Showing posts with label Taazia. Show all posts
Showing posts with label Taazia. Show all posts

Thursday 15 February 2018

ALHUDA, Februari 15, 2018
Taazia
Buriani Mwalimu Iddi Kikong’ona akiwa shule ya msingi alijitahidi kusoma vitabu vya Maududi
Na Mussa Ally Bwakila
Mwanaharakati wa Uislamu na Mwalimu wa somo la dini ya Kiislamu Iddi Suleiman Kikong’ona amefariki dunia.

Kiko(45) alifariki siku ya Ijumaa usiku na kuzikwa Jumamosi iliyopita jioni katika makaburi ya Kola Mjini Morogoro, baada ya kuswaliwa katika Msikiti wa Al-Fiqihiya chini ya Sheikh Ayub Salum Muwinge.

Mmoja wa walimu wake aliyehusika pakubwa katika kumjenga mwanaharakati huyo ambaye ni sehemu ya watendaji wa Al-Huda anamuelezea marehemu kuwa ni kijana aliyekua akiwa na mapenzi ya dini yake.

“Nilimfahamu Iddi akiwa darasa la tano shule ya msingi Kikundi mjini Morogoro wakati huo nikihudhuria kufundisha elimu ya dini ya Kiislamu, nikiwa chini ya taasisi ya Munadhamat al Daawa al Islamiya ambayo ilikuwa chini ya Ukurugenzi wa Sheikh Abdulkarimu baadaye AbdulRahman Khalil wakisaidiwa na marehemu ustaadh Mtengwa Burhan, tangu siku ya kwanza ya vipindi vyangu Iddy alipenda kusikiliza mafunzo ya dini ya Kiislamu akiwa katika umri mdogo sana”, anaeleza Mwalimu wake huyo.

Ustaadh huyo anataja program hiyo ya ufundishaji elimu ya dini ya Kiislamu iliendeshwa na Munadhamat katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Tabora.

“Wakati Munadhamat daawa al islamiya ikianza shughuli zake rasmi Tanzania mwaka 1988 Ofisi yetu ikiwa shule ya Alharamain baadaye tukahamia mtaa wa Agrrey upande wa Mishen Kota, Mimi nilikuwa mmoja wa waanzilishi wa shughuli hizo nikiwa mmoja wanaohudumu chini ya taasisi hiyo, wengine walikuwa ni pamoja na Mwalimu Said Nsigarila, Mwalimu Mohammed Kassim Rulengelule na Mwalimu Adam Salim Kaoneka”, ameeleza Mtendaji huyo wa gazeti hili la ALHUDA.

“Wengine ni Mwalimu Subira Nzole, baadaye waliongezeka Mwalimu Hashim Kassim, Mwalimu Zainab Mweche na Marehemu Mwalimu Iddy Juma” na Sekretary wetu akiwa mmoja wa waanzilishi wa TAMWA, Asmah Basafari, tukiongozwa na Ustaadh Mtengwa Burhan, timu yetu hii ndiyo iliyotafuta vile viwanja vilivyojengwa shule za sekondari za Ununio na Kunduchi”, ameongeza.

Akimzungumzia Marehemu Kikong’ona ameongeza kuwa kutokana na shauku aliyoonesha kutaka kuijua dini yake, alikuwa akifika mara kwa mara nyumbani kuangalia na kujaribu kusoma vitabu kadhaa vya Kiislamu katika maktaba yake, viliyokuwa katika lugha ya kiingereza akiwa hajaijua hiyo, wakati huo huo akihudhuria Madrasa iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu wake Ustaadh dady Ramadhani Kambi maeneo ya mtaa wa Mtoni mjini humo.

“Mimi na Bwana Mussa Nzige tuliiboresha Madrasa hii(Alfiqhiya) wakati huo ikiwa katika nyumba ya aliyekuwa mfanyabiashara wa kiarabu Mzee Swalah ambaye hivi anaishi Temeke jijini Dar es Salaam, tulinunua bati tukapaua, awali watoto walikuwa wakisoma huku jua likiwachoma, tukaweka utaratibu mzuri wa masomo, asubuhi na mchana walikuwa wakisoma Qur’an, jioni nilikuwa nikifika pale kuwafundisha tabia za Kiislamu(Akhlaq) na tawhiid(Kumjua Muumba vilivyo)”, Iddy aliweza kuhifadhi majina yote ya Muumba katika umri ule mdogo”, ameeleza.

Mwalimu huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini amesema aliendelea kuwa na Iddy akimpa kila aina ya usaidizi vikiwemo vitabu vya masomo yake ya msingi hadi alipomaliza shule ya msingi na kufaulu kuingia shule ya sekondari ya Morogoro ambako pia alikutana naye wakati wa somo hilo ambalo pia Mwalimu huyo alikuwa akifundisha katika shule hiyo na shule nyingine za sekondari mjini humo.

“Nilikutana tena na Iddy pale nilipowakusanya wanafunzi wa Kiislamu wa shule za sekondari kidato cha pili katika kituo cha Jabal Hira ambako niliandaa masomo ya ziada kwao pamoja na kuwafundisha elimu ya dini yao, Iddy akiwa kidato cha pili alikuwa mmoja wa wanafunzi hao”, ameeleza.

Aidha anasema Iddy alikuwa mtoto pekee aliyekuwa akihudