Showing posts sorted by date for query baraza la mitihani. Sort by relevance Show all posts
Showing posts sorted by date for query baraza la mitihani. Sort by relevance Show all posts

Tuesday, 2 January 2018


Prof. Juma Mikidadi


SHEIKH PROFESA JUMA MIKIDADI MTUPA: Kutoka kuchunga mbuzi hadi udaktari wa falsafa ya Sheria na sharia
NA RASHID MTAGALUKA
Kama unadhani ipo siku utashushiwa mafanikio kutoka mbinguni mithili ya vyakula vya Manna na Sal-wa ambavyo Allah aliwashushia Wana wa Israeli enzi za Nabii Musa (amani ya Allah imshukie), utakuwa umekosea!
Hilo ni somo kubwa tunalojifunza tunaposoma maisha ya Sheikh Profesa Dkt Juma Mikidadi Omar Mtupa, aliyewahi kuwa mchunga mbuzi na kuwa msomi wa kutegemewa mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya Sheria na Sharia kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza.
SHEIKH PROFESA JUMA MIKIDADI NI NANI?
Yeye ni katika wasomi wachache wa Falsafa ya Sheria na Sharia (Legal Philosophy & Islamic Law) hapa nchini na ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki aliyezaliwa Deta, kijiji cha Mbwela, wilaya ya Rufiji (sasa Kibiti) mkoani Pwani Julai 7, 1949 akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto 14 wa marehemu baba yake.
Katika mahojiano naye nyumbani kwake Mkundi, Manispaa ya Morogoro hivi karibuni, Prof Mikidadi alinambia, akiwa na umri mdogo, kabla hata hajaanza shule, alilazimika kufanya kazi ya uchungaji mifugo kwa sababu watoto wawili wakubwa wa Mzee Mtupa walikuwa wanawake na mwingine, kaka yake, alikuwa masomoni.
“Nilichelewa kuanza masomo yangu ya sekula kutokana na kibarua cha uchungaji mbuzi na kondoo wa marehemu mzee, ila kaka yangu aliyekuwa akisoma Dar es Salaam aliacha akarudi nyumbani ili mimi nami nianze kusoma, akaniokoa na kazi ya uchungaji mbuzi,” alisema huku akiangua kicheko.

SAFARI YAKE YA KIMASOMO
Sheikh Prof. Mikidadi alianza masomo mwaka 1957 katika Shule ya Msingi Mbwela hadi darasa la nne alipopelekwa Shule ya Kati (Middle School) ya Manerumango, Kisarawe mkoani Pwani. Akiwa darasa la sita, alihama kutoka Shule ya Kati Manerumango, Kisarawe na kuhamia Shule ya Kati Utete ambako alimaliza darasa la nane mwaka 1964 na kufaulu mitihani yake yote.
Mwaka 1965 Sheikh Prof. Mikidadi alijiunga na Shule ya Indian Sekondari (sasa Azania) kwa ajili ya darasa la tisa. Hata hivyo, ada ya shilingi 900 kwa mwaka ilikuwa kubwa mno kwa hali ya maisha ya mzee wake ambaye hakuwa muajiriwa wa serikali. Hivyo, akiwa kidato cha pili aliomba uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mpwapwa, Dodoma ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1968 na kurudi Mbwela kuendelea na masomo ya dini.
“Elimu yangu ya dini ya awali niliipata kwa baba yangu mzazi ambaye alifungua madrasa kubwa mara baada ya kurudi Zanzibar alikokwenda kusoma kwa Sheikh Hassan bin Amir Al Shirazy miaka hiyo kabla hatujazaliwa.Hivyo wakati nikisubiri matokeo ya kidato cha nne, nikawa naendelea kusoma na kufundisha wenzangu Qur’an, Hadithi, Fiq’h na kadhalika” alisimulia Sheikh Prof Mikidadi.
Kwa bahati, Sheikh Mikidadi alichaguliwa kwenda kusomea ualimu katika Chuo cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam ambako alijifunza mbinu nzuri za kufundisha pamoja na kufundishwa Sayansi mpya (New Science) kwa shule za msingi. “Mpango ule wa sayansi mpya ungeendelea, nchi isingekuwa na uhaba wa wataalamu wa sayansi shule za msingi hadi vyuo vikuu, sijui hata serikali waliuuaje mpango mzuri wa elimu kama ule,” alisema kwa mshangao.
Alipomaliza chuo na kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, Profesa Mikidadi aliajiriwa na Wizara ya Elimu kwenda kufundisha katika Shule ya Msingi Ndundunyikanza, Rufiji mkoani Pwani, kisha alihamishwa Kihongoroni, Mbwela karibu na kwao ambako alipangwa kuwa Mwalimu Mkuu Msaidizi na baadaye kupandishwa daraja kuwa Mwalimu Mkuu.
Miongoni mwa wanafunzi wake akiwa Kihongoroni ni pamoja na Abdul Jabir Marombwa, Mbunge wa Kibiti aliyemrithi baada ya Prof Mikidadi kuachia jimbo hilo mwaka 2005.
Baada ya miaka miwili, Kihongoroni, Sheikh Prof. Mikidadi aliomba uhamisho kwenda kufundisha Dar es Salaam akilenga kujifunza zaidi elimu ya dini ya Kiislamu, jambo ambalo alifanikiwa na alipangiwa Shule ya Msingi Darajani. Kuishi Dar es Salaam ikawa ni fursa nyingine ya kusoma zaidi Misingi ya Qur’an, Fiqh, Hadithi na lugha ya Kiarabu, mmoja wa walimu wake akiwa ni Katibu Mkuu wa kwanza wa Bakwata, Marehemu Sheikh Muhammad Ali Al-Buhriy.
Aidha, Sheikh Prof Mikidadi pia alisoma kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma Markaz ya Chang’ombe ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Azhar Sharif cha nchini Misri, na alimtaja Sheikh Jabir Katura kuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliomsaidia sana kupata vitabu.
Kutokana na watu kufuatilia juhudi zake, mwaka 1971/72 Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) chini ya Sheikh Mkuu, Mufti Hemed Bin Jumaa Bin Hemed, lilimuomba kutoka Serikalini ili akafundishe katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim.
“Kutokana na uchapaji kazi wangu, nilipandishwa na kuwa Makamu Mkuu wa Shule kabla sijapata ufadhili wa kwenda Saudi Arabia mnamo mwaka 1972 kusoma masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina,” alisema.
Profesa alianza kusoma lugha ya Kiarabu kwa miezi sita, na alipofaulu vizuri alipelekwa moja kwa moja katika kitivo cha Sheria.
Kwa mujibu wa Profesa, alisoma masomo mengi yakiwemo Qur’an, Hadithi, Lugha ya Kiarabu na alimtaja msomi maarufu nchini humo ambaye alipata kuwa Mufti wa Saudia, Sheikh Abdulaziz bin Abdallah bin Baz kama mwalimu aliyechangia mafanikio yake makubwa ya kielimu.
“Ingawa alikuwa kipofu, alihifadhi Hadithi nyingi kama siyo zote alizokuwa akitufundisha pale Chuo Kikuu kiasi kwamba, sisi wazima tulikuwa tukikosea kuzisoma, yeye alikuwa akisahihisha,” alisifu.
Alipomaliza Shahada yake ya kwanza mwaka 1979 alirejea nyumbani Tanzania na kuripoti Wizara ya Elimu. Hata hivyo, Bakwata waliendelea kumng’ang’ania arudi kwao aongoze Idara ya Elimu iliyohitaji msomi kama yeye. “Nilirudi Bakwata na kupangiwa nafasi ya Katibu wa Idara ya Elimu Makao Makuu hadi mwaka 1982 nilipopata tena ufadhili kutoka kwa taasisi ya Mfalme Faisal (King Faisal Foundation) kwenda Riyadh kusoma Shahada yangu ya pili,” alisimulia.
Alipofaulu mtihani wake wa usaili mjini Riyadh aliambiwa aende Kampasi ya Madina akaanze kusoma kozi mpya ya Falsafa ya Sheria (Legal Philosophy) ambayo kwa maelezo yake haikuwa na wanafunzi wengi.
“Kwa kuwa nilichelewa kozi hii kwa miezi mitatu nyuma, nilijitahidi kujisomea hadi mwalimu wetu mmoja alipogundua mimi naelewa vizuri lugha ya Kiingereza, aliniteua kuwa mkutubi katika maktaba ya Chuo, jambo lililonisaidia kusoma zaidi kila kitabu kilichokuwemo kwenye maktaba ile,” alisema huku akicheka akifananisha hali ile na Fisi aliyepewa ulinzi wa ngozi za mbuzi!
Mwaka 1985, Sheikh Prof Mikidadi alihitimu shahada yake ya pili. Ufaulu wake mzuri ulimpelekea mmoja wa walimu wake kumshawishi akatafute Chuo nchini Uingereza kwa ajili ya PhD ya Falsafa ya Sheria.
“Ili uweze kukubalika kusoma ngazi hiyo ya elimu, ilikuwa lazima ufaulu mtihani wao wenye maswali 200 kwa dakika 30 tu, nilijitahidi na hatimaye nilifaulu na hivyo mwaka 1987 nilianza masomo yangu katika fani ya Falsafa ya Sheria ya Kimagharibi na Sharia za Kiislamu (Legal Philosophy & Islamic Law) katika Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza,” alibainisha.
Mwaka 1989, Prof. Mikidadi alimaliza masomo yake na kurejea nchini. Alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutafuta ajira lakini alikosa kwa kuwa wakati huo chuo hicho hakikuwa na Kitivo cha Falsafa ya Sheria na Sharia.
Mwaka 1991 alifanikiwa kupata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya ambacho kilikuwa na kitivo hicho mpaka mwaka 1994 alipoomba likizo.

