Thursday 19 April 2018

Sheikh Yahya Hussein: ‘Mjawiid’, Mnajimu, Tabibu na Mtabiri bingwa Africa Mashariki - Sehemu ya Kwanza na Alhaji Abdallah Tambaza


Shajara ya Mwana Mzizima
Sheikh Yahya Hussein: ‘Mjawiid’, Mnajimu, Tabibu na Mtabiri Bingwa Africa Mashariki 
Sehemu ya Kwanza

Na Alhaji Abdallah Tambaza

Sheikh Yahya Hussein
Raia Mwema 20 - 22 April 2018

NIANZE kwa kuwashukuru wale wote waliofanya mawasiliano na mimi baada ya kusoma zile makala nne zilizopita kuhusu kuvunjika kwa EAC ya zamani na athari zake kwa nchi wanachama. Nimefarajika sana na nasema ahsanteni sana.

Jumatatu ya leo, Shajara inamwangazia Mwana Mzizima mwengine aliyeaga dunia takriban miaka 7 iliyopita, na ambaye ametoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Sheikh Yahya Hussein Juma Karanda, aliyefariki dunia mnamo Mei 20,2011 alikuwa na maarifa na akili nyingi mno, hivyo akawa gwiji na bingwa kwenye tasnia mbalimbali alizozipitia katika uhai wake. Sheikh Yahya alikuwa mjawiid (msomaji Qurani maarufu duniani wa kiwango cha kimataifa); mwanasiasa aliyepigania uhuru wa taifa letu; gwiji wa utabiri wa kutumia nyota; tabibu wa kutumia vitu vya asili na  pia alikuwa mwalimu wa madrassa na shule pia.


Kulia Sheikh Hussein Juma na Sheikh Hassan Juma

Babake Sheikh Yahya, alikuwa Mzee Hassan Juma, lakini Sheikh Yahya yeye alikuwa akitumia jina la babake mdogo Sheikh Hussein Juma, ambaye ndiye aliyemlea na kumwongoza kwingi kwenye safari yake ndefu ya maisha hapa duniani.

Habari zinasema, familia hii ya kina Sheikh Yahya na baba zake, ilihamia hapa Mzizima miaka mingi nyuma, wakitokea Bagamoyo ambako walikuwa wakifundisha watu elimu ya dini ya Kiislamu. Kutokana na umahiri na uhodari wao katika ufundishaji, watu wa Mzizima wakati huo - kwenye karne ya 18 hivi - akiwemo Mzee Mussa Pazi na Mzee Abeid Mwinyikondo Uweje - waliwaendea na kuwaomba wahamie hapa ambako kulikuwa na uhaba mkubwa wa walimu wa madrassa wa kiwango kile.

Walikubali na wakaanzisha madrassa iliyojulikana kama Al-Hassnain Muslim School pale Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo na ikawa madrassa ya mwanzo jijini iliyokuwa ikitoa elimu hiyo na ile ya ‘kisekula’ huku wanafunzi wakiwa wamekaa juu ya madawati. Madrassa hiyo ilikuwa imesomesha vijana wengi wa hapa jijini wakati huo, ambao walipojiunga na shule zile za serikali walikuwa wakishika namba za juu madarasani.

Mzee Ibrahim Abeid Uweje, akinisimulia habari za Al-Hassnain, anasema yeye na kaka zake Abdulkheir na Abubakar, walisoma hapo na alishuhudia hata mchezo wa mpira wa miguu ukifundishwa pale chuoni wakati huo.

“Pale Al-Hassnain tulikuwa tunafundishwa mpaka kucheza mpira, na hayati Sheikh Yahya ndiye aliyekuwa kocha na ndiye aliyenifanya mimi niwe golikipa,” alisema Mzee Uweje.

Madrassa nyingine ambazo zikitoa wachezaji mpira mahiri wakati ule ni pamoja na ile ya Maalim Mzinga & Sons, ambapo walimu wake watatu walikuwa wakicheza mpira wa kiwango kikubwa - Maalim Abbas Mzinga alikuwa mchezaji wa timu ya Tanganyika iliyochukua Gossage Cup 49; Maalim Mambo Mzinga akichezea Sunderland (Simba sasa); Juma Mzinga aliyechezea Yanga; Mwlimu Tumu Ramadhani (kocha New Style na baadaye Yanga katika miaka ya 1960s na hayati Juma Mzee aliyekuwa mchezaji na mwalimu wa klabu ya Sunderland. Hapa pia elimu ya kisekula ilikuwa ikitolewa. Mwandishi huyu alipata elimu ya dini ya Kiislamu chuoni hapo.

