Shajara ya Mwana Mzizima
KUVUNJIKA KWA JUMUIYA EAC NA ATHARI ZAKE – III
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Maandamano ya kudai mafao ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki |
Raia Mwema Aprili 2-3, 2018
SASA ni
dhahiri Jumuiya ile maridadi ilivunjwa na wenye mali yao (Kenya, Uganda na
Tanzania) kama ambavyo tumeona kwenye makala iliyopita, huku kila mmoja
akijaribu kujifanya yeye hakuhusika na uvunjifu ule, lakini ukimwuliza; je,
kama hukuhusika, ulichukua hatua gani kuinusuru? Jibu atakuwa hana hata chembe.
Kwa upande wa
Tanzania, kama ilivyokuwa kwa wenzetu wale wawili, haraka haraka tulijipanga
upya kuyasimamisha tena mashirika yale ili mambo yaende kama mwanzo maana
huduma zake zilikuwa za lazima mno zisizoweza kukosekana.
Naam, kwa
msaada mkubwa wa kifedha kutoka serikalini (hasara ya kujitakia), mashirika
yale yalirejea upya baada ya muda mfupi tu, kwa sababu waliokuwa wafanyakazi
wake walikuwa na ujuzi, uwezo, weledi, nia pamoja na uzalendo wa hali ya juu na
hivyo kuazimia kwamba ‘hatutoiangusha’ nchi yetu kwa kushindwa kutoa huduma
zile.
Kila shirika
na kila idara, watu walijipanga wakaunda ‘task forces’ za kutengeneza upya
ofisi zao. Alhamdullilah! Tulifanikisha jambo hilo kwa mafanikio kabisa.
Shirika la Ndege likaundwa, tena zuri tu likawa chini ya Meneja Mkuu (General
Menager), Jaji Yahya Rubama (sasa marehemu) ambaye alikuja na uzoefu mkubwa wa
kiuongozi kutoka Shirika la Ndege la EAAC alikokuwa mwanasheria wake mkuu
(Company Secretary).
Sasa ndege
tulizipata wapi? Ndege mbili tatu za EAAC zilikuwapo hapa nchini wakati Jumuiya
ilipokufa, na ndugu zetu Msumbiji wakatuazima ndege kiasi nne hivi, maana wao
walikuwa ndio kwanza wanapata uhuru na walikuwa na vitu vyote hivyo
walivyoachiwa na Wareno.
Air Tanzania,
ikawa angani bila taabu maana marubani wa Ki-Tanzania — tena kwenye ngazi ya ukepteni— na wafanyakazi wengine wazoefu kwenye idara
tofauti za EAAC walikuwapo wa kutosha na kusaza.
Hivyo hivyo
watu wa Posta wakaunda shirika jipya; wakajenga na Chuo cha Posta na Simu
(majengo ya chuo sasa tayari yameuzwa) pale Kijitonyama, mjini Dar es Salaam.
Mzee Rajab Yusuf akawa ndiye mkuu wake wa kwanza.
Watu wa
Bandari na wao halikadhalika wakaunda Shirika la Bandari jipya wakaendeleza
kazi kama kawaida, Mzee Bakilana akawa Mkurugenzi Mkuu. Chuo cha Bandari cha
Ki-Tanzania (Bandari College) kikaanzishwa pale Temeke, karibu na Mwembe Yanga
hapa jijini.
Idara ya Ushuru
na Forodha ikahamishiwa Hazina, pale katika Wizara ya Fedha, nao wakawa
wanaendelea na kazi huko. Kazi za pale zinafanana fanana na za kwao hivyo
haikuwa tabu kubwa.
Watu wa iliyokuwa
EARC (Reli) nao walijipanga vizuri wakatengeneza kitu safi kabisa wakiongozwa
na watu mashuhuri wa mambo ya reli wakati huo akina Mzee Mtambalike, Juma Lweno
na nduguye Hussein Lweno, na Juma Shamte (aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga). Treni zikawa zinakwenda
na kurudi kama kawaida; wakati chuo kidogo cha Reli pale Tabora nacho kikawa
kinatoa wafanyakazi wapya kila kukicha.
Idara ya
Usalama wa Anga (Civil Aviation), ikaundwa pia chini ya Mkurugenzi wake mkuu
Lot Mollel, akisaidiwa kwa karibu na kina Mahmuud Shamte, Charles Newa, Dk
Charles Mgana, Dk Jaafar Mpilli na Dk Mworia. Waliiunda idara ile nyeti
inayohitaji utaalamu mkubwa ikawa safi sana baada ya kazi nzuri iliyofanywa na
Kikosi Kazi (task force) kilichosheheni wataalumu bobezi wa masuala ya Safari
za Anga (Air Navigational Services).
Mwandishi
huyu, akiwa mfanyakazi mwandamizi pale Civil Aviation, kwenye Uwanja wa Ndege
wa DIA wakati huo (Terminal One), ni shuhuda wa jinsi watu walivyoharakisha
kurudisha huduma zile muhimu kwenye taifa letu. Baadaye kidogo, pale Uwanja wa Ndege
wa DIA ulipohamia Terminal Two, na kwa kutumia maofisa wake wazoefu kikaanzishwa
chuo cha Civil Aviation Training Centre (CATC), kikawa kinatoa maofisa wa
uongozaji safari za anga na mainjinia wa mitambo pamoja na rada wa kiwango cha kimataifa.
Wataalamu wengine ilibidi wakasome zaidi kwenye Chuo cha Civil Aviation kule
Toulouse Ufaransa kilichojulikana kama L’ENAC na wengine kule Cairo, Misry.
Idara ya Hali
ya Hewa (Meterological Department) nao wakapewa nafasi kubwa pale Jumba la
Customs, mtaa wa Sokoine, wakaweka mitambo yao na kuanza kazi kama vile hakikutokea
kitu chochote. Mkurugenzi Mkuu akawa Bingwa wa kutabiri Hali ya Hewa hayati Mzee
Lifiga. Taarifa muhimu za hali ya hewa zikawa zinatoka kwenye viwanja vya ndege
mbalimbali kote nchini kwa ajili ya safari za ndege, meli, uvuvi na kilimo.
Mashirika
yale yakawa yanapiga hatua na kuishauri serikali kila inapobidi ni kwa namna
gani inaweza kuyaendeleza ili yasiyumbe. Amini usiamini, kule Serikalini
hapakuwapo na watu waliokuwa wakielewa vyema namna mashirika yale ya EAC yalivyokuwa
yakijiendesha. Nadhani ingekuwa ‘majanga mkubwa’ kama si uzalendo na moyo wa
kujitolea waliokuwa nao wazee wale waliotoka EAC wakaiundia nchi yao huduma
zile zikasimama dede halafu wima.
Kama kawaida
yake kiutendaji, Serikali hii ya kwetu ikawa na uzito kwenye suala la ajira. Watendaji
wake wakuu wakaanza kidogo kidogo kuleta roho mbaya ya ‘korosho’ na ‘kwanini’.
Wakati
wenzetu wa Kenya wakiwa wamepata ajira zao moja kwa moja kwenye serikali yao
wakiwa na mwendelezo uleule (continuation of service) kama vile hakikuvunjika
kitu; Tanzania wakakataa hilo na hivyo kuwataka watu waajiriwe upya huku miaka
yote ya utumishi EAC ikawa imepotea pale June 30, 1977 ilipotamkwa rasmi
Jumuiya ile imekufa.
Watanzania, wakasahau
kwamba sisi kule EAC, tulikuwa kama vile tunawawakilisha Watanzania wengine.
Katu hatukujipeleka wenyewe; tukawaacha ndugu na jamaa zetu wakiwamo wazazi
tuliowapenda na kwenda kuishi sehemu za mbali na kwetu tukiweka maslahi ya
taifa mbele.
Wakubwa wale wakagoma, wakisisitiza ‘yale ya
kule yamekwisha, hapa mtaanza upya’. Kwa hali hiyo wapo waliopoteza miaka mpaka
25; wapo wa 20, 15, 10 na wengine sisi tuliokuwa na miaka chini ya 10 iwe
imekwenda tu kipuuzipuuzi. Uko wapi utu hapo? Yako wapi hapo majigambo yetu ya,
eti, Watanzania tu wakarimu!
Hata pamoja
na hali kuwa hivyo, hapo nako kukawa na figisufigisu nyengine zisizokwisha;
mikataba ya ajira ikawa haitoki pia. Kila mara walipotoa barua za ajira, basi
hazipiti siku mbili wanarudi mbio ‘ah! Rudisheni zile barua zina makosa
makubwa’. Ingawa kila mwezi tuliweza kupata mishahara ileile tuliyokuwa
tukipata katika utumishi wa EAC, lakini tukabakia hivyo nenda rudi; nenda rudi
bila ajira.
Sasa uzalendo
ukawa basi. Sisi wa Civil Aviation katika viwanja vya ndege hali ya kufanya
kazi namna ile ilikuja kutushinda pale tulipoona mtu amekufa kazini na hakuwa
anapata chochote kwa sababu Hazina hawana rekodi yake ya ajira na Mafao ya EAC
hayajulikani yalipo.
Nitatoa
mfano; siku moja watu walikuwa wanarudishwa nyumbani usiku baada ya kutoka
kazini. Gari, mali ya Serikali ya Tanzania, lilipata ajali wakafa watu watatu na
wengine wakaumia, kwenye makutano ya Barabara ya Shauri Moyo na Uhuru hapa
jijini. Waliofariki ni Waongozaji Safari za Anga (ATCOs), Kapela, Alibhai na
dereva wao Maliki Chumu (Mungu awarehemu walipo).
Serikali
iligoma kutoa malipo hata senti tano kwa familia zao, kwa kudai kwamba wale
hawakuwa wafanyakazi wa serikali bado. Hawakuwa na mafaili Hazina, hivyo basi wakaambulia sanda na ubao siku ya
mazishi.
Watu
wakaingiwa na wasiwasi, wakiwazia itakuwaje mtu mwengine akifa kesho yake?
Tukawatisha Serikali kwamba tutaweka nyenzo chini (tutagoma) ifikapo tarehe fulani
kama watakuwa hawakutupa ajira stahiki. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano na
Uchukuzi wakati huo Agustine Mwingira, aliogopa sana na akapewa maagizo na
serikali kumalizana na suala hilo haraka.
Alitukimbilia
mbio na kutubembeleza kwamba tumpe wiki mbili atakuwa keshamwajiri kila mmoja
na huku akiahidi nyongeza na marupurupu kibao. Ajira ilirudishwa nyuma
(retroactive) ikaanzia Julai 1,1977, ingawa barua zenyewe zilitoka 1984 hivi.
Wakati
huohuo, Benki ya Dunia chini ya Msimamizi wa Mirathi ile ya EAC, Dk Victor
Umbritch ilikuwa imemaliza kazi yake ya kulipa madeni na kugawa mali za
iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki, kwa kutoa ripoti ndefu iliyojulikana kama
‘East African Community Mediation Agreement 1984’.
Dk Umbritch,
aliikabidhi mwenywe ripoti yake kwa marais Nyerere, Moi na Obote wakati huo
akimwendea kila mmoja nchini kwake.
Ndani ya
ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine, imeonyesha mgao mzima wa mali na
rasilimali za iliyokuwa EAC, kwa kueleza nani anapata nini na kiko wapi.
Imeelezwa vilevile nani kumfidia nani kwa yeye kupata kitu kikubwa labda.
Vilevile
ripoti ile imeeleza kwa ufasaha kabisa hesabu zote za malipo ya ‘mirathi’ kwa
waliokuwa wafanyakazi wa EAC. Ile ilikuwa ‘mirathi’ hayakuwa mafao kama
inavyoelezwa na wasiofahamu au viongozi wababaishaji kwa njia za kutaka kufanya
dhulma.
Mafao
hutolewa kwa mtu aliyestaafu, kufukuzwa au kuachishwa kazi. Kwa muktadha wa
EAC, ni yeye ndiye aliyekufa au kukatisha mikataba ya watu ambao alikuwa awe
nao mpaka watakapostaafu. ‘East African Treaty of Coorporation’ au mikataba tu
ya mfanyakazi mmoja mmoja ndani ya mafaili, inamtaka kulipa mambo mengi ya
ziada zaidi ya hayo mafao au ile inayoitwa mikono ya kwaheri ‘hand shake’ kwa
kule kufa kwake au kuvunja mkataba makusudi. Sasa ‘wajanja na wajuaji
serikalini’ walitulipa sisi nauli na hiyo ‘handshake’ (vocha zao za malipo
zinaonyesha hivyo), wakapiga kelele nyingi ‘tumewalipa Sh bilioni 117’ kama
vile hela za mgao wa jangusho la nazi, faida ya kuuza korosho au mgao wa pesa
za sanda msibani.
