USHAURI WA WAZI KWA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, PROFESA PALAMAGAMBA KABUDI:
“SULUHISHO LA MGONGANO KATIKA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971 NI UREJESHWAJI
WA MAHKAMA YA KADHI TANZANIA BARA”
Sheikh Mohamed Iddi Mohamed (Abuu Iddi) |
Ndugu zangu Wanahabari,
Assalaam Alaykum,
(Amani ya Mwenye ezi Mungu iwe
kwenu)
Maudhui ya tamko langu hili ni
hitajio la Waislam wa Tanzania Bara kuwa na Mahkama ya Kadhi.
Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni kupitia Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumemsikia Mheshimiwa Waziri wa Sheria na
Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, akitoa nasaha alisema (nanukuu):
“…Mashauri ya
ndoa, mashauri ya mirathi, mashauri yanayogusa mila na desturi, mashauri
yanayogusa dini, ni vyema tukayaendea kwa uangalifu mkubwa. Na niseme kwa unyenyekevu
mkubwa somo hili la ndoa nimelifundisha kwa miaka kumi na tisa, sio eneo
jepesi” (mwisho wa kunukuu).
Maneno hayo ya Mheshimiwa Waziri
Kabudi yanamaanisha mambo makuu mawili:
Kwanza,
anatuthibitishia kwamba yapo matatizo au kero nyingi katika masuala ya sheria
ya ndoa na masuala ya dini.
Pili,
anatunasihi tuwe na umakini mkubwa katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo au
kero hizo.
Ndugu Wanahabari,
Kupitia taarifa hiyo ya
Mheshimiwa Waziri Kabudi, nimeonelea nimshauri kwamba njia mojawapo ya kuiendea
katika kuyatatua matatizo hayo ni urejeshwaji wa Mahkama ya Kadhi.
Ni vizuri nikamkumbusha
Mheshimiwa Waziri kwamba maombi ya Waislam wa Tanzania Bara kutaka warejeshewe
Mahkama ya Kadhi sio jambo jipya na tayari limeshapitia michakato kadhaa lakini
kwa sababu haikuwepo dhamira ya dhati kwa Serikali kuwarejeshea Waislam Mahkama
ya Kadhi, mafanikio hayakufikiwa.
Mheshimiwa Waziri anakumbuka
mengi juu ya kadhia ya Mahkama ya Kadhi lakini kamwe hawezi kusahau kwamba
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliwahi kuunda Tume ya Kibunge chini
ya uenyekiti wa Mheshmiwa Athumani Janguo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kisarawe
Mkoa wa Pwani.
Tume hiyo ilihoji na kujiridhisha
juu ya hitajio la Waislam kurejeshewa Mahkama ya Kadhi lakini ripoti hiyo
haikusomwa Bungeni kama tulivyozoea kuona ripoti za Kamati na Tume mbalimbali
za Kibunge.
Ndugu Wanahabari,
Mheshimiwa Waziri atakumbuka pia;
Juhudi zilizosimamiwa na
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ndugu Mizengo Peter Pinda, ambazo zilikwamishwa pia kwa hofu ya ‘turufu ya
urais’.
Juhudi za mchakato wa kuifanyia
marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili sheria hiyo izitambue hukumu
zitakazotolewa na Makadhi hawa wasiokuwa na meno (wasiotambuliwa na sheria za
nchi) pia zilikwamishwa tena kwa hatua ya kusikitisha.
Ukweli ni kwamba hakuna ‘njia ya
mkato’ katika kutatua migogoro inayotokana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971
zaidi ya kufanya mojawapo kati mambo matatu yafuatayo:
(1) Kurejeshwa Mahkama ya Kadhi yenye
‘meno yake’ kamili;
(2) Kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa
ya mwaka 1971 ili kiwepo kipengele kitakachotambua hukumu zinazotolewa na
Makadhi hawa waliopo sasa;
(3) Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 itambue
Ndoa ya Kiislamu kwa ujumla wake na ukamilifu wake (kwa maana itambue
kufungishwa kwake, maisha yake, talaka yake, rejea yake, eda yake na
kadhalika).
Ndugu Wanahabari,
Nina hakika kwamba Mheshimiwa
Waziri Kabudi ambaye amekiri kusomesha somo la Ndoa kwa takriban miaka kumi na
tisa, anafahamu wazi migongano iliyopo kati ya matakwa ya Sheria ya Ndoa ya
mwaka 1971 na usahihi wa Sheria ya Ndoa ya Kiislam.
Nitoe mifano michache ya
migongano hiyo, kwa mfano:
• Sheria ya Kiislam katika
ufungishaji wa Ndoa inahitajia kuwepo Walii (mfungishaji ndoa) ambaye huwa ni
Baba, Babu, Kaka na kadhalika (mtu yeyote atakayefungisha ndoa ukimuondoa Walii
atakuwa amewakilishwa na Walii). Wakati Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inamtambua
Sheikh tena mwenye leseni kuwa ndiye mfungishaji ndoa na wala haimtambui Baba
kama mhusika mkuu wa ndoa.
• Sheria ya Ndoa ya Kiislam
hailazimishi kuwa ndoa ili iwe ni halali ifanywe maeneo yaliyo wazi bali
kuitangaza ndoa ni sunnah (jambo jema lenye malipo kwa Mungu). Lakini Sheria ya
Ndoa ya mwaka 1971 inalazimisha hilo suala la uwazi katika kufunga ndoa.
• Sheria ya Ndoa ya Kiislam inampa
Walii (Baba na kadhalika) nguvu ya kukataa Binti yake kuolewa na mwanamume wa
dini nyengine kwa kuwa ndoa hiyo haiswihi (haikubaliki) na waliooana kwa ndoa
hiyo wanahesabiwa kuwa ni wazinifu kama wazinifu wengine katika jamii. Lakini
kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaiona na kuitambua ndoa hiyo kuwa
sahihi haswa baada ya kutolewa tangazo la kusudio la ndoa na kukosekana
pingamizi lolote kuzuia kusudio hilo.
Ndugu Wanahabari,
Huo ni mgongano kati ya Sheria ya
Ndoa ya mwaka 1971 na matakwa ya Sheria ya Ndoa ya Kiislam kwa upande wa
kufunga ndoa (kuoana).
Ama kwa upande wa Talaka na
kuvunjika kwa ndoa:
• Talaka anayoitoa Muislam inatosha
kuvunja ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Kiislam. wakati talaka kwa upande
wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haipati uzito wa kisheria mpaka kipatikane
cheti cha Mahakama kinachothibitisha kuvunjika kwa ndoa hiyo. Kwa muktadha huo,
Muislam hana uwezo wa kutoa talaka na talaka yake ikatambulika kisheria kwani
talaka anayoitoa Muislam inahesabika kuwa ni kusudio la kuivunja ndoa.
• Aidha, hiyo Talaka ya Muislam
ambayo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haiitambui mpaka ithibitishwe na Mahakama,
katika Uislam imegawanyika katika makundi kadhaa ambayo hiyo Mahakama ya nchi
na Mahakimu wake hawawezi kuzitambua wala kujua kinachozaliwa baada ya talaka
hizo.
Naomba nitoe mifano michache
katika eneo hilo la Talaka ya Kiislam:
(a) Kuna talaka iliyo wazi ambayo inaitwa
“TWALAQ SWARIIH”.
(b) Kuna talaka ya fumbo ambayo inaitwa
“TWALAQ KINAAYAH”.
(c) Kuna talaka iliyotundikwa ambayo
inaitwa “TWALAQ MU’ALLAQ”.
(d) Kuna talaka inayopita haikutundikwa
inaitwa “TWALAQ MUNAJJAZ”.
(e) Kuna talaka ya kurejeleka ambayo
inaitwa “TWALAQ RAJI’IYYAH” (katika talaka ya kurejeleka, kama mke ameachwa talaka
ya rejea pindi mume akifariki kabla eda haijakwisha mke huyo atamrithi mtalaka
wake).
(f) Kuna talaka isiyo ya kurejeleka
ambayo inaitwa “TWALAQ BAIN”. Na hiyo BAIN kuna SUGHRAA (ndogo) na KUBRAA
(kubwa).
(g) Kuna talaka kabla ya kukutana kimwili.
(h) Kuna talaka ya kujivua ambayo inaitwa
“KHUL-I”.
(i) Kuna ndoa inayovunjika yenyewe bila
ya kutamkwa talaka pale mmoja kati ya wanandoa anapobadilisha dini.
Kwa uchambuzi huo, Mheshimiwa
Waziri Kabudi ataungana nami kwamba Ndoa na Talaka katika Uislam ni jambo kubwa
sana na pana linalohitajia Mahakimu maalum wenye utaalamu usiotiliwa shaka.
Ndugu Wanahabari,
Naomba nitumie fursa hii kumuomba
Mheshimiwa Waziri Kabudi kwa kuzingatia kwamba katika wakati huu ambayo yeye ni
Waziri wa Sheria na Katiba, Mwalimu wa Sheria na Mtaalam katika Somo la Ndoa
alilolifundisha kwa takriban miaka kumi na tisa; naamini ndio wakati muwafaka
wa kuitafutia ufumbuzi migongano na migogoro inayotokana na Sheria ya Ndoa ya
mwaka 1971.
Wakati mwengine wowote kamwe
hauwezi kuwa ni muwafaka kwani Mahkama ya Kadhi kwa muda wote imekuwa ni kadhia
iliyotumiwa kama ‘chambo’ cha kuvuna kura za Waislam katika chaguzi zilizopita
na kamwe hitajio lake halichukuliwi kuwa ni kutatua kero na migogoro
inayowasibu sehemu ya jamii ya Watanzania.
Ndugu Wanahabari,
Nimalizie mazungumzo yangu kwa
kusema mambo matano:
Jambo la kwanza, nimuombe
Mheshimiwa Waziri Kabudi aniruhusu kumuona anapokuwa Jijini Dar es Salaam ili
tubadilishane mawazo katika kuiendea kadhia hii. Katika hili nimuombe pia
Mheshimiwa Waziri aombe kupatiwa Hansad za Bunge na taarifa mbalimbali juu ya
kadhia hii ya Mahkama ya Kadhi ili tutakapokutana zitusaidie katika mazungumzo
yetu.
Jambo la pili, nimkumbushe
Mheshimiwa Waziri Kabudi na Watanzania kwa ujumla kwamba ukimya, upole na
ustahamilivu wa Waislam wa Tanzania Bara katika kunyimwa haki yao hii ya
Mahkama ya Kadhi ambayo wakipewa haina madhara yoyote kwa jamii nyengine ya
Watanzania sio endelevu bali ni wa msimu tu.
Jambo la tatu, namuomba
Mheshimiwa Waziri Kabudi akumbuke pia kwamba uwepo wa Makadhi hawa wa sasa
ambao hawana ‘meno’ wala kinga ya kisheria pale watakaposhtakiwa katika
Mahakama ya Tanzania kwa kosa la kuvunja ndoa ya mtu ambaye hakuridhishwa na
maamuzi yao, kamwe hauwezi kuwa ndio ‘dozi’ ya nusu kaputi ya kuwasahaulisha
Waislam wa Tanzania Bara madai ya hitajio lao hili yaliyodumu kwa takriban
miaka thelathini sasa.
Jambo la nne, kupitia mkutano
wangu nanyi ndugu wanahabari nichukue nafasi hii kumkumbusha na kumuomba
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Job Ndugai.
Nimkumbushe azikumbuke ‘mbinu
chafu’ zilizotumiwa na baadhi ya Wabunge katika ‘kukwamisha’ rasimu ya
marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 isiingie na kujadiliwa ndani ya
Bunge katika Bunge lililopita ambalo yeye Mheshimiwa Ndugai alikuwa ni Naibu
Spika.
Rasimu hiyo ililenga mjadala wa
kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili itambue hukumu za ndoa
za Waislamu kupitia Makadhi hawa waliopo ambao kwa mujibu wa sheria za nchi
‘hawana meno’. Nimkumbushe Mheshimiwa Spika Ndugai tena na tena kwamba
waathirika wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 hawajasahau na wala hawatasahau
mbinu ile iliyotumika kuwanyima haki zao.
Nimuombe Mheshimiwa Spika Ndugai
kwamba kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Taasisi na Mhimili
unaojitegemea, atoe agizo kwa watendaji wa Bunge wazirejee na waziandae
kumbukumbu zote za Bunge ikiwemo mchakato wa Kamati za Bunge kuhusu kadhia ya
Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara kupitia Bunge ili hoja hii itakapoibuka tena
katika awamu hii ya tano isionekane ni hoja mpya bali ni muendelezo wa maombi
ya Waislamu wa Tanzania yaliyodumu takriban miaka thelathini.
Jambo la tano, kupitia mkutano huu
pia nimuombe Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John
Pombe Magufuli, amtake Waziri wake wa Sheria na Katiba, Mheshimiwa Profesa
Palamagamba Kabudi, amuandalie taarifa ya madai ya Mahkama ya Kadhi Tanzania
Bara tangu mwanzo mpaka hapa tulipofikia.
Taarifa hiyo pia ijumuishe hoja
za wanaodai na hoja za wanaokataa uwepo wa Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara na
hitimisho lake ili Mheshimiwa Rais Magufuli kupitia vyombo vyake alifahamu
suala hili ukweli wake bila ya wasiwasi na shaka yoyote.
Nimuombe Mheshimiwa Rais Magufuli
alichukulie suala hili la Mahkama ya Kadhi kwa uzito wake kwa kuwa ni miongoni
mwa kero zinazohitajia ufumbuzi na hata Chama Cha Mapinduzi (CCM)
anachokiongoza kwa nafasi ya uenyekiti Taifa kiliahidi kulitafutia ufumbuzi
suala hili kupitia Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Kwa kuhitimisha, nimuombee dua
Mheshimiwa Rais Magufuli ili Mola Muumba amuwezeshe kulisimamia hili ili kero
hii itatuke katika wakati wake na historia imkumbuke kwa mengi ikiwemo na hili
pia.
Ndugu Wanahabari,
Nawaomba ujumbe huu muufikishe
kwa jamii ya Watanzania kwa usahihi wake.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Wabillaahi Ttawfiiq,
Sheikh Mohamed Iddi Mohamed (Abuu
Iddi)
Mwenyekiti – Arrisaalah Islamic Foundation
Tarehe: 09.05.2018
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment