Showing posts sorted by relevance for query ebby sykes. Sort by date Show all posts
Showing posts sorted by relevance for query ebby sykes. Sort by date Show all posts

Monday, 16 February 2015

Ebby Sykes

Ebby Kwenye Msiba wa Baba Yake Mdogo Ally Sykes 20 May 2013

Dully Sykes
Kushoto:Kleist Abdulwahid Sykes, Ebby Abdulwahid Sykes, Sauti Thomas Plantan na Abdulwahid Ally Sykes


Khitma Nyumbani kwa Kaka Yake Kleist Sykes

Jaji Joseph Sinde Warioba, Paul John Rupia na Mzee Shomari Nyuma Aliyevaa Suti Nyeusi ni
Mohamed Maharage Juma "Contemporary" wa Ebby wote walikuwa Wanamuziki Katika Ujana Wao
Mohamed Maharage ni Mkuu wa Itifaki, Ikulu
Kushoto wa Kwanza Mohamed Maharage Juma Katika Miaka ya 1970
Sheikh Mahdi Akisoma Talakini Kwenye Kaburi la Ebby


Mwinyi Mangara na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki (Katikati)
 Kulia kwa Mangara ni Ahmed mwinge na Kushoto ni Kube, Chande na Hussein
Kushoto: Abbas Sykes, Mshike, Abdul Faraj, Mwinyi Mangara na Said Mecky Sadiki

Baada ya Maziko


Katika maisha yangu sijapata kuandika taazia ya mtu aliyekuwa karibu nami. Hii itakuwa ya kwanza In Sha Allah. Hata hivyo sijui kama itakuwa na maneno mengi kwa kuwa mengi niliyonayo ni binafsi zaidi kwa hiyo nahisi kama hakuna ambae atataka kusoma kitu kama hicho.

Ngoja  nijaribu.

Ebby alinitangulia kuja duniani kwa siku moja. Yeye kazaliwa tarehe 24 Februari, 1952 mimi nikazaliwa siku ya pili yake tarehe 25 Februari na mama yangu Bi. Baya biti Mohamed akalala kunizaa mimi kitanda kile kile alicholala jana yake mama yake Ebby Bi. Regina. Nilikuja kumuona mama yetu miaka mingi sana baadae mimi nishakuwa kijana mkubwa nyumbani kwa rafiki yangu Yassin Idd (marehemu) Mtaa wa Bonde ambae alikuwa amemuoa dada yake Ebby, Miski. Miski alikuwa kajifungua mtoto na mama alikuja pale kutoka Morogoro kuja kumkalia binti yake.

Mimi na Ebby tumekuwa pamoja toka utoto wetu tukawa pamoja katika ujana na tukawa watu wazima pamoja ingawa baada ya kutoka katika ujana kila mtu akawa ameshughulika na maisha yake. Babu zetu hata kabla hatujazaliwa sisi wao walikuwa marafiki na bibi zetu wakiwa mashoga. Hiyo ilikuwa katika miaka ya 1930. Ebby alikuwa Kipata karibu na New Street (sasa Lumumba) na sisi tulikuwa Kipata ya Mtaa wa Nyamwezi. Sina mengi ya kusema kuhusu babu zetu ila kuwa walikuwa majirani wakiishi Mtaa wa Kipata (sasa Kleist Sykes) na wote wakifanya kazi Tanganyika Railways lakini nina kumbukumbu nyingi za bibi yake Ebby Bi. Mruguru biti Mussa ambae shoga yake alikuwa bibi yangu Zena biti Farjalla. Tulipokuwa watoto tukipenda sana kula kaukau. Hii ni "snack" inayotengenezwa na unga wa ngano. Kaukau ilikuwa inauzwa katika hoteli ya Mzee Saidi. Huyu alikuwa Mzee wa Kiyemeni na hoteli yake ilikuwa Mtaa wa Narung’ombe na Sikukukuu.

Mtaa wa Kipata Kama Ulivyokuwa Katika Miaka ya 1970 Nyumba zote Hizo Sasa ni Magorofa
Mimi nimezaliwa Hiyo Nyumba Baada ya Nyumba Yenya Rangi Nyeupe Nyumba ya Pili Na. 32
Hii ilikuwa mitaa yetu na dunia yetu yote ikizunguka hapo. Mwenye hela atanunua na tutagawana kisha ikisha tunatazamana kupiga akili vipi tununue kaukau nyingine hadi kifu yetu. Nawakumbuka wenzangu wa wakati ule, Hamza Msanga Mapesa (marehemu), Mohamed Abdulrahman maarufu kwa jina la Mohamed Kitunguu, Ali Hussein (marehemu) maarufu kwa jina la Ali Kioze, Abdu Mgunya na Juma Kube. Basi tukifika hapo kuwa kaukau tumemaliza na bado tuna hamu Ebby atatuchukua hadi kwa bibi yake Bi. Mluguru, Mtaa wa Kirk (sasa Lindi) na Sikukuu. Lakini hatutomsindikiza hadi kwao kwa bibi yake. Sisi tutabana kwenye kona ya mtaa. Hapo alikuwa kinyozi Mzee Mwingereza. Huyu ndiye alikuwa kinyozi wa watoto wote wa Gerezani na barza yake ilikuwa maarufu kwani wakati wa siasa za kudai uhuru katika miaka ya 1950.

Hapo ndipo baba yake Ebby marehemu Abdulwahid Sykes, Dossa Aziz na wanasiasa wengine walikutana kupoteza wakati. Palikuwa hakuna viti wakikaa kwenye kigogo cha mnazi. Ebby atakwenda kwa bibi yake Bi. Mluguru kuomba hela ya kaukau. Bi. Mluguru pale barazani kwake alikuwa na biashara yake akiuza togwa. Siku ikiwa shetani wa kaukau katuondokea tunakwenda kumwamkia Bi. Mluguru na yeye hatatutoa kapa. Atatupa chupa moja moja ya togwa tujiburudishe. Turejee kwa Ebby. Punde Ebby atarudi na hela na safari itaanza kuelekea hoteli kwa Mzee Said kununua kaukau. Ebby alikuwa kiongozi wetu na iko siku ataamua leo tusicheze mpira twendeni sokoni Kariakoo tukaokote mabua tutengeneze miti ya kurukia “high jump.” Ebby ndiye aliyenifundisha mimi “high jump.” Mchezo huu tulikuwa tukifanyia kwetu Mtaa wa Gogo kwa mama yangu mdogo Bi. Mtoro biti Mohamed, kwa kuwa kulikuwa na tifutifu. Haya yote tukifanya wakati wa likizo.

Miaka ikenda sasa tukawa vijana. Michezo ya kitoto tukaiacha. Hiki ndicho kipindi mimi nilishakamana sana na Ebby. Huu sasa ulikuwa ule wakati Waingereza waliuita, "The Roaring 60s." Ebby alizaliwa katika nyumba ya muziki. Baba zake wakati wa ujana wao walikuwa na bendi iliyoitwa, "The Skylarks." Hii ilikuwa katika miaka ya 1950 wakati sisi tunazaliwa. Ebby katika miaka ile ya 1960 katikati yeye tayari akiwa kijana mdogo wa miaka kama 14 hivi tayari alikuwa amekwisha kuwa mpiga gitaa mzuri. Alikuwa Ebby ndiye alinifunza mimi "chords" za gitaa. Ebby alikuwa na gitaa lililokuwa kwao. Nalikumbuka hili gitaa aina yake ilikuwa “Gibson.” Gibson lilikuwa gitaa mashuhuri Marekani na Marekani ya Kusini kwa ajili ya sauti yake ya kuvuma tofauti na magita yaliyokuwa yakitumika Ulaya ambayo yalikuwa yanaitwa, “solid” yakitoa sauti kavu, maarufu katika haya lilikuwa, “Hofner.”

Siku moja nazugumza na Balozi Mohamed Maharage nyumbani kwake Makongo, akanambia, "Unajua Sidney (hii ilikuwa nickname yangu) wewe ndiye ulionifunza mimi "chords.” Ebby alikuwa mwimbaji mzuri pia. Akiwaiga waimbaji wa wakati ule - Percy Sledge, Wilson Picket, Ottis Redding na wengineo. Mimi nilichelewa kuhama nilikokuwa wakati "Soul" ishaingia Dar es Salaam. Mimi bado nilikuwa kwa Elvis Presley na Cliff Richard. Nakumbuka wakati ule nikifanya mazoezi na rafiki yangu Abdul Yusuf kuupiga mwimbo wa Cliff Richard, "You and I," wakati Ebby rafiki yangu akishika gitaa anapiga, “Hold On,” ya Sam and Dave. Abdul Yusuf  tulisoma darasa moja St, Joseph's Convent na wakati ule umri wetu ulikuwa miaka 15. Abdul Yusuf alikuja kuwa Aeronautical Engineer.  Ebby akizisikiza "soul" kwenye "record player," nyumbani kwao kisha akizikopi na kuzipiga kwa "key" ile ile waliopigia wenyewe. Wakati huo baba yake, Bwana Abdul Sykes alikuwa kajenga nyumba Magomeni Mikumi na wamehamia hapo.

Kushoto: Kamili Mussa, Yusuf Zialor (marehemu), Abdallah Mgambo, Othmani Chande
Aliyekaa Kleist Sykes, Ebby Sykes, Miriam Max, Janeth Zebedayo, Erica Kissa, Elizabeth Frisch (1960s)
(Picha kwa Hisani ya Abdallah Mgambo)

Mitaa hiyo kwa wakati ule wazee wetu wengi walijenga hapo, Chifu Fundikira alikuwa na nyumba Mikumi, Mzee Mzena, Chihota, Mzee Amri, Mzee Mgone, Mzee Muhuto, Ally Sykes, Abbas Max, Mzee Mwakinyo ili muradi mitaa hiyo ilikuwa na uchangamfu wa aina yake kwa ajili ya watoto wa wazee hawa, wa kike na wa kiume. Sisi tuliokuwa tukiishi, Upanga, Karikoo, Temeke na kwengineko mchezo wetu ulikuwa Mikumu na tukapaita, "Soulville." Hii ni kwa sababu wakati ule muziki uliokuwa ukitamba dunia ulikuwa "soul" na bingwa wa "soul music," alikuwa James Brown. Ikawa sasa tukijifunza kupiga muziki kwa staili ya Motown. Hii ndiyo ilikuwa “record label,’ mashuhuri ya muziki wa “soul,” kutoka Detroit. Miaka mingi sana baadae naingia Marekani na “entry point” yangu ilikuwa Detroit. Nilipokuwa nimesimama kwenye foleni kusubiri kugonga pasi yangu, fikra zangu zilinirudisha nyuma sana.


Kushoto: Adam Kingui, Vuli, Ebby Sykes, kwenye drums Khalid,
Kulia Bob Dean, Nasser (Mick Jagger), Choge Sly 
Siku ya Jumatano shule mwisho saa sita. Hiyo ndiyo ilikuwa siku tunakutana Magomeni Mikumi nyumbani kwa akina Mohamed “Captain Mike” kufanya mazoezi ya nyimbo zetu. Ebby siku zote alikuwa "centre stage." Huu ndiyo wakati Adam Kingui, katika vijana waliokuwa na kipaji kikubwa cha muziki akiwa na kundi la The Rifters pamoja na Simon Ngocho (Simon alikuja akawa Civil Engineer) sasa ni marehemu, Mohamed Ali Abbas (marehemu), Vuli kijana kutoka Afrika Kusini, Nassoro maarufu kwa jina la Mick Jagger, na vijana wengine siwakumbuki.  Leo nikiangalia nyuma naona wakati ule ulikuwa mgumu sana kwetu lakini sioni sababu ya sisi kujilaumu tulikuwa tunaitika mazingira ya wakati uliokuwapo. Miaka ya 1970 tunamaliza sekondari. Sasa tunaanza kuwa na akili zilizotulia. Ebby akaenda Mombasa kujaribu bahati yake katika muziki. Hakukaa sana Mombasa akenda Piraeus Greece. Huo ulikuwa wakati vijana wengi wanatafuta kazi ya ubaharia. Ebby hakukaa sana Ugiriki akarudi Dar es Salaam.  Miaka ikapita...
Kushoto: Dimitri, Vyas, Kleist Sykes, Abdallah Mgambo na Adam Kingui 1965

Ebby alikuwa mpole lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kumdhibiti mbabe yoyote. Siku zile za madansi ya mchana tukiita "Boogie," tukimaliza dansi wakati wa kurudi nyumbani tunachokozana. Kulikuwa na “gang,” za vijana wa Temeke, Magomeni na kwengineko. Ukiwa umefuatana na Ebby jua uko salama. Wababe wakimjua hivyo wakimfanyia staha. Ebby Mungu alimjaalia mshipa wa kula. Alikuwa anaweza kula sana kiasi ilikuwa zamani tukienda kula chips haikuwa ajabu Ebby kupiga sahani mbili za chips kwa samaki au kuku peke yake kisha akashushia na soda. Nakumbuka siku moja naingia kwenye kimgahawa kimoja kilikuwa Maggot hii ilikuwa hoteli maarufu katikati ya mji. Ebby alikua ameshaniona toka nakuja akawa kapiga oda yangu. Nafika tu tunasalimiana muhudumu namuona ananiwekea kilima cha kababu. Mimi nimeshangaa. “Ebby akanambia, “Sidney yako hiyo nimekuodea.” Sasa nikaanza kulalamika kuwa siwezi kumaliza na nini. Ebby hakusema kitu. Alinyanyua ile sahani yangu akajipunguzia kababu kwenye sahani yake ambayo tayari ilikuwa ni kilima akaendelea kula.

Buriani ndugu yangu, rafiki yangu Ebby. Si haba Allah katukadiria umri wa kutosha na tushukuru kwa hilo. Miaka 63 si haba ingawa mwenzangu ulibakisha siku tisa tu kukamilisha hiyo miaka 63.

Allah akuweke mahali pema peponi.

Amin


Ebby na Mimi 2010

Thursday, 19 February 2015

Abbas Sykes Msikiti wa Kipata

Kushoto: Boi Juma Risasi na Mussa Shagoo Viongozi Waandamizi wa
Saigon Club Nyuma Kushoto ni Salum Hariz na Adilla Abraham Sykes

Sheikh Ali Basaleh Akiomba Dua



Kushoto:Abdulwahid Ally Sykes, Kleist Abdulwahid Sykes, Mwinyi Mangara
Baada ya Khitma Nyuma Yao ni Abdulwahid Kelist Abdulwahid Kleist Sykes
na Balozi Abbas Sykes


Sunday, 19 June 2016


Juma Mwapachu na Julius Nyerere













Nguruvi3,
Ama ingekuwa si kwa kuwa naburudika kufanya mjadala na wewe
mie muda mrefu ningelikwisha nyanyua mikono juu lakini nastarehe
kuongea na wewe.

Allah amekupa kipaji cha aina yake.

Majibu nimekupa kuhusu katiba ya TAA Political Subcommittee kuwa
nyaraka na microfilm zote hazionekani Maktaba ya CCM Ddodoma
na TNA.

Sikuishia hapo nimekueleza kuwa kabla yangu katiba hiyo ilitajwa na
Listowel mwaka wa 1965 na Pratt 1976.

Bado unataka nikuletee hiyo document.
Kama wewe hodari sana mbona huwaulizi CCM nyaraka hizo zilipo?

Lakini ninastarehe katika mnakasha huu kwa kuwa natoa darsa na
wengi wanasoma historia ambapo hawakupatapo kuisikia hata kwa
mbali.

Ndiyo maana narudi hapa tena na tena na tena.
Nakushukuru sana kwa hili.

Sasa nisikilize kwa makini na tuliza ubongo wako nikufunze mbinu
za ''critical analysis'' na kujifunza kusoma katikati ya mistari.

Sitakujibu hayo yote uliyoandika nitakujibu hayo tu ambayo umeweka
rangi nyekundu.

Hamza Mwapachu alimjulisha Nyerere kwa uongozi wa TAA 1949.

Akili yako mara moja imekwenda kuwa walikuja hadi New Street na
kuzungumza na Mwalimu Thomas Saudtz Plantan aliyekuwa rais na
Clement Mohamed Mtamila aliyekuwa katiibu wa TAA wakati ule.

Lakini ukweli ni kuwa Mwalimu Thomas Plantan na Clement Mtamila 
walikuwa hawajapata kukutana na Nyerere hadi alipokuja kwa Abdul
Sykes 
1952.

Inawezekana ujulisho huo ulikuwa wa salam za mdomo au wa barua.

Nakuwekea picha nikifanya mahojiano na Bi. Maunda Thoams Plantan
mtangazaji wa kwanza wa kike Tanganyika, Sauti ya Dar es Salaam 1952
na mwalimu wa shule.

Mjukuu wa Affande Plantan na mtoto wa Mwalimu Thomas Saudtz
Plantan
.

[​IMG]
Kushoto Bi. Maunda Plantan na Mwandishi

Katika mazungumzo yetu hakupatapo kunambia kuwa baba yake
alipata hata kwa siku moja kuonana na Nyerere.

Nimezungumza pia na Happy Mtamila hata mara moja hajanieleza
kama baba yake alipata kuonana na Nyerere kabla ya 1952.

[​IMG]
Kulia Bi. Happy Mtamila na Mwandishi

Ningependa kukufahamisha tu kuwa uamuzi wa Nyerere kuacha kazi
ulifanyika nyumbani kwa Clement Mtamila Mtaa wa Kipata na Sikukuu.

Nyumba hii ilikuja kununuliwa na ukoo wa Baharoon ikavunjwa na
sasa ni ghorofa. 

Kushoto: Kleist Abdulwahid Sykes, Ebby Abdulwahid Sykes, Saudtz
Thomas Plantan na Abdulwahid Ally Sykes

Wednesday, 6 December 2017

Buriani ‘Kaka Kleist’
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Mwandishi wa makala Abdallah Tambaza ni huyo wa kwanza kushoto, Bubby Bokhari, Kleist Sykes, Yusuf  Zialror, Mohamed Said, waliochutama kushoto ni Kaisi, Wendo Mwapachu na Abdul Mtemvu, 1968

AWALI ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Allah (SW) na kumtakia rehma Mtume wetu Muhammad (SAW) kwa kuniwezesha kukaa mbele ya kompyuta na kuandika taazia hii ngumu na nzito ya marehemu kaka yangu; ndugu yangu; sahib yangu; na rafiki yangu kipenzi kabisa kupata kutokea, Kleist Abdulwahid Abdallah Sykes – Inna Lillah Waina Ilayhi Rajiun.

Mwezi Januari mwaka huu nilimwandikia rafiki yangu mwengine, SACP Mohammed Chico, taazia nzito kama hii iliyonitoa jasho na machozi pale ilipokamilika. Sikudhani hata kidogo kama hautapita muda mrefu nitarudi kuandika tena taazia nyengine kwa mtu anayefanana na yeye ­­– wote ni watu wa kwetu Dar es Salaam niliowajua vilivyo. Wazungu wa kule Ulaya Ingereza na Marekani, wanapofikwa na msiba wa ukubwa kama huu, husema kwamba umekuja ‘untimely’ (haukutarajiwa kwa wakati ule, wakati sio ule na labda ungesubiri baadaye hivi). Wanasema ‘untimely’, kwa sababu bado wasingependa kuachana na mpendwa wao kwa wakati ule; wanasema ‘untimely’ kwa sababu wanajua uchungu wa kuondokewa; na wanasema ‘untimely’ kwa sababu kwa anayeondokewa hategemei tena kupata mbadala wake! Kwa kiasi fulani wako sahihi, kwani yu wapi leo ‘Kaka Kleist’ mwengine? Marehemu ‘Kaka Kleist’, alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumatano, Novemba 22, mwaka huu, katika Chumba cha Watu Wenye Kuhitaji Uangalizi Maalumu (ICU), pale katika spitali ya Agakhan ya hapa Dar alikokuwa amelazwa jana yake.

Mara baada ya kifo kutokea, dadake, Misky Sykes, ambaye alikesha kucha pale spitali kufuatilia hali ya mgonjwa wake, akanipigia simu kunipa habari za msiba ule mzito huku akilia na kuomboleza: “…Kaka Abdallah eh …nadhani Kaka Kleist amefariki sasa hivi, naona madaktari na manesi wanahangaika pale… nafikiri ametutoka kwani hawasemi kitu… Ooh! Ooh! Ooh!” alikatiza Misky mazungumzo na kutoweka na kilio chake. Kleist alizikwa siku ya Alhamisi jioni katika makaburi ya Kisutu, katika mazishi yaliyoongozwa na aliyepata kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu (mstaafu) Mohammed Chande Othman. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, na Waziri wa Ujenzi na Miundombinu, Makame Mbarawa, ambaye ndiye aliyemwakilisha Rais JPM. Alikuwapo pia Prof. Haruna Lipumba wa CUF, Mbunge Mussa Azzan Zungu na Iddi Azzan zamani Mbunge pale Kinondoni, pamoja na mameya na madiwani mbalimbali wa jiji hili la Dar es Salaam. Walikuwapo pia vijana wengi wa Dar es Salaam wa kizamani ambao pengine wamesoma au kucheza pamoja na marehemu katika maeneo mbalimbali ya jiji hili.Walikuwapo pia watoto wa marafiki wa Kleist ambao waliongozana na wazee wao kuja kumsindikiza katika safari yake ya mwisho mwana wa jiji mwenzao ambaye habari zake na ukarimu wake pengine walikuwa wakisimuliwa na wazee wao kwenye sebule zao.

Jaji Chande Othman, pamoja na kwamba alikuwa pale kwenye turubai lilowakinga viongozi, sidhani kwamba moyoni mwake alikuwa akihisi kuwa pale alipo alikuwa akihudhuria mazishi ya mtu wa kiserekali tu, kwani siku zile za utotoni kwake, si tu alisoma pamoja na Kaka Kleist, lakini pia yeye pamoja na kakake mkubwa Prof. Othman Chande, walikuwa kundi moja la Boys Scouts tawi la Saint Joseph’s Convent School, Forodhani. Mohammed Chande na Kleist pia walisoma wakati mmoja pale H.H. AgaKhan Secondary School (1964-1967).Hawa kina Chande wawili, waliungana na vijana wengine wa pale Shule ya Mtakatifu Joseph, Forodhani wakaunda kikundi cha vijana kilichojulikana kama The Scorpions, madhumuni yake yakiwa ni kupendana, kusaidiana na kutembea pamoja pale inapobidi.

Scorpions wengine waliokuwapo pale siku ile ni Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo, Abdul Mtemvu, Wendo Mwapachu, Yusuf Zialor, Christopher Faraji, Kamili Mussa, Bhobby Bokhari pamoja na mimi mwandishi wa makala haya. Nilimwona pia Mbunge Mussa Azzan ‘Zungu’ pale makaburini. Zungu hakuwa anamwakilisha Spika Ndugai pale. Kwa vyovyote vile alikuwapo kwa ajili ya kuwa amecheza na Kleist utotoni kwenye mitaa ya Kariakoo na Gerezani ambako wote ndiko walikokulia. Mzee Warioba, pamoja na nasaba yake ya Musoma, alikuwa mtu wa hapa mjini siku nyingi. Kabla hata hajajiunga na Chuo Kikuu, pale Mlimani alikuwa akionekana akivinjari mitaa ya New Street, Gerezani na Mission Kota, siku nyingi sana na hivyo akawa amezoeana vilivyo na vijana wengi wa jiji hili akiwamo marehemu Kleist Sykes. Isitoshe, mke wa Jaji Warioba ni mwenyeji wa Dar mwenye uhusiano wa karibu sana na kina Sykes.




Mwingine ni Mzee Kikwete. Huyu hakuwapo pale kumzika kada mwenziwe wa CCM tu. Kikwete naye Dar es Salaam ni yake na vijana kama Kleist ni rika lake, hivyo wakigongana hapa na pale kwenye kumbi za starehe na burudani hasa miziki ya ‘’Buggy,’’ na kwenye viwanja vya mpira. Kikwete alipotea njia kidogo akawa anapenda Yanga, wakati Kleist ni Simba wa kutupwa. Mapema, katika nasaha zake kwa waombolezaji mara baada ya sala ya jeneza pale Msikiti wa Maamur, Upanga, Imam Mkuu Sheikh Issa aliwataka waumini kujiandaa na kile alichokiita ‘certainty of mortality,’ akiimaanisha kwamba kifo kimedhihiri na kwa hakika kitamfika kila mmoja; kwa hiyo hapana budi watu kukifanyia maandalizi yake kabla. “Katika maisha yetu ni vizuri basi watu wakakaa mbali na yale yote ambayo Allah (SW) ameyakataza na kuyafanya kwa wingi (kuyakimbilia) yale ambayo Allah (SW) ameyaamrisha kwayo,”amesema Sheikh Issa.  


Nyuma kulia ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete
Sasa wakati nikiyatafakari maneno yale adhimu ya msomi yule pale msikitini, nilijihisi kama vile alikuwa akiniambia mimi au labda alikuwa akijua namna marehemu alivyokuwa mtu wa kheri, hasa katika utoaji wa sadaka na mambo kama hayo. Kaka Kleist, alipenda sana kusaidia wengine na wala hakusubiri kufuatwa kwa shida ndiyo afanye hivyo. Kuna wakati unaweza kukutana naye tu iwe ofisini au sehemu yeyote na ghafla atakurushia swali: “Vipi wewe uko vizuri mifukoni?” Kabla hujajibu tayari atakuwa amekwishatoa pochi lake na kukuvurumushia pesa ukafanyie jambo lolote. Kwa watu wazima na vikongwe hapo tena ndio usiseme. Hivyo ndivyo alivyoishi katika jamii inayomzunguka na kwenye makundi ya marafiki zake. Sasa wakati Sheikh Issa akitoa nasaha zile ikaja taswira fulani hivi ya kwamba rafiki yangu yule, njia yake ya kuelekea kwa Mola wake ilikuwa kwa kiasi fulani imesafishika tayari.

Siku moja wakati ugonjwa umeshamtopea kwelikweli na figo hazipatikani, nilifika kumwona pale kwake Mbezi Beach. Tulitazamana machoni na yeye akagundua kwamba mimi nimehuzunika sana. Alinitazama na akaniambia: “Sikiliza we ‘timbwa’ wala usihuzunike mimi tayari nimewasomesha watoto wangu wote vizuri sana …sina kinyongo hata kama Mwenyezi Mungu atanichukua leo… niko tayari kwa hilo,”alisema. Yale yalikuwa ni maneno mazito kuyasema mtu aliyekuwa kwenye hali kama yake. Palepale nilijua ile ilikuwa ni kama ananiaga kiaina, kwani tayari alikwishahisi dalili kuwa safari yake haiko mbali. Kamwe, hakuwa mtu wa kukata tamaa kirahisi, kwani aliujua vizuri ugonjwa wa kisukari na madhara yake ikafikia hata wakati mwengine kupendekeza tiba mwenyewe kwa madaktari wake. Katika juhudi zake za kupambana na maradhi, marehemu kwa nyakati tofauti alikwenda sehemu mbalimbali duniani kutafuta tiba. Juhudi za kila aina zilifanyika kupata figo mbadala (transplants), lakini ilishindikana kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya umri mkubwa n.k. Na hapa napenda kumfariji shemeji yangu Stella Mallya ambaye alijitolea sana kuhakikisha mume wake anapona kwa namna yeyote ile.

Kwa upendo na hali ya kawaida, tulikuwa tukipenda kumwita ‘Kaka Kleist’, hata kwa wale ambao hawakuwa wadogo zake wa damu. Sababu ni kwamba wadogo zake walikuwa marafiki pia, na hivyo kwa kawaida huchanganyika na watu wengine kutembea na kustarehe pamoja. Sasa, inakuja katika mazungumzo, majadiliano ya hoja au kutaniana kwa aina yeyote, watu wengine walikuwa wakimwita Kleist kavukavu hivihivi; wakati wadogoze (akiwamo Abraham, Ayoub, Mussa, Misky, Omar (sasa marehemu), Adam (sasa marehemu), Ebby (sasa marehemu) ilikuwa inawashinda; kwani kila mara ni lazima waanze na kitu ‘kaka’. Hivyo tamko ‘Kaka Kleist’ likawa linaleta ladha fulani kulisikia; maana nduguze hawakumwita mtu mwengine yeyote kaka zaidi ya Kleist, hata kama ni mkubwa kama huyo kaka yao. Wengine waliitwa tu, kwa majina yao ya utani na mzaha (nicknames) kama kawaida.

Katika miaka hiyo, mwandishi huyu, kwa marafiki zake alikuwa akipachikwa majina mengi ya masikhara na utani kama vile ‘Nene’ au ‘Timbwa’, kutokana na wingi wa kilo mwilini. Lakini kamwe sikusikia mtu akiniita ‘Kaka Nene’. Tamko hilo lilikuwa ni makhsusi kwa marehemu Kleist peke yake. Sababu nyengine ya kuitwa kaka ni kwamba, alikuwa ni mtu wa upatanishi na usuluhishi panapotokea sintofahamu baina ya marafiki zake. Alikuwa na kipaji, uwezo na akili nyingi sana za kuweza kuleta suluhu au ushawishi katika kujenga hoja kwenye vikao mbalimbali. Mambo hayo ni miongoni mwa sifa zilizomfanya watu wamwite, ‘Kaka Kleist’.

Mara ya kwanza kabisa kukutana na Kleist, ilikuwa pale kwenye Shule ya Aljamiatul-Islamiya fi Tanganyika, mtaa wa New Street (sasa Lumumba) kwenye miaka ya 50s, tulikopelekwa na wazee wetu kupata elimu ya dini ya Kiislamu. Hapa Kleist alikuwa akijulikana sana maana shule haikuwa mbali na kwao. Pia waasisi wa mwanzo wa taasisi ile pamoja na mchango mkubwa  wa jengo zima ilikuwa kutoka kwa familia ya Sykes, hasa babu Mzee Kleist Abdallah Sykes ambaye alijitolea hali na mali kuhakikisha Uislamu na Waislamu hawaachwi nyuma. Walimu mashuhuri pale kwa siku zile nakumbuka alikuwa Maalim Simba, Maalim Mataar, Maalim Adam Issa na Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo ndiye aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa taasisi ile. Palikuwepo pia na walimu wanawake kama vile mwalimu Sakina Arab na mwalimu Tahia. Namkumbuka huyu mwalimu Tahia kwa sababu alikuwa pia ni mke wa Mzee Juma Mwinyimkuu rafiki mkubwa wa marehemu babangu wakicheza mpira pamoja timu ya Morning Star iliyokuwa timu ya pili ya Sunderland wakati huo (sasa Simba). Mwalimu Sakina yeye alikuwa ni mwanamke mmoja maarufu sana katika harakati za wanawake hapa kwetu, kwani alifikia hadhi ya kuwa na kiti cha kudumu cha udiwani katika Manispaa ya Dar es Salaam siku hizo za ukoloni wa Kingereza. Habari za Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ni ndefu mno na mchango wa Mzee Sykes pamoja na watoto wake Abdul, Ally na Abbas katika jamii ya Kiislamu na ukombozi wa nchi hii kwa ujumla, zimeelezwa kwa kina na mwanahistoria maarufu nchini ndugu yangu Sheikh Mohammed Said, katika kitabu chake mashuhuri, “The Life and Times of Abdulwahid Sykes 1968 The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ kinachosambazwa na Ibn Hazm Media Centre ya Dar es Salaam. Ndani ya kitabu hicho, Mohammed ameuelezea mchango mkubwa wa familia ya Sykes katika kuanzisha chama cha TAA kabla ya TANU na namna walivyoweza kupambana na Waingereza kwa namna mbalimbali mpaka pale uhuru ukapatikana. Msomaji ikutoshe tu kusema hata pale TANU ilipoanzishwa, akina Sykes walikuwa na kadi namba za mwanzo mwanzo kabisa ambazo zilibuniwa na kugharimiwa na Mzee Ally Sykes (sasa marehemu).

Rafiki yangu, marehemu ‘Kaka Kleist, alizaliwa jijini Dar-es-Salaam miaka 68 iliyopita akiwa mtoto wa pili kwa baba Abdulwahid na mama Mwamvua Mrisho Mashu (maarufu mama Daisy). Watoto wengine ni dada Aisha-Daisy Buruku, ambaye alizaliwa mwanzo kabla ya Kleist, wakafuatia Adam na Omar ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki. Adam alikufa yapata nusu mwaka sasa. Anao pia nduguze wa mama mwengine, kwa sababu mzee Abdulwahid alioa mara tatu. Huku utamkuta Ebby (sasa marehemu), Elyassar (anayeishi Canada) na wanawake Misky na Mariamu (sasa marehemu). Hakukuwa na mtoto yoyote kutoka kwa yule mke wa tatu ambaye alikuwa naye baada ya kuwa ameshaachana na mama Daisy na mama Ebby.

Baada ya kupata elimu ya dini pale Aljamiatul, ‘kaka’ Kleist, kama ilivyokuwa kwa kina Sykes wote wakati huo, alijiunga na shule ya H.H. The Aga Khan (sasa Tambaza High School na Muhimbili primary) pale Upanga Dar es Salaam, shule ambazo zilikuwa mahsusi kwa watoto wa jamii ya Kihindi wakati huo wa elimu ya kibaguzi ya utawala wa Kiingereza. Kina Sykes, walipata hadhi hiyo nadra wakati huo, kutokana na heshima kubwa iliyokuwa imepewa familia yao kwa sababu ya mchango wa Babu Mzee Sykes katika jamii. Na kwa heshima hiyo hiyo Mzee Abdulwahid Sykes (babake ‘kaka’ Kleist) aliingizwa katika Bodi ya Aga Khan Schools, na kwa hivyo ikawa ni rahisi ‘ujiko’ kwa kina Sykes wote kupata elimu pale. Kaka Kleist, alisoma pale kuanzia chekechea mpaka Form IV alipomaliza mwaka 1967. Baadaye akachaguliwa kujiunga na Chuo cha Kilimo kule Ukiriguru, Mwanza. Kufuatia kifo cha ghafla cha marehemu babake, mnamo mwaka 1968, kijana Kleist Sykes, ilibidi akatize masomo yake Mwanza na kusafiri kwenda kwa babake mdogo Abbas Sykes aliyekuwa Balozi wa Tanzania kule Canada kwa ajili ya malezi na masomo mapya.

Nakumbuka kama vile jana, nikiwa bado kijana mdogo nilihudhuria mazishi ya mzee Abdul pale mtaa wa Lindi, Gerezani, jijini yaliyofurika watu wengi— wengi kwelikweli— akiwemo Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa taifa hili. Tofauti na marais Kikwete, Mwinyi na Mkapa, katika uongozi wake, Mwalimu hakuhudhuria mazishini mara kwa mara. Ukiacha mazishi haya, mazishi mengine aliyohudhuria Mwalimu ni ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, aliyekuwa waziri wake wa Sheria na Katiba wakati huo, aliyefia nchini Ujerumani mwanzoni mwa miaka ya 1960s na mwili kuletwa nyumbani kwa mazishi, akiwa kiongozi wa kwanza mwandamizi kufariki akiwa kazini. Alishiriki pia mazishi ya makamu wake wa rais Abeid Amani Karume kule Zanzibar na yale ya waziri wake mkuu Edward Moringe Sokoine, kule Monduli Juu, Arusha.

Katika mazishi ya Mzee Abdul Sykes, mwandishi huyu, alimshuhudia Nyerere akiwa kwenye majamvi pale mtaani Lindi na baadaye kulisindikiza nyuma jeneza mpaka Msikiti wa Ijumaa, Kitumbini. Katika hali isiyo ya kawaida, Nyerere alisubiri nje mwili uswaliwe swala ya jeneza na ulipotoka, aliusindikiza kwa miguu mpaka makaburini Kisutu pasi na kutaka asaidiwe usafiri. Kufuatia kifo kile, serikali ya Nyerere ilitangaza kujitwika mzigo wa kuwasomesha na kuwaangalia watoto wa marehemu rafiki yake yule, ambaye ndiye aliyempokea katika harakati za kugombania uhuru wetu akawa anakula na kulala kwake baada ya kuacha kazi ya ualimu Pugu ili ajiunge na harakati za kudai uhuru.

Katika maisha yake ya kule Canada, Kleist alihitimu shahada yake ya kwanza na ya  pili (uzamili) kwenye masuala ya Ustawi wa Jamii. Aliweza pia kupata ajira kwenye taasisi iliyojulikana kama Canadian University Students Organisation (CUSO). Kazi kubwa za shirika hilo ni kama lile la kule Marekani la American Peace Corps, lenye malengo na madhumuni ya kutoa misaada ya kimaendeleo kwa nchi changa duniani.  Sasa baada ya miaka kadhaa pale kazini, nafasi ikatokea ya kuja kuwa Mkurugenzi (Director of CUSO –Tanzania). Wakati huo Kleist alikuwa tayari ameoa kulekule Canada na kubahatika kupata mtoto wake wa kwanza Latifa. Kwa sababu ambazo hazikuelezwa, mamake Latifa alikataa katukatu kuongozana na mumewe kuja Tanzania, akihofia labda pengine wasingerudi tena Canada. Kwa mapenzi ya nchi yake na nduguze, Kleist aliondoka akaja yeye akiwa amembeba mtoto wake mdogo Latifa, wakati huo akiwa na umri takriban miaka mitatu hivi. Kwa kweli ilikuwa ni nderemo na hoi hoi kwenye ukoo wa Sykes kwa ujio wa Latifa. Bibi yake, marehemu mama Daisy, alishereheka sana kupata mjukuu yule kwa mtoto wake wa kiume. Latifa alikuwa juu juu—mara Upanga, mara Temeke, mara Mbezi Beach kwa babu Ally Sykes.


Kushoto: Mama Daiy mbele kulia Bi. Titi Mohamed
Mamake hayati Kleist Bi. Mwamvua Mrisho Mashu, alikuwa ni mwanaharakati mkuu wa masuala yanayohusu maendeleo ya wanawake hapa nchini. Katika uhai wake anatajwa kwamba alikuwa ni mmoja wa waasisi wakuu wa Chama Cha Wazazi nchi (TAPA), siku nyingi kabla uhuru wa nchi haujapatikana. Bi. Mwamvua anatajwa pia mmoja wa watu walioshirikiana kwa karibu na kina Bibi Titi kuanzisha UWT, ambako yeye alidumu kuwa mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi kirefu akishinda chaguzi mbalimbali. Mama Daisy pia alikuwa Mwenyekiti wa TANU/CCM tawi la Miburani pale Wailes, Temeke kwa miaka kadhaa. Mwandishi huyu mara nyingi alimshuhudia Kleist akiwa na mamake wakipanga na kupangua mipango ya siasa, hasa zile zilizomhusu Kleist, kwani Bi. Mwamvua alikuwa na hazina kubwa ya uongozi wa nchi hii kichwani mwake kutokana na kule kuwa mke wa Mzee Abdul Sykes. Bila shaka yeyote ile, nguvu kubwa na uwezo aliokuwanao Kleist ulitokana na maelekezo na mafunzo kutoka nyumbani kwa mama yake baada ya kuwa babake aliaga dunia mapema.   

Sasa, mnamo miaka ya 1970 mwishoni, ili kuziba ombwe la kukosekana mama wa kumlea mtoto Latifa, Kleist aliamua kumchumbia Stella Mallya aliyekuwa akiishi jirani na nyumbani kwake pale mbele ya Shule ya Tambaza. Mzee Mallya ambaye ndiye baba wa bibi harusi hakuwa ameridhia kabisa binti yake kuolewa nje ya Uchagani kwao Moshi.  Baada ya tafakuri ndefu, wawili wale, bwana na bibi harusi wakaamua kuwa ndoa lazima ifungwe ‘iwe jua iwe mvua’, itakiwe isitakiwe. Ndoa ikafungwa kwa siri kwa DC pale Ilala na hapakuwa na sherehe wala mialiko yeyote. Mimi nikawa ndiyo mpambe ‘best man’ wa Bwana harusi, wakati Bi Bernadetta Majebelle akawa mpambe wa Bibi harusi. Baada ya shughuli ile pale bomani, tuliondoka mahala pale tukaenda peke yetu maeneo fulani kule Sea View tukajipongeza kwa vinywaji na vyakula kidogo mpaka usiku ulipoingia tukaagana.

Siku kadhaa baadaye, na kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa binti yake, mzee Mallya alirudi matawi ya chini akawa tayari kumpokea tena binti yake. Aliwatembelea nyumbani pale Upanga akakaribishwa kwa vyakula na vinywaji, ambapo mwandishi huyu alimshuhudia Mzee Mallya akiwa mwenye furaha kwelikweli baada ya kuwa amepata ‘kinywaji moto’ na ‘kinywaji baridi’. Ndoa ile imedumu kwa miongo zaidi ya mitatu na ikaajaliwa kupata watoto watatu ambao ni watu wazima sasa; Aisha, Abdulwahid, Ally na Latifa akawa dada yao mkubwa.

Uzoefu, uaminifu na utumishi uliotukuka pale CUSO, ulimpatia sifa Kleist za kuchaguliwa kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo alifanya kazi kule Geneva, Switzerland na Zambia kama mwakilishi mkazi. Baada ya kuwa ametumikia UNHCR muda mrefu, ‘Kaka Kleist’ alirejea nyumbani na kujikita kwenye biashara mbalimbali ikiwemo kuanzisha kampuni yake ya kuhudumia meli iitwayo Prevention and Indemnity (P&I), ofisi zake mpaka leo zikiwapo pale mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.

Kwa kutumia uzoefu wake wa biashara, utawala na nidhamu ya kazi, na kwa ushawishi mkubwa kutoka kwa marafiki zake wa utotoni (akina Yusuf Zialor na Wendo Mwapachu), ambao nao ni mabingwa katika masuala ya biashara, wakaanzisha kampuni iliyojulikana kama Business Center International (BCI) iliyokuwa na ofisi zake pale kwenye jumba la Bushtracker kwenye makutano ya Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi.  Marafiki wengine waliokuwa pamoja utotoni kwenye kundi la Scorpions ndio waliokuwa maofisa mbalimbali pale Bushtracker. Alikuwapo dada Mariam Zialor, Abdul Mtemvu, Booby Bhokari, Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo na Ramadhani Madabida. Business Center International (BCI) ilikuwa na kampuni tanzu kadha wa kadha ikiwamo ofisi mashuhuri ya safari za ndege ya KEARSLEY LTD pale Barabara ya Samora jijini na kiwanda kikubwa cha uchapishaji cha PRINTFAST kule Nyerere Road.

Kwenye jamii, Kleist alikuwa mwanachama mwandamizi wa Klabu maarufu ya Saigon ya Dar es Salaam, kama ilivyokuwa kwa wanafamilia wengine wa ukoo wa Sykes. Michango ya kina Sykes kwenye klabu hii haisemeki—wako mstari wa mbele kila pale wanapohitajika.
Kila mmoja aliwashuhudia vijana kutoka klabu ya Saigon walivyokuwa mstari wa mbele siku ya maziko kuanzia uhudumu wa chakula kwa wageni pale nyumbani mpaka makaburini Kisutu, kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawasawa kwenye mazishi ya mpendwa wao. Alikuwa mwanachama pia wa klabu mashuhuri ya viongozi pale Leaders Club, iliyoko mbele ya Klabu ya Usiku ya Bilicanas, kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mwanachama mwandamizi kutoka Leaders Club, Zainul Dossa, ndiye aliyeratibu shughuli zote za mazishi ya Kleist kuanzia chakula nyumbani mpaka makaburini Kisutu akihakikisha kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa.

Katika upande wa siasa, marehemu Kaka Kleist alikuwa kada mzuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akifuata nyayo za familia yake katika harakati za siasa. Alipata kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake chini ya uongozi wa Jakaya Mrisho Kikwete. Akiwa diwani wa Kata ya Kivukoni, marehemu Kleist aligombania na kuchaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwenye miaka ya 1990, na moja ya mafanikio makubwa ambayo amekufa akijivunia ni kuweza kutatua tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kwa kubuni na kusimamia mradi mkubwa wa Usafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dar Rapid Transit). Aliweza kuwashawisha maofisa wa Benki ya Dunia, akiwamo rais wake, ambao awali walikuwa wamepanga kupeleka mradi ule kwenye moja ya nchi za kule Afrika Magharibi, kubadili mawazo na kuleta mradi ule mkubwa hapa kwetu, mradi ambao umeiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kuwa na mradi mkubwa ambao, si tu utakidhi haja, lakini pia imekuwa ni fursa nyingine kwenye ajira na hivyo kupeleka mbele maendeleo ya nchi kwa jumla. Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali ulimwengu wamekuwa wakimiminika kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kwenye hili. Akizungumza kabla jeneza la marehemu Kleist Sykes halijaondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kuzikwa, mwakilishi aliyetumwa na shirika la UDART, ambalo ndilo linatoa huduma za mabasi ya mwendo kasi jijini, alisema daima marehemu atakumbukwa kwa kubuni, kupanga na kukamilisha  hatua zote za utekelezaji wa miradi yote sita ya mpango mzima wa mabasi ya mwendo kasi.“...mpaka sasa tayari phase moja tu imekamilika yaani kutoka Kivukoni mpaka Kimara na kwamba mradi mzima una phase 6 ikiwamo Kariakoo – Mbagala; Morocco—Tegetta; na Kariakoo—Gongo la Mboto,...pale phase zote zitakapomalizika nchi itakuwa imepiga hatua kubwa …” amesema.

Mpaka umauti unamfika, marehemu Kleist, alikuwa amewekeza nguvu zake kwenye biashara ya kilimo cha mkonge kwani tayari alishanunua mashamba makubwa kule Kibaranga, wilayani Muheza, akiongozwa kitaalamu na mtaalamu bobezi wa Kilimo cha Mkonge nchini, Abdallah Mussa Kamili. Kwenye kazi hiyo, tayari alikuwa akishirikiana kwa karibu na wanawe katika uendeshaji na utawala wa shughuli hiyo. Sidhani kama kutatokea ugumu wowote, maana katika kipindi kirefu ambacho amekuwa akiugua ni watoto haohao ndio waliokuwa wakifanya shughuli hizo. InshaAllah kwa uwezo wa Mungu watajiunga pamoja na mama yao kumalizia pale ambapo baba amekomea. 


Sheikh Abdallah Awadh alipata kumbeba Kleist akiwa mtoto akisoma dua kwenye kaburi
Kushoto ni Kleist Abdul Sykes na kulia ni Abdallah Tambaza na katikati ni Mussa Abbas Sykes

INNA LILLAH WAINA ILLAYHI
RAJIUUN
simu: 0715808864

Tuesday, 27 June 2017

Chief Makwaia Mohamed Mwandu

Nimeona tangazo la Busiya Chiefdom katika mitandao ya kijamii na nikaangalia, ‘’clip,’’ yake. Hili ni tamasha linalofanyika hapo Busiya kulipokuwa na uchifu wa Makwaia. Mwalimu Nyerere alifuta uchifu katika baada ya uhuru wa Tanganyika lakini taratibu uchifu unarejea kwa kuona umuhimu wa kuenzi asili za watu na utamaduni wao. Uchifu huu hauna mamlaka ya utawala ila heshima na kumbukumbu.


Chief Michael Lukumbuzya

Historia ya Mwalimu Nyerere na machifu waliokuwapo Tanganyika toka enzi na enzi, kama baba yake Chief Edward Makwaia, Chief David Kidaha Makwaia, Chief Abdallah Said Fundikira, Chief Haruna Msabila Lugusha, Chief Thomas Marealle, Chief Makongoro, Chief Abdiel Shangali, Chief Kunambi, Chief Majebele, Chief Adam Sapi Mkwawa, Chief Ngua na mkewe Mwami Theresa Ntare, Chief Mang’enya, Chief Michael Lukumbuzya na wengineo ni historia yenye msisimko wa kipekee kabisa.


Chief Thomas Marealle

Nimebahatika katika maisha yangu kufahamiana na baadhi ya hawa machifu katika siku zao za mwisho wa maisha yao na pia kufahamiana na watoto wao kwa karibu na kutoka kwao nimejifunza mengi katika yale yaliyokuwa katika fikra za wazee wao na yale waliyokuwanayo wao wenyewe binafsi.


Kulia: Abraham Ally Sykes na Kibo Marealle nyumbani kwa Mwandishi Tanga1999



Kuwa hivi sasa uchifu wa Makwaia wa Busiya Usukumani umerejea hakika ni kitendo cha kupigiwa mfano.

Kumbukumbu nyingi za machifu waliokuwapo aidha zimekufa kabisa au hazipo na zile zilizokuwapo ziko taabani.

Chief Abdallah Said Fundikira

Labda nieleze kwa nini nimeguswa na uchifu Mkwaia wa Busiya.

Nimeguswa na uchifu wa Busiya kwa kuwa kiongozi wa uchifu huu ni rafiki yangu toka utotoni.
Nimejuana na Chief Edward Anthony Makwaia mwaka wa 1967 sasa imepita miaka 50, yaani nusu karne.

Nilimfahamu Edward pale nilipoingia St. Joseph’s Convent mwaka wa 1967 kujiunga na elimu ya sekondari na tulisoma darasa moja hadi mwaka wa 1970. Yeye alikuwa anatolea Salvatorian College na mimi Kinondoni Primary School.

Katika miaka hii minne ya shule tuliingiliana sana na Edward akawa rafiki yangu kipenzi na kupitia kwake nikajuana na jamaa zake wengi kama akina Mwapachu na akina, Yunge na Gordon. Lakini katika maajabu ya maisha ni kuwa hata kabla sisi hatujazaliwa wazee wetu kwa njia za ajabu kabisa walikuwa na uhusiano wa hapa na pale.

Mmoja katika ukoo wa kina Yunge aliingiliana sana na wazee wangu katika miaka ya 1950 na nina picha nilipiga na Kapufi Yunge sote tukiwa watoto ingawa Kapufi alikuwa kanitangulia labda kwa miaka miwili hivi. Picha hii ninayo katika maktaba na nikiitia mkononi nitaiweka hapa. Picha hii ilikuwa ukutani kwa mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed kwa kipindi chote cha maisha yake na kila alipokuwa akiizungumza ile picha alikuwa akimwita Kapufi, ‘’Chapa Ng’ombe,’’ kwa ajili ya ule Usukuma wake kwani Wasukuma ni wafugaji wakubwa wa ng’ombe.

Picha hii ilipigwa mwaka wa 1956 katika studio ya Gomes, iliyokuwa Acacia Avenue (Baada ya uhuru 1961 mtaa ukaitwa Independence Avenue na sasa ni Samora Avenue. Huyu Gomes ndiye aliyepiga ile picha maarufu ya waasisi wa TANU mwaka wa 1954). 


Waasisi wa TANU
Picha iliyopigwa na Gomes 7 Julai, 1954


Katika mwingiliano huu nikamkuta Edward ambae siku zile tulizoea kumwita Teddy akiwa na udugu na jamaa zangu wengi, mmoja wa ‘’cousin sister,’’ wake Lilian amabe tulizoea kumwita Lilly akiwa ni binti ya Abbas Sykes. Mimi, Teddy, Lily (ambae tulikuwa sote St. Josephs), Kleist Abdul Sykes, Ebby Abdul Sykes, Monalisa na Alma Ally Sykes ikawa sote tumekuwa pamoja utotoni tukiwa  na watoto wa koo mashuhuri katika Dar es Salaam ya wakati ule kama akina Lyabandi, Abbas Max, Sykes, Tsere, Singano, Bizuru, Msikinya, Lukindo, Mkwawa, Maharage, Masayanyika, Mang’enya, Muhuto, Fritsch, Kondo, Kafumba, Mzena, Bomani, Kahama, Kharusi na nyingineo nyingi. Kundi hili ambalo ndilo rika langu sasa sote sisi ni watu wazima na umri wetu wastani ni miaka 60.


Kulia: Balozi Mohamed Maharage Juma, Balozi Anthony Cheche, Balozi Patrick Tsere (mtoto wa Dr. Luciano Tsere)
Dr. Tsere ni mmoja wa madaktari watano ambao walisaidia sana kuijenga TAA baada ya Vita Kuu ya Pili, wengine ni Dr Vedasto Kyaruzi, Dr Wilbard Mwanjisi, Dr Michael Lugazia na Dr Joseph Mutahangarwa

Nyuma kulia ni Haitham ''Angela Davis'' Rashid, Mwandishi na Kamili Mussa.
Kushoto waliokaa ni Stella Emanuel. Esther Mzena na Wendo Mwapachu hii ilikuwa picnic tulifanya
Kigamboni kwenye nyumba ya mapumziko ya Rais Nyerere na aliyetupeleka hapo ni Magombe Makongoro, 1968
Katika familia hizi kuna historia kubwa ambazo kwa wakati ule wa utoto sikuzijua hadi nilipofika utu uzima. Historia ambazo zinakwenda na historia ya Tanganyika kuanzia kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar hadi kufikia mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. Historia ya mauaji kwa Zanzibar hadi vifungo vya siasa na kudhulumiwa kwa mali kote Tanganyika na Zanzibar.



Kulia: Ali Muhsin Barwani, Dr. Idarus Baalawy, Mohamed Shamte, Juma Aley na Ibun Saleh


Ilinichukua miaka mingi kuja kuijua historia ya ukoo wa Kharusi, Ibun na Shamte wa Zanzibar ingawa marafiki wawili wa baba yangu, Abdulaziz Twala na Jaha Ubwa walikuwa wameuawa baada ya mapinduzi. Ilinichukua miaka mingi pia kuja kuijua historia ya Chief Kidaha Makwaia. Nilipigwa na bumbuazi siku nilipoambiwa kuwa Abdul Sykes alimtaka Chief Kidaha Makwaia awe Waziri Mkuu Tanganyika itakapokuwa huru kwa Chief Kidaha kuwa rais wa TAA kisha waunde TANU yeye Chief Kidaha akiwa rais wa TANU. Hii iikuwa katika miaka ya 1950 wakati ule Chief Kidaha mjumbe wa LEGCO.


Kulia: Chief Edward Anthony Makwaia wa Busiya alipokwenda kumpa pole Kleist Sykes (kushoto) alipofiwa na mdogo wake Adam Abdulwahid Sykes. Kiasi cha nusu karne iliyopita baba zao watu hawa walikaa mara kadhaa wakijadili namna bora ya kuwaondoa Waingereza Tanganyika. Wakati ule Chief David Kidaha Makwaia alikuwa mjumbe wa LEGCO na Abdul Sykes alikuwa Katibu na Kaimu Rais wa TAA. Mengi ya mazungumzo haya yakifanyika nyumbani kwa baba yake Kleist.  Hakika dunia inazunguka.

Ilinichukua pia miaka mingi kuijua kwa undani historia ya ukoo wa Sykes lau kama hawa walikuwa jamaa wa karibu sana na wazee wangu kuanzia mababu zangu katika miaka ya 1920. Kwa hakika ilinichukua miaka mingi kuijua historia ya babu yangu mwenyewe katika kupigania uhuru wa Tanganyika na kupigania haki za wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi. Wakati ule sikuweza kutambua kuwa ule urafiki niliyokuwa nashuhudia baina ya Edward Makwaia na Kleist Sykes umetoka mbali kwa baba zao wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Sikuweza kwa wakati ule kujua kuwa ule ukaribu wa Wendo Mwapachu na Kleist ulitoka huko nyuma pia.


Kulia: Asya Kharusi na Sambayawo Nyirenda hawa wote ni madaktari wa binadamu.
Baba yake Sambayawo, Alexander Gwebe Nyirenda ndiye aliyepandisha bendera ya Tanganyika Mlima
Kilimanjaro usiku wa uhuru
Kwa miaka ile ya utoto sisi watoto kutoka familia hizi sote tulikuwa wamoja tukicheza pamoja wakati mwingine watoto wa washindi na washindwa au ukipenda watoto wa waliodhulumu haki za watu na wadhulumiwa tukiwa wamoja bila kujua yale yaliyopitikana siku za nyuma kati ya wazee wetu na watawala waliokuwa madarakani.Ilinichukua miaka mingi kujua kuwa eneo lote la Upanga hadi kufikia Selender Bridge hadi Ikulu ilikuwa hodhi ya ukoo waTambaza hadi kufikia miaka ya 1800 na wakanyang'anywa na Wajerumani na hadi leo kuna makaburi ya mababu zao ndani ya Ikulu. Katka miaka ya 1980 waliamua kutoa ardhi iliyokuwa makaburi ya wazee wao Upanga ujengwe msikiti uliopewa jina, ''Masjid Maamur.'' Huu uliongeza misikiti inayowahusu Dar es Salaam kuwa mitatu wa kwanza ukiwa Masjid Mwinyikheri Akida ambao (una zaidi ya miaka 100 na ndiyo msikiti wa kale kupita yote Kariakoo) na Masjid Tambaza.

Kama ulivyo wastani wa umri wetu miaka 60 na miaka ya utoto wetu ilikuwa katika 1960s na Waingereza waliipa jina miaka hii wakaiita, ‘’The Roaring 60s,’’ na kwa hakika hii ilikuwa miaka ya aina yake. Tulikulia katika mazingira na utamaduni wa aina yake. Waingereza walikuwa wameondoka na wamewaachia utawala wazee wetu. Wazee wetu waliathirika na sisi watoto wao pia. 


Waliokaa kulia: Yusuf Zialor, Wendo Mwapachu
Kulia waliosimama ni Abdallah Tanbaza Abdul Mtemvu na Abdallah Mggambo

Palikuwa na aina mpya ya maisha ambayo kwa kiasi fulani yalitia afueni kwa wazee wetu kwa kukamata nafasi za kazi ambazo zamani zilikuwa zikishikiliwa na Wazungu na Waasia.




Wazee wetu walikuwa wanapumua kutokana na kazi ngumu ya kupigania uhuru katika miaka ya 1950.


|Chief David Kidaha Makwaia

Hata hivyo katika hali hii palikuwapo pia na majeruhi ya harakati za ukombozi wa Tanganyika. Baadhi ya majeruhi hawa walikuwa machifu ambao jana tu walikuwa watu wenye hadhi zao katika jamii lakini ghafla baada ya uhuru kupatikana na Mwalimu Nyerere kufuta uchifu, machifu hawa wakajikuta katika hali ambayo hawakuitegemea kamwe.

Hii ni historia ya pekee inayohitaji ipatiwe nafasi iandikwe.

Juu ya haya yote mmoja kati yetu watoto tuliolelewa katika miaka ya 1960 wakati Tanganyika inapata uhuru wake kutoka kwa Waingereza, leo ni Chief wa Busiya, utawala uliokuwa na nguvu katika wakati wake.

Vipi Edward na watu wa Busiya wameweza kurejesha uchifu wa mababu zao, vipi waliweza kumtawaza  Chief Edward Anthony Makwaia na mengi mengine nadhani iko siku yataelezwa.

Kwa sasa muhimu ni kuwa kila mwaka wakati wa Saba Saba, Wasukuma wa Busiya huwa wanafanya tamasha kuhuisha utamaduni wao na uchifu uliozaliwa upya wa Busiya.


Chief Edward Anthony Makwaia katika vazi la kichifu

Chief Edward Anthony Makwaia akicheza ngoma ya Kisukuma
2016

Kushoto aliyepiga magoti ni Mama Mary Mackeja mama yake Edward Makwaia
siku ya sherehe ya kuzaliwa kwake kulia wa kwanza ni Mwandishi, William Mfuko, Juma Volter Mwapachu na nyuma ya Mama Mackeja ni Wendo Mwapachu
1967

Kulia waliochutama: Edward Anthony Makwaia, Salma Bhatia, Asya Kharusi, Razia Bhatia, Iddi Mvule, David Gabba,
Waliosimama kulia: Mwandishi, Shayo, Maximillian Mafuru
Kulia waliosimama: Gulamabbas Jivraj, Israel, Charles Mesquita


Picinic Form One D St. Joseph's Convent 1967 Kigamboni Beach
Kulia waliokaa: Iqbal Bapumia, Salma na Razia Bhatia wengine majina sikumbuki
Kulia waliosimama: David Gabba nyuma ya Daivid ni Edward Makwaia anefatia jina sikumbuki baada yake ni Sambayawo Nyirenda, Fortunata, Zariha Juma, Wun Siang Chou, Shenaz na wa mwisho ni mwalimu wetu wa darasa Miss Kindy.
Nyuma kabisa baada ya Edward Makwaia ni Khalid Abdallah

Kulia: Edward Makwaia, Willliam Mfuko, Mwandishi na Khalid Abdallah

Kulia: Mwandishi, Yusuf Zialor, Kleist Abdulwahid Sykes, Bubby, Abdallah Tambaza waliokaa kulia ni Abdul Mtemvu, Wendo Mtega Mwapachu na Kessy 

Kushoto Lilian Abbas Sykes akizungumza na Jaji Mark Bomani mwisho kulia ni Mohamed Chande Jaji Mkuu Mstaafu
Kulia waliokaa: Shayo, Iqbal Bapumia
Kulia waliosimama: David Gabba, John Gondwe, Sambayawo Nyirenda, Khalis Abdallah, Abdul Yusuf, Shaib Salum
Nyuma: Maxmillian Mafuru, Asya Kharusi Jennnifer Gordon, Mwandishi na Edward Makwaia

Mwandishi katika sherehe ya siku za kuzaliwa Iqbal Bapumia ''class mate,'' 1969
Picha kapiga Iqbal