Pia,
Watanzania wenzangu ni muhimu ieleweke hapa mikataba ya kufanya kazi katika EAC
ilikuwa ya kimataifa na wala haikuhusu nchi wanachama. Barua za ajira zilitamka
wazi kwamba unaajiriwa kazi kadhaa; kwa mshahara kadhaa ambao utalipwa kwa
Sterling pound ya Uk kadhaa kwa mwezi—kamwe haikuwa kwa shilingi ya Kenya,
Uganda au Tanzania. Kwenye EAC hiyo ilionekana kama ‘pesa ya madafu!’
Nchi zote
wanachama zilitakiwa kuufanya mkataba wa Umbritch sheria ya Bunge baada ya
kuutia saini ukiwa kamilifu kama ulivyoletwa. Hapa Tanzania ilipofika mwaka
1987 walipeleka bungeni mkataba uliojulikana kama East African Community
Mediation Aggrement Act no 2 of 1987, na ukawa sheria ya nchi baada ya kuwekwa
saini na Rais Ali Hassan Mwinyi wakati huo.
Sasa
kilichotokea hapa kwetu ni kwamba Serikali yetu, ikiwa na nia isiyo nzuri
ilivitoa vipengele kadhaa ndani ripoti ile ili iwezekane kufanya ‘figisufigusu’
katika malipo ya watumishi ambapo ripoti ilielekeza namna ya ulipaji wake.
Ukiangalia
EAC Mediation Agreement ya Umbritch na EAC Mediation Agreement Act no 2 ya
Kenya 1987, kwa upande mmoja halafu uweke ya Tanzania kwa upande wa pili, basi
utaona vipengele saba (7) vilivyomo ndani ya ripoti mama humu havimo— (Articles
1,2,6,7,13,16,17 na 18).
Subhannallah!
Hivyo ndivyo ilivyofanya Serikali kwa wazee wastaafu waliolitumikia taifa lao
na kulijenga upya wakati ule wa shida. Zile sehemu zote zinazohusu namna ya
kukokotoa fedha na iwe kwa sarafu gani (imeelekezwa dollar ya Kimarekani) wao
wanasema uongo hamna kumbe wamenyofoa! Huku wakija na kelele nyingi za kukwepa
kulipa, eti ‘… mheshimiwa Spika wale wazee walikuwa vibarua tu serikali ndio
imewaonea huruma ikawalipa …hawakustahili kitu,”
Ah! Hebu
msalieni mtume nyie Watanzania au ombeni maji mnywe kwanza; hivyo kazi zile za
mashirika yale ya kitaalamu ya Ndege, Posta, Bandari, Customs, Uongozaji Ndege,
Hali ya Hewa… mnayaita ya kibaruabarua!
Msomaji
ripoti zote za EAC Mediation Agreement zinapatikana kwenye mtandao. Tembelea
google halafu andika: East African Community Mediation Agreement 1984 utapata
ya Dk Umbritch; na ukiitaka ile ya Tanzania iliyochakachuliwa, tembelea google
halafu andika: East African Community Mediation agreement Act No 2 1987.
Halikadhalika fanya hivyo ukiitaka ya Kenya uone tofauti.
Tatizo
lililopo mpaka sasa kuhusu malipo yale ni kuhusu thamani ya pesa (real value
and compound interest). Hii imeelezwa waziwazi ndani ya article 1(n), ambayo
ripoti ya Tanzania imeondoa! Umbritch kaandika ‘7% compound interest’ wao
wanalipa ‘15% simple interest’. Ni hesabu mbili zenye majawabu mawili tofauti
hizo. Mko wapi wasomi mtusaidie hili Babu na Baba zenu tumedhulumiwa; mko wapi?
Tusaidieni;
msiwe, kama wale wanaoshangilia na kufurahi wanapoona wazee wakipigwa mabomu na
kumwagiwa maji ya upupu wanapodai haki yao?
Tukutane
Jumatatu ijayo.
Simu:0715808864
No comments:
Post a Comment