TAAZIA: SHEIKH SAUD BIN AHMED AL BUSAIDI
Nimepata
taaarifa ya msiba wa Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi jana usiku kutoka Abu
Dhabi kwa rafiki yangu Abdul Aleem Attas. Mara ya mwisho tulionana Dar es
Salaam yapata zaidi ya miaka 20 iliyopita na tukapoteana hadi siku tatu
zilizopita bada ya mmoja wa jamaa zake kuniunganisha na yeye baada ya kusoma
historia fupi niliyoandika ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na
nikamtajaa baba yake mdogo Shariff Abdallah Attas, mtu maarufu katika Dar es
Salaam ya 1950. Akijua mapenzi yangu ya vitabu Abdul Aleem akaniambia kuwa
kaninunulia kitabu cha marehemu mzee wetu, ‘’Memoirs of an Oman Gentlemn from
Zanzibar.’’ Nilimfahamisha kuwa kitabu ninacho toka kilipotoka na alinipa
mwandishi mwenyewe na kina sahihi yake.
Nawapa
pole wafiwa wote khasa Dr. Rawya Saud Al Busaidi. Allah awape subra wafiwa wote
na Allah amweke baba yetu mahali pema peponi.
Hakika
ni vigumu sana kuandika taazia ya mtu ambae hukupata kumjua kwa karibu. Lakini juu
ya ukweli huu naamini nina dhima ya kusema kitu kidogo kuhusu msomi huyu wa
Chuo Kikuu Cha Oxford kutoka Zanzibar ingawa lazima nikiri kuwa nimemjua Sheikh
Saud kwa kusoma kitabu chake, ambacho kwa ukamilifu si tu ni histori ya maisha
yake binafsi bali pia ni historia ya Zanzibar inayorudi nyuma kiasi cha karne
moja hivi sasa. Kitabu hiki ninacho na
namshukuru Allah kuwa alinipa mwenyewe kupitia rafiki yangu Dr. Harith Ghassany
na kama nilivyokwisa kusema kina sahihi yake. Kitabu hiki kipo katika Maktaba
yangu. Nina furaha ya kusema pia kuwa kitabu hiki nilikifanyia pito (book
review) ili wasomaji wafahamu umuhimu wa kukisoma.
Kama
ilivyo kawaida ya kumbukumbu zilizoandikwa na wa wale ambao walishuhudia
mainduzi na kisha walikimbia Zanzibar baada ya mapinduzi, historia ya Sheikh
Saud bin Ahmed Al Busaidi inafuata mkondo ule ule wa kuanza kuelezea Zanzibar
iliyokuwa imetulia na mahali pazuri pa kuishi kisha ikafuatia maisha ya shida,
wasiwasi, vifungo na mauaji na mwisho kwa wale waliiobahatika kukimbia nchi
wakiwa hai, maisha ya uhamishoni na mwisho kuishia takriban wengi wao, katika faraja
na ustawi katika nchi mpya walizohamia, iwe ni UAE au Oman. Haya nimeyasoma katika kitabu cha Sheikh Ali
Muhsin, ‘’Conflict and Harmony in Zanzibar,’’ na katika kitabu cha Muhammad Al - Marhuby kuhusu maisha ya
baba yake Sheikh Amor Ali Ameir Al Marhubi, ‘’Amor Ali Ameir His Life and
Legacy My Father.’’ HIstoria hii kwa wengi ni faraja.
Kumbukumbu hizi zimatuachia elimu ya kutosha ya
kuweza kuijua kwa undani historia ya kweli ya Zanzibar. Historia ya maisha ya Sheikh
Saud bin Ahmed Al Busaidi unaweza ukaipa jina, ‘’A Tale of Two Revolutions.’’
Aliondoka Zanzibar baada ya mapinduzi ya mwaka wa 1964 kisha akaondoka Libya baada
ya mapinduzi ya 1969 yaliyomuingiza Muammar Gadafi madarakani. Kati ya
mapinduzi haya Sheikh Saud hakukata tamaa katika maisha yake alifanya kazi kwa
juhudi kubwa na hakutaka kuangalia nyuma na kujisikitikia. Kila siku yake
ilikuwa siku mpya iliyompa nafasi ya kuangalia mbele na kushinda changamoto
mpya zilizojitokeza ama akiwa Kenya baada ya kukimbia Zanzibar, Misri, Libya au
Oman.
Mwaka
wa 1970 Sultan Qaboos alichukua uongozi wa Oman na akafungua milango kwa
Waomani waliokuwa nje warejee kwenye nchi yao ya asili, Oman na watapokelewa
kwa mikono miwili. Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi alifunga mizigo na kwenda
Oman mwaka wa 1971 na huu ukawa mwanzo wa maisha mapya ya furaha na umafanikio
makubwa akiwa Oman akishiriki katika kutumikia nchi yake mpya kwa juhudi na mapenzi
makubwa.
Mzee
wetu katika kitabu chake kwa furaha amehitimisha kwa nukuu kutoka kwa William
Shakespeare, ‘’All’s well that ends well.’’ Ameandika maneno haya akirudi nyuma
kuiangalia nchi yake Zanzibar aliyoikimbia miaka 50 iliyopita lakini kwa rehma
zake Allah amejikuta yuko tena Zanzibar kwa mapumziko akitokea Oman akiwa visiwani
na wanae na wajukuu zake. Hii ilikuwa kwa hakika moja ya ndoto zake kuwa ifike
siku arudi nchini kwake na aweze kukanyaga ardhi ambayo aliikanyaga akiwa mtoto
mdogo akicheza katika vichochoro vya Mji Mkongwe.
Napenda
kuhitimisha k kusem kuwa Sheikh Saud ameishi maisha yaliyokamilika akipanda
milima na kushuka mabonde akiwa na ustahamilivu na mategemeo mema. Katika
maisha yake ukisoma kitabu chake kunzia maisha yake Zanzibar hadi kuishia Oman yapo
mazingatio mengi sana.
Allah
ampanulie kaburi lake alijaze nuru na amweke mahali pema peponi.
Amin
No comments:
Post a Comment