Showing posts with label historia. Show all posts
Showing posts with label historia. Show all posts

Monday 7 May 2018


Shajara ya Mwana Mzizima
Jumbe Muhammad Tambaza
Alimsomea Dua Nyerere, Nyota Yake Ikang’ara
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Jumbe Muhammad Tambaza
Raia Mwema
Mei 7 - 8, 2018

JUMBE Muhammad Tambaza, ni mmoja katika wapigania uhuru mashuhuri wa nchi hii ambao, historia inawataja kama ni watu waliotoa mchango mkubwa sana katika kufanikisha kumng’oa Mkoloni Mwingereza, katika ardhi yetu tukufu.

Hayati Mzee Tambaza, ambaye alifariki mnamo mwaka 1978 hivi, anaingizwa katika kundi moja la watu wa mwanzo kabisa waliompokea kwa furaha na upendo kijana Julius Nyerere kutoka Butiama, alipofika jijini Dar es Salaam kwa kumuunga mkono ‘mia kwa mia’, katika harakati zake za kupigania uhuru wa Tanganyika kwenye miaka ya 1950s.

Wanaharakati wengine aliokuwa nao ni pamoja na Mzee Mwinjuma Mwinyikambi wa Mwananyamala; Mzee John Rupia wa Mission Quarters; Sheikh Suleiman Takadir; Sheikh Haidar Mwinyimvua (Kisutu); Mzee Max Mbwana (Kariakoo); Zubeir Mwinshehe Mtemvu (Gerezani) pamoja na familia ya Mzee Azizi Ali (Mtoni) na ile ya Kleist Sykes (Gerezani), Dar es Salaam.   

Ukoo wa Diwan Tambaza Zarara bin Mwinyi-Kitembe, ndio waliokuwa wenyeji wa maeneo ya katikati ya jiji wakati huo, wakihodhi eneo la ardhi yote ya Upanga, iliyosambaa kuanzia Daraja la Selender kuelekea Palm Beach Hotel, hadi Ikulu ya Magogoni kwa upande mmoja; na kwa upande mwengine maeneo yote kutoka Aga Khan Hospital, Ocean Road Hospital, Kivukoni Front (makaburi ya asili ya wanandugu wengine yako pale Wizara ya Utumishi, Magogoni) kwenda Mnara wa Saa pale Uhuru Street na vilivyomo ndani yake.

Habari zinasema kwamba, katika siku za mwanzo tu za kupambana na Mwingereza, wazee mashuhuri wa hapa Dar es Salaam walikutana na kuamua kumfanyia ‘zindiko’ na ‘tambiko’ la kijadi, pamoja na kumwombea dua maalumu kijana mdogo, Julius Nyerere, ili kumkinga na waovu na pia kuifanya nyota yake ing’are juu ya wote wenye nia mbaya naye; wakiwamo watawala wa Kiingereza, hasa Gavana Twinning.

Katika moja ya hotuba zake za kuaga aliyoitoa mnamo Novemba 5, 1985, Nyerere alilikumbumbuka tukio hilo na hapa chini anasimulia:

“…Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania…na mambo makubwa kama haya kama hayana baraka za wazee hayaendi… huwa magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani; tangu awali kabisa.

“Sasa siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (nyumbani kwake) akasema: ‘Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.” 

Anahadithia Mwalimu na kuendelea:

“Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika… zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee… za jadi, “…walikuwa na beberu la mbuzi… wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama beberu akachinjwa huku anaambiwa Twinning ‘umekwisha’… nikaambiwa tambuka… nikavuka lile shimo na baada ya hapo nikaambiwa …basi nenda zako kuanzia leo Twinning amekwisha!”

Mwalimu alimaliza kusimulia namna alivyofanyiwa dua na tambiko nyumbani kwa Mzee Tambaza, Upanga jijini.

(Picha ya Baraza la Wazee wa TANU kutoka kitabu cha Saadan Abdu Kandoro, ''Wito wa Uhuru.'')

Kutawaliwa na Wazungu kuliwakera na kuwakasirisha watu wengi sana, kutokana na kule kudharauliwa ndani ya nchi yao wenyewe na watu wengine; hasa pale walipominywa katika kupatiwa huduma muhimu kama elimu bora, matibabu na mahala pazuri pa kuishi.

Pamoja na mambo mengi mengine yaliyokuwa mabaya kutokana na kutawaliwa, yamo pia na yale ya kuwekwa kwa madaraja katika utoaji huduma muhimu. Sisi, wana wa nchi hii, hatukuwa na shule za maana hata kidogo; watu wote sisi tukasomee shule moja tu (Mchikichini) mpaka darasa la nne; kwa nini hasa kama siyo dharau?

Nyumba zetu za kukaa zilikuwa za ovyo zilijengwa kwa miti na kukandikwa udongo na juu ni makuti, tena hapa hapa mjini Dar es Salaam, sikwambii vijijini; umeme uko kwenye taa za barabarani na siyo majumbani mwetu. Tukiwasha vibatari na taa za ‘chemli za Aladin’ kwa wenye uwezo kidogo kila siku.

Hospitali ziliishia kutoa kama huduma fulani ya mwanzo tu (First Aid). Haikuwapo hospitali ya Amana, Temeke, Mnazi Mmoja, Mwananyamala wala Mbagala. Tuliponea kibahatibahati tu kwa mizizi na majani ya porini. Ukiwa na homa kali basi chemsha mwarobaini; tumbo la kuendesha chemsha majani ya mpera au mpapai nani akupe ‘antibiotic wewe’.

Hospitali ya Muhimbili, yenye maabara na vipimo pamoja na madaktari bingwa, ilijengwa mwaka 1957 - ni juzi tu - kwa heshima ya Binti Mfalme Margareth II, aliyekuwa na ziara ya kutembelea makoloni ili aje kufungua rasmi hospitali hiyo. Kiwanja kilitolewa kwa hisani ya familia ya Mzee Jumbe Tambaza, ambapo miembe ile mikubwa inayoonekana mpaka leo pale ilikuwa shambani kwa kina Tambaza.

Kwa hivyo basi, ukiacha labda homa na vidonda, magonjwa mengine yote kwetu ilikuwa ni kifo tu. Umri mkubwa wa kuishi kwa wastani ulikuwa ni miaka 30.

Mzee Jumbe Tambaza, ambaye jina lake linanasibishwa na shule maarufu ya Sekondari ya Tambaza ya jijini - hana uhusiano wowote na shule hiyo - shule ilipewa jina lake kutokana na eneo iliyopo na kwa kuthamini mchango wake katika kupigania uhuru.

Kabla ya hapo, wakati huo wa ubaguzi wa rangi na matabaka, shule hiyo na ile ya msingi iliyo jirani nayo inayoitwa Muhimbili Primary, zilikuwa mahsusi kwa vijana wa Kihindi tu – hasa Ismailia - zikijulikana kama ‘Aga Khan Schools’ na kamwe hawakuwa wakisoma Waswahili na Kiswahili pale.
Shamba la Mzee Jumbe Tambaza pale Upanga, lilianzia mbele kidogo ilipo Shule ya Jangwani Wasichana (ambayo wakati wa ukoloni ilijengwa na serikali wasome watoto wa kike wa Kihindi tu, na ile Shule ya Azania ilikuwa kwa watoto wa Kihindi wa kiume), na kutambaa moja kwa moja mpaka lilipo Daraja la Selender pale baharini.

