinga Nyerere. Sasa TANU ilikuwa ikichukua mkokoto wake wa kampeni hadi
ndani ya ardhi ya Mponda ambayo yeye alikuwa liwali na mjumbe wa Baraza la
Kutunga Sheria. Nyerere alipomaliza ziara yake ya Jimbo la Kusini, fikra za
Wakristo zilibadilika. Wakristo hawakuamini tena kuwa TANU ilikuwa harakati za
Waislam sawasawa na Vita Vya Maji Maji. Nyerere, Tambwe na Diwani walipokuwa
wanashika njia kurudi Dar es Salaam, matawi ya TANU yalikuwa yamefunguliwa
Masasi, Ndanda na Newala ambazo zilikuwa sehemu za Ukristo na ngome ya
Ukatoliki katika Tanganyika.
Nyerere
aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu sana na ilikuwa imekumba
kila mtu. Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo, walio kuwa
wakiibeza TANU mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Waislam ëwasiokuwa
na elimu,í ukweli ulikuwa umewadhihirikia na sasa walikuwa wakionyesha heshima
kwa chama. Hawakuwa na khiyari na ilibidi waonyeshe heshima kwa sababu bwana
mwenyewe, yaani serikali ya kikoloni, ilikuwa na heshima kwa TANU. Serikali
ilikuwa imetambua kuwa dhamiri ya watu ya kukataa kutawaliwa haiwezi tena
kupuuzwa. Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa
mara mbili, mara ya pili ikiwa mwaka 1957. Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa
Tanganyika walikuwa tayari kujitawala. Kila siku zilivyopita ndivyo TANU
ilivyopata nguvu. Rashidi Salum Mpunga, dereva wa lori, aliweza kumshawishi na
akafanikiwa kumuingiza TANU mmoja wa masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini
Lindi na mshairi maarufu, Sheikh Mohamed bin Yusuf Badi. Sheikh Badi alipoingia
TANU kwa ajili ya heshima yake na kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam
walimfuata na kukata kadi za TANU. Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la
kura tatu na uongozi wa Jimbo la Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere
na madras yake, wanafunzi wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu. Kuanzia
hapo sasa kila mtu alijiunga na TANU. Si Mponda wala Kanisa lilikuwa na uwezo
wa kupambana na TANU kwa wakati ule. Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU
ilingia ndani ya maeneo ya Kikristo huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala,
nyumbani kwa Yustino Mponda.
Lakini
matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika safari ya pili ya Nyerere
alipozuru tena Jimbo la Kusini. Kumbukumbu ya kwanza ilikuwa tawaswil aliyosomewa
Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na Waislam aliowachagua yeye
sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na waliochaguliwa na masheikh
wengine.Kumbukumbu ya pili ni ile karamu
iliyoandaliwa kwa heshima ya Nyerere na Mussa Athumani Lukundu, kiongozi
wa Dockworkers’ Union. Hii ilikuwa heshima kubwa aliyoonyeshwa Nyerere, ilikuwa
kilele cha upendo na heshima kwa Muislamu yoyote anaweza kumfanyia asiyekuwa
Muislamu.
Siku
ya ukumbusho mkubwa sana mjini Lindi ilikuwa siku ya uhuru, tarehe 9 Desemba,
1961. Sheikh Badi, bingwa wa mashairi, aliombwa na TANU kuandika hotuba ya
uhuru itakayotolewa na Yusuf Chembera mbele ya DC akiwa kama mwakilishi wa
utawala wa Kiingereza uliokuwa uking’oka. Hotuba hiyo ya Sheikh Badi na
iliandikwa kwa Kiarabu na Chembera. Akiwa mtoto mdogo Chembera alipelekwa kwa
Sheikh Yusuf Badi na baba yake kwenda kusoma elimu ya dini na aliendelea kuwapo
hapo chuoni kwa Sheikh Badi hadi alipohitimu. Sheikh Badi hakuona kama ipo
hotuba yoyote iliyoandikwa na mwanadamu iliyostahiki hafla kama ile ya siku ya
kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni. Sheikh Badi alimsomea mwanafunzi wake
Chembera, dua ya kunut ambayo husomwa na Waislam katika kila sala ya alfajir.
Usiku wa manane wa tarehe 9 Desemba, 1961 ulikuwa usiku adhim sana kwa wote
wawili, mwalimu na mwanafunzi wake, pale watu walipokusanyika katika ule uwanja
wa gofu na kumsikiliza Chembera akisoma kunut kupokea uhuru wa Tanganyika.
Lakini mara tu baada ya uhuru Wakristo walianza kuuchimba ule waliouona kuwa
uongozi wa Waislam katika TANU kwa kisingizio kuwa uongozi ule haukuwa na
elimu. Suleiman Masudi Mnonji alikamatwa na kutiwa kizuizini kwa amri ya
Nyerere chini ya Preventive Detention Act ya mwaka 1962 kwa kile kilichoitwa
‘’kuchanganya dini na siasa,’’ na Waislam wengine waanzilishi wa harakati za
kudai uhuru walitupwa nje ya uongozi.
No comments:
Post a Comment