Madrassa nyingine zilizokuwa mahiri wakati huo ni ile ya Sherrif Hussein Badawwy, pale sokoni, Kisutu, ambapo ilikuwa ikiongoza katika fani ya tajwiid, lakini pia kwa mchezo wa mpira. Mwalimu wake mkuu Sherrif Hussein Badawwy, ndiye aliyeasisi klabu mashuhuri ya mpira ya Cosmopolitan, ambayo yeye mwenyewe alikuwa mchezaji na kocha. Klabu hiyo ndiyo iliyokuwa ikitwaa makombe kwenye miaka hiyo ya 50 na 60.


Shariff Hussein Badawy
Kote huko kwenye madrassa hizo kulifundishwa pia elimu ya kisekula ‘Kizungu’, ambapo watoto waliotokea humo kujiunga na shule za kawaida walikuwa wakipata alama za juu sana kutokana na misingi ya awali waliyowekewa. Si kweli hata kidogo, kama ilivyozoeleka kusemwa, kwamba Waislamu hawakuitilia maanani elimu ya kisekula. 

Sheikh Yahya Hussein yeye alipata elimu ya msingi pale Mchikichini na, ile ya kati, pale Kitchwele African Boys Middle School, hapa jijini. Alikuwa ni mwanafunzi aliyeongoza kwa kila jambo darasani, hasa somo la Kingereza na hisabati, na hivyo kumfanya awe na kiburi cha aina fulani. Habari zinasema, siku moja alikosana na mwalimu wake wa Kiingereza (Mr. Monday) darasani, kwa kumwambia kwamba alikuwa hawafundishi vizuri somo hilo maana alikuwa akiwabaniabania hivi.

Ule ukawa ni utovu wa nidhamu na kijana Yahya akafukuzwa shule mara moja. Yahya alipenda sana kuzungumza ‘kimombo’ na habari zinasema, kwake ilikuwa jambo dogo kufunga safari kila siku kwenda sehemu za mbali na kwao, ili kumfuata rafiki yake yeyote azungumze naye Kiingereza tu, ili roho yake iridhike.

Baada ya kufukuzwa shule, alibakia pale madrassani kwao na akawa akisaidiana na wazee wake kufundisha dini ya Kiislamu. Babake Mzee Hussein, akiwa mtu mashuhuri jijini, hakukata tamaa; alikwenda kumbembelezea ili arudishwe tena kuendelea na masomo yake pale shuleni Kitchwele.

Alikubaliwa kurudi na kipindi kile kikawa ni karibu na mitihani kwa ajili ya uteuzi wa kujiunga na Tabora School, kwani pale Kitchwele, wakati huo mwisho ilikuwa ni darasa la 10 tu. Sasa, pamoja na kwamba hakuhudhuria masomo kwa miezi 6, kijana Yahya alifaulu kwa alama za juu na kuwapiku wenziwe wote.

Walimu walipigwa na butwaa; wakasema haiwezekani labda pengine anatumia ‘ndumba na tunguri’ (uchawi). Matokeo yalipotoka yakawa vilevile kama mwanzo na njia ikawa nyeupe kwake sasa kwenda Tabora School. Hakwenda! Ule ulikuwa utawala wa kikoloni, pakafanyika ‘figisufigisu’ akakatwa jina lake. 

Babake hakuchoka; akampeleka Zanzibar kujiunga na Zanzibar Muslim Accademy. Hapa akaonekana hana vigezo vya kujiunga na taasisi ile iliyosheheni walimu bobezi kutoka Chuo Kikuu cha Al-azhar Sherrif cha Cairo, Misri. Akaondoka zake akaenda mjini Zanzibar akawa anasoma Qurani Sauti ya Unguja pale wakati inapofungua matangazo yake jioni.

Usomaji wa Sheikh Yahya katika fani ya tajwiid ulikuwa wa hali ya juu sana. Mudir (mkuu) wa chuo pale Muslim Accademy, siku moja katika pitapita zake akaisikia Qurani ikisomwa redioni na mtu ambaye hakupatapo kumsikia.

Siku ya pili akauliza pale chuoni ni nani yule aliyekuwa akisoma Qurani redioni jana yake? Akajibiwa kwamba yule alikuwa ni yule kijana aliyetaka kujiunga na chuo chake akamkataa. Mudir wa Muslim Academy Sheikh Mohammed Addahani, akaamrisha haraka atafutwe aje ajiunge na chuo.
 Yahya akawa yuko hapo kwa miaka kadhaa, na siku moja akazusha tafrani nyengine tena. Hapa akamlaumu Sheikh Addahani kuwa anapendelea katika utoaji wake maksi, kwani huwa anawapendelea wanafunzi fulani fulani na kuwapa alama za juu. Mudir hakuvumilia, Yahya akafukuzwa chuo.