Eneo la Majengo ya Hospitali ya Muhimbili ilikuwa mali ya Jumbe Tambaza na marehemu nduguze (Msakara, Kudura na Mwamtoro Tambaza). Kutokana na kukosekana kwa hospitali ya maana ya rufaa kwa ajili ya Waafrika (kwa sababu ya ubaguzi tu), hayati Mzee Tambaza alitoa eneo lote lile la Muhimbili ijengwe hospitali ya Waafrika ili kupunguza vifo vilivyotokana na kukosa tiba sahihi.

Kijihospitali kidogo kwa ajili ya watu Weusi kilikuwapo pale jirani na Kituo cha Kati cha Polisi (Central Police Station) jijini, ikiitwa Sewa Haji Hospital, kwa heshima ya mfadhili aliyeijenga kusaidia jamii masikini. Sewa Haji alikuwa mkazi wa Bagamoyo mwenye asili ya Kibulushi kutoka Persia. Baada ya kujengwa hospitali ya Muhimbili, jengo moja katika yale matatu makuu, likaitwa Sewa Haji kama kumbukumbu yake.

Mjini Dar es Salaam wakati huo wa kibaguzibaguzi, serikali ya kikoloni haikutenga sehemu ya kuzikia watu weusi ambao walikuwa daraja la nne. Yale makaburi mashuhuri ya Kisutu, wakati huo yalikuwa ni ya watu wenye asili ya Kiarabu tu! Mwengine yoyote, ilibidi apelekwe kijijini kwao tu nje ya mji – Kunduchi, Mbweni, Msasani, Bagamoyo, Kisarawe, Maneromango na mikoani pia.

Sasa, ili kuondoa adha hiyo na usumbufu, Babu Mzee Tambaza, alitoa bure sehemu kubwa ya eneo lake itumike kwa watu wenye kuwa na shida ya kuzika ndugu zao jijini. Makaburi ya Tambaza siku hizo yalikuwa maarufu sana kuliko yalivyo yale ya Kisutu kwa sasa. Kamwe watu weusi hawakuwa wakizikwa Kisutu, kama ilivyo wakati huu.

Kufuatia hali hiyo, Jumbe Tambaza aliwashawishi binamu zake wawili, Mwinyimkuu Mshindo na Diwan Mwinyi Ndugumbi na wao wakatoa sehemu watu waweze kuzikana kule maeneo ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa na Ndugumbi, Magomeni Makuti; makaburi ambayo mpaka leo yameendelea kutumika kuzikia watu wote.

Neno Tambaza, limetokana na neno kutambaa au kusambaa eneo kubwa. Diwan Tambaza na nduguze walikuwa watawala wa sehemu mbalimbali za hapa Mzizima siku za nyuma kabla Waarabu, Wajerumani wa Wangereza kufika hapa. Nduguze wengine ni Diwan Uweje; Diwan Uzasana; Diwan Mwenye-Kuuchimba na Diwan Mwinyi Ndugumbi.

Majina hayo walijipachika wenyewe kiushindani, kujigamba na kujitukuza kuliko ndugu wengine; hivyo kimafumbo mafumbo, huyu akajiita hivi na yule akamjibu mwenzake vile; mwengine akajiita naye atakavyo, kutokana na uhodari na tawala thabiti walizoziongoza.

Majina hayo pandikizi, hata hivyo yalikuwa na maana yake kila moja; kama vile mtu aseme mimi ‘Mobutu Sese Seku Kuku Mbenju wa Zabanga’, ikiwa na maana ya ushujaa kwa ‘Batu ba Kongo na fasi ya Zairwaa!’

Sasa Diwan Tambaza alipojiita vile, nduguye Diwan Uweje akamjibu na kumwuliza hata ukiwa umesambaa ndio uweje? Mwengine naye akasema, ‘’Ah! Uliza sana wewe uambiwe.’’ Hivyo yeye akajita Diwan Uzasana. Diwan Mwenye-Kuuchimba, yeye alikuwa akitawala maeneo ya Mtoni Kijichi na Mbagala yake, akasema, ‘’Nyie wote mnacheza tu, ‘mimi ndiye mwenye kuuchimba!’’ Kwa maana ya kwamba ndio kiboko ya wote. Ilimradi hali ikawa ndiyo hiyo; na hizo ndio zama zao, kwani husemwa kila zama na kitabu chake.

Mwandishi wa makala haya, jina langu naitwa Abdallah Mohammed Saleh Tambaza. Babu yangu Mzee Saleh bin Abdallah Tambaza wa Zarara, anakuwa binamu wa Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, yaani baba zao walikuwa ndugu.

Shamba la babu yangu mimi pamoja na kaka yake Kidato Tambaza, linasambaa kuanzia Don Bosco, Makao Makuu ya Jeshi, Diamond Jubilee, Msikiti Maamur (kaburi la babu na babake babu yamo ndani ya Msikiti wa Maamur unapoingia mkono wa kulia pale ukutani), kuelekea kwenye Jamat la Wahindi mpaka Mahakamani kule Kisutu.

Miembe, minazi na mizambarau ile ya asili inayoonekana Upanga, ilipandwa na babu yangu kwa ajili ya urithi wa wajukuu zake, itakapofika zamu yao kumiliki maeneo yale.

Kwa bahati mbaya sana, Wazungu Waingereza, wakaona mandhari ile nzuri ya Upanga, hawakustahili watu weusi kuishi pale na wakawaamuru babu zangu wahame wawapishe Wahindi raia daraja pili. Hii ni baada ya wao Wazungu daraja la kwanza kuchukua eneo lote la Oysterbay (sasa Masaki). Maeneo yote hayo mawili yenye upepo mwanana ni karibu kabisa na bahari.

Kitendo cha kumhamisha mtu nyumbani kwake kwa namna ile, halafu kumpa fidia uitakayo wewe, ni dharau, dhuluma na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Wazee wale wastaarabu na wajanja hawakuwa na haja ya kuyauza maeneo yale, kwani ukiyaangalia utaona waliyapangilia ili vizazi na vizazi vya kwao viishi hapo.

Hii haihitaji mjadala wala maelezo marefu, lakini ni ushahidi tosha kwamba inaweza ikawa ndiyo sababu kubwa iliyomfanya Mzee Jumbe Tambaza awe mstari wa mbele kabisa katika kuwachukia watawala wa Kizungu na kumuunga mkono Nyerere kwa nguvu kubwa kama ile.

Mchango wa Mzee Jumbe Tambaza katika ukombozi wa nchi yetu haukutetereka hata kidogo, kwani hata pale rafiki yake mpenzi Sheikh Suleiman Takadir, alipotahadharisha watu kuwa makini na Nyerere maana ameonyesha kwamba siku za usoni angependelea zaidi jamaa zake, Mzee Jumbe hakumuunga mkono na akakubali Sheikh Takadiri atengwe na jamii kwa manufaa ya umoja wa kitaifa.

Jumbe Tambaza pia hakumuunga mkono Zubeir Mtemvu, kwenye suala la Kura Tatu ambalo ilibaki kidogo tu chama cha Tanu kingesambaratika na kuwa vipande viwili; lakini yeye alibaki na Nyerere wake mpaka dakika ya mwisho kule Tabora hadi kukasainiwa waraka wa ‘Uamuzi wa Busara’ ambao uliwapeleka TANU kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu.

Katika picha ya pamoja iliyopigwa baada ya kutangazwa ushindi wa kuingia kwenye Kura Tatu kwa chama cha TANU, anayeonekana nyuma ya Mwalimu Nyerere pale Tabora ni Mzee Jumbe Tambaza. (Rejea kitabu Mohammed Said, ‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes… uk 275).

Kutokana na uaminifu wao usiotetereka kwa chama chao, Mzee Jumbe Tambaza na mwenziwe Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; wazee wale wawili wa Kimashomvi kutoka Mzizima, kwa muda mrefu wamekuwa wajumbe wa kudumu (permanent seats) kwenye Kamati Kuu ya TANU bila kupigiwa kura; achilia mbali ule uwepo wao kwenye Baraza la Wazee wa TANU.

Mnamo mwanzo wa miaka ya mwanzoni 1950, Mzee Tambaza alitumbukizwa tena kwenye mgogoro mkubwa na serikali pale ilipokuwa inajenga upya Barabara ya Umoja wa Mataifa kutokea Faya kuelekea Daraja la Selander, ilipoamuliwa kwamba sehemu ya eneo la makaburi iondoke kupisha ujenzi huo.

Hayati Mzee Tambaza, alifungua kesi mahakamani dhidi ya serikali, kesi ambayo inatajwa kama moja ya kesi nzito (landmark cases) sana kutokea hapa nchini na Afrika Mashariki iliyogusa imani ya Dini ya Kiislamu; kwamba je, ni halali au si halali kufukua makaburi ya watu waliokufa?

Kesi ya Makaburi, kama ilivyokuja kujulikana, iliunguruma kwa muda mrefu na kujaza kurasa za mbele za magazeti wakati huo, kutokana na mabishano makali ya hoja (cross examinations) mahakamani baina ya mawakili wa pande mbili hasimu.

Wakati Serikali ikiwatumia masheikh wazawa wa hapa waliosema kwamba inakubalika kufukua makaburi, Jumbe Tambaza aliwatumia masheikh wakubwa kutoka Mombasa na Zanzibar, akiwemo aliyekuwa Kadhi wa Zanzibar Abdallah Saleh Farsy kupinga hoja hizo.

Kwa kishindo kikubwa, Mzee Tambaza alishinda kesi ile na ikabidi barabara ile ipindishwe pale kwenye mteremko wa kutokea Faya na kuyaacha makaburi na vilivyo ndani yake kama yalivyo. Haraka haraka, Hayati Mzee Tambaza akafanya maamuzi ya kujenga msikiti ambao haukuwapo mahala hapo kabla ya tukio hili, kuepusha kujirudia.

Huyo ndiye Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, mwanaharakati wa kupigania uhuru wa taifa hili wa kupigiwa mfano, aliyetetea na kutoa vyake kusaidia wanyonge wenziwe katika jamii yetu katika kipindi cha manyanyaso ya utawala dhalimu wa Malkia wa Uingereza. Alimfanyia madua na matambiko ya jadi Mwalimu Nyerere ili nuru yake ing’are kama mwezi na jua!
Ewe Mola Mghufirie madhambi yake – Ameen.

Thursday 3 May 2018





Kulia: Ali Mwinyi Tambwe (Katibu Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika).
Saadan Abdul Kandoro, Abeid Amani Karume, Bi. Titi Mohamed,
Mwinjuma Mwinyikambi na Maneno Kirongola mkutano wa Afro Shirazi Party
(ASP) Zanzibar wakati wa kupigania uhuru wa Zanzibar

Chief David Kidaha Makwaia
wa Siha Shinyanga

Kushoto: Kleist Sykes na wanae mbele Abbas,
nyuma kulia Abdulwahid na Ally

Hamza Kibwana Mwapachu
Kushoto Japhet Kirilo baba yake Mzee Kirilo na Anthon
Nelson 1955



Monday 30 April 2018


Shajara ya Mwana Mzizima
Rashidi Mfaume Kawawa
Mtetezi Wanyonge aliyekuja kuwa Waziri Mkuu
Na Alhaji Abdallah Tambaza


Raia Mwema Aprili 30 - May 1, 2018 


UTAWALA dhalimu wa Kikoloni wa Ulaya Ingereza hapa kwetu, ulijaa uonevu, udhalilishaji na ukandamizaji katika utoaji wake wa huduma muhimu miongoni mwa wanajamii. Raia tuliwekwa kwa madaraja ambayo Wazungu walikuwa daraja 1; Wahindi daraja II; Waarabu daraja III na Watu weusi tukawa kwenye daraja la IV la mwisho.

Miongoni mwa mateso hayo ni pamoja na watu ‘mababa majitu mazima’, kuchapwa viboko Bomani na Ma-DC na PC (wote walikuwa Wazungu wanaotisha na masharubu yao mazito) pindi inapotokea ukawa umefanya kosa la aina fulani, ambalo kwa wakubwa itabidi upigwe viboko.

Tiba, makazi pamoja na elimu, ilikuwa kwa matabaka vilevile, hata ikawa kwa sisi wananchi wenyewe kutokuwa na sehemu bora ya kuishi; tukiumwa tiba yetu ni panadol tu; kujifungua ni kienyeji nyumbani ambako wengi wa wazazi walipoteza maisha; na shule zilikuwa chache tu za ‘Kayumba’, utake usitake. Katu, haikuwezekana watu weusi kuchanganywa na Wazungu ama Wahindi kwenye elimu hata kama baba yako anao uwezo wa kukulipia ada kubwa - afadhali ilikuwapo kidogo kwa watoto wa machifu.

Watesaji wakubwa kwenye ajira walikuwa ni Wahindi wakati huo, maana wao ndio waliokuwa wakilimiliki uchumi pamoja na nyenzo zake zote kuu (maduka, viwanda, mashamba, pamoja na ajira za nyumbani). Wenyewe wakituita ‘golo’, jina ambalo maana yake pengine ni fisi, sokwe au nyani mweusi - walitudharau sana hata ni aibu kuhadithia.

Malkia wa Uingereza, pamoja na kwamba alikuwa ni mkubwa wa Kanisa Anglikana duniani, alishindwa kutuona sisi kama binadamu kama alivyo yeye na watu wa kwao; na akashindwa kutufanyia uadilifu kwa miaka yote aliyoikalia nchi yetu.

Hali ikawa mbaya sana isiyovumilika kwa Waafrika wanyonge hata ikasababisha kuwaibua watetezi wengi wa haki waje kuongoza mapambano ya kupigania haki  kwenye ajira na utumishi. Miongoni mwao alikuwamo mwanaharakati wa kukumbukwa na kupigiwa mfano, hayati Rashidi Mfaume Kawawa. 

Hayati Mzee Kawawa, ambaye baadaye alikuja kuwa mpaka Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hii, alikuwa ni kiongozi asiyetetereka kwenye masuala ya utetesi wa Haki za Binadamu kwenye masuala ya wafanyakazi.

Alipambana vikali sana wakati huo wa ukoloni, kwani anasifika na kukumbukwa kwa kuandaa migomo bila woga pamoja na kwamba ilipigwa marufuku na Serikali ya Kikoloni.  Habari zinasema, Kawawa alikuwa na sauti na nguvu kubwa kwa jamii ya wanyonge wakati huo kiasi kwamba alichokisema yeye basi kilitekelezwa mara moja.

Aliongoza muungano wa vyama vingi vya wafanyakazi hapa nchini wakati  huo kikiwemo kile cha ‘Makuli’ (wapakiaji na wapakuaji mizigo melini) wa bandarini cha Dockworkers Union 1948, Tanganyika Railways African Union, African Cooks Union na Domestic Workers Union (Chama cha Watumishi wa Majumbani)

Wakati ule, ukiacha Serikali na Railways, mwajiri mwengine mkubwa alikuwa ni Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kazi nyingi za Waafrika pale Pwani zilikuwa za ‘daily pay’, yaani ya malipo kila siku jioni. Iliwezekana kufanya hivyo kwa sababu kazi za bandarini ni za msimu maana kuna wakati meli zinakuwa nyingi na wakati mwengine zinaadimika; hivyo watu wachache sana walikuwa na ajira za mwezi hata mwezi.

Kazi zile za Bandari zilikuwa ni za kuhatarisha maisha sana. Wengi wa watu walipata vilema ama kupoteza maisha, hivyo kufanyishwa kazi za namna ile bila mikataba stahili ulikuwa ni uonevu mkubwa sana. Hali hiyo ilisababisha migomo isiyokwisha kutoka kwa wafanyakazi kwa kule kutotendewa ipasavyo.

‘’Katika miaka ile kazi ya bandarini ilikuwa ni hatari, ikishindana na kazi ya migodi.

“Lakini bado serikali ya kikoloni ilijifanya kutoelewa ukweli kwamba Mwafrika alikuwa mwanadamu kama alivyo Mzungu Muasia au Mwarabu …Serikali ilikuwa na dhana ya ajabu na wakati mwengine ya kusikitisha kuhusu Mwafrika kama binadamu,”anaandika Mohammed Said, Uk 64 katika kitabu chake mashuhuri cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, kinachosambazwa na Kampuni ya Ibn Hazm Media Center, Dar es Salaam.

Wanaharakati wawili wakubwa ndio waliojitokeza mbele zaidi katika kuwapigania na kuwatetea Waafrika wenzao wakati huo. Abdulwahid Sykes akajikita kwenye  Dockworkers Union na Rashidi Kawawa akiwa zaidi kule TRAU; huku  wakisaidiwa kwa karibu na watetezi wengine shupavu wakati huo kama vile Kassanga Tumbo, Michael Kamaliza, Alfred Tandau na Jacob Namfua.

Vuguvugu hizi na mwamko huu mkubwa ukazaa chombo kikubwa zaidi kilichounganisha vyama vya wafanyakazi wote wakati huo kilichojulikana kama Tanganyika Federation of Labour na Rashidi Mfaume Kawawa akawa ndiye Katibu Mkuu wa mwanzo. Chama kingine machachari wakati huo ni kile cha madereva na hasa madereva Teksi, kilichoongozwa na kada mashuhuri wa CCM, Mustapha Songambele.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa harakati za vyama vya wafanyakazi, kwenye harakati za kudai uhuru chama cha TANU kilikuwa kikihitaji sana kuungwa mkono na kila sekta ya wazalendo wa Tanganyika wakati huo. Rashidi Kawawa, haraka akaunganisha nguvu na TANU kwa kupeleka umma wote ule wa watumishi kutoka vyama vilivyoungana na kuwa wanachama wa rasmi wa TANU.

Kwa namna ile viongozi wote wale waandamizi kutoka TFL wakachukua nafasi za juu na kuwa na sauti kwenye masuala ya ukombozi wa taifa hili. Chama cha TANU kikawa hakishikiki kutokana na chachu mpya aliyoingiza Kawawa kwenye mapambano. Huo ukawa ndio mwanzo wa Kawawa kuwa karibu na Nyerere kiasi kile.

Nilimfahamu Rashidi Mfaume Kawawa, nikiwa bado kijana mdogo kabisa kwenye miaka ya mwanzo 1950s pale alipokuwa Ofisa kwenye Idara ya Ustawi wa Jamii (Community Development Department) ya Serikali ya Kikoloni, alipokuwa akicheza filamu za vichekesho. Filamu alizocheza hayati Mzee Kawawa zilikuwa zikitupa burudani tosha sisi vijana wadogo wa wakati huo, kwani filamu zile hazikuwa za kuburudisha peke yake, lakini pia kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali. Jina lake la kwenye sinema lilikuwa ‘Muhogo Mchungu’.

Sinema nyingine maarufu aliyoicheza Mzee Kawawa ni ile iliyojulikana kama, ‘’Mgeni Mwema,’’ ambapo kila mwanzo wa mwezi kwa jiji la Dar es Salaam zilikuwa zikionyeshwa pale viwanja vya Mnazi Mmoja, Ilala na Magomeni na baadaye kuhamia sehemu nyengine mikoani. Pamoja na sinema za Muhogo Mchungu, usiku huohuo huonyeshwa pia sinema nyingine za wale Wazungu wawili wasanii, Stan Laurel na Oliver Hardy, hapa kwetu Dar es Salaam tukiwaita ‘Chale Ndute na Chale Mbwambwambwa’, ambao vichekesho vyao kwenye zile sinema vimekuwa kivutio mpaka leo duniani kote.

Kwa sababu ambazo hazikuelezwa sawasawa mpaka leo, jamii ya Watanzania wamenyimwa nafasi ya kuburudika na uhondo wa filamu za Mzee Rashidi Kawawa - hatujui zilipo, zimevichwa kama zilivyofichwa nyaraka nyingi za historia ya muhimu ya nchi yetu.

Katika miaka ile ya 50s, nikiwa mwanafunzi pale Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, mjini Dar es Salaam kila mara nilikuwa namwona Mzee Kawawa akirandaranda nje ya nyumba ile ndogo iliyokuwa mkabala na shule yetu akiwa ama anatoka au kuingia mle ndani kukutana na wapigania uhuru wenzake. Pale Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, ndipo yalipokuwa makao makuu ya Chama TANU wakati wa kudai uhuru.

Hayati Mzee Kawawa, wakati ule alikuwa kijana mtanashati kwelikweli; kila mara akiwa amependeza kimavazi, hasa pale alipokuwa akivaa ile migolole ya vitenge vya Afrika Magharibi, hususan kutoka Ghana na Nigeria, iliyokuwa ikipendwa na wapigania uhuru wengi sana wakati ule, akiwamo Dk Kenneth Kaunda na Harry Chipembere wa Zambia; Kanyama Chiume na Yatuta Chisiza wa Malawi; na Nyerere, Kassanga Tumbo na Michael Kamaliza wa Tanganyika.

Mtoto mkubwa wa hayati Mzee Kawawa, dadangu Rehema, nilikuwa nasoma naye darasa moja pale shuleni Mnazi Mmoja pamoja na Silas Munanka mtoto wa Mzee Bhoke Munanka. Wengine waliokuwapo pale wakati ule ni pamoja na Wendo, mtoto wa Mzee Hamza Kibwana Mwapachu, Muharrami Kilongola na Mohammed Rashid Sisso, ambao baba zao walikuwa viongozi waandamizi pale Lumumba Makao Makuu.

Sasa asubuhi moja ya mwaka 1960, nchi ikiwa ndio kwanza imepata Utawala wa Ndani (Internal Government), ambayo hata maana yake hatukuijua ni nini siku hizo; tuliiona gari nyeusi aina ya Humber yenye kibao cha namba kilichosomeka MWP, kwa maana ya Minister Without Portfolio inaingia mpaka ndani mle shuleni. Dereva akiwa amevalia sare zinazomereta kabisa akashuka kuja kumfungulia mlango abiria wake. Abiria alikuwa ni Rehema Rashidi Kawawa, ambaye sasa hakuwa mwenzetu tena, kwani babake alikuwa amechaguliwa kuwa “Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalumu’ katika Serikali ile ya Madaraka ya Ndani.

Kwetu sisi vijana wadogo siku zile, lile lilikuwa ni tukio kubwa la kukumbukwa, kwa sababu haikupata kutokea hata siku moja pale shuleni, mwenzetu au mwalimu, akaletwa na gari mpaka ndani.

Kama vile sinema ndoto usingizini! Tulianza kuona cheche za kuelekea uhuru kamili. ‘Golo mdogo’ anakuja shule na gari la aina yake! Ule ukawa ni wakati kutafakari na kusubiri lini na sisi wengine tutahamia kwenye magorofa ya Upanga na Uhindini wanakokaa Wahindi; kwani moja ya ilani au ahadi za wanasiasa siku zile ni kwamba huru utakapopatikana, basi sisi ‘makabwela’ tutachupa kutoka raia daraja la IV hadi la kwanza.

Tumesubiri sana; na mpaka leo bado tunaendelea kusubiri siku hiyo ifike. Ni mapambano ambayo bado yanaendelea mpaka leo tumefikisha miaka zaidi ya 60 ya uhuru wetu na bado hayajafikiwa kisawasawa.

Kwa sababu ambazo mpaka leo hazijawekwa hadharani, kipande hiki cha historia yetu hakitajwi, hakiadhimishwi na wala hakienziwi hata kidogo. Nilidhani, kuwa na madaraka ya ndani lilikuwa jambo zuri sana katika safari ya kuelekea kupata uhuru kamili. Pale nchini Kenya, ambako mwandishi huyu alipata kuishi zaidi ya miaka mitano kwenye miaka ya 1970s, Sikukuu ya Madaraka Day, husherehekewa kwa shangwe, nderemo na vifijo vikubwa sana pengine kuliko hata siku ya uhuru kamili mwaka 1962.     

Shermax Ngahemera, ni mhariri mwandamizi wa gazeti la Kiingereza la The African, linalochapishwa kila siku na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, pale Sinza, Kijiweni. Siku moja wakati ilipotangazwa kwamba Rashidi Kawawa hatunaye tena hapa duniani; watu wakawa wanahaha kujaribu kumpamba na kumpembua ili wapate kuandika taazia iliyo bora kuhusu mwanamajumui yule shupavu. Shermax alisema hivi:

“Unajua huyu mzee ana mchango mkubwa sana katika kufanikisha kupatikana kwa haraka uhuru wa nchi hii pengine kuliko mtu mwengine Mwalimu, wakati fulani aliitwa na Gavana Sir Richard Turnbull na kuulizwa anafikiri lini tutakuwa tayari kujitawala ili maandalizi yaanze mara moja. Nyerere aliruka mita 100 juu akikataa kabisa kupewa uhuru kwa haraka hivyo kwa sababu nchi ilikuwa bado haina wasomi ambao wangeweza kusaidiana na Mwalimu kuendesha nchi,” anasimulia Shermax na kuendelea, ‘’ ”Siku kadhaa baadaye Nyerere aliulizwa na  Kawawa juu ya safari yake kwa Gavana. Nyerere alimwambia Kawawa kwamba Gavana alikuwa anataka tumwambie kama tuko tayari kujitawala maana yeye alikuwa amechoka na anataka kurudi kwao,” amesema Shermax na kuendelea, “Nyerere alimwambia Kawawa kwamba hakutaka kupata uhuru wakati ule maana watu wa kuweza kufanya kazi nyeti za kisomi za Serikali hawakuwapo bado. Kawawa akamwambia Mwalimu akachukue nchi hata saa ile, maana tuko kwetu na kama tutaanguka basi lazima tutasimama tena. Hatuna wa kumwogopa hata kidogo. Nyerere alirudi tena kwa Gavana na kumwambia kwamba amefuta usemi wake yuko tayari kujitawala wenyewe!” alimaliza Ngahemera.

Uhuru ulipopatikana mwaka 1961, hayati Mzee Kawawa alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini, na ile Humber yake nyeusi iliendelea kumleta shuleni Rehema.
Habari zinasema, baada ya miezi kadhaa ya kuwa huru, hayati Mwalimu Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu na kumpisha Rashidi Kawawa aongoze serikali maana ni yeye aliyesema ‘tutaweza tu hatumwogopi mtu’. Mwalimu alirudi uraiani na kuzunguka nchi nzima kutafuta wasomi japo walikuwa wachache waje kuchukua nafasi kwenye serikali ifikapo 1962 tutakapokuwa Jamhuri, yaani mamlaka kamili.

Rashidi Kawawa, aliitumia vyema nafasi hii, kwani hakusita hata kidogo, pale alipoona kuna Mwafrika mwenye ujuzi wa kazi ambayo imeshikwa na Mzungu, basi mara moja alimpa mzalendo kazi hiyo. Kipindi hicho kilijulikana maarufu kama Afrikanizesheni (Africanisation). Watu wengi walipandishwa vyeo bila kutegemea. Mmoja wa watu hao alikuwa Mzee Mangara Tabu Mangara, aliyekuwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali (Government Printer), nafasi ambayo haikuwa inashikwa na Mwafrika kabla uhuru.

Nakumbuka pia shule za sekondari hapa jijini ambazo zikiongozwa na Wazungu siku zote wakapewa kuwa Headmasters wake akina Abdulrahman Mwalongo (Azania), Borry Lilla (Agha Khan), Rahma Mwapachu (Zanaki).

Huyo ndiye Rashidi Mfaume Kawawa; msanii wa filamu za maigizo; mtetezi wa wanyonge wakati wa ukoloni; kiongozi wa vyama vya wafanyakazi; Waziri Mkuu na Makamu wa Rais nchini; Waziri wa Ulinzi na ‘Simba wa Vita’; Mwanasiasa nguli aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM.
Alamsiki!
sim

Thursday 26 April 2018


Prince Badru Kakungulu na Kabaka Mutesa, 1955 


Kuhusu uhusiano wa Kabaka na Masultani wa Zanzibar watu wengi wameniandikia kutaka ati mimi niseme kitu. Sijaweza kwa kuwa najua Sayyid Bargash yuko na yeye ni aula zaidi kumsemea babu yake mkuu kuliko mtu yeyote yule. 

Nataka kueleza niliyoshuhudia Kampala nyumbani kwa mmoja wa maprince katika ukoo wa Kabaka ambao ni Waislam walipotualika katika chakula cha usiku nami nikiwa mmoja wa wajumbe wa mkutano uliofanyika hapo Kampala nilipata mwaliko na nilihudhuria.

Kulia Prince Badru Kakungula na Prof. Ali Mazrui


Nitamueleza Prof. Ali Mazrui nini alihadithia alipokaribishwa kuzungumza:

''Tukiwa katika mkutano ule tulialikwa chakula cha jioni nyumbani kwa mmoja wa wajukuu wa Badru Kakungulu na Prof. Ali Mazrui alipoombwa kuzungumza alieleza uhusiano wake na viongozi wa Uganda na khasa ukoo wa Kabaka ambao ni mmoja na akina Kakungulu. Alisema kuwa akiwa mtoto mdogo akikuwa pale Mombasa, Kabaka Mutesa alitembelea Mombasa na katika hadhira moja Kabaka alizungumza na watu wa Mombasa. Kabaka alitoa hotuba yake kwa Kiingereza na mkalimani wake alikuwa Ali Mazrui. Prof. Mazrui akaieleza hadhira ile kuwa Kabaka Mutesa alikuwa akizungumza Kiingereza kwa lafidhi ya Kizungu khasa kiasi ambacho ikiwa humuoni utadhani anaezungumza ni Muingereza mwenyewe. Sasa katika mazungumzo na kijana mdogo Ali Mazrui Kabaka alishangazwa sana na umahiri wa Ali Mazrui katika kusema Kiingereza. Huu ukawa ndiyo mwanzo wake wa kufahamiana na Kabaka Mutesa na Prince Badru Kakungulu alipokuja Uganda kusomesha Makerere.''

Prince Badru kakungulu alifanya mengi wakati wa EAMWS katika kuusukuma mbele Uislam.

Kilichowaunganisha Wazanzibari na akina Mazrui wa Mombasa ni Uislam na hiki kikiwauma sana baadhi ya watu Tanganyika. Yaliyokuja kutokea sote tunayajua. Inasikitisha kuwa baadhi yetu tunafanya haya na mambo ya kuyafanyia maskhara.

Hayo hapo juu yanadhihirisha umuhimu wa Zanzibar katika Afrika ya Mashariki. Prince
Kakungulu anaombewa nafasi aje Zanzibar kusoma. Hii ilikuwa 1923.
The Life of Prince Badru Kakungulu Wasajja na ABK Kasozi
Kulia kwa Prof. Ali Mazrui Tamim Faraj na Kushoto Kwake ni Mwandishi



1. Princess Amal bint Khalifa

2. Bi Khola bint Said Al-Busaidiyah

3. Yaya wa Prince Mutabi

4. Prince Sayyid Jamshid bin Abdalla bin Khalifa (Baadae akawa Sultan wa Zanzibar)

5. Sayyida Nunuu bint Ahmed Al-Busaidiyah (Mke wa Sayyid Khalifa bin Harub, Sultan wa Zanzibar)

6. Prince David Ssimbwa, mdogo wake Kabaka Mutesa II. (Prince David amefariki November 2014)

7. Prince Mutebi (he is now Kabaka Ronald Muwenda Mutebi II of Buganda)

8. ADC to the Kabaka Mutesa II

9. Bi Samira bint Salim Al-Maamariyah

10. & 11. Wageni kutoka kwa Kabaka 

12. Shaikh Mohammed bin Abeid Al-Hajj

13. Sayyid Soud Ahmed Al-Busaidy

14 Riadh bin Abdalla Al-Busaidy

Kitukuu cha Sayyid Bargash anasema maneno hayo hapo chini:

Sisi hatuandiki kwa mate tunadika kwa wino.

Huyo mtoto ni mwanawe  Kabaka wa Buganda na wafuasi wake katika ziara waliokuwa wakifanya Prince Badru Kakungulu ndiye aliyeletwa siku za sherehe za uhuru wa Zanzibar na ndiye aliyenichukua miye kusoma skuli ya Kibuli Kampala katika picha yumo Sayyid Jamshid na Bi.  Nunu mke wa Sayyid Khalifa.


Monday 23 April 2018

Shajara ya Mwana Mzizima
Sheikh Yahya Hussein
‘Mjawiid,’ Mnajimu, Tabibu na Mtabiri Bingwa
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Raia Mwema
23 - 24 April 2018



Sheikh Yahya Hussein na King Hussen wa Jordan,  Amaan 1950s

JUMA lilopita kwenye safu hii ya Shajara ya Mwana Mzizima, tulimwangazia hayati Sheikh Yahya Hussein, aliyefariki dunia miaka kama 7 iliyopita na tuliona misukosuko aliyoipitia maishani mwake mpaka hatimaye kuja kuweza kupata mialiko ya mazungumzo na watu mashuhuri duniani wakiwamo wafalme wa kule nchi za Mashiriki ya Kati na Mashariki ya Mbali— Middle and Far East. Ile ilikuwa ni sehemu ya kwanza; sasa endelea na sehemu ya pili…

Mzee Juma Hussein Juma Karanda, ni babake mkuu Sheikh Yahya Hussein. Mzee Hussein, alipata elimu yake miongo mingi nyuma kutoka kwenye vyuo mbalimbali nchini Yemen; elimu ambayo aliitumia vizuri kwa kuwatoa ujingani vijana wengi sana wa Kitanzania wakati huo pale madrassani kwake Al- Hassnain Muslim School, Dar es Salaam.

Kitendo hicho cha kupigiwa mfano cha Mzee Hussein, kilisaidia sana kuziba pengo la kukosa elimu bora kwa wengi wa watu wa hapa Mzizima wakati ule wa utawala wa kidhalimu wa Kiingereza. Elimu ya Waingereza ilikuwa ikitolewa kwa upendeleo na ubaguzi mkubwa kwa watu wenye asili ya Kiafrika, ambao tuliwekwa kwenye daraja la nne baada ya Wazungu, Wahindi na Waarabu.

Madrassa ya Al Hassnain pale Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam, iliyomilikiwa na Sheikh Hussein na nduguye Sheikh Hassan, ilijitoa muhanga kwa kutoa elimu ya dini ya Kiislamu na ile ya Kidunia (sekula) kwa kiwango kikubwa sana, pengine kuzidi ile iliyokuwa ikitolewa na serikali ya kikoloni. Hili lilithibitika pale Sheikh Yahya alipojiunga na shule za serikali, kwani alikuwa akiwaacha kwa mbali wanafunzi wenzake kwenye matokeo ya kila siku darasani na mitihani ya mwisho pia.

Kwa hili la elimu, Mzee Hussein Juma –babake Sheikh Yahya - ameweza kutupatia majibu na kufuta usemi unaonezwa kwamba ‘jamii ya Kiislamu haipendi kusoma elimu dunia hata kidogo’. Ni uzushi ambao watu wamekuwa wakiuamini bila ushahidi kwa sababu umekuwa ukirejewarejewa mara kwa mara na kuzoeleka.

Msomaji, hebu fanya tafakuri ndogo tu; kwenye miaka hiyo ya 1920 na 1930, Sheikh Hussein Juma amewezaje kutoa watoto wake mwenyewe kama watatu hivi wakiwa wasomi wa hali ya juu; kama huko siyo kuthamini elimu tukuiteje?

Miongoni mwao yumo Professa Mansour Hussein Juma, msomi bobezi wa hisabati anayehadhiri kule Ibadan, Nigeria mpaka leo. Mwengine ni hayati Muhiddin Hussein, aliyekuwa Inspekta wa Jeshi la Polisi kabla uhuru. Inspekta ndio cheo cha juu kabisa alichoweza kushika mtu mweusi kwenye serikali ya kibaguzi ya Kikoloni. Muhiddin yeye alipata degree yake Makerere kabla ya uhuru.

Sheikh Yahya Hussein mwenyewe, mbali na unajimu na utabibu wake, naye pia tayari alishakuwa mwalimu; si wa madrassa peke yake, bali wa shule pia kwani kule Zanzibar amewahi kufundisha shule moja na Rais (mstaafu) Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Mtoto mwengine mkubwa wa Sheikh Hussein Juma ni Kanali (mstaafu) wa JWTZ Juma Hussein Karanda, ambaye alipata kuwa Mkuu wa Karakana ya Magari ya Kijeshi kule Tabora na Lugalo Barracks. Kwa sasa anaishi Kibaha, mkoani Pwani alikoweka makazi baada ya kulitumikia Jeshi muda mrefu.

Watoto wengine wa Sheikh Hussein Juma ni wale mabinti zake watatu Saphia, Zawadi na Husna ambao mwandishi huyu alisoma nao pale Shule ya Msingi Mnazi Mmoja na Uhuru Middle School hapa jijini kwenye miaka ya mwanzo ya 1960s.

Sheikh Hussein Juma, kwa kuchukia ile dharau ya kutawaliwa iliyosababisha wazawa wawe hawana haki yeyote; alijitosa kwenye kupigania uhuru wa nchi yetu ili tusiwe tena wanyonge, sisi na wanawe wale aliowaenzi na kuwapenda.

Alijiunga na chama cha United Tanganyika Party (UTP), ambacho kilikuwa hasimu mkubwa wa chama cha TANU kwa kutokubaliana kimaono na itikadi. Hussein Juma alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa UTP hapa nchini.

Habari zinasema, UTP kiliundwa kwa msaada mkubwa wa tajiri mmoja wa Kihindi kutoka kwenye mashamba ya Katani ya Tanga, kikiungwa mkono pia kwa karibu na Gavana Lord Twinning, ili kije kukipunguzia makali chama cha TANU; na kwa namna hiyo kiwe mbadala kwa wale wasiokubaliana na siasa za Nyerere kutoka Butiama.     

Sasa wakati babake akijiunga na UTP, Sheikh Yahya yeye, bila shaka kwa ushauri wa babake, akajiunga na chama kingine cha siasa kilichojulikana kama All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), kilichoongozwa na Shneider Plantan na Katibu wake akiwa Marijani Shaaban Marijan, aliyewahi kuwa Kocha wa Mpira wa Miguu wa Timu ya Taifa.

Vyama hivyo viwili, pamoja na kile cha African National Congress (ANC) cha hayati Mzee Zubeir Mtemvu (babake Abbas Mtemvu wa Temeke), vilitoa changamoto kubwa kwa chama cha TANU na hivyo kustawisha upinzani uliokuwapo wakati huo kwenye ulingo wa siasa hapa nchini.

Kuwa mwanachama wa UTP wakati ule, ilikuwa ni majanga makubwa kwa mtu yeyote yule. Umaarufu na upenzi kwa chama cha TANU ulikuwa juu sana kiasi cha yeyote yule anayejaribu kukipinga kuonekana kama ni msaliti anayestahili kutengwa na jamii ya watu weusi.

Kwa kukipinga kwake chama cha TANU, Sheikh Hussein Juma alipoteza heshima, hadhi, umaarufu na mambo kama hayo. Popote pale alipoonekana iwe barabarani, mazikoni au kwenye hafla yeyote alikuwa akizomewa na kutupiwa matusi hata na watoto wadogo tu alioweza kuwajukuu:

“Huyo! hilo! Sheikh Hussein Juma UTP huyoo!!!!” alizomewa Sheikh Hussein pamoja na Sheikh mwengine maarufu hapa jijini Sheikh Hashir wa kule Temeke ambao wote walikuwa wanachama wa UTP.

Masheikh hao waliokuwa wakiheshimika kwelikweli kwenye jamii ya Kiislamu kabla ya siasa za TANU wakawa maadui wakubwa wa jamii inayowazunguka; waliishia kuwa watu wa kukaa ndani tu pekee. Hawakuonekana tena misikitini, misibani au kwenye mijumuiko ya watu. Zuberi Mtemvu na Congress yake, yeye alikaza kamba akaendelea kama kawaida na hakutishwa na jambo lolote.

Uhuru ulipopatikana, watu hao watatu - Sheikh Hussein, Sheikh Takadir, Zubeir Mtemvu - kama vile walikuwa wamekufa, wakatengenezewa majeneza (effigies), yakazungushwa kwenye mitaa ya Dar es Salaam na baadaye yakachomwa moto kuashiria mwisho wao.

Madrassa ya Al - Hassnain, nayo ikafa polepole kwa vile watu walikuwa wakiwatoa watoto wao chuoni hapo mmoja mmoja na mwisho ikafunga milango yake kwa chuki za kisiasa. Wazee wale, pamoja na heshima walizokuwa nazo hapo mwanzoni, wakawa wanaiaga dunia hii kwa kihoro na unyonge, mmoja baada ya mwengine - Inna lillah Waina Illayhi Rajuun!

