Shajara ya Mwana Mzizima:
Historia ya Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar-es Salaam
Sehemu ya Pili
Na Alhaji Abdallah Tambaza
JUMA lililopita
katika safu hii, tulielezea historia ndefu ya eneo la Mnazi Mmoja la hapa
jijini Dar es Salaam na matukio au mambo makubwa ya kukumbukwa yaliyokuwa, ama
yakifanyika hapo kila wakati; kwa vipindi maalumu, au pale linapotokea tukio
muhimu linalohitaji mjumuiko mkubwa wa watu viwanjani.
Kwa muktadha
huo basi, tulielezea ile mikutano mikubwa iliyofanyika hapo kabla ya kupatikana
uhuru wetu na baada yake; ambayo ilihutubiwa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na
hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake wa mwanzo wa
TAA na TANU, aliokuwa nao katika mapambano ya kuikomboa nchi yetu hii adhimu ya
Tanganyika kutoka kwa wakoloni Waingereza.
Tulipokea
simu kadhaa za pongezi kutoka kwa wasomaji wetu ambao walitoa maombi maalumu ya
kuendeleza simulizi za mahala pale kwa mara ya pili, kwani bado walikuwa
hawajakatika kiu zao; sababu maeneo mengi ama tuliyaruka au kuyaacha kutokana
na uhaba wa nafasi gazetini, ambayo haimpi mwandishi uwanda mpana kucheza nao.
Mwisho wa
makala ile tulielezea kwa kifupi namna Mwalimu na wenzake serikalini
walivyokusudia kuifanya Mnazi Mmoja iwe ndiyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam
(kwa maana ya City Center pale ulipopatikana uhuru), kwa kuzileta ofisi kuu na
muhimu za Serikali kutoka kule mjini na kuzijenga upya kwenye eneo hilo.
Mpango ule
ulishindikana kutekelezwa kutokana na wakazi wengi wa eneo lile kutoridhika kuhamishiwa
maeneo mengine, pamoja na kuwapo kwa ushawishi na kampeni iliyofanywa na
Mwalimu Nyerere mwenyewe.
Mwanahistoria
maarufu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Sheikh Mohammed Said,
alipozungumza nami hivi karibuni alinihadithia kwamba katika kutilia mkazo
jambo lile, kuna watu ilibidi Mwalimu awaandikie barua yeye binafsi kutokana na
kuwaheshimu na uzito wao katika jamii.
Mmoja kati ya
hao ni Bi Mruguru bint Mussa wa Mtaa wa Kipata, Gerezani, ambaye ni mama wa
wanasiasa mashuhuri wa harakati za kudai uhuru, akina Abbas, Ali na Abdulwahid
Sykes. Mohammed anasema:
“…Nimehadithiwa na Balozi Abbas Sykes kwamba katika kadhia ile, Mwalimu
alimwandikia mama yao barua binafsi kumtafadhalisha aridhie nyumba yake
kuvunjwa na kupewa mbadala ili nchi ipige hatua kimaendeleo kwa kulijenga upya
jiji letu… Bwana Abbas alisema: ‘unajua Nyerere akimuheshimu sana mama kwani
alimchukulia kama ni mamake mzazi vile.’
“Bi Mluguru
kutokana na mapenzi yake kwa Mwalimu, yeye alikubali kuvunjwa kwa nyumba yake.
Sasa
tunapoliangalia eneo hilo leo, takriban miaka karibu 60 kupita, ingawa hakuna
majumba ya kiserekali mahala hapo, lakini majengo yake si yale tena yalikuwapo
kwenye miaka ile ya 1960s; kwani sasa nyumba zote karibu ni za ghorofa tupu
zilizojengwa na wafanyabiashara; ama kwa kuzinunua za zamani au kwa kufanya
‘ubia’ na wenye mali.
Jirani na ile
Hospitali ya Mnazi Mmoja, ambayo kwa sasa imeboreshwa kwa kuwa na wodi mpaka za
wazazi kujifungulia, huduma za macho na meno, wakiwamo pia hata na Madaktari Bingwa
(zamani ni Mabwana Mganga tu wa kufunga vidonda na kutoa dawa za kikohozi na
mafua); kunapatikanwa jengo mashuhuri la Arnautoglo.
Likijulikana
kama Holi la Arnautoglo, mahala hapo palikuwa sehemu muhimu sana iliyokuwa
ikitumika kwa kufanyia mikutano ya ndani ya kila aina, ikiwamo ile ya siasa na
ya kijamii, vikao muhimu na mambo ya namna hiyo.
Holi hilo pia
lilitumika kwa shughuli za harusi, michezo ya kuigiza, michezo ya masumbwi
(boxing), na miziki ya dansi kila wakati ikishirikisha bendi mashuhuri za
wakati huo za Kilwa Jazz (Dar es Salaam), Moro Jazz (Morogoro), Kiko Kids
(Tabora) na Dar Jazz (Dar es Salaam).
Vikundi vya
Muziki wa Taarab asilia, ambayo hupigiwa watu wakiwa wamekaa kwenye viti; na si
kuruka na kucheza na chupa ya bia mkononi, pia vilikuwa vikiutumia ukumbi huo
kwa shughuli zake. Wakati huo vikundi mashuhuri kabisa vilikuwa ni Egyptian
Musical Club, Alwatan Musical Club na ile ya Bombay Musical Club, iliyokuwa
maeneo ya Kisutu karibu na Makaburi ya Kisutu kabla hakujavunjwa na kujengwa
vile vyuo vya Biashara na kile cha Ufundi.
Kwa siku za
Jumamosi na Jumapili, vijana wadogo wengi waliokuwa wakisoma shule za sekondari
kwenye miaka ile ya mwanzo ya uhuru (1960s), ilikuwa ni zamu yao kuja kucheza ‘’Buggie’’
muziki wa Kizungu, hasa ule wa Kimarekani uliojulikana kama Soul, Jazz na Blues.
Wakati huo bendi za vijana wadogo zikipiga nyimbo za kina James Brown, Ottis
Redding, Aretha Franklin, Percy Sledge, Ray Charles na Babu BB King.
|
Mzee Mustafa Songamebele alivyo hivi sasa |
Hali hii
haikumfurahisha hata kidogo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dar es Salaam wakati
huo, Mzee Mustapha Songambele. Haraka haraka, Mzee Songambele akatoa tamko kwa
Vyombo vya Habari kwamba Serikali ya Tanganyika imepiga marufuku muziki wa Soul
kupigwa kwenye kumbi za starehe na redioni. Tangazo lile lilishitua sana, kwani
muziki na uja uzito ni vitu viwili tofauti; na kwamba ule muziki ilikuwa ni
sehemu ya utamadauni (culture) wa Wamerekani.
Bila shaka
yeyote, kuitangazia Dunia kwamba Tanganyika imepiga marufuku nchini mwake
kupigwa muziki wa Kimarekani, lilikuwa ni tukio baya kidiplomasia, hasa kwa
nchi changa kama yetu wakati ule. Haikupita hata wiki moja, likatoka tangazo
jengine kwamba ‘ni ruhsa’ sasa kupiga muziki ule nchini bila matatizo. Vijana
wakashangilia kwelikweli, kwani ndio waliokuwa wapenzi wakubwa wa muziki huo
kama ambavyo labda leo ukataze muziki wa kizazi kipya wa kina Diamond, Ali
Kiba, Dully Sykes, sijui Q-Chief na labda Lady JD—utachokoza nyuki wakuume
bure!
Kwa wakati
ule wa ukoloni, mtu mweusi hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda kufanya starehe
zaidi ya hapo Arnautoglo na Ukumbi wa Amana pale Ilala, wakati huo ukijulikana
kama ‘Kwa Ramadhani Minshehe’. Huyu Ramadhani Minshehe ndiye aliyekuwa baba
mzazi wa mwanasiasa mashuhuri na kada wa Chama Cha Mapinduzi hapa nchini hayati
Ditopile Mzuzuri.
Katika wakati
huo mgumu, Mzee Minshehe alikuwa ni mmoja wa wazalendo waliokuwa na uwezo
mkubwa wa kifedha hapa jijini, kwani pamoja na jumba hilo, pia alimiliki
mashamba na majumba mengi kule maeneo ya Ilala yaliyokuwa yakimwingizia kipato
si haba.
Sehemu
nyingine za burudani kwenye mahoteli yale kule mjini, mtu mweusi hakuruhusiwa
kuingia humo na kuchanganyika na mabwana wakubwa. Iwe kwenye vilabu vya starehe
au mahotelini, utakaribishwa na maandishi mazito milangoni yanayosomeka, tena
kwa Kingereza, ‘Members Only’ au ‘Management Reserves the Right of Admission’.
Hayo yalifanyika hapa; na huo ndio ukoloni maana yake.
Ni ubaguzi;
ubaguzi mtupu kila mahala na kutuona mtu mweusi ni kinyaa! Sasa sijui wale ndugu
zangu wanaojiita wao ni Liverpool; sisi Manchester, Arsenal, Chelsea…
watasemaje Wazungu wale wakikasirika kunasibishwa na wewe pia kwenye club yao! Ingeeleweka
kama pengine mtu angesema anapenda tu namna Manchester inavyocheza, lakini
anadiriki kusema “sisi (Chelsea si wa kuchezea) tuna mtoto mpya huyo balaa,
lazima tukufungeni tu!” Duh! Tafadhalini tupunguze hiyo. ‘Mazungu yale ni
mabaguzi’ wala hayashituki kupendwa na sisi.
Jumba la Arnautoglo
pia limekuwa ndio mahala kwa kina mama wakati huo wa zamani za kale kwenda
kujifunza kazi za mikono kama ushonaji nguo, ufumaji vitambaa na kazi za
nyumbani kama mapishi (wenyewe wakiita domestiki).
Masomo ya
Watu Wazima pia yalikuwa yakitolewa hapo kwa wale walioikosa elimu hiyo
utotoni, na hivyo ikawa mkombozi mkubwa kwa wale waliotaka kuondoka kwenye
ujinga kwa kujua kusoma na kuandika. Kwa sasa, jengo la Arnautoglo limesheheni
ofisi mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya na Jiji la Dar es Salaam.
Jamiatul
Islamiya ni madrassa kubwa yenye jengo la gorofa moja iliyojengwa kwa nguvu za wakazi wa jijini hapa
chini ya uongozi wa hayati Mzee Kliest Sykes. Taasisi hiyo kongwe ambayo haipo
tena sasa, ilianzishwa baada ya Waafrika chini ya Mzee Sykes tena, kuanzisha
African Association ili kuja kuziba mapengo makubwa yalikuwamo katika
upatikanaji wa elimu miongoni mwa wazalendo wa Kiafrika.
Wakoloni
waliwaachia Wamissionari jukumu kubwa la kutoa elimu na hivyo watu wengi wa
dini ya Kiislamu wakawa na woga kwamba watoto wao wangebatizwa na kubadilishwa
dini kirahisi.
Jamiatul
Islamiya, iliyohamiya mjengoni hapo mwaka 1935, ilifanya kazi kubwa kusomesha
vijana wa kike na wa kiume elimu zote mbili, kwa maana ya Sekula na ya Kiislamu, ni mahala ambapo
watoto wengi jijini walipitia kupata manufaa yake. Ilikuwa ni mahala hapo
ambapo watu mashuhuri walisoma kama vile akina Abdulwahid Sykes na nduguze,
baba mzazi wa mwandishi huyu hayat Mzee Mohammed Tambaza, Imam Mkuu wa Masjid
Mwinyikheri Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua na nduguze, hayati Mzee Zubeir
Mtemvu na nduguze pamoja na wazee wengi ambao tayari wameshatangulia mbele ya
haki.
|
Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika Muslim School |
Jengo lile,
ni kielelezo tosha kwamba watu wanapoungana na kuazimia kufanya lao basi Mungu
hubariki jambo hilo na bila shaka mafanikio hupatikana. Linaweza likaonekana ni
la kimasikini kwa dunia ya leo, lakini ukichukulia mazingira ya ukoloni na hali
dhalili za watu wake wa Kiafrika haikuwa kazi ndogo kusimamisha mjengo pale.
“Wazazi wa
Kiislamu waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe … Aljamiatul
Islamiya ilienda nyumba kwa nyumba ikikusanya michango kutoka kwa Waislamu …
“Kwa bahati
nzuri mnamo mwaka 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu
ujenzi wa shule ile. Alitoa fedha na shule ikajengwa jirani kabisa na mahala
ilipokuwa African Association kwenye Barabara ya New Street (sasa Lumumba).
“Hii ni moja
ya shule za mwanzo kabisa kujengwa na Waislamu wa Tanganyika wakati huo wa …ni
moja ya mifano hai ya kuonyesha juhudi za Waislamu wa Tanganyika katika
kujiletea maendeleo wenyewe…,”anaandika Mohammed Said katika kitabu chake cha
Maisha na Nyakati za Abdul Wahid Sykes, ukurasa 45.
Balozi Abbas
Sykes, ni mmoja katika wale mashujaa wa mwanzo kabisa walioitoa TAA ilipo na
kuifanya iwe TANU mwaka 1954, kwa kuipa meno kuja kupambana na Mwingereza kudai
nchi yetu. Ndiye mtu aliyeshika wadhifa wa kuwa Mkuu wa Jimbo la Pwani (PC siku
hizo) ikiwamo na mji wa Dar es Salaam na Mzizima yake, akichukua madaraka
kutoka kwa PC (Provincial Commissioner) Mzungu.
|
Abbas Sykes katika miaka ya 1950/60 |
Wakati huo
Balozi Sykes akiwa PC, alifanikiwa kumwoa mmoja wa wanawake warembo kabisa
(celebrity) jijini na mtangazaji maarufu na mahiri wa redio; mwenye sauti
nyororo na ya kuvutia wa Idhaa ya Kiingereza ya Sauti ya Tanganyika, Tahia
Abdulwahaab.
Akiwa bado
kijana mdogo na mbichi kama alivyo Mheshimiwa Makonda sasa hivi, utawala wake jimboni
ulivuma kweli kweli Pwani nzima; kwani alikuwa mtu asiyetaka masikhara hata
kidogo kwa raia na watendaji.
Spidi yake
ilikuwa kali kwelikweli, na hivyo Kamishna Sykes hakudumu sana katika wadhifa
ule, kwani alibadilishiwa kazi na kupelekwa kuwa balozi kwenye nchi kadhaa duniani.
Miongoni mwa
nchi hizo alikopita kwenye safari yake ndefu, ni pamoja na Paris, Ufaransa,
Montreal Canada, United Nations, New York na Khartoum, Sudan. Akiwa kule
Ufaransa aliwakilisha nchi pia kwenye Shirika la UNESCO (Shirika la Umoja wa
Mataifa la Sayansi na Utamaduni), kama Mwakilishi Mkazi.
Balozi Sykes,
amestaafu kazi miaka mingi na sasa amepumzika tu nyumbani kwake pale Sea View. Alamsiki!
Tukutane juma lijalo InshaAllah.
Simu: 0715
808 864
atambaza@yahoo.com