NAMNA ALIVYOINGIA KWENYE SIASA
Mwaka 1994 akiwa Chuo Kikuu cha Nairobi, aliitwa na wazee wa Kibiti ili akagombee ubunge wa jimbo hilo jipya ambalo awali lilikuwa ni sehemu ya jimbo la Rufiji.
Alisema haikuwa rahisi kuwakatalia wazee hao walioonesha imani naye. Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Prof Mikidadi alishinda ubunge na aliliongoza jimbo hilo hadi mwaka 2005 alipoamua kwa hiyari yake kuachana na kazi hiyo na kurejea darasani kufundisha.
Akiwa Mbunge wa kwanza wa jimbo la Kibiti linalozungukwa na visiwa 16 Sheikh Prof Mikidadi alifanikiwa katika mambo mengi ikiwemo kuimarisha elimu, afya na miundombinu, ingawa alikiri katika baadhi ya maeneo hakukamilisha mahitaji na matarajio yake mwenyewe na wananchi wake.

KWA NINI ALIACHA UBUNGE
Nilitaka kujua sababu iliyomfanya Sheikh Prof Mikidadi aache kuwania tena ubunge wakati wanasiasa wengine ‘wanakomaa’ zaidi ya miaka 20.
“Kulikuwa na sababu tatu za msingi. Kwanza Afya yangu haikuruhusu kuendelea na kazi ya ubunge, ukizingatia ni kazi ya kuwazungukia wananchi kila mara. Pili ilikuwa tayari vijana wa kushika nafasi hiyo wapo, na mimi sikuona haja ya kung’ang’ania. Na tatu, nilipata taarifa ya kuyumba kwa Kitivo cha Falsafa kule Chuo Kikuu cha Nairobi, kwa hiyo nilikusudia nirudi kuendelea na kazi yangu niliyoisomea,” alibainisha.
Hata hivyo, wakati akijiandaa kwenda Nairobi, aliombwa na watu anaowaheshimu aache kwenda kujenga nyumba ya wenzake wakati yake inaporomoka, akimaanisha alitakiwa akafundishe kwenye Chuo Kikuu kipya cha Waislamu cha Morogoro (MUM).
Alikubaliana na fikra hiyo na kuanzia mwaka 2006 Sheikh Prof Mikidadi alianza kazi MUM kama Mhadhiri wa muda mfupi katika Idara ya Sheria na Sharia, na ilipofika mwaka 2007 aliajiriwa na kukabidhiwa Kitivo cha Sheria na Sharia kama Mkuu wake, kazi aliyoitumikia mpaka mwaka 2013 alipoomba na kupewa likizo kutokana na kutetereka kwa afya yake.

ALIVYOUPATA UPROFESA
Sheikh Prof Mikidadi alisema uprofesa katika mchakato wa elimu unaweza kuwa mzunguko mrefu sana au unaweza kuwa mfupi sana, inategemea na jitihada za muhusika katika kufanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema mbali ya tafiti, uandishi wa vitabu na machapisho mbalimbali yanayoweza kutumika kama rejea kwenye taasisi za elimu na nyinginezo, kunaweza kukamfanya msomi afikie daraja la uprofesa.
“Kwa upande wangu imenichukua miaka zaidi ya 10 kukamilisha tafiti na uandishi wa vitabu katika fani yangu ya Falsafa ya Sheria na Sharia ambayo hapa nchini sina hakika tuko wangapi, lakini idadi yetu ni ndogo sana,” alisema.

ANAZUNGUMZIAJE MITAALA YA DINI TANZANIA
“Kwa kweli mitaala ya dini hapa kwetu haijakaa vizuri, hivyo ni vema wadau wote wa elimu ya dini ya Kiislamu wakajadiliana kwa maslahi mapana ya kizazi hiki na kijacho,” alishauri Sheikh Prof Mikidadi.
Prof Mikidadi pia alitoa wito kwa wasomi wa dini ya Kiislamu wakutane na kupeana majukumu ya kufanya utafiti katika fani yao ili kupata majibu yatakayoisaidia jamii ya Waislamu kuendelea kuwa Umma mmoja. Sheikh Prof Dkt Juma Mikidadi Omar Mtupa ameoa na ana watoto 12.



Kulia: Dr, Ramadhani Dau, Rostam Aziz, Adam Malima, Sheikh Talib,
Prof. Juma Mikidadi na Mohamed Said Eid El Fitr, Masjid Maamur
21 February 1996

Monday, 18 December 2017



''Allah ni Mjuzi Allah na ni Mbora wa kulipa. 
Sheikh Ponda utayakuta malipo yako kwa Allah yakiwa makubwa kwa subra na ustahamilivu kwa ajili ya dini yake. 
Hukuwa tayari kuuza uhuru wako kwa matakwa ya wenye kudhulumu. 
Muda wote ulitutia moyo mawakili wako kila tulipokutana na vitimbi. 
Mara nyingi sisi mawakili tulikuwa kama wateja na wewe ndiye wakili. 
Hakika wewe ni kiongozi. 
Umma huu wa Waislam wa Tanzania utaishi kwa mfano wako. 
Alhamdulilah leo uko huru baada ya miaka miwili na miezi mitatu jela ukiwa na jeraha kubwa la risasi. 
Allah anayo siri kubwa katika maisha yako Sheikh Ponda. 
Allah akuhifadhi kiongozi wetu.
Amin.''
Wakili Juma Nassoro

Sheikh Ponda na Wakili Juma Nassoro wakiwa Mahakamani

Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa katika pingu Mahakamani

Ilikuwa katika semina ya Vijana wa Kiislam Tanzania mwaka wa 1988 ndipo kwa mara ya kwanza nilipofahamiana na Sheikh Issa Ponda. Ninachokumbuka kwa Sheikh Ponda ni kuwa alitusalisha sala moja na niliusikia usomaji wake mzuri wa Qur'an. Nilimpenda kutoka siku hiyo. Semina hii ilikuja baada ya mambo mengi dhidi ya Uislam kutokea nchini. Kulikuwa na sakata la Sophia Kawawa kutaka Qur'an ibadilishwe. Hii ilitokea mwezi Mei 1988. Baada ya kauli hiyo palifanyika maandamano makubwa Zanzibar kumpinga Sophia Kawawa na Waislam walishambuliwa, baadhi wakauliwa na wengine wakapata ulemavu wa maisha. Sheikh Said Gwiji mshtakiwa namba moja na wenzake walishitakiwa na wakafungwa jela miezi 18. Kosa lao likiwa ni kuihami Qur'an ya Allah isichezewe. Kulikuwa na vita vikipigwa dhidi ya vazi la hijab na kesi maarufu ilikuwa ya Fikira Omari mfanyakazi wa Kiltex. Kulikuwa na kesi ya Kurwa Shauri  aliyeshitakiwa kwa ''uchochezi'' na mambo mengine. Katika hayo kulikuwa na tatizo la Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa akimbughudhi Rais Mwinyi na kuwashambulia Waislam hasa wenye asili ya Kiasia na Kiarabu. Kulikuwa na pia na ''Christian Lobby,'' mtandao wa siri katika vyombo vya habari vilivyokuwa vikiwapiga vita Waislam waliokuwa katika serikali ya Rais Mwinyi achilia mbali kuupiga vita Uislam wenyewe wakitumia nafasi zao katika vyombo hivyo. 

Historia ya Waislam wa Tanzania itakapokuja kuandikwa jina la Sheikh Ponda Issa Ponda litaunganishwa na jina la Mufti Sheikh Hassan bin Amir kwa kitu kimoja nacho ni ardhi ya Chang'ombe Dar es Salaam ambako Waislam chini ya uongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) walikusudia kujenga Chuo Kikuu mwaka wa 1968. Katika uwanja huu ndipo Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere akishuhudiwa na Tewa Said Tewa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir aliweka jiwe la msingi la chuo hicho. Chuo hakikujengwa na EAMWS ikapigwa marufuku na serikali. Mambo hayakuishia hapo. Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa na kufukuzwa nchini akarudishwa ''kwao'' Zanzibar. Serikali ikaunda BAKWATA na Chuo Kikuu cha Waislam hakikujengwa. Nini kilisababisha nakma hii? Waliokuwa karibu na Sheikh Hassan bin Amir wanasema katika siku zake za mwisho kila alipotajiwa ule mradi wa chuo kikuu alikuwa akilia na kusema ilikuwa hamu yake kujenga chuo Kikuu kama Azhar ya Misri na akifika hapo alikuwa akibubujikwa na machozi. Wakati ule Sheikh Hassan bin alikuwa na miaka zaidi ya 90 na aliishi na simanzi hizi hadi alipokufa mwaka 1979. Huu uwanja wa Waislam ndiyo Sheikh Ponda alipouchukua kuurudisha mikononi kwa Waislam ndipo alipokusudia kujenga msikiti na kuupa jina la Sheikh Hassan bin Amir. 

Kulia Sheikh Ponda Issa Ponda, Wakili Juma Nasoro na Rajab Katimba
Mahakama Kuu baada ya ushindi wa kesi ya rufaa

Sheikh Ponda akifunguliwa pingu na Askari Magereza Mahakamani

Kushoto ni Mzee Bilali Rehani Waikela Muasisi wa TANU Tabora 1955,
Katibu wa EAMWS Jimbo la Magharibi na Inaaminika ni Yeye Peke Yake
Aliyehai Aneijua Historia Yote ya Kiwanja Cha Chang'ombe na Ujenzi wa Chuo 
Kikuu Cha Waislam.

Historia ya uhuru wa Tanganyika ina mashujaa wengi katika siasa ambao walikuwa
masheikh tena wa sifa na kutajika.

Hawa walikuwa mstari wa mbele katika kupambana na dhulma za wakoloni na ndiyo

walikuwa bega kwa bega na Baba wa Taifa.

Kulikuwa na Sheikh Hassan bin Amir na Sheikh Said Chaurembo katika
TAA - Political Subcommittee.

Kushoto: Sheikh Hassan bin Amir, Julius Nyerere, Sheikh Abdallah Chaurembo,
Rashid Kawawa na Tewa Said Tewa
Hii ilikuwa 1950.
Kulikuwa na Sheikh Mohamed Ramiyya wa Bagamoyo katika TAA na TANU.

Kushoto: Idd Faiz Mfungo, Sheikh Mohamed Ramiyya, Julius Nyerere,
Saadani Abdu Kandoro,Haruna Taratibu Dodoma 1956
Kulikuwa na Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa
TANU.



Kulia: Bi. Titi Mohamed, Clement Mohamed Mtamila, Sheikh Suleiman Takadir, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
Waliosimama nyuma kulia ni John Rupia, Rajab Diwani na Mama Maria Nyerere
Kulikuwa na Sheikh Yusuf Badi wa Lindi katika TANU.

Kulikuwa na Sheikh Rashid Sembe shujaa wa Kura Tatu katika mkutano wa
TANU kujadili Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 1958.

Sheikh Abdallah Rashid Sembe
Mifano iko mingi inachotakiwa ni kwa kuisoma historia ya TANU na uhuru wa 
Tanganyika itakudhihirikia kuwa masheikh siku zote wamekuwa mstari wa mbele 
katika kupambana na dhulma ya aina yoyote katika jamii.


Picha ya Mwaka 2012 ya Sheikh Ponda Akisimama Kuomba Dua Mbele ya
Kibla Cha Msikiti wa Kichangani, Magomeni Dar es Salaam Kabla ya 
Kuongoza Maandamano ya Waislam Kupinga Dhulma Dhidi ya Wanafunzi 
Waislam Katika Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)


Ulinzi Mahakamani Morogoro katika kesi ya Sheikh Ponda

Askari wakilinda usalama wakati Waislam wa Morogoro wakitoka mahakamani
Waislam akina mama Morogoro wakitoka katika kesi ya Sheikh Ponda
Ulinzi katika kesi ya Sheikh Ponda Mahakamani Morogoro

Waislam wa Morogoro wakitoka kusikiliza kesi ya Sheikh Ponda
Mahakama ya Morogoro


Sheikh Ponda na Mzee Bilal Rehani Waikela nyumbani kwa
Mzee Waikela Tabora

Kushoto: Mzee Bilal Rehani Waikela na Mwandishi Mahakamani Morogoro

Sheikh Ponda katikati ya mawakili wake Mahakamani Morogoro

Sheikh Ponda Akipelekwa Mahabusi Mwanzo wa Kesi Dar es Salaam




Saturday, 5 August 2017



WALIOCHAGULIWA KUPATA ELIMU YA JUU CHINI YA UFADHILI WA SERIKALI YA OMAN


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein,(kulia) akizungumza na Waziri wa Elimu ya Juu wa Nchini Oman,Dk.Rawya Saud Al Busaid, Ikulu Mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein,(kulia) akizungumza na Waziri wa Elimu ya Juu wa Nchini Oman,Dk.Rawya Saud Al Busaid, Ikulu Mjini Zanzibar
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kamati ya pamoja inayoratibu program ya “Oman Academic Fellowship” (OAF) inayodhaminiwa na Falme ya Oman, inapenda kutangaza kwamba waombaji wafuatao wamekubaliwa kupata udhamini wa masomo kwa ngazi za Masters na PhD kwa mwaka
2014/2015 katika masomo walioomba kama inavyoonekanwa kwenye Jadweli.
Waombaji hawa wanatakiwa wafuate maelekezo yafuatayo:
– Wawasilishe kopi za vyeti na vyeti vyao vya asili kwa Naibu Makamu Mkuu wa
Chuo, Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar, kwa ajili ya kuthibitishwa
– Watafute vyuo kwa ajili ya masomo yao. Muombaji anaweza kuomba Chuo chochote
ulimwenguni ambacho kimo katika vyuo 200 bora ulimwenguni katika mfumo wa
Shanghai Ranking inayoparikanwa katika tovuti: http://www.shanghairanking.com
– Wafanye mitihani ya lugha ya Kiingereza na wapate alama kama ilivyotangazwa
Kwa taarifa zaidi, waombaji waliokubaliwa wawasiliane na Naibu Makamu Mkuu –
Taaluma, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Tunguu Campus. Au watumie anuani
za barua pepe zifuatazo: dvcacademic@suza.ac.tz au haji.mwevura@suza.ac.tz
No Name Program

IMG_8057
1 Mohamed Mbarouk Suleiman Teacher Education/ Curriculum Development (PhD)
2 Rajab Kheir Rajab Teacher Education/ Curriculum Development (PhD)
3 Mwanajuma Salim Othman Rural Development (PhD)
4 Salha Abdalla Said Internal Medicine (Masters)
5 Aida Mohammed Ali Pediatrics (Masters)
6 Sakina Ahmed Alawy Al
Jamalullayl
Biochemistry (Masters)
7 Miza Silima Vuai Microbiology (Masters)
8 Amne Nassor Issa Microbiology (Masters)
9 Patima Kheri Koba Early Childhood Education (Masters)
10 Yussuf Ali Said Majid Jahaadir Early Childhood Education (Masters)
11 Tamasha Juma Therea Early Childhood Education (Masters)
12 Adam Abdulla Makame Oil and Gas Management (Masters)
13 Zaituni Mussa Ali Tourism Marketing (Masters)
14 Moh’d Idrissa Haji Jecha Inclusive Education (Masters)
15 Kassim Omar Tourism and Hospitality Management (Masters)
16 Fatma Khamis Said Tourism marketing (Masters)
17 Alawiya Nasser Finance (Masters)
Chanzo: SUZA

Wednesday, 24 May 2017


Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma, 1999


Annur Na.187- Feb.5-11, 1999
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma


Kitwana Selemani Kondo
Mh. Kitwana S. Kondo: Mheshimiwa Spika, naomba nikushuru sana.  

Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 4 Novemba, 1998 hapa Bungeni. Hotuba hii Mheshimiwa Spika ina ukweli, ina usahihi na pia ina uungwana. (Makofi). 

Mimi nataka ninukuu vifungu viwili katika hotuba hii, navyo ni vifungu vya mwisho. Lakini kabla sijafanya hivyo, nataka nimwambie rafiki yangu, mpenzi wangu Dr. Msina kwa manung’uniko yake ya mambo aliyofanyiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, mimi ninazo habari na sio mimi tu, watu wengi wanazo habari kwamba Wasukuma na Mkuu wa Mkoa wa Tabora ni Msukuma na Wanyamwezi na kidogo Wadigo wana tabia ya wizi. Kwa hiyo yaliyomkuta ni mahali pake. (Kicheko/Makofi) 

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ningependa sasa niende kwenye vile vifungu nilivyosema kuwa nitavinukuu. Katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, mwisho inasema hivi, "Mheshimiwa Spika, baada ya miaka mitatu ya Urais, nathubutu kubadili maneno ya msanii mashuhuri wa visiwani, Siti bint Said na kusema Tanzania ni njema atakaye na aje. Nchi yetu Mwenyezi Mungu ameibariki sana. Ni nchi ya umoja, amani, upendo, bashasha, ukarimu uliopindukia. Ni nchi ya wapenda usawa na haki. Umoja wetu wa Kitaifa unatokana na imani yetu ya dhati juu ya usawa wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya sheria. Umoja unaoimarishwa na sera sahihi za kujenga jamii na kuandaa mazingira ya maendeleo ya haki, amani na utulivu kwa wote". (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, Mheshimiwa Rais anaendelea. Anasema hivi, "Umoja unaotahadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania". Ningependa niyarudie maneno haya. "Umoja unaotahadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania. Umoja unaolindwa kwa vita vya kudumu dhidi ya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, jinsia au majimbo". 

Mheshimiwa Spika, miaka mingi iliyopita, kwenye 1658 A.D. Mtu mmoja Galileo alisema, "Dunia ni mviringo". Makuhani wakamwambia huyu anakufuru, akashitakiwa akahukumiwa kuuawa na akachomwa moto. Leo Galileo amekuwa Vindicated. Kwa bahati mbaya Galileo mwenyewe hayupo kujua kwamba amepata Vindication. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni hiki cha umoja unaotadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano. Nimesema mara nyingi hapa kwako. Mheshimiwa Rais, hivi karibuni aliwahutubia Waislamu kwenye Baraza la Idd, akawaambia kwamba manung’uniko yao na malalamiko yao yote atayatazama na atayashughulikia akishirikiana na Baraza lake la Mawaziri. 

Sasa nina mambo mawili au matatu ambayo nataka kuyasema ambayo yanaweza kuleta mfarakano. Yanapandwa na serikali. Moja, karibuni hivi katika mwezi wa Ramadhani, mwezi wa Ramadhani kwa Waislamu ni mwezi Mtukufu, ni mwezi wa toba. 

Wale jamaa zangu wasiojua toba ni mwezi wa kurudi kwa Mungu. Wakati wa ukoloni na mimi nilisoma wakati wa Ukoloni mwezi wa Ramadhani shughuli zote zinafungwa, baadaye kwenye serikali yetu wenyewe shule hazifungwi. Lakini baada ya muda wanaachiwa watoto kurudi majumbani kwao au kwenda kwenye mabweni. Lakini mwaka jana na mwaka huu serikali ikaamua kuwa mitihani ya watoto wa kidato cha nne ifanywe mwezi wa Ramadhani na iendelee mpaka siku za Idd. Hiyo ni moja ya cheche za mifarakano. 

Kwa Rehema ya Mungu Alhamdulillah, baada ya kunung’unika Waislamu, Waziri wa Elimu na Utamaduni alitoa maelezo. Maelezo yale yakawaridhisha Waislamu na Mheshimiwa Rais akakubali kwa siku za Iddi, watoto wasifanye mitihani na haikufanywa mitihani. (Makofi) 

Lakini mimi ninalouliza ile sababu ya kuamua mwezi wa Ramadhani ifanywe mitihani ni nini? Ni Insensitivity, ni jeuri, ni kiburi, kwa sababu kuna wengine ambao ni wazito tuliwasikia wakisema, wakitaka kufanya mtihani na wafanye hawataki basi. Mimi nasema watu kama hao ndiyo watu wasioitakia kheri nchi hii. Siyo sisi tunakuja kusema hapa hadharani. Hao wanaosema wakitaka kufanya na wafanye na hawataki kufanya basi. Hao ndio wasioitakia kheri nchi hii. (Makofi) 

La pili, linaloweza kuleta mfarakano ni tabia ya serikali ya kuchelewesha makusudi kuandikisha taasisi za Kiislamu. Taasisi yoyote ya Kiislamu ikitaka kuandikishwa serikalini itachukua miaka miwili au mitatu. Sababu hazitolewi, hata kama kuna uchunguzi, watu waende wakatafute habari kwa nini inachukua miaka miwili, miaka mitatu? 

Mheshimiwa Spika, nilipata kusema hapa kwamba mimi ni mlezi wa Baraza la Maimamu Tanzania. Tumeomba Baraza la Maimamu kuandikishwa, sasa ni miaka mitatu, sababu haijulikani. Wengine kila wakiomba wanasema lazima kipatikane kibali toka BAKWATA. Leo ningependa nijue ipo sheria inayosema hivyo? Au ni matakwa tu ya wakubwa? Hilo la pili. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, la tatu, Sura ya 33 Aya ya 30 na ya 31 ya Qur’an inamtaka mwanamke akifika umri wa miaka 9 avae hijabu. Hijab maana yake avae nguo ya mikono mirefu, avae shungi, avae gwanda zuri na avae suruali inayoficha mapaja na mpaka magoti. Mimi najua ya kwamba serikali imetoa agizo kwa watoto wa shule kwamba wafanyiwe hivyo wale wa Kiislamu wanaotaka, sheria zote zinavunjwa. Dini ya Kiislamu inakataza pombe, Waislamu wanakunywa pombe. Sasa hilo anafanya mwenyewe. 

Lakini ninajua pia ya kwamba kuna shule nchini huku, kuna viongozi wa Idara ya elimu ambao wanakataa kutekeleza sheria hii au agizo hili na serikali imekaa kimya, nataka nijue ni kwa sababu gani? Tujue ni kwa nini. Hii ni amri ya Mwenyezi Mungu na serikali, Rais anasema tusifanye chochote kinachoweza kuleta mifarakano. 

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba huu mwaka wa 30 wa uhuru. Siku ya Ijumaa ni siku muhimu kwa Waislamu kama ilivyo kwa siku ya Jumamosi ni siku muhimu kwa Wasabato kama ilivyokuwa siku ya Jumapili ni siku muhimu kwa Wakristo wengine. Lakini siku ya Ijumaa ingawa kuna agizo la serikali kwamba Waislamu waachiwe waende wakasali. Kuna viongozi siku ile ndiyo siku ya kufanya Board Meeting, ili kumzuia Mkurugenzi ambaye ni Muislamu ambaye anapenda kazi yake aogope. Shule zinafungwa saa 7. Jumapili vitoto vidogo vidogo vya Kikristo vinakwenda kusali. Jumamosi vitoto vidogo vidogo vya Kikristo vinakwenda kusali. Siku hizi vitoto vidogo vidogo vya Kiislamu vinataka kwenda na wazazi wao. Naomba utaratibu ufanywe wa dhamiri kabisa kwamba Ijumaa saa 6 kazi basi kwa Waislamu. Wale wanaofanya Board Meeting waache wafanye saa 8, wafanye saa 9 na shule zote za Primary na Secondary zifungwe saa 6 ili kuwapa nafasi watoto wa Kiislamu waende wakasali. 

Mheshimiwa Spika, nina mengi lakini nitakuambia mwisho. La mwisho, Rais aliwaambia Waislamu wote pale Dar es Salaam kwamba atalishughulikia suala la elimu. Lakini akawashauri kwamba wale wafadhili ambao hivi sasa wanatujengea Misikiti wajenge pia shule. Hilo jambo zuri, na Waislamu wamelisikia na ninajua ya kwamba Waislamu wanataka hivi karibuni kumwendea Rais kwenda kumshukuru. Ila nina jambo moja, natoa mfano wa Dar es Salaam, Waislamu wanafikia asilimia 70 au zaidi. Kwenye magereza Dar es Salaam wengi kuliko Wakristo au watu wengine. Hawa wengi, hawana kazi, jela watakuwa wengi. (Kicheko) 

Lakini tuende kielimu. Ninayo ripoti ya mwaka huu. Waliofanya mtihani wa darasa la saba kuingia darasa la tisa, asilimia 71 Waislamu. Asilimia 29 ni wengine. Walioshinda katika wale asilimia 71 ni asilimia 21. Katika wale 29 walioshinda tena sema mwenyewe. Katika asilimia 29 waliokwenda shuleni ni asilimia 79. Katika asilimia 71 waliokwenda darasa la tisa ni asilimia 21. 

Sasa kuna moja, ama Waislamu wajinga ama akili yao haifanyi kazi, ama mtu ukiwa Muislamu wewe huna kitu, ama kuna kitu. Sasa namwomba Waziri anayehusika, anaposema aseme ya kwamba kwa hali ilivyo Waislamu wameumbwa wajinga. Au kwa hali ilivyo kuna sababu kadha, kadha. Mwalimu Nyerere alisema zamani ifanywe bidii ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Sasa bidii hii siyo ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Bidii hii ni ya kuwakandamiza waliokuwa chini. 

Mheshimiwa Spika, Rais Mkapa anawasaidia Waislamu. Tulimwendea, mimi mmojawapo kwa mambo mengi ambayo ameyashughulikia. Nina hakika ya kwamba mambo haya tuliyoyasema na aliyoambiwa na viongozi wa Kiislamu kule bungeni atayashughulikia. Lakini ninaamini kabisa ya kwamba hataweza peke yake bila ya msaada wa viongozi wangu hao walioko hapa. Wakisema hawa kwamba ndiyo kawaida yao hiyo. Atapata tabu Rais wangu. 

Mheshimiwa Spika, kengele ya pili imelia. Nashukuru sana. Lakini nataka niseme kwamba haya niliyoyasema, nasema kwa sababu najua mimi kwamba suala hili la mfarakano ni suala kubwa. Penye mfarakano hakuna maendeleo. Penye mfarakano hakuna cha uchumi. Kwenye mfarakano kuna ghasia. Kwa kuwa Rais ameomba tufanye kila jambo mfarakano usiwepo, basi serikali imsaidie Rais katika kutekeleza wajibu wake kwa makundi yote ili pawepo na usawa. (Makofi)  


Kitwana Selemani Kondo akifanya kipindi cha televisheni (TV Imaan) ''Walioacha Alama Katika Historia,''
nyumbani kwake Upanga tarehe 12 Septemba, 2012 akihojiwa na Mohamed Said

Sunday, 16 October 2016


Ni vigumu kuandika kwa lengo la kumkosoa mtu anayeheshimiwa na wengi kiasi cha kuitwa Baba wa Taifa la Tanzania na ambaye mengi mazuri ya nchi yetu – ikiwemo amani, umoja na mshikamano - vinatajwa kuwa vilitokana na uongozi wake mzuri ulioweka misingi imara ya utaifa  na maendeleo. 

Ni ngumu zaidi kama anayelengwa kukosolewa ameipa heshima nchi yetu huko kama mmoja wa kiafrika waliokuwa na uzalendo wa hali ya juu ambaye ukizungumzia  watu watano waliochangia kwa kiasi kikubwa ukombozi wa bara la Afrika kutoka mikononi mwa wakoloni huwezi kuacha kumtaja.

Ugumu wa kukosoa ni maradufu pale ambapo anayekosolewa yupo katika utaratibu wa kufanywa mtakatifu kupitia dini yake, tena kupitia harakati za kimataifa, kwa matendo yake makuu.

Ni ngumu zaidi kukosoa unapokusudia makala yako isomwe na watu wa wote kama uchambuzi huru usioegemea upande wowote na itoke katika kipindi ambacho watu wanakumbuka kifo cha muhusika kwa matamasha, mikutano, sherehe mbalimbali, huku wito ukitolewa kuwa tuzidi kumuezi kwani tulivyofanya sasa haitoshi!

Kazi ya kukosoa inakuwa ngumu zaidi  ikiwa mlengwa anakosolewa  kwenye mambo ambayo wengi wanaamini ndiyo mazuri yake, yaani ujenzi wa taifa (nation building). Licha ya hayo yote, lakini ntajaribu kukosoa, licha ya unyeti wa mada hii, na kukosoa bila kuingiza hisia zangu binafsi

Ujenzi wa Taifa
Kazi kubwa ya kwanza iliyofanywa na viongozi waasisi wa mataifa yetu ya kiafrika ilikuwa ni kujenga utaifa, kuwafanya watu wajisikie wamoja na washikamane bila kujali tofauti zao za makabila, dini, mahali wanapotoka na kadhalika. Ikumbukwe wakati wa ukoloni.
Katika nchi za Afrika ambako wazungu walitawala kwa sera ya wagawanye uwatawale (divide and rule) hii haikuwa kazi rahisi na ndiyo maana waliofanikiwa wanasifiwa mpaka leo – mmojawapo akitajwa kuwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania aliyeongoza nchi yetu kwa miaka 23 kuanzia 1961 hadi 1984 alipotangaza kung’atuka. 

Inasemwa kuwa shukran kwa uongozi wake Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano kwa amani na utulivu.  Watu wake ni wamoja na wanapendana sana. Inaelezwa na kuaminika kuwa mafanikio haya hayakuja hivi hivi bali ni kwa juhudi za Mwalimu Nyerere.

Katika baadhi ya mikakati ambayo inatajwa kuwa Nyerere aliitumia katika kujenga utaifa ni pamoja na kufifisha nguvu za taasisi za kimila, kukuza lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa kiunganishi cha watu wa makabila mbalimbali na pia kuwa na utaratibu wa lazima kwa vijana kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako walichanganyika na kujifundisha uzalendo.

Udini - Dosari Katika Utaifa Wetu
June 14, 1995, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikutana na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimanjaro kuzungumzia mustakbali wa taifa wakati taifa likijipanga kuchagua rais wa awamu ya tatu baada ya miaka kumi ya mrithi wa Mwalimu, Ali Hassan Mwinyi.

Katika hotuba yake Mwalimu Nyerere alielezea Tanzania kama nyumba mpya na imara iliyojengwa lakini ilikuwa haijatikiswa na dhoruba yoyote kuthibitisha uimara wake.  Baaade ilipopitiwa na dhoruba na misukosuko, nyumba ikaanza kuonesha udhaifu na nyufa zikajitokeza. Kumbe haikuwa imara kihivyo! Tukatanabahi. 

Nyerere alisema nyufa zilizojitokeza baada ya Tanzania kutikiswa zilikuwa za ukubwa tofauti, nyingine katika dari, nyingine katika ukuta na nyingine hata katika misingi.  Katika hotuba ile Nyerere alikusudia kuzungumzia kuhusu nyufa hizo za kushughulikiwa na kutaja sifa ya mtu aliyestahiki kuongoza nchi wakati ule ili ashughulikie nyufa hizo.

Katika hotuba yake nyingine aliyoitoa  katika mkutano Mkuu wa CCM Dodoma mwaka 1995 ambapo alizungumzia nyufa mojawapo  inayoonekena katika nchi yetu: suala la udini.  Alisema: “Watu wameanza kuzungumzia udini. Tulikuwa hatuzungumzi mambo ya udini-udini katika nchi hii. hata kidogo.''

Aliongeza: “Tulikuwa hatujali dini ya mtu, alikuwa anaijua peke yake. Ilikuwa haiji katika akili yetu kwamba tunapompima mtu tumchague huyu, tumfanye rais au tumfanye nani tunauliza dini yake, hatuulizi hata kidogo. Dini inatuhusu nini sisi. Hiyo ndiyo Tanzania tuliyokuwa tunajaribu kuijenga. Sasa watu  wanazungumza dini, udini bila haya, bila aibu. Wanajitapa kwa udini. Tunataa mtuchagulie mgombea ambaye atatusaidia kuondoa mawazo haya ya kipumbavu katika nchi yetu.”

Swali muhimu ambalo Mwalimu Nyerere hakuhangaika kulitafutia majibu ni kuwa kwa nini hiyo zamani watu walikuwa hawazungumzi mambo ya udini na siku hizo zilizofuata udini ukaanza kuzungumzwa waziwazi bila aibu?

Mahusiano ya Kidini
Watu wanaoijua Tanzania watakubaliana nami kuwa hakuna jambo linalotishia utaifa wetu kama mahusiani kati ya mbili kuu na vilevile kati ya dini hizi na serikali. Kumekuwa na malalamiko hususan kutoka kwa Waislamu kuwa serikali, hususan ya awamu ya kwanza ilipendelea sana Wakristo na kuwaonelea Waislamu.

Kauli za malalamiko haya zinazungumzwa na viongozi wakubwa, wasomi, wenye ushawishi na wanaotegemewa katika jamii ya Waislamu, na kwa hivyo lipo kundi kubwa la Waislamu ambalo linaamini hivyo.

Si nia yangu kujadili ukweli wa kauli hizi lakini naamini ni kutokana na hatua ambazo serikali ilizichukua, (labda kwa nia njema) Mungu anajua zaidi kuhusu hilo,  ambazo zimepelekea malalamiko haya. Ni hatua za mbaya zinazodhihirisha makosa aliyoyafanya Mwalimu Nyerere katika mradi wake wa ujenzi wa utaifa.

Kwanza, kabla sijazungumza makosa mahususi ya Nyerere yaliyopelekea malalamiko haya na kauli za udini, nitaje kuwa kosa la ujumla la viongozi waasisi wa nchi zetu ambalo hata Nyerere alilifanya.  Kosa lenyewe  ni kuamini kuwa wangeweza kujenga utaifa kwa mabavu. Tatizo la mbinu hii ya ujenzi wa taifa ni kuwa mafanikio yake ni ya muda mfupi.

Akiondoka madarakani yule mtawala waliyemuoga aliyelazimisha hisia za utaifa wakati watu hawaridhiki na mambo fulani, na hakutaka kuwasikiliza, basi lile kundi linalohisi linaonelewa huamka na kuanza kulalamika. Ukiangalia njia alizotumia Nyerere kujenga utaifa, ilikuwa ni lazima hisia na malalamiko ya udini ambao Mwalimu Nyerere alikemea mwaka 1995 ilikuwa ni lazima yaibuke.

Utaifa wa Tanzania ulikuwa ni wa kulazimsisha, watu wakatii kwa sababu walimuogopa Nyerere. Hapa tunazungumzia kipindi ambacho tetesi zinasema kila penye watu kumi tambua kuwa kuna shushushu mmoja. Katika hofu hii iliyojengwa nani angethubutu kutoa madai yoyote na wakati mifano ya kilichowapata waliopinga Nyerere ilishadhihiri?

Kosa Mahususi la Nyerere
Kosa mahsusi alilolifanya Nyerere na serikali yake ni kuingilia mno mambo ya Waislamu, hususan pale serikali yake ilipoifutilia mbali jumuiya ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kuwaundia Waislamu wa Tanzania chombo kiitwacho ‘Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) iliyorithi mali za EAMWS mwaka 1968.

Wakati EAMWS ilikuwa ni taasisi iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo, BAKWATA ya leo haina kikubwa cha kuonesha kimaendeleo tangu mwaka 1968.  Wakati baadhi ya taasisi za kidini leo hii zinashindana na serikali kuanzisha mashule, vyuo vikuu na hospitali; BAKWATA licha ya ukongwe wake imeishia kumiliki vizahanati na vishule vichache vya sekondari zinazoongoza kwa matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne na sita, tena vya kurithi kutoka EAMWS.

Kwa nini serikali ya awamu ya kwanza ilijiingiza katika kuingilia mambo ya Waislamu kiasi cha kusaidia kuwaundia chombo cha kuendesha mambo yao – chombo ambacho mwishowe kikageuka kuwa sumu kwa Waislamu? Hili lilikuwa kosa kubwa la Nyerere na ndiyo msingi wa malalamiko ya udini.

BAKWATA katika miaka ya uwepo wake imelalamikiwa mno. Zipo taarifa za ufisadi wa kutisha tangu enzi hizo ikiwemo kuuza mali za wakfu, matumizi mabaya ya mali za Waislamu, ufisadi wa misaada iliyotolewa kwa ajili ya Waislamu wote, kushiriki katika shughuli ambazo ni kinyume na maadili ya Uislamu nk. Mwenendo wa BAKWATA tangu ianzishwe ni aibu tupu.

Watetezi wa Nyerere na serikali yake wanaweza kusema yeye hakushiriki  katika uendeshwaji wa BAKWATA, lakini kwa kusaidia tu kuua EAMWS na kuunda BAKWATA, hawezi kukwepa lawama hususan ukizingatia kuwa sera yetu  imekuwa ni ‘serikali haina dini’. Ilikuwaje Nyerere aingie na kuwaamulia Waislamu taasisi ya kuwaongoza?

Katika moja ya hotuba zake, Nyerere aliwahi kukemea kuingizwa maswala ya dini katika sensa kwa hoja kuwa suala hilo haliihusu serikali, lakini je serikali inahusika vipi na Waislamu hadi iamue kuwaundia taasisi? 

Tatizo kubwa zaidi ni kuwa BAKWATA ilikuwepo yenyewe bila mshindani kwa miaka mingi ikidhibiti mambo yote ya Waislamu. Waislamu waliipoteza bure miaka yote ambayo BAKWATA ilikuwa ndiyo taasisi pekee lakini ikiwa ni chombo cha hovyo ambacho kilikuwa ni cha Kiislamu kwa jina tu na kikiongozwa na wale waliuooekana kutekeleza ajenda za serikali kwa Waislamu.

Tatizo aliloliunda Nyerere limeendelea kuwagharimu Waislamu mpaka leo. Awamu zilizofuata za serikali zimeendelea kuipa BAKWATA hadhi kuliko taasisi nyingine na kuifanya ndiyo msemaje mkuu wa Waislamu.
Labda Nyerere aliyafanya haya kwa hoja kuwa anajenga utaifa, lakini matokeo yake ameweka nyufa kubwa katika utaifa,  tena katika msingi, nyufa ambayo huenda inaendelea kukua kila uchao maana waliomrithi kwa kiasi kikubwa wamefuata utamaduni uleule uliojengeka.

Watu tunampenda sana Nyerere lakini ukweli nao usemwe pale alipokosea. Ni vigumu kuamini kuwa wakina Profesa Shivji hawaoni makosa haya ya Nyerere ili hata tunapomuadhimisha tuwe na hadithi nzuri ya maisha ya Nyerere yenye uwiano wa mabaya na mazuri – kama walivyo binadamu na viongozi wote.