Sasa basi, wakati hayo tukiyaweka pembeni, hebu tumwangazie tena na kumkumbuka Sheikh Yahya Hussein, katika sifa yake nyengine kubwa ya ukarimu na kusaidia kwa wasiokuwa nacho. Kwa kawaida yao, masheikh wengi tumezoea kuwaona wakiwa wapokeaji na wala si watoaji wa sadaka; huyu hakuwa hivyo!

Wakati ule wa uhai wake, na pale anapokuwapo jijini Dar es Salam, marhum Sheikh Yahya hutoka asubuhi na mapema pale nyumbani kwake Magomeni Mikumi na kufanya mazoezi ya kutembea mpaka Kariakoo akiwa ameongozana na kundi la jamaa na nduguze wa karibu.   

Safari yao hiyo huwachukua mpaka Seiyun Hotel, pale Msimbazi, Kariakoo, jirani kabisa na ile Madrassa ya kwao ya Al-Hassnain. Wakiingia hapo, kila mmoja huagiza chakula akitakacho kwa ajili ya kifungua kinywa.

Seiyun Hotel, ni hoteli maarufu sana jijini inayokaribia uwepo wake kwa zaidi ya miaka 70 au 80 hivi, ikisifika sana kwa kutengeneza maandazi mazuri na laini pamoja na michuzi ya kuku na mbuzi iliyopikika sawasawa.

Sasa, Sheikh Yahya anapofika na kundi lake, huwa anamlipia kila aliyemo mle hotelini bili yake ya chakula hata kama hakuja naye yeye, ile michuzi, vitafunio na chai. Chai ya Seiyun, nadhani inaweza kuingizwa ndani ya mashindano ya Zawadi za Guinness duniani na ikashika namba moja!

“Ah! Mwache tu kila mtu aende zake sisi tutalipa hiyo bili,” husikika Sheikh Yahya akiwaambia wenye hoteli wasichukue pesa kwa yeyote yule anayemaliza kula.

Wakati akiyafanya hayo hapo hotelini, mara zote anakuwa tayari asubuhi ile, ameshatoa sadaka nyingi nyingine kule nyumbani kwake kwa watu wengine waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake atoke na kuwapa ‘chochote kitu’ wakajikimu.

Basi huyo ndiye Sheikh Yahya; hakuwa Sheikh mpokeaji sadaka, bali mtoaji sadaka mara zote. Kama siku hiyo hakwenda Kariakoo basi hufika pale hoteli ya Shibam, Magomeni Mapipa na kufanya kama alivyofanya kule Seiyun, Kariakoo.

Tumwombe Mungu na sisi atupe uwezo wa kuyafanya hayo ili tulipwe malipo mema kesho mbele ya hesabu.

Jamil Hizam, ni Mtanzania mwengine aliyehamia Dubai kule Falme za Kiarabu. Alikuwa mchezaji mpira mashuhuri wa timu za Dar Young Africans na Cosmos ya Dar es Salaam pia kwenye miaka ya 70s kabla hajahamia Arabuni.

Wapenzi wake mpirani walimbatiza jina wakimwita ‘Dennis Law’ (mchezaji mpira wa zamani wa Timu ya taifa ya Uingereza), kwa umahiri wake wa kusakata ‘kabumbu’. Jamil ni mzungumzaji ‘barzani’ kwenye kijiwe chetu pale Kariakoo kila anapokuja Dar es Salaam.

Siku moja tulikuwa tunamzungumzia Sheikh Yahya na mikasa yake. Jamil akasema ngoja nikupeni kisa kimoja; kisa ambacho na mimi mwandishi naona nikisimulie kwa wasomaji wangu leo hii tucheke pamoja.

Jamil anasema:

“…Mwaka 1967 kulikuwa na mechi kati ya Yanga na Sunderland (sasa Simba) ambapo Sheikh Yahya alitabiri Abdulrahman Lukongo angefunga goli kwenye mechi hiyo.

“Mechi ilivyoendelea Abdulrahman Lukongo aligongana kichwa na beki wa Simba aitwaye Durban, katika kugombania mpira wa juu ambapo marehemu Lukongo akapasuka juu ya jicho ikabidi atolewe nje asiendelee tena na mchezo; Lukongo aligoma katukatu kutoka akapewa ‘handkerchief’ kushikilia kuzuia damu na akaendelea kucheza kusubiria utabiri utimie;

“hatimaye, ingawa Simba walishinda 2-1, hilo bao moja la Yanga alilifunga Lukongo ambaye hakukubali kutoka mpaka alipofunga goli alilotabiriwa na Sheikh Yahya …teh! …teh! …teh!”

Mambo ya Sheikh Yahya hayo, ilimradi ni mikasa na mazingatio.

Mkasa mwengine ulitokea kule Nairobi bungeni wakati wabunge wa Kenya walipochachamaa wakitaka Sheikh Yahya kutoka Tanzania afukuzwe arudi kwao, kwani alikuwa akiwanyonya Wakenya na kupata utajiri mkubwa.

Sheikh Yahya Hussein akimpa Rais Jomo Kenyatta zawadi
ya bakora ya kutembelea

Akiwa kule Nairobi, Sheikh Yahya, wateja wake wakubwa walikuwa watu matajiri wa kibiashara, wabunge, mawaziri, wakiwamo viongozi wakuu kama vile Mzee Jomo Kenyatta mwenyewe na familia yake na za nduguze. Alikuwamo pia Rais Daniel Arap Moi. Alikuwamo pia aliyekuwa Meya wa Jiji la Nairobi, Alderman Charles Rubia. 

Mjadala mkali ulizuka bungeni kwa ajili ya chuki tu na kuuchukia Utanzania wake. Kwenye fani ya utabiri alikuwapo mtu mwengine kutoka Kongo DRC alijulikana kama Dk. Ng’ombe, lakini hakuna mtu aliyepiga kelele zozote kama afukuzwe au vipi:

“…Mr. Speaker… hii mutu kutoka pande ya Tandhania ni vizuri akwende kwa nchi yake, yeye  ako na pesa mingi anapata hapa kwa nchi yetu tukufu ya Kenya na kufanya yeye kuwa tajiri kupindukia…

“Mr. Speaker… ni bora akwende kwao kule, maana wao natukana tukana Kenya yetu kila mara…”

hayo ni baadhi ya maneno ya wabunge wa Kenya na Kiswahili chao kibovu wakimlalamikia Sheikh Yahya.

Daniel Arap Moi, aliyekuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo y Ndani (Home Affairs Minister) na Kiongozi wa Serikali bungeni; ndiye aliyekuja kuumaliza mgogoro kwa kuufunga mjadala ule na kusema Sheikh hakuvunja sheria yoyote pale Kenya; na hivyo aachiwe aendelee na shughuli zake kama kawaida.

Sheikh alipanua zaidi shughuli zake kwa kuwa na ofisi sehemu mbalimbali hapa Afrika Mashariki na Kati na nyengine akafungua pale London, Uingereza ambako Wazungu walitokea kumkubali vizuri kutokana na uwezo wake wa kuzungumza lugha kwa ufasaha kama amesomea pale kwao Oxford na Cambridge!

Alamsiki! Tukutane wiki ijayo InshaAllah.
simu : 0715808864