Showing posts sorted by date for query Taazia kleist. Sort by relevance Show all posts
Showing posts sorted by date for query Taazia kleist. Sort by relevance Show all posts

Wednesday, 27 December 2017

BURIANI ALHAJ SHEIKH AHMED ISLAM

Ramadhani K. Dau

Kulia: Sheikh Ahmed Islam, Ahmed Rashad na Prof. haroub Othman Uwanja wa
Ndege wa Dar es Salaam uzinduzi wa safari ya Jeddad kwa Shirika la Ndege la Tanzania
7 August 1997

Ilikuwa siku ya Jumamosi tarehe 23 Disemba 2017, majira ya saa 5 usiku kwa saa za Malaysia nilipopata ujumbe mfupi wa sms kutoka kwa Sheikh Issa Othman, maarufu Mufti wa London, Imam wa Masjid Maamur ukiniarifu msiba wa mzee wetu Sheikh Ahmed Islam. Ujumbe wake ulikuwa mfupi sana: “Mzee wetu Ahmed Islam amefariki sasa hivi. Maiti inaletwa msikitini hivi sasa. Maziko kesho In Shaa Allah. Innallillahi Wainnaillahi Raajiuun”.

Mara tu baada ya kupata taarifa hiyo na baada ya kumtakia maghfira mzee wetu, nikajua kuwa kwa mara nyingine tena umeniangukia wajibu wa kuandika taazia ya mtu ambaye namfahamu, namheshimu na alikuwa na ukaribu sana na mimi. Nimeshawahi kuandika huko nyuma kuwa kuandika taazia ni jambo zito na gumu sana. Kila niandikapo hutamani sana taazia hiyo iwe ndiyo ya mwisho. Lakini kwa mipango Yake Mwenyezi Mungu, najikuta nashindwa kukwepa wajibu huo. Hata hivyo, mara hii nilidhani ningeweza kuukwepa wajibu huo kwa kumuomba rafiki yangu na ndugu yangu mwanahistoria maarufu Sheikh Mohamed Said aandike taazia hiyo nami nilikuwa tayari kumpa maelezo yoyote ambayo yangemsaidia katika uandishi wake. Pamoja ya kuwa alikubali kuifanya kazi hiyo, Mohamed alisisitiza kuwa lazima na mimi niandike. Kwa jinsi ya msisitizo aliouweka Sheikh Mohamed, nimejikuta kwa mara nyingine tena  nalazimika kuandika taazia hii huku nikiwa na moyo wa huzuni sana kwa kuondokewa na mzee wangu ambaye alikuwa mithili ya baba yangu mzazi.

Marehemu mzee Ahmed Islam ana mambo mengi na sura nyingi. Wapo wanaomfahamu kama ni miongoni mwa wazee maarufu na kiongozi katika jamii ya Waislamu, wapo wanaomfahamu kama mtaalamu wa masuala ya Rasilimali Watu (Human Resources) na wapo wanaomfahamu mzee Ahmed Islam kama mwana michezo mahiri.

Marehemu Mzee Ahmed Ijhad Islam alizaliwa Zanzibar tarehe 22 Disemba 1930 akiwa ni mtoto pekee wa Sheikh Ijhad Islam na bibi yetu Bi Maryam Mussa. Kwa bahati mbaya, mzee Ijhad Islam alifariki wakati mzee Ahmed akiwa mdogo na hivyo akalelewa na mama yake. Baada ya msiba huo, bibi yetu Bi Maryam aliolewa na kupata mtoto mmoja wa kike ambaye jina lake ni Zerah.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi na Sekondari kwenye Government School (sasa Ben Bella) Zanzibar mwaka 1948, ilipofika mwaka 1957 marehemu mzee Ahmed Islam alikwenda Cornwall, Uingereza kuchukua masomo katika fani ya Mawasiliano yaani Telecommunications. Wakati huo alikuwa ameajiriwa na kampuni ya Cable and Wireless (C&W) ambako alikuwa Meneja Msaidizi (Assistant Manager). Kampuni hii ilikuwa ndiyo kampuni kubwa ya mawasiliano Afrika Mashariki. Baada ya kurudi masomoni, marehemu aliendelea na kazi yake na baada ya kampuni ya C&W kumezwa na Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki (East African Post and Telecommunication), Mzee Islam akahamia Dar es Salaam mwaka 1970.

Akiwa Dar es Salaam Mzee Islam alifanyakazi katika Shirika hilo na baada ya mgawanyiko yakaundwa Mashirika mawili tofauti; Shirika la Posta (TPC) na Shirika la Simu (TTCL). Marehemu mzee Islam alihamishiwa TTCL hadi alipostaafu mwaka 1986 akiwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu yaani Director of Manpower. Baada ya kustaafu, marehemu alifanyakazi Ubalozi wa Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu. Wakati wa uhai wake, Mzee Islam amefanya mengi katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi wa dini, ujenzi wa nchi, uendelezaji wa michezo na utoaji nasaha kwa taasisi na vijana mbalimbali katika masuala ya ndoa na kujiendeleza kwenye elimu ya juu. 

Kwa upande wa dini, marehemu ametoa mchango mkubwa sana. Miongoni mwa matunda ya kazi yake ni usimamizi wa ujenzi wa Masjid Maamur iliyopo Upanga, Dar es Salaam. Kwa wanaokumbuka vizuri jiografia ya Upanga, kabla 1987 pale palipojengwa Masjid Maamur hapakuwa na msikiti. Lakini kwa kushirikiana na wazee wenziwe marehemu Mzee Islam aliweza kusimama kidete katika kusimamia ujenzi wa Masjid. Si wengi wanaofahamu kuwa ujenzi wa Masjid Maamur ulianza na msukusuko mkubwa kwa sababu kulikuwa na mwanajeshi ambaye alikuwa amepanga kwenye nyumba ya jirani ambayo ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).  Mwanajeshi yule alikuwa anatumia kiwanja cha msikiti kufugia mifugo na kulima mboga. Historia ya kiwanja kile ni kuwa pale palikuwa makaburi ya ukoo wa Tambaza toka zamani sana. Siku moja marehemu Mzee Islam alikwenda kwenye kiwanja kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa msikiti. Yule mwanajeshi hakutaka msikiti ujengwe pale pamoja ya kuwa kiwanja hicho kilikuwa mali halali ya Msikiti. Wakati ule ukoo wa Tambaza walikuwa wamekitoa kiwanja kile wakfu pajengwe msikiti na Meya Kitwana Kondo alikuwa amesaidia pakubwa kufanikisha hilo. Hivyo basi yule mwanajeshi akatoka na bastola na kutaka kumshambulia Mzee Islam kwa risasi.  Marehemu Mzee Islam hakuogopa. Badala yake alimwambia yule mwanajeshi afyatue risasi haraka ili amfungulie njia ya kwenda peponi.  Mwanajeshi akabaki ameduwaa na hatimaye akaondoka. Baada ya hapo ujenzi ukaendelea kwa amani na yule mwanajeshi akahamishiwa Songea. Ilipofika mwaka 2013, marehemu Mzee Islam pia alichangia kwa kiasi kikubwa usimamizi wa ukarabati mkubwa wa msikiti huo kwa ufadhili mkubwa wa kampuni ya Oil Com.

Kushoto: Abdallah Kassim, Himid Ashraf, Sheikh Aboud Maalim, Sheikh Ali
Hassan Mwinyi Rais Mstaafr wa Tanzania, Sheikh Ahmed Islam
Mbali na Masjid Maamur, marehemu Mzee Islam pia alitoa mchango mkubwa sana katika ujenzi wa Masjid Ngazija hapa Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya sana tokea ukoloni hadi leo, katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Central Business District), hakuna msikiti wowote mkubwa wala mdogo zaidi ya msikiti wa Ngazija. Lakini msikiti huo ambao ulijengwa wakati wa ukoloni ulikuwa ni mdogo sana kiasi cha kutokidhi mahitaji ya Waumini. Hivyo basi kwa kushirikiana na viongozi wengine kama vile marehemu Sheikh Aboud Maalim, marehemu Profesa Haroub Othman Miraji, Sheikh Saidi Kassim, Habibu Nuru, AbdulHamid Mhoma na wengineo, marehemu mzee Islam alishiriki kusimamia ujenzi wa msikiti mpya wa Ngazija ambao kwa sasa una ghorofa tatu na ndiyo msikiti pekee uliopo Dar es Salaam Central Business District. Pamoja na usimamizi wa ujenzi wa misikiti, Mzee Islam ameandika vitabu mbali mbali vya dua na nyiradi na alikuwa mmoja wa wasimamizi wa uradi wa kila wiki Masjid Ngazija na Masjid Rawdha.


Kulia: Dr. Gharib Bilal Makamu wa Rais Zanzibar Mstaafu, Sheikh Saleh, Sheikh
Ahmed Islam na Sheikh Zubeir Yahya Imam Mkuu wa Msikiti wa Mtoro wakiwa
Masjid Ngazija

Mchango wa marehemu Mzee Islam katika kuwaendeleza vijana wa Kiislamu kielimu ni mkubwa bila kifani. Nina hakika si watu wengi wanaofahamu kuwa mzee Ahmed Islam ndiye ambaye aliyefanikisha kupatikana kwa kiwanja ambacho kwa sasa imejengwa shule ya Sekondari ya Al Haramain jijini Dar es Salaam. Naishauri BAKWATA ambayo ndiyo Wamiliki wa Shule ya AlHaramain wathamini mchango wa Mzee Ahmed Islam kwa kulipa jina lake moja ya madarasa au kumbi za shule. Aidha Mzee Islam alikuwa mstari wa mbele kwenye Taasisi ya Tanzania Muslim Solidarity Trust Fund katika kusimamia nafasi za masomo za vijana wa Kiislamu wanaokwenda kusoma Uturuki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kiislam (Islamic Development Bank) iliyopo Jeddah, Saudi Arabia. Chini ya ufadhili huo, kwa karibu miaka 30 sasa Benki hiyo imekuwa ikifadhili vijana wa Kiislamu 15 kwenda kusoma masomo ya Uhandisi (Engineering) na Utabibu (Medicine) kwenye Vyuo Vikuu nchini Uturuki. Miongoni mwa watu walionufaika na mpango huu ni Dr. Hussein Mwinyi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr. Asante Rabi Kighoma Malima wa Chuo Kikuu cha Northeastern Marekani, Dr. Mashavu, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, Dr. Munawwara Kaguta daktari wa hospitali ya Aga Khan na wengine wengi. 

Moja ya mafanikio makubwa ya jitahada za marehemu Mzee Islam ni uvumbuzi ambao ulifanywa mwezi Agosti 2014 na Dr. Asante Rabi Kighoma Malima ambaye alivumbua kifaa cha kuweza kubaini maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na saratani (cancer) yakiwa katika hatua za awali kabisa. Kutokana na uvumbuzi wa kifaa hicho ambacho amekiita Biolom, Dr. Malima alipewa tuzo na Gavana wa jimbo la Massachusetts, Bwana Deval Patrick. Haya ni matunda ya mzee wetu Ahmed Islam ambayo yameiletea sifa kubwa sana nchi yetu katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia. Aidha mwaka 2002, mzee Islam aliishawishi Taasisi ya Muslim Aid ya London kuja kujenga maabara tatu za kisasa katika shule ya Sekondari ya Twayyibat iliyopo Temeke Dar es Salaam. Katika kipindi hicho hicho, kwa kupitia Muslim Aid, Mzee Islam pia alifanikisha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Sotele, Kisiju Mkoa wa Pwani. Harakati za marehemu Mzee Islam kuwasaidia vijana katika kutafuta elimu hazikuanzia Dar es Salaam. Wakati akiwa Zanzibar, marehemu alikuwa akiwahimiza sana vijana kusoma na yeye binafsi alikuwa akijitolea kuwapa vijana mafunzo ya ziada (tuition) usiku kwa kutumia taa za kibatari/koroboi. Abdallah Mbamba aliyekuwa Radio ya Umoja wa Mataifa, New York na sasa anaishi Oman anakumbuka sana mafunzo haya ya ziada kuanzia darasa la sita hadi la nane kabla ya Mapinduzi masomo ambayo yalimsaidia yeye na wenzake wengi kufaulu vyema mitihani yao.

Kulia Sheikh Ahmed Islam na Dr Dau
Minna katika safari ya Umrah August 1997


Marehemu Mzee Islam alikuwa Mcha Mungu sana. Pamoja na kuwa na umri mkubwa wa miaka 87 na kuandamwa na maradhi ya miguu, kamwe hakuacha kuswali swala zote katika msikiti Maamur. Siku zote alikuwa wa kwanza kuingia msikitini na kuswali kwenye kiti msitari wa mbele. Hata wakati alipopata maradhi ambayo yalihitimisha safari yake hapa duniani, hakuacha kwenda kuswali msikitini. Wiki tatu kabla ya kufikwa na umauti, kwa muda wa siku mbili mfululuzo alikuwa hawezi kula vizuri na matokeo yake akawa hana nguvu. Hata hivyo ilipofika siku ya Ijumaa akataka lazima aende msikitini. Watoto wake walimsihi sana lakini hakukubali. Ikabidi abebwe apelekwe Masjid Maamur kwa ajili ya swala ya Ijumaa na hiyo ndio ikawa Ijumaa yake ya mwisho kuswali msikitini. Ijumaa iliyofuata wazee wa Masjid Maamur pamoja na watoto wake wakamsihi sana awe anaswali nyumbani. Ikabidi akubali kwa shingo upande kwani hakuwa na njia nyingine ya kwenda msikitini isipokuwa kwa kubebwa na wabebaji ndio hao waliomtaka aswali nyumbani.

Mwaka 1997, nilibahatika kusafiri kwenda Umra na marehemu Mzee Islam wakati Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lilipofanya safari yake ya kwanza kwenda Jeddah, Saudi Arabia. Katika safari yetu walikuwepo marehemu mzee Ahmed Rashad Ali, marehemu Siraju Juma Kaboyonga na mkewe marehemu Jaji Madina Muro, marehemu Prof. Haroub Othman, marehemu Balozi Selemani Hemedi, Dr. Idris Rashid, Jenerali Ulimwengu, mama Fatma Maghimbi, Mhe Hamad Rashid, Hamza Aziz, Yahya Sinani na mwanahistoria Sheikh Mohamed Saidi na wengineo. Wengi walimshuhudia takriban kwa siku zote tulizokuwa safarini, marehemu Mzee Islam alikuwa anaamka usiku kufanya ibada. Iko siku tukiwa Makka baada ya tawafu Mzee Islam kundi kubwa likiwa nyuma yake alisimama kuomba dua mbele ya Kaaba hadi akatokwa na machozi.

Jambo hili la kuswali Tahajud limethibitishwa na mmoja kati ya watoto wake ambaye alizaliwa mwaka 1961. Anasema yeye amemshuhudia baba yake akiswali Tahajud kila siku tokea apate fahamu. Inasemekana alianza utaratibu huu wa kuswali usiku kuanzia mwaka 1951 na hakuacha kisimamo cha usiku mpaka maradhi yalipomzidi mwishoni mwa mwaka huu. Siri nyingine aliyokuwa nayo marehemu Mzee Islam ni kudumisha sunna ya kufunga siku za Jumatatu na Alhamisi. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanawe, amemuona baba yake akifunga sunna hii tokea yeye alipokuwa mdogo.

Mzee Islam alikuwa mtu wa watu na alikuwa mwepesi sana wa kusaidia watu wenye matatizo. Aidha mzee Islam alikuwa anapenda sana kusuluhisha watu. Milango ya nyumba yake ilikuwa wazi saa zote ambapo watu wa rika zote walikuwa wanaenda kila siku kutaka misaada au ushauri.  Mzee Islam alikuwa jeshi la mtu mmoja na alikuwa zaidi ya Taasisi. Hapa ntasimulia matukio matatu kati ya matukio mengi sana ambayo yanaonesha ukarimu na utayari wa marehemu katika kusaidia watu. Siku moja mama mmoja kutoka mkoa wa Kilimanjaro alikwenda nyumbani kwa Mzee Islam akiwa na watoto wa kike watatu ambao wote walikuwa yatima. Baada ya kueleza matatizo yake na ugumu wa maisha ya kulea wale mayatima, marehemu Mzee Islam akamshauri wale watoto wabaki kwake na yeye atachukua jukumu la kuwalea na kuwasomesha. Yule mama akakubali rai ile. Hivi niandikavyo Taazia hii, mtoto mmoja amemaliza masomo ya Shahada ya Kwanza katika Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa sasa anafanyakazi Tanga. Mwingine amemaliza Shahada ya Uzamili katika fani ya Uthamini vifaa vya ujenzi (Masters Degree in Quantity Survey) kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam. Na wa mwisho hivi sasa anachukua Stashahada (Diploma) ya Uhasibu.

Tukio la pili lilitokea mwaka 1991 wakati kijana mmoja alipokwenda nyumbani kwa Mzee Ahmed Islam kumuomba msaada wa kwenda masomoni Ujerumani. Kama ilivyo kawaida yake, Mzee Islam hakusita na alisimamia uchangishaji wa fedha kwa ajili ya safari masomo ya kijana huyo. Leo hii, kijana huyo ni Daktari Bingwa nchini Ujerumani. Mifano kama hii ipo mingi na nafasi haitoshi kuisimulia yote.

Tukio la tatu lilitokea mwaka 2008 na linamhusu kijana ambaye alikuwa na tatizo la ada ya kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kijana yule alihitaji nusu ya ada (shs. 400,000) ili asajiliwe na Chuo. Baada ya kuhangaika sana alipata shs. 100,000. Hatimaye kuna mtu alimwelekeza kwa Mzee Ahmed Islam. Alipofika nyumbani kwake na kueleza shida yake, mzee Islam akamwomba arudi siku ya pili. Naam, aliporudi siku ya pili alimpa shs. 300,000 na yule kijana akarudi chuoni kuendelea na masomo. Kana kwamba haitoshi, wakati yule kijana yupo masomoni, kuna mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mzumbe ambaye ni yatima alikuwa na tatizo sugu la nyonga. Kwa kuona hali yake ilivyo, yule kijana wa Chuo Kikuu akamchukua mgonjwa hadi nyumbani kwa mzee Ahmed Islam. Kwa kuwa uso umeumbwa na aibu, yule kijana akabaki barabarani na akamuelekeza mgonjwa nyumba anayokaa mzee Islam. Marehemu alimtafuta daktari bingwa wa kumshughulikia yule yatima hadi akapona. Hivi sasa yule yatima ni mhandisi baada ya kuhitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa upande wa michezo, Mzee Islam hakuwa nyuma. Wakati wa uhai wake, alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu kiasi cha kuitwa mchawi wa mchezo huo. Alipokuwa Zanzibar alicheza timu ya Vikokotoni na timu ya Taifa ya Zanzibar. Akiwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Mzee Islam alishiriki katika mashindano kadhaa ikiwemo mashindano maarufu ya kombe la Gossage akicheza namba 10. Mwaka 1952 timu ya Taifa ya Zanzibar ilifika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika Nairobi Kenya na kushika nafasi ya pili baada ya kuzifunga timu za Tanganyika na Uganda. Pamoja wachezaji wengine, timu ya Zanzibar iliwakilishwa na marehemu Mzee Ahmed Islam, marehemu Mzee Abdul Majham Omar, Mzee Mwinyi (Mpiringo), Seif Rashid na Maulid Mohamed (Machaprala). Pamoja na umahiri wake wa kucheza mpira wa miguu, Mzee Islam alikuwa mchezaji hodari wa Kriket na mpira wa magongo (hockey). Kama ilivyo kwenye mpira wa miguu, marehemu Mzee Islam alichezea timu za Taifa za Zanzibar kwenye Kriket na Hockey. 

Wakati wa uhai wake, Mzee Islam alikuwa mzungumzaji wangu sana sio tu kwenye masuala ya jamii lakini pia masuala ya michezo. Mimi na marehemu tulikuwa tunakubaliana kwenye mambo mengi sana isipokuwa mambo mawili ambayo tulikubaliana kutokubaliana. Kwanza kwenye upenzi wa mpira kwa timu za hapa nyumbani  marehemu mzee Islam alikuwa mpenzi mkubwa wa Yanga wakati mimi ni mpenzi wa Taifa Stars. Kwa upande wa timu za nje ya nchi, Mzee Islam alikuwa anaipenda sana Manchester United. Bahati mbaya sikuwahi kumuuliza sababu ya yeye kuipenda Manchester United. Kama sababu ni kutembelea jiji la Manchester wakati alipokuwa masomoni Uingereza, basi nilitarajia angeipenda Manchester City kwa sababu klabu hiyo ndiYo ipo katika jiji la Manchester wakati timu ya Manchester United ipo shamba kabisa kwenye kitongoji kidogo kinachoitwa Old Trafford. Kwa hapa nyumbani, kitongoji cha Old Trafford mfano wake ni kama vile Dar es Salaam na Ruvu Darajani pale panapouzwa samaki wakavu au mbele kidogo kwenye kijiji cha Vigwaza. Wenyewe Waingereza wanasema, ‘’There is only one team in Manchester,’’ (Manchester kuna timu moja tu) ambayo ni Manchester City. Pia wanao msemo wao unaosema, ‘’There is only one football team in London; the Gunners!’’ (London kuna timu moja tu ya mpira wa miguu; washika Bunduki). Najua Balozi Saleh Tambwe na Balozi Juma Mwapachu watalipinga hili. Lakini haya si maneno yangu.

Niliwahi kuandika mapema mwaka huu kuwa kutokana na vifo vilivyoongozana vya wazee wa Dar es Salaam, jiji letu limebaki kuwa na ukiwa. Mwaka huu tumeshuhudia kuondokewa kwa Kamanda Dr. Mohamed Chiko, Mzee Iddi Sungura, Mzee Issa Ausi (Smart Boy), Ali Bob, Mzee Kitwana Selemani Kondo, Balozi Abdul Karim Omar Mtiro (Cisco), Kleist Abdul Wahid Sykes na sasa Mzee Ahmed Islam. Jiji la Dar es Salaam limegubikwa na huzuni kubwa. Lakini kwa sababu kifo ni faradhi hatuna budi tuikubali hali hiyo.

Kulia: Sheikh Ahmed Islam, Mussa Sykes na Dr. Ramadhani Dau
Jeddah katika safari ya Umrah wakipata kifungua kinywa

Mzee Islam ametangulia lakini ameacha simulizi ambazo zitazungumzwa kwa miaka mingi sana baada ya yeye kuondoka. Wakati wa uhai wake, marehemu Mzee Islam na mama yetu Bi Rukia Ahmed Iddi ambaye alifariki 1989 walijaaliwa kupata watoto sita ambao ni Islam, Biubwa, Mohamed (maarufu Eddy), AbdulRahman, Abubakar na Mussa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Amrithishe mzee wetu Ahmed Islam Jannat Firdous kama Alivyosema Mwenyewe kwenye Quran Sura 23 Aya 1-11 pale Alipozitaja sifa za watu wema kisha Akamalizia kwa kusema Atawarithisha Firdous na wataishi humo milele. Pia tunamwomba Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema na Atukutanishe na mzee wetu Ahmed Islam kwenye Firdous. Aaamiin.



Wednesday, 6 December 2017

Buriani ‘Kaka Kleist’
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Mwandishi wa makala Abdallah Tambaza ni huyo wa kwanza kushoto, Bubby Bokhari, Kleist Sykes, Yusuf  Zialror, Mohamed Said, waliochutama kushoto ni Kaisi, Wendo Mwapachu na Abdul Mtemvu, 1968

AWALI ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Allah (SW) na kumtakia rehma Mtume wetu Muhammad (SAW) kwa kuniwezesha kukaa mbele ya kompyuta na kuandika taazia hii ngumu na nzito ya marehemu kaka yangu; ndugu yangu; sahib yangu; na rafiki yangu kipenzi kabisa kupata kutokea, Kleist Abdulwahid Abdallah Sykes – Inna Lillah Waina Ilayhi Rajiun.

Mwezi Januari mwaka huu nilimwandikia rafiki yangu mwengine, SACP Mohammed Chico, taazia nzito kama hii iliyonitoa jasho na machozi pale ilipokamilika. Sikudhani hata kidogo kama hautapita muda mrefu nitarudi kuandika tena taazia nyengine kwa mtu anayefanana na yeye ­­– wote ni watu wa kwetu Dar es Salaam niliowajua vilivyo. Wazungu wa kule Ulaya Ingereza na Marekani, wanapofikwa na msiba wa ukubwa kama huu, husema kwamba umekuja ‘untimely’ (haukutarajiwa kwa wakati ule, wakati sio ule na labda ungesubiri baadaye hivi). Wanasema ‘untimely’, kwa sababu bado wasingependa kuachana na mpendwa wao kwa wakati ule; wanasema ‘untimely’ kwa sababu wanajua uchungu wa kuondokewa; na wanasema ‘untimely’ kwa sababu kwa anayeondokewa hategemei tena kupata mbadala wake! Kwa kiasi fulani wako sahihi, kwani yu wapi leo ‘Kaka Kleist’ mwengine? Marehemu ‘Kaka Kleist’, alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumatano, Novemba 22, mwaka huu, katika Chumba cha Watu Wenye Kuhitaji Uangalizi Maalumu (ICU), pale katika spitali ya Agakhan ya hapa Dar alikokuwa amelazwa jana yake.

Mara baada ya kifo kutokea, dadake, Misky Sykes, ambaye alikesha kucha pale spitali kufuatilia hali ya mgonjwa wake, akanipigia simu kunipa habari za msiba ule mzito huku akilia na kuomboleza: “…Kaka Abdallah eh …nadhani Kaka Kleist amefariki sasa hivi, naona madaktari na manesi wanahangaika pale… nafikiri ametutoka kwani hawasemi kitu… Ooh! Ooh! Ooh!” alikatiza Misky mazungumzo na kutoweka na kilio chake. Kleist alizikwa siku ya Alhamisi jioni katika makaburi ya Kisutu, katika mazishi yaliyoongozwa na aliyepata kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu (mstaafu) Mohammed Chande Othman. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, na Waziri wa Ujenzi na Miundombinu, Makame Mbarawa, ambaye ndiye aliyemwakilisha Rais JPM. Alikuwapo pia Prof. Haruna Lipumba wa CUF, Mbunge Mussa Azzan Zungu na Iddi Azzan zamani Mbunge pale Kinondoni, pamoja na mameya na madiwani mbalimbali wa jiji hili la Dar es Salaam. Walikuwapo pia vijana wengi wa Dar es Salaam wa kizamani ambao pengine wamesoma au kucheza pamoja na marehemu katika maeneo mbalimbali ya jiji hili.Walikuwapo pia watoto wa marafiki wa Kleist ambao waliongozana na wazee wao kuja kumsindikiza katika safari yake ya mwisho mwana wa jiji mwenzao ambaye habari zake na ukarimu wake pengine walikuwa wakisimuliwa na wazee wao kwenye sebule zao.

Jaji Chande Othman, pamoja na kwamba alikuwa pale kwenye turubai lilowakinga viongozi, sidhani kwamba moyoni mwake alikuwa akihisi kuwa pale alipo alikuwa akihudhuria mazishi ya mtu wa kiserekali tu, kwani siku zile za utotoni kwake, si tu alisoma pamoja na Kaka Kleist, lakini pia yeye pamoja na kakake mkubwa Prof. Othman Chande, walikuwa kundi moja la Boys Scouts tawi la Saint Joseph’s Convent School, Forodhani. Mohammed Chande na Kleist pia walisoma wakati mmoja pale H.H. AgaKhan Secondary School (1964-1967).Hawa kina Chande wawili, waliungana na vijana wengine wa pale Shule ya Mtakatifu Joseph, Forodhani wakaunda kikundi cha vijana kilichojulikana kama The Scorpions, madhumuni yake yakiwa ni kupendana, kusaidiana na kutembea pamoja pale inapobidi.

Scorpions wengine waliokuwapo pale siku ile ni Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo, Abdul Mtemvu, Wendo Mwapachu, Yusuf Zialor, Christopher Faraji, Kamili Mussa, Bhobby Bokhari pamoja na mimi mwandishi wa makala haya. Nilimwona pia Mbunge Mussa Azzan ‘Zungu’ pale makaburini. Zungu hakuwa anamwakilisha Spika Ndugai pale. Kwa vyovyote vile alikuwapo kwa ajili ya kuwa amecheza na Kleist utotoni kwenye mitaa ya Kariakoo na Gerezani ambako wote ndiko walikokulia. Mzee Warioba, pamoja na nasaba yake ya Musoma, alikuwa mtu wa hapa mjini siku nyingi. Kabla hata hajajiunga na Chuo Kikuu, pale Mlimani alikuwa akionekana akivinjari mitaa ya New Street, Gerezani na Mission Kota, siku nyingi sana na hivyo akawa amezoeana vilivyo na vijana wengi wa jiji hili akiwamo marehemu Kleist Sykes. Isitoshe, mke wa Jaji Warioba ni mwenyeji wa Dar mwenye uhusiano wa karibu sana na kina Sykes.




Mwingine ni Mzee Kikwete. Huyu hakuwapo pale kumzika kada mwenziwe wa CCM tu. Kikwete naye Dar es Salaam ni yake na vijana kama Kleist ni rika lake, hivyo wakigongana hapa na pale kwenye kumbi za starehe na burudani hasa miziki ya ‘’Buggy,’’ na kwenye viwanja vya mpira. Kikwete alipotea njia kidogo akawa anapenda Yanga, wakati Kleist ni Simba wa kutupwa. Mapema, katika nasaha zake kwa waombolezaji mara baada ya sala ya jeneza pale Msikiti wa Maamur, Upanga, Imam Mkuu Sheikh Issa aliwataka waumini kujiandaa na kile alichokiita ‘certainty of mortality,’ akiimaanisha kwamba kifo kimedhihiri na kwa hakika kitamfika kila mmoja; kwa hiyo hapana budi watu kukifanyia maandalizi yake kabla. “Katika maisha yetu ni vizuri basi watu wakakaa mbali na yale yote ambayo Allah (SW) ameyakataza na kuyafanya kwa wingi (kuyakimbilia) yale ambayo Allah (SW) ameyaamrisha kwayo,”amesema Sheikh Issa.  


Nyuma kulia ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete
Sasa wakati nikiyatafakari maneno yale adhimu ya msomi yule pale msikitini, nilijihisi kama vile alikuwa akiniambia mimi au labda alikuwa akijua namna marehemu alivyokuwa mtu wa kheri, hasa katika utoaji wa sadaka na mambo kama hayo. Kaka Kleist, alipenda sana kusaidia wengine na wala hakusubiri kufuatwa kwa shida ndiyo afanye hivyo. Kuna wakati unaweza kukutana naye tu iwe ofisini au sehemu yeyote na ghafla atakurushia swali: “Vipi wewe uko vizuri mifukoni?” Kabla hujajibu tayari atakuwa amekwishatoa pochi lake na kukuvurumushia pesa ukafanyie jambo lolote. Kwa watu wazima na vikongwe hapo tena ndio usiseme. Hivyo ndivyo alivyoishi katika jamii inayomzunguka na kwenye makundi ya marafiki zake. Sasa wakati Sheikh Issa akitoa nasaha zile ikaja taswira fulani hivi ya kwamba rafiki yangu yule, njia yake ya kuelekea kwa Mola wake ilikuwa kwa kiasi fulani imesafishika tayari.

Siku moja wakati ugonjwa umeshamtopea kwelikweli na figo hazipatikani, nilifika kumwona pale kwake Mbezi Beach. Tulitazamana machoni na yeye akagundua kwamba mimi nimehuzunika sana. Alinitazama na akaniambia: “Sikiliza we ‘timbwa’ wala usihuzunike mimi tayari nimewasomesha watoto wangu wote vizuri sana …sina kinyongo hata kama Mwenyezi Mungu atanichukua leo… niko tayari kwa hilo,”alisema. Yale yalikuwa ni maneno mazito kuyasema mtu aliyekuwa kwenye hali kama yake. Palepale nilijua ile ilikuwa ni kama ananiaga kiaina, kwani tayari alikwishahisi dalili kuwa safari yake haiko mbali. Kamwe, hakuwa mtu wa kukata tamaa kirahisi, kwani aliujua vizuri ugonjwa wa kisukari na madhara yake ikafikia hata wakati mwengine kupendekeza tiba mwenyewe kwa madaktari wake. Katika juhudi zake za kupambana na maradhi, marehemu kwa nyakati tofauti alikwenda sehemu mbalimbali duniani kutafuta tiba. Juhudi za kila aina zilifanyika kupata figo mbadala (transplants), lakini ilishindikana kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya umri mkubwa n.k. Na hapa napenda kumfariji shemeji yangu Stella Mallya ambaye alijitolea sana kuhakikisha mume wake anapona kwa namna yeyote ile.

Kwa upendo na hali ya kawaida, tulikuwa tukipenda kumwita ‘Kaka Kleist’, hata kwa wale ambao hawakuwa wadogo zake wa damu. Sababu ni kwamba wadogo zake walikuwa marafiki pia, na hivyo kwa kawaida huchanganyika na watu wengine kutembea na kustarehe pamoja. Sasa, inakuja katika mazungumzo, majadiliano ya hoja au kutaniana kwa aina yeyote, watu wengine walikuwa wakimwita Kleist kavukavu hivihivi; wakati wadogoze (akiwamo Abraham, Ayoub, Mussa, Misky, Omar (sasa marehemu), Adam (sasa marehemu), Ebby (sasa marehemu) ilikuwa inawashinda; kwani kila mara ni lazima waanze na kitu ‘kaka’. Hivyo tamko ‘Kaka Kleist’ likawa linaleta ladha fulani kulisikia; maana nduguze hawakumwita mtu mwengine yeyote kaka zaidi ya Kleist, hata kama ni mkubwa kama huyo kaka yao. Wengine waliitwa tu, kwa majina yao ya utani na mzaha (nicknames) kama kawaida.

Katika miaka hiyo, mwandishi huyu, kwa marafiki zake alikuwa akipachikwa majina mengi ya masikhara na utani kama vile ‘Nene’ au ‘Timbwa’, kutokana na wingi wa kilo mwilini. Lakini kamwe sikusikia mtu akiniita ‘Kaka Nene’. Tamko hilo lilikuwa ni makhsusi kwa marehemu Kleist peke yake. Sababu nyengine ya kuitwa kaka ni kwamba, alikuwa ni mtu wa upatanishi na usuluhishi panapotokea sintofahamu baina ya marafiki zake. Alikuwa na kipaji, uwezo na akili nyingi sana za kuweza kuleta suluhu au ushawishi katika kujenga hoja kwenye vikao mbalimbali. Mambo hayo ni miongoni mwa sifa zilizomfanya watu wamwite, ‘Kaka Kleist’.

Mara ya kwanza kabisa kukutana na Kleist, ilikuwa pale kwenye Shule ya Aljamiatul-Islamiya fi Tanganyika, mtaa wa New Street (sasa Lumumba) kwenye miaka ya 50s, tulikopelekwa na wazee wetu kupata elimu ya dini ya Kiislamu. Hapa Kleist alikuwa akijulikana sana maana shule haikuwa mbali na kwao. Pia waasisi wa mwanzo wa taasisi ile pamoja na mchango mkubwa  wa jengo zima ilikuwa kutoka kwa familia ya Sykes, hasa babu Mzee Kleist Abdallah Sykes ambaye alijitolea hali na mali kuhakikisha Uislamu na Waislamu hawaachwi nyuma. Walimu mashuhuri pale kwa siku zile nakumbuka alikuwa Maalim Simba, Maalim Mataar, Maalim Adam Issa na Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo ndiye aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa taasisi ile. Palikuwepo pia na walimu wanawake kama vile mwalimu Sakina Arab na mwalimu Tahia. Namkumbuka huyu mwalimu Tahia kwa sababu alikuwa pia ni mke wa Mzee Juma Mwinyimkuu rafiki mkubwa wa marehemu babangu wakicheza mpira pamoja timu ya Morning Star iliyokuwa timu ya pili ya Sunderland wakati huo (sasa Simba). Mwalimu Sakina yeye alikuwa ni mwanamke mmoja maarufu sana katika harakati za wanawake hapa kwetu, kwani alifikia hadhi ya kuwa na kiti cha kudumu cha udiwani katika Manispaa ya Dar es Salaam siku hizo za ukoloni wa Kingereza. Habari za Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ni ndefu mno na mchango wa Mzee Sykes pamoja na watoto wake Abdul, Ally na Abbas katika jamii ya Kiislamu na ukombozi wa nchi hii kwa ujumla, zimeelezwa kwa kina na mwanahistoria maarufu nchini ndugu yangu Sheikh Mohammed Said, katika kitabu chake mashuhuri, “The Life and Times of Abdulwahid Sykes 1968 The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ kinachosambazwa na Ibn Hazm Media Centre ya Dar es Salaam. Ndani ya kitabu hicho, Mohammed ameuelezea mchango mkubwa wa familia ya Sykes katika kuanzisha chama cha TAA kabla ya TANU na namna walivyoweza kupambana na Waingereza kwa namna mbalimbali mpaka pale uhuru ukapatikana. Msomaji ikutoshe tu kusema hata pale TANU ilipoanzishwa, akina Sykes walikuwa na kadi namba za mwanzo mwanzo kabisa ambazo zilibuniwa na kugharimiwa na Mzee Ally Sykes (sasa marehemu).

Rafiki yangu, marehemu ‘Kaka Kleist, alizaliwa jijini Dar-es-Salaam miaka 68 iliyopita akiwa mtoto wa pili kwa baba Abdulwahid na mama Mwamvua Mrisho Mashu (maarufu mama Daisy). Watoto wengine ni dada Aisha-Daisy Buruku, ambaye alizaliwa mwanzo kabla ya Kleist, wakafuatia Adam na Omar ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki. Adam alikufa yapata nusu mwaka sasa. Anao pia nduguze wa mama mwengine, kwa sababu mzee Abdulwahid alioa mara tatu. Huku utamkuta Ebby (sasa marehemu), Elyassar (anayeishi Canada) na wanawake Misky na Mariamu (sasa marehemu). Hakukuwa na mtoto yoyote kutoka kwa yule mke wa tatu ambaye alikuwa naye baada ya kuwa ameshaachana na mama Daisy na mama Ebby.

Baada ya kupata elimu ya dini pale Aljamiatul, ‘kaka’ Kleist, kama ilivyokuwa kwa kina Sykes wote wakati huo, alijiunga na shule ya H.H. The Aga Khan (sasa Tambaza High School na Muhimbili primary) pale Upanga Dar es Salaam, shule ambazo zilikuwa mahsusi kwa watoto wa jamii ya Kihindi wakati huo wa elimu ya kibaguzi ya utawala wa Kiingereza. Kina Sykes, walipata hadhi hiyo nadra wakati huo, kutokana na heshima kubwa iliyokuwa imepewa familia yao kwa sababu ya mchango wa Babu Mzee Sykes katika jamii. Na kwa heshima hiyo hiyo Mzee Abdulwahid Sykes (babake ‘kaka’ Kleist) aliingizwa katika Bodi ya Aga Khan Schools, na kwa hivyo ikawa ni rahisi ‘ujiko’ kwa kina Sykes wote kupata elimu pale. Kaka Kleist, alisoma pale kuanzia chekechea mpaka Form IV alipomaliza mwaka 1967. Baadaye akachaguliwa kujiunga na Chuo cha Kilimo kule Ukiriguru, Mwanza. Kufuatia kifo cha ghafla cha marehemu babake, mnamo mwaka 1968, kijana Kleist Sykes, ilibidi akatize masomo yake Mwanza na kusafiri kwenda kwa babake mdogo Abbas Sykes aliyekuwa Balozi wa Tanzania kule Canada kwa ajili ya malezi na masomo mapya.

Nakumbuka kama vile jana, nikiwa bado kijana mdogo nilihudhuria mazishi ya mzee Abdul pale mtaa wa Lindi, Gerezani, jijini yaliyofurika watu wengi— wengi kwelikweli— akiwemo Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa taifa hili. Tofauti na marais Kikwete, Mwinyi na Mkapa, katika uongozi wake, Mwalimu hakuhudhuria mazishini mara kwa mara. Ukiacha mazishi haya, mazishi mengine aliyohudhuria Mwalimu ni ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, aliyekuwa waziri wake wa Sheria na Katiba wakati huo, aliyefia nchini Ujerumani mwanzoni mwa miaka ya 1960s na mwili kuletwa nyumbani kwa mazishi, akiwa kiongozi wa kwanza mwandamizi kufariki akiwa kazini. Alishiriki pia mazishi ya makamu wake wa rais Abeid Amani Karume kule Zanzibar na yale ya waziri wake mkuu Edward Moringe Sokoine, kule Monduli Juu, Arusha.

Katika mazishi ya Mzee Abdul Sykes, mwandishi huyu, alimshuhudia Nyerere akiwa kwenye majamvi pale mtaani Lindi na baadaye kulisindikiza nyuma jeneza mpaka Msikiti wa Ijumaa, Kitumbini. Katika hali isiyo ya kawaida, Nyerere alisubiri nje mwili uswaliwe swala ya jeneza na ulipotoka, aliusindikiza kwa miguu mpaka makaburini Kisutu pasi na kutaka asaidiwe usafiri. Kufuatia kifo kile, serikali ya Nyerere ilitangaza kujitwika mzigo wa kuwasomesha na kuwaangalia watoto wa marehemu rafiki yake yule, ambaye ndiye aliyempokea katika harakati za kugombania uhuru wetu akawa anakula na kulala kwake baada ya kuacha kazi ya ualimu Pugu ili ajiunge na harakati za kudai uhuru.

Katika maisha yake ya kule Canada, Kleist alihitimu shahada yake ya kwanza na ya  pili (uzamili) kwenye masuala ya Ustawi wa Jamii. Aliweza pia kupata ajira kwenye taasisi iliyojulikana kama Canadian University Students Organisation (CUSO). Kazi kubwa za shirika hilo ni kama lile la kule Marekani la American Peace Corps, lenye malengo na madhumuni ya kutoa misaada ya kimaendeleo kwa nchi changa duniani.  Sasa baada ya miaka kadhaa pale kazini, nafasi ikatokea ya kuja kuwa Mkurugenzi (Director of CUSO –Tanzania). Wakati huo Kleist alikuwa tayari ameoa kulekule Canada na kubahatika kupata mtoto wake wa kwanza Latifa. Kwa sababu ambazo hazikuelezwa, mamake Latifa alikataa katukatu kuongozana na mumewe kuja Tanzania, akihofia labda pengine wasingerudi tena Canada. Kwa mapenzi ya nchi yake na nduguze, Kleist aliondoka akaja yeye akiwa amembeba mtoto wake mdogo Latifa, wakati huo akiwa na umri takriban miaka mitatu hivi. Kwa kweli ilikuwa ni nderemo na hoi hoi kwenye ukoo wa Sykes kwa ujio wa Latifa. Bibi yake, marehemu mama Daisy, alishereheka sana kupata mjukuu yule kwa mtoto wake wa kiume. Latifa alikuwa juu juu—mara Upanga, mara Temeke, mara Mbezi Beach kwa babu Ally Sykes.


Kushoto: Mama Daiy mbele kulia Bi. Titi Mohamed
Mamake hayati Kleist Bi. Mwamvua Mrisho Mashu, alikuwa ni mwanaharakati mkuu wa masuala yanayohusu maendeleo ya wanawake hapa nchini. Katika uhai wake anatajwa kwamba alikuwa ni mmoja wa waasisi wakuu wa Chama Cha Wazazi nchi (TAPA), siku nyingi kabla uhuru wa nchi haujapatikana. Bi. Mwamvua anatajwa pia mmoja wa watu walioshirikiana kwa karibu na kina Bibi Titi kuanzisha UWT, ambako yeye alidumu kuwa mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi kirefu akishinda chaguzi mbalimbali. Mama Daisy pia alikuwa Mwenyekiti wa TANU/CCM tawi la Miburani pale Wailes, Temeke kwa miaka kadhaa. Mwandishi huyu mara nyingi alimshuhudia Kleist akiwa na mamake wakipanga na kupangua mipango ya siasa, hasa zile zilizomhusu Kleist, kwani Bi. Mwamvua alikuwa na hazina kubwa ya uongozi wa nchi hii kichwani mwake kutokana na kule kuwa mke wa Mzee Abdul Sykes. Bila shaka yeyote ile, nguvu kubwa na uwezo aliokuwanao Kleist ulitokana na maelekezo na mafunzo kutoka nyumbani kwa mama yake baada ya kuwa babake aliaga dunia mapema.   

Sasa, mnamo miaka ya 1970 mwishoni, ili kuziba ombwe la kukosekana mama wa kumlea mtoto Latifa, Kleist aliamua kumchumbia Stella Mallya aliyekuwa akiishi jirani na nyumbani kwake pale mbele ya Shule ya Tambaza. Mzee Mallya ambaye ndiye baba wa bibi harusi hakuwa ameridhia kabisa binti yake kuolewa nje ya Uchagani kwao Moshi.  Baada ya tafakuri ndefu, wawili wale, bwana na bibi harusi wakaamua kuwa ndoa lazima ifungwe ‘iwe jua iwe mvua’, itakiwe isitakiwe. Ndoa ikafungwa kwa siri kwa DC pale Ilala na hapakuwa na sherehe wala mialiko yeyote. Mimi nikawa ndiyo mpambe ‘best man’ wa Bwana harusi, wakati Bi Bernadetta Majebelle akawa mpambe wa Bibi harusi. Baada ya shughuli ile pale bomani, tuliondoka mahala pale tukaenda peke yetu maeneo fulani kule Sea View tukajipongeza kwa vinywaji na vyakula kidogo mpaka usiku ulipoingia tukaagana.

Siku kadhaa baadaye, na kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa binti yake, mzee Mallya alirudi matawi ya chini akawa tayari kumpokea tena binti yake. Aliwatembelea nyumbani pale Upanga akakaribishwa kwa vyakula na vinywaji, ambapo mwandishi huyu alimshuhudia Mzee Mallya akiwa mwenye furaha kwelikweli baada ya kuwa amepata ‘kinywaji moto’ na ‘kinywaji baridi’. Ndoa ile imedumu kwa miongo zaidi ya mitatu na ikaajaliwa kupata watoto watatu ambao ni watu wazima sasa; Aisha, Abdulwahid, Ally na Latifa akawa dada yao mkubwa.

Uzoefu, uaminifu na utumishi uliotukuka pale CUSO, ulimpatia sifa Kleist za kuchaguliwa kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo alifanya kazi kule Geneva, Switzerland na Zambia kama mwakilishi mkazi. Baada ya kuwa ametumikia UNHCR muda mrefu, ‘Kaka Kleist’ alirejea nyumbani na kujikita kwenye biashara mbalimbali ikiwemo kuanzisha kampuni yake ya kuhudumia meli iitwayo Prevention and Indemnity (P&I), ofisi zake mpaka leo zikiwapo pale mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.

Kwa kutumia uzoefu wake wa biashara, utawala na nidhamu ya kazi, na kwa ushawishi mkubwa kutoka kwa marafiki zake wa utotoni (akina Yusuf Zialor na Wendo Mwapachu), ambao nao ni mabingwa katika masuala ya biashara, wakaanzisha kampuni iliyojulikana kama Business Center International (BCI) iliyokuwa na ofisi zake pale kwenye jumba la Bushtracker kwenye makutano ya Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi.  Marafiki wengine waliokuwa pamoja utotoni kwenye kundi la Scorpions ndio waliokuwa maofisa mbalimbali pale Bushtracker. Alikuwapo dada Mariam Zialor, Abdul Mtemvu, Booby Bhokari, Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo na Ramadhani Madabida. Business Center International (BCI) ilikuwa na kampuni tanzu kadha wa kadha ikiwamo ofisi mashuhuri ya safari za ndege ya KEARSLEY LTD pale Barabara ya Samora jijini na kiwanda kikubwa cha uchapishaji cha PRINTFAST kule Nyerere Road.

Kwenye jamii, Kleist alikuwa mwanachama mwandamizi wa Klabu maarufu ya Saigon ya Dar es Salaam, kama ilivyokuwa kwa wanafamilia wengine wa ukoo wa Sykes. Michango ya kina Sykes kwenye klabu hii haisemeki—wako mstari wa mbele kila pale wanapohitajika.
Kila mmoja aliwashuhudia vijana kutoka klabu ya Saigon walivyokuwa mstari wa mbele siku ya maziko kuanzia uhudumu wa chakula kwa wageni pale nyumbani mpaka makaburini Kisutu, kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawasawa kwenye mazishi ya mpendwa wao. Alikuwa mwanachama pia wa klabu mashuhuri ya viongozi pale Leaders Club, iliyoko mbele ya Klabu ya Usiku ya Bilicanas, kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mwanachama mwandamizi kutoka Leaders Club, Zainul Dossa, ndiye aliyeratibu shughuli zote za mazishi ya Kleist kuanzia chakula nyumbani mpaka makaburini Kisutu akihakikisha kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa.

Katika upande wa siasa, marehemu Kaka Kleist alikuwa kada mzuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akifuata nyayo za familia yake katika harakati za siasa. Alipata kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake chini ya uongozi wa Jakaya Mrisho Kikwete. Akiwa diwani wa Kata ya Kivukoni, marehemu Kleist aligombania na kuchaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwenye miaka ya 1990, na moja ya mafanikio makubwa ambayo amekufa akijivunia ni kuweza kutatua tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kwa kubuni na kusimamia mradi mkubwa wa Usafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dar Rapid Transit). Aliweza kuwashawisha maofisa wa Benki ya Dunia, akiwamo rais wake, ambao awali walikuwa wamepanga kupeleka mradi ule kwenye moja ya nchi za kule Afrika Magharibi, kubadili mawazo na kuleta mradi ule mkubwa hapa kwetu, mradi ambao umeiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kuwa na mradi mkubwa ambao, si tu utakidhi haja, lakini pia imekuwa ni fursa nyingine kwenye ajira na hivyo kupeleka mbele maendeleo ya nchi kwa jumla. Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali ulimwengu wamekuwa wakimiminika kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kwenye hili. Akizungumza kabla jeneza la marehemu Kleist Sykes halijaondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kuzikwa, mwakilishi aliyetumwa na shirika la UDART, ambalo ndilo linatoa huduma za mabasi ya mwendo kasi jijini, alisema daima marehemu atakumbukwa kwa kubuni, kupanga na kukamilisha  hatua zote za utekelezaji wa miradi yote sita ya mpango mzima wa mabasi ya mwendo kasi.“...mpaka sasa tayari phase moja tu imekamilika yaani kutoka Kivukoni mpaka Kimara na kwamba mradi mzima una phase 6 ikiwamo Kariakoo – Mbagala; Morocco—Tegetta; na Kariakoo—Gongo la Mboto,...pale phase zote zitakapomalizika nchi itakuwa imepiga hatua kubwa …” amesema.

Mpaka umauti unamfika, marehemu Kleist, alikuwa amewekeza nguvu zake kwenye biashara ya kilimo cha mkonge kwani tayari alishanunua mashamba makubwa kule Kibaranga, wilayani Muheza, akiongozwa kitaalamu na mtaalamu bobezi wa Kilimo cha Mkonge nchini, Abdallah Mussa Kamili. Kwenye kazi hiyo, tayari alikuwa akishirikiana kwa karibu na wanawe katika uendeshaji na utawala wa shughuli hiyo. Sidhani kama kutatokea ugumu wowote, maana katika kipindi kirefu ambacho amekuwa akiugua ni watoto haohao ndio waliokuwa wakifanya shughuli hizo. InshaAllah kwa uwezo wa Mungu watajiunga pamoja na mama yao kumalizia pale ambapo baba amekomea. 


Sheikh Abdallah Awadh alipata kumbeba Kleist akiwa mtoto akisoma dua kwenye kaburi
Kushoto ni Kleist Abdul Sykes na kulia ni Abdallah Tambaza na katikati ni Mussa Abbas Sykes

INNA LILLAH WAINA ILLAYHI
RAJIUUN
simu: 0715808864

Sunday, 26 November 2017


TAAZIA: BURIANI NDUGU NA RAFIKI YANGU MPENZI
MUUNGWANA KLEIST…
(27 June, 1950 – 24 November, 2017)

Kleist Abdulwahid Sykes

Usiku wa Jumanne tarehe 23 nimeona katika ukurasa wa FB wa kaka kaka yangu Prof. Charles Mgone kuwa yuko Glasgow, Scotland akaandika kuwa anafurahi kurudi tena katika mji huo. Nami nikaandika kumwambia kuwa amenikumbusha Dumbarton Road mtaa ambao yeye akiishi na mimi nikienda kumtembelea katika miaka ya mwanzoni ya 1990 kwanza nikitokea Dar es Salaam na baadae nikitokea Cardiff, Wales. Asubuhi yake nikapokea ujumbe mfupi kutoka kwake ukisema, ‘’Nasikitika kuwa sintokuwapo kumsindikiza ndugu na rafiki yangu katika safari yake ya mwisho.’’ Jina la aliyefariki hakuliandika bila shaka akiamini kuwa taarifa tayari ninazo. Nikashtuka kwani ujumbe huu ulikuwa ukinitaarifu msiba na haraka nikarejesha ujumbe kumuuliza nani kafariki? Mimi ndiyo kwanza nilikuwa nimeamka na kuwasha simu yangu. Jua lilikuwa limeshapanda pakubwa. Hata sekunde tatu hazikupita taarifa nyingi zikawa zinaingia kwa kufukuzana katika simu zikitoa taarifa ya kifo cha Kleist na taarifa ya kwanza ilikuwa kutoka Saigon Club.

Imesadifu kifo cha Kleist ikutane na kumbukumbu zangu za Glasgow ambako takriban miaka 30 iliyopita kila nilipokuwa hapo Dumbarton Road kwa labda ule upweke wa Ulaya tulikuwa tukikumbushana habari za utoto wetu Dar es Salaam Mtaa wa Kipata tulipozaliwa na Charles mara kwa mara atanihadithia habari zake za udogoni na Kleist. Hawa walikuwa marafiki toka utoto na mama zao walikuwa mashoga. Charles alimtangulia Kleist kwa mwaka mmoja. Charles kazaliwa 1949 na Kleist 1950. Charles alikuwa akinihadithia mchezo aliokuwa akicheza na Kleist kwenye bomba la maji lililokuwa Mtaa wa Kipata na Swahili pembeni ya nyumba ya Mama Kilindi. Miaka ile ya 1950 si kila nyumba ilikuwa na maji ndani na haya mabomba yalikuwa kila mtaa kwa ajili ya watu kuteka maji.

Taarifa ya kifo cha Kleist haraka ilinirudisha nyuma katika historia hii ya Dar es Salaam ya Tanganyika ya miaka 1950 wakati sisi tunazaliwa wazee wetu ndiyo walikuwa wanaanza harakati za wazi za kupambana na Waingereza kuidai Tanganyika. Baba yake Kleist, Abdulwahid Sykes katika mwaka wa 1950 ndiye alikuwa Katibu na Kaimu rais wa Tanganyika African Association (TAA). Siku hizo wakiishi Mtaa wa Stanley na Sikukuu katika nyumba ya kupendeza katika hali za wakati ule, nyumba iliyoezekwa bati ina maji na umeme na nyumba ambayo si ya mtindo wa vyumba sita bali numba yenye veranda na vyumba vya kulala na ua mkubwa na vyoo vyenye mabomba ya mvua ya kuogea. Nyumba nyingi wakati ule zilikuwa za makuti na zilizoezekwa kwa madebe na kujengwa kwa udongo, fito na kutomelewa kwa chokaa na sementi. Hii ndiyo Dar es Salaam ambayo Kleist alikuwa kazaliwa pamoja na wengi ambao niliwaona pale mazikoni walipokuja kumsindikiza ndugu yao katika safari yake ya mwisho.

Bomba la maji la Kipata lilikuwa pembeni ya nyumba ya Mama Kilindi mumewe Mzee Hassan bin Khamis kabila Mnubi ambae kivazi chake siku zote kilikuwa ni kanzu koti na tarbush. Mzee Hassan alikuwa akifanya biashara Soko la Kariakoo ambako baba yake Kleist alikuwa ndiyo Market Master yaani Mkuu wa Soko. Watu mfano wa Mzee Hassan diyo walikuja kununua kadi za kwanza za TANU pale sokoni wakiuziwa na Abdul Sykes na ndiyo watu wa mwanzo kumtia machoni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka wa 1952 akiwa na Abdul Sykes katika mitaa ya Gerezani au pale Sokoni Kariakoo. Makaburi ya Kisutu wakati tunamzika Kleist, nilimuona kasimama Amani, mjukuu wa Mama Kilindi na Mzee Hassan bin Khamis. Amani hakumuwahi Kleist katika mitaa ya Gerezani akicheza jirani ya kwao kwenye bomba la maji kwani yeye ni uzawa wa miaka ya 1970, lakini siku hii Gerezani na Dar es Salaam yote kwa ujumla ilitoka kuja kumzika mwana wa mji kindakindaki kuanzia babu, bibi na baba. Makaburini niliwaona pia wajukuu wa Hassan Machakaomo. Huyu Machakaomo ni katika kizazi cha kwanza cha Wazulu. Mzee wa Kizulu Machakaomo aliingia Tanganyika akiwa askari mamluki kama alivyoingia babu yake mkuu Kleist, Sykes Mbuwane miaka ya mwishoni 1800 wakiwa wamebeba mikuki na ngao mikononi. Ukoo wa Machakaomo hadi leo hawa bado wanaishi Kipata.

Kleist wazee wengi waliokuwa wanamfahamu baba yake wanasema alishabihina sana na baba yake kwa tabia na hulka hususan katika uungwana na ukarimu. Nilipatapo kumsikia Mzee Kitwana Kondo akisema, ‘’Abdul alikuwa mtu muugwana sana.’’ Sifa hii ya ungwana aliitoa pia Mhariri wa Africa Events (London) Mohamed Mlamali Adam katika utangulizi wa makala niliyoandika mwaka wa 1988 ambamo nilimtaja Abdul Sykes. Katika utangulizi wake Mlamali alimwita Abdul Sykes, ‘’…the sweet Abdul Sykes…’’ kwa tafsiri nyepesi ni sawa na kusema, ‘’Muungwana Abdul Sykes.’’ Hivi ndivyo ilivyokuwa tabu sana Kleist kukikwepa kivuli cha baba yake lau kama katika uhai wake Kleist aliweza kujijengea haiba na historia yake mwenyewe nje ya haiba na historia ya baba na babu yake ambao wote walitoa mchango mkubwa katika kukita misingi ya Tanganyika kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni wa Waingereza. Juu ya juhudi zake za kusimama na miguu yake mwenyewe miwili siku zote kivuli cha historia ya baba na babu yake ilimwandama Kleist na kumuelemea sana.

Ingekuwa labda si kwa udugu waliokuwanao wazee wetu na pengine pamoja na mapenzi yangu ya kupenda kusoma kuandika na kuvutiwa na stori yoyote ya kusisimua nisingepata hamu ya kuandika maisha ya Abdulwahid Sykes. Historia ya ukoo wa Sykes dhidi ya ukoloni na juhudi yao kaika kuwaunganisha Waafrika ni kisa cha kuvutia. Hii ilikuwa historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika na Kleist akijua mengi katika historia hii na vipi asijue ilhali Baba wa Taifa alipokelewa Dar es Salaam na kutiwa katika uongozi wa TAA na TANU kwa juhudi za baba yake? Historia hii ya kusisimua ilinisogeza karibu zaidi na Kleist kiasi cha sasa kufunika ule urafiki na udugu wetu wa asili ulioanza na babu zetu hadi sasa kutufikia sisi wajukuu, historia ambayo sasa imetimiza karne moja.

Kleist alikuwa na kisa cha kueleza cha historia hii ambayo kwa sababu zisizoweza kufahamika ilikuwa inatoweka taratibu, lakini alikuwa hana msikilizaji wala mtu anaetaka kuijua. Nilipotokea mimi kama muulizaji maswali na msikilizaji kifua cha Kleist na moyo wake vyote vilifunguka na kuanza kueleza mambo ambayo kwangu yalikuwa kama vile nimekaa kwenye kiti cha Empire Cinema naangaalia filamu nzuri mfano wa ‘’Hercules in the Land of Cyclopes,’’ filamu iliyotusisimua watoto wote wa wakati ule. Siku moja mdogo wake Kleist marehemu Omari alinambia, ‘’Mohamed dada Daisy ameandika kitabu kuhusu babu kitafute ukisome.’’ Ikasadifu kuwa nilikuwa nakwenda Arusha na nilipokuwa nimemaliza shughuli zangu nikaingia Maktaba ya Taifa, Arusha na hapo nikakikuta kitabu kilichohaririwa na John Iliffe, ‘’Modern Tanzanians,’’ na ndani nikamkuta Daisy kamwandika babu yake ‘’The Townsman: Kleist Sykes,’’ yaani, ‘’Mwanamji: Kleist Sykes. Kuanza kusoma utangulizi tu nikawa nimeshatoka katika karne ya 20 hii, dada yangu Daisy amenipeleka karne ya 19 niko Mozambique, Mhambane katika kijiji cha Kwa Likunyi nipo na Mjerumani Herman von Wissman anawapakia askari mamluki wa Kizulu katika manowari bandari ya Laurenco Marquis (leo Maputo) anawaleta Pangani kuja kupigana na Abushiri bin Salim na Chief Mkwawa. Katika askari hawa mamluki wa Kizulu waliokuwa wanakuja Tanganyika alikuwapo babu yake mkuu Kleist, Sykes Mbuwane na nduguye kipofu Ally Katini.


Bushiri bin Salim Al Harith
Nilibakia na maswali mengi sana nayatafutia majibu. Nilifahamu fika kuwa huyu aliyeandika maisha ya Kleist katika mji wa Dar es Salaam ya 1900 hakuwa Daisy Sykes. Hii ni kalamu ya mtu mwingine kabisa. Siku hizo Kleist yuko Geneva anafanya kazi United High Commission for Refugees (UNHCR). Maswali yangu yakawa yanamsubiri Kleist. Nyumba ya Kleist ilikuwa inaangalia shule yake aliyosoma, Aga Khan School. Kiasi Kleist asome shule hiyo maana baba yake alikuwa kwa miaka mingi wakati wa uhai wake mjumbe katika Aga Khan Education Committee. Kleist alikuwa naamini akifurahi sana kuzungumza na mimi kuhusu historia ya ukoo wao. ‘’Sheikh Mohamed ngoja nikuletee kinywaji chako.’’ Kleist alikuwa akijua kuwa mimi ni mpenzi wa muziki wa jazz kama yeye basi hapo ataniwekea santuri baada ya santuri ya muziki wa wapigaji maarufu kutoka maktaba yake, muziki ukija kwa sauti ya chini sana.

Tulikuwa kama vile tuna ratiba yetu maalum tunayoifuata. Ilikuwa kwanza lazima tubadilishane ‘’notes,’’ kuhusu baba zetu na maisha yao walipokuwa vijana mitaa ya Gerezani. Hapo tukicheka sana na kuwarehemu wazee wetu. Baba yangu katika umri mdogo sana alikuwa na wake wawili na baba yake Kleist pia alikuwa na wake wawili. Basi tutatia yetu huku tunacheka na kushangaa maisha ya wazee wetu na hawa wakijiona kuwa wao walikuwa watu wa kisasa kwa wakati wao. Wazee wetu wote walikuwa ‘’sharp dressers’’ na wapenzi wakubwa wa muziki. Baadhi ya mambo naona na sisi watoto waliturithisha na yameathiri sana mtindo w maisha yetu.

Tukimaliza hapa ndipo tutaingia katika mazungumzo mazito. Nitakuwa na maswali ya kumuuliza Kleist kuhusu historia ya baba yake na ukombozi wa Tanganyika kupitia TAA na kisha TANU. Ghafla ile hali ya vicheko itatoweka na Kleist anabadilika anazungumza kwa kuchunga sana ulimi wake akichagua maneno na hali ya simanzi nyepesi itatanda.  Kleist alinifahamisha kuwa katika vitu ambayo yeye vimemstaajabisha sana ni kuwa Iliffe akimtegemea sana Daisy katika kupata taarifa za African Association kuasisiwa kwake na mambo mengine na Daisy akimuuliza baba yake lakini kitu cha kustaajabisha ni kuwa Iliffe hakutaka kukutana na Abdul Sykes kupata historia ile moja kwa moja. Wakati ule Daisy alikuwa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam akiwa mmoja wa wasichana wachache wa Kariakoo kupata elimu ya juu.  Namna hii ikawa nakusanya ‘’notes,’’katika mazungumzo yangu na Kleist na nilihisi kama vile Kleist alikuwa kama mtu aliyekuwa anahitaji, ‘’therapy,’’ ya aina fulani kupunguza joto katika nafsi yake. Alikuwa ni mtu ambae alitaka sana mchango wa baba yake utambuliwe katika kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika. Kwa miaka mingi haya ndiyo yakawa maisha yetu mimi na Kleist. Mimi nikijichukua kama mwanafunzi na Kleist ndiyo mwalimu wangu.

Mimi na Kleist tukawa sasa tuna maisha yetu tumejizingirisha sisi wawili tu tuko nje ya lile duru letu la kawaida la marafiki zetu wengine kama marehemu Yusuf Zialor, Wendo Mwapachu, Abdallah Tambaza, Abdul Mtemvu kwa kuwataja wachache na ikawa kama chama cha wachawi. Huingii hadi nawe uwe mwanga. Hii ikawa ‘’Exclusive Club,’’ yaani chama makhsusi cha watu wawili tu. Miaka ilivyokuwa ikipita nami ndivyo nilivyokuwa nafaidika na kuzidi kuchota elimu ile kutola kwa Kleist. Akienda Geneva na akija Dar es Salaam tunakutana kama ada yetu na mazungumzo yanaendelea. Lakini Kleist hakuwa mtu wa kusukumwa aharakishe. Kila kitu kilikuwa kikienda kwa kasi aliyokuwa akiitaka yeye. Alipatapo kuniambia mwanzo kabisa nilipomwambia kuwa nataka kuandika kitabu cha baba yake, ‘’Mohamed haya mambo yanataka subira na wewe ujue lipi la kusema na lipi la kuacha kusemwa.’’ Maneno haya aliyoniambia Kleist yalikuwa sawasawa na maneno ambayo Daisy aliambiwa na mwalimu wake wa historia, John Iliffe mwaka wa 1968 alipotaka kuandika historia ya baba yake. Sababu ya haya ni kuwa tayari palishazuka sintofahamu chinichini katika historia ya TANU.


Kulia waliosimama ni Mohamed Said, Yusuf Zialor, Kleist Sykes, Bubby, Abdallah Tambaza,
waliochutama Abdul Mtemvu, Wendo Mwapachu na Kaisi 1968

Siku moja nikamwambia Kleist maneno aliyonieleza Dossa Aziz nyumbani kwake Mlandizi Nilimwambia Kleist, ‘’Mzee Dossa kaniambia kuwa TANU ilitaka kuandika historia ya TANU miaka ya mwanzoni ya uhuru.’’ Kleist akanijibu kuwa hiyo ni kweli na yeye alikuwa akienda pale Ofisi ya TANU akitoka shule kwenda nyumbani wakati baba yake na Dr. Wilbert Klerruu wakiandika historia ile. Kwa huzuni Kleist akanieleza kuwa kazi ule haikuweza kukamilika licha ya kuwa baba yake alikuja na nyaraka zote za TAA na TANU. Kleist hakunambia kwa nini ile kazi iliishia njiani. Miaka mingi ya mazungumzo na Kleist nilijua wapi nisimame. Akitumia lugha ya kiungwana Kleist alikuwa akinambia kuwa TANU ilikuwa inaikataa historia ya baba yake katika uhuru wa Tanganyika. Jambo hili lilichoma sana moyo wa Kleist. Nilijua hapa ni mahali pa kusimama nirejee wakati mwingine kwa mazungumzo. Mambo haya yalinifikirisha sana.


Kushoto mbele Kleist Sykes na mwanae Abbas Sykes
Waliosimama kulia ni Abdul Sykes katika sare ya King's African Rifles (KAR) na Ally Sykes, 1942
Mwaka wa 1988 katika kukumbuka ya miaka 20 baada ya kifo cha Abdul Sykes, Ally Sykes alinunua nafasi katika Daily News na Uhuru ili kuchapa kumbukumbu ya kifo cha kaka yake.  Usiku Kleist akapokea simu kutoka kwa Reginald Mhango wa Daily News akimwomba radhi kuwa ingawa wamelipia tangazo la kumbukumbu ya baba yake lakini yeye hawezi kuidhinisha ichapwe hadi atakapopata ruhusa kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma kwa sababu maisha ya baba yake yamegusa historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika. Kleist alisoma na Mhango Aga Khan School kwa hiyo wakijuana vizuri. Kleist alimwambia Reginald kuwa hayo ndiyo yalikuwa maisha ya baba yake na hana namna ya kuweza kubadili historia hiyo. Kleist akamshauri Mhango aende kwenye gazeti la Sunday News la tarehe 20 October 1968 atakuta taazia ya baba yake iliyoandikwa na Mhariri wa Tanganyika Standard Brendon Grimshaw  inayoeleza hayo yaliyopelekwa Daily News.  Kumbukumbu zile zilichapwa na Daily News na Uhuru lakini uhariri uliopitishwa uliondoa utamu wote wa kumbukumbu ile. Lile ambalo lililokusudiwa halikupatikana.


Earle Seaton na Julius Nyerere
Inawezekana huu mtiririko wa dharau kwa baba yake ndiyo uliomfanya Kleist anipe moja ya labda siri kubwa katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Ilikuwa mkakati aloweka baba yake na Hamza Mwapachu katika kuunda TANU toka mwaka wa 1950. Hiyo ndiyo siku aliponitajia jina la Earle Seaton. Mimi nilikuwa nikimjua Seaton kijuujuu tu. ‘’Earle Seaton alikuwa rafiki ya baba yangu,’’ Kleist alianza. ‘’Seaton alikuwa anatoka Bermuda. Seaton alikuwa mwanasheria Moshi. Seaton akimsukuma baba aondoke Tanganyika aende kusoma Amerika baada ya kujua kuwa baba alikosa kwenda Makerere College 1942 kwa kuwa Waingereza walimtia katika jeshi lao, King’s African Rifles (KAR) kwenda Burma katika Vita Kuu ya Pili.’’ Mkakati huu wa Abdul Sykes na Hamza Mwapachu pamoja na Stephen Mhando na Dr, Vedasto Kyaruzi na Dossa Aziz ndiyo uliomwingiza Seaton katika siasa za Tanganyika kupitia TAA Political Subcommittee. Seaton akawa mshauri mkuu wa TAA na akaisaidia TAA katika kutayarisha mapendekezo ya katiba yaliyoitishwa na Gavana Edward Twining mwaka wa 1949. Kleist akanambia kuwa hotuba ya Nyerere UNO ilitoka katika mapendekezo haya ambayo pia yalijadiliwa katika mkutano wa kuasisi TANU 1954.  Sasa nikawa namwangalia Kleist kwa jicho jingine. Huyu anaezungumza na mimi hakuwa Kleist kwani ilinidhihirikia kuwa haya hayakuwa maneno yake Kleist, huyu ni baba yake anazungumza na mimi kutoka kaburini.  Kleist alikuwa mtu wa subira kubwa sana. Yote haya akiyajua na akikaa kimya wakati baadhi ya watu ndani ya TANU baada ya uhuru kupatikana 1961 wakawa akiifanyia dhihaka TAA na kukipa chama kile kila aina ya majina ya kebehi kuwa hapakuwa na siasa katika TAA bali starehe nk. nk. Kleist sasa akawa moja ya funguo katika uandishi wa maisha ya baba yake na historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.

Ndiyo siku moja Kleist akaniangushia bomu nusura likatishe maisha yangu. Akanionyesha shajara (diary) za baba yake akaniambia, ‘’Hizi shajara siwezi kuzitoa humu ndani nikakupa kwani zina na mengi sana kuhusu historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika na sijaweza kuzisoma zote kwa kuwa baadhi zimeandikwa katika hati mkato.’’ Kleist akanambia kuwa amesoma nini baba yake aliandika siku alipozaliwa tarehe 27 June, 1950. Kleist akacheka akanambia, ‘’Baba aliniita, ‘’Prince.’’ Hakika baba yake hakukosea kumvika taji mwanae kwani Kleist alikuwa na sudi ya kupendeka. Alipokuwa UNHCR Lusaka, Zambia naambiwa Thabo Mbeki alikuwa akitembea na ufunguo mmoja wa nyumba ya Kleist ili aweze kuingia wakati hata kama yeye hayupo. Huu ndiyo ulikuwa wakati ule wa mapambano ya ANC na makaburu wa Afrika Kusini yamepamba moto.

Halikadhalika mmoja wa mawaziri wakuu wa Mozambique alipata kumuomba Kleist arejee ‘’nyumbani,’’ Msumbiji ampe kazi. Ilikuwa wakati yupo na UNHCR, Lusaka basi siku moja katika mazungumzo na Waziri Mkuu huyu mjini Maputo, Kleist akamueleza kuwa yeye asili yake ni Msumbiji, Kleist akanambia Waziri Mkuu akashtuka sana Kleist alipompa historia ya ukoo wake. Waziri Mkuu akamwambia, ‘’Kleist tuko huru sasa rudi nyumbani nikupe kazi.’’ Kleist anasema huyu bwana alidhamiria khasa kuwa arudi ‘’nyumbani,’’ ampe kazi waijenge pamoja Msumbiji. Kleist alikuwa na mengi na si rahisi kuyaeleza yote.

Siku chache kabla hajafariki Kleist alikuwa alinipigia simu akaniahidi kunipa nyaraka mbili.  Moja ilikuwa ''Admission Letter,'' ya 1953 ya baba yake kutoka Princeton University na nyingine barua pia ya 1953 kutoka kwa Earle Seaton. Ndani ya barua ile Seaton alimwambia Abdul Sykes kuwa asiache kufika UNO kufuatilia mijadala ya Mandate Territories atakapokuwa Princeton, New Jersey. Akaniambia pia alikuwa anataka niende kwake akanionyeshe picha za ufunguzi wa Petrol Station ya baba yake iliyokuwa Ilala mkabala na Ilala Boma. Petrol Station hii ilikuwa chanzo cha fedha nyingi ambazo baba yake alizitoa kwa TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Namuomba Allah amsamehe ndugu yetu Kleist Abdulwahid Sykes madhambi yake na ampe kitabu chake kwa mkono wa kulia.
Amin.