Aliondoka akatimkia nchi za Kiarabu. Kipaji chake cha kusoma Qurani kikampatia umaarufu na akaweza kufanyiwa hafla kubwa pale Continental Hotel, Cairo, akasoma mbele ya makari, yaani wasomaji wakubwa wakubwa akina kama Abdulbasit, Mahmud na nduguye Mohammed Al-Minshawi na Sheikh Mustapha Ismail. Tukio lile likawa mubashara ‘live’ kwenye Redio ya Cairo. Kwa wale wasomaji waliomjua Sheikh Yahya watapata picha ni kitu gani alikifanya siku hiyo. Habari zinasema kuna msomaji mmoja mkubwa alipangwa asome baada ya Sheikh Yahya, alitoweka mwenyewe pale ukumbini na alipotafutwa haikujulikana kaenda wapi! Kajua hatofua dafu tena mbele ya Yahya Hussein.

Aliondoka hapo akaenda Malaysia ambako alikaribishwa na kula chakula na Waziri Mkuu wa siku hizo Tunku Abdulrahman ambaye pia alimsomea Qurani ndani ya Jumba la Serikali.


Sheikh Yahya Hussein na King Hussein wa Jordan miaka ya 1950s

Mjini Amman, Jordan alikaribishwa na King Hussein kwenye Kasri ya Mfalme akala naye ‘dinner’ na baadaye kumsomea Qur’an tukufu mfalme ambayo aliliwazika kwelikweli.

Alikaribishwa pia na King Hassan wa Morocco, ambako pia alipata wasaa wa kula na mfalme na kusoma kwenye Kasri ya Mfalme. Msomaji kuwa na mazungumzo ya aina yeyote na wafalme wale wa Kiarabu siyo jambo dogo kwa mtu kutoka katika vijiinchi vidogo hivi kama Tanganyika.

Alijitengenezea jina na kupatiwa, ‘’schorlaships,’’ nyingi sana kuwasaidia Watanganyika wengine kwenda kusoma katika nchi hizo. Watoto kadhaa walinufaika na ‘’schorlaships’’ za kupitia kwa Sheikh Yahya. Kama ilivyo kawaida, nabii huwa hakubaliki nchini mwao, lakini aliyekuwa Rais wa Kenya hayati Jomo Kenyatta, alimteua Sheikh Yahya kuwa mwakilishi wake binafsi kwa nchi za Kiarabu kutokana na kule kuwa  na uwezo wa kukutana na wafalme wale wakati  wowote. Akawa sasa yuko kule Mombasa na Nairobi akiwa katibu katika East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Hapa napo alitoa mchango mkubwa katika kupeleka vijana masomoni nchi za Uarabuni.

Alirejea nyumbani na kutembelea Zanzibar wakati Abeid Karume akiwa kiongozi baada ya Mapinduzi. Sheikh Yahya alikamatwa na kuwekwa jela kwa sababu alikuwa mara nyingi akionekana anazungumza na watu wenye asili ya Kiarabu. Serikali ya Mapinduzi ikahisi labda anataka kufanya ubaya.

Akiwa kifungoni kule Unguja, alikutana na mfungwa mwengine Mwarabu kutoka Yemen. Huyu alikuwa mjuzi wa fani ya utabiri na mambo ya uganga. Mwarabu yule alimpenda Sheikh Yahya kwa kuwa alikuwa anawaliwaza wafungwa wenziwe kwa kuwasomea Qur’an mle jela. Aliamua kumfundisha fani ya unajimu na tiba. Siku moja yule Mwarabu aliwaaga wenzake mle jela na akaondoka hivi hivi na mlango ukiwa umefungwa! Yakawa maajabu makubwa kwa askari na wafungwa pia.

Hazikupita siku, Sheikh Yahya naye kwa kutumia fani ile mpya, akajitabiria kwamba siku fulani atatoka mle jela na kuwa huru. Ikawa kama vile ghafla, wanasiasa pale Unguja wakaanza kuhoji kwa nini mtu yule kutoka Tanzania Bara, awe amefungwa kule Zanzibar badala ya kwao. Sijui paliongelewa nini, lakini ndege ikatumwa kwenda kumbeba kule Zanzibar, akakabidhiwa kwa Julius Nyerere na baada ya siku chache akawa yuko huru mitaani Dar es Salaam.

Hapo akaanza kazi yake mpya ya kuwa mtabiri akawa anatabiri matokeo ya mechi za mipira, ndondi, ajali, vifo vya watu mashuhuri, kuanguka kwa ndege na kuzama kwa meli, pamoja na vita duniani kote. Alitabiri pia matokeo ya chaguzi mbalimbali za kisiasa duniani na kuweza kumtaja nani atakayeibuka mshindi kwenye vinyang’anyiro hivyo.

Hapa kwetu alipata kutabiri kwamba Mzee Mkapa, wakati ule akiwa anamaliza muda wake uongozini, ataongezewa muda wa kuongoza, na ikatokea kuwa kweli maana palitokea kifo cha Mgombea Mwenza wa kiti cha urais kupitia Chadema na hivyo uchaguzi ukaahirishwa.

Mambo aliyoyatabiri na kutokea yako mengi kurasa za gazeti hazitoshi kuyaorodhesha. Kuna wakati aliitabiria timu ya mpira wa miguu ya Kenya kwamba ingeibuka kidedea kwenye mashindano ya Kombe la Challenge yaliyokuwa yakifanyika Tanzania. Kenya na Uganda waliingia fainali za mashindano hayo. Sheikh Yahya aliitabiria Kenya ushindi na aliweza kutaja wachezaji watakaong’ara siku hiyo na magoli yatapatikana kutoka kwa mchezaji namba ngapi na dakika ipi.


Sheikh Yahya Hussein na Jomo Kenyatta akimpa Rais Kenyatta
zawadi ya fimbo Nairobi miaka ya 1970

Kwa tukio hilo, serikali ya Kenya ilimletea ndege maalumu kwenda Nairobi kwenye sherehe za ushindi na huo ukawa tena ndio mwanzo wa yeye kuhamia huko moja kwa moja; akafikia kuwa mtu tajiri sana kutokana na kazi zake za unajimu na utabiri, wateja wake wakubwa wakiwa ni viongozi wa serikali ya Kenya.

Alikuwa na ofisi kubwa sana pale Moi Avenue Nairobi na alimiliki fahari ya jumba kule Kileleshwa (mfano labda wa Masaki hapa Dar es Salaam), nje kidogo ya jiji la Nairobi. Magari aliyokuwa akiendesha yakawa ni yale ya kisasa kabisa yanayouzwa bei ‘mbaya’ na suti zake zikawa zile za ‘designers’ wakubwa kutoka New York, Paris na Italy.

Sheikh Yahya vilevile alikuwa mtu wa mwanzo kabisa katika Afrika Mashariki, kutoa utabiri wa nyota magazetini, unaojulikana kama ‘horoscope’ au ‘nyota zenu’; kwani kabla yake magazeti kote Afrika Mashariki yalitegemea habari hizo kutoka magazeti ya Uingereza na Marekani.

Wakati wa kudai uhuru hapa nchini, Sheikh Yahya alijihusisha na siasa za vyama na alipata kuwa mpinzani mkubwa wa chama cha TANU na Mwalimu Nyerere akiwaita Nyerere na wenzake kama waropokaji na wapayukaji wasiojua A na B.

Alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Kabila wa Congo- DRC, Mfalme Mswati wa Swaziland (aliyempa uraia wa heshima wa nchi yake), Rais Daniel Arap Moi wa Kenya; na watu wengi wengine mashuhuri duniani.

Mtoto wa kiume wa mnajimu huyu, Maalim Hassan Yahya Hussein amejikita kuendelea na fani ya unajimu na utabiri kama marehemu babake. Na kwenye usomaji wa Qurani kwa njia ya tajwiid, pamoja na kwamba ametoa mchango mkubwa kwa kufundisha vijana wengi wanaondeleza fani hiyo, lakini amemwacha kwa makusudi, Sheikh Mohammed Nassor, awe kiongozi wa Taasisi  ya Usomaji na Kuhifadhi Qurani Tanzania, ambayo aliianzisha kwa nguvu na juhudi zake binafsi.

Kwa hivyo basi, wakati tukiadhimisha kumbukizi zake, ni vyema basi tukamuenzi na kumkumbuka mwanamajumui huyu aliyeipenda na kuitangaza nchi yake kimataifa kupitia fani na ujuzi aliojaaliwa na Mungu.

Simu:0715 808 864
atambaza@yahoo.com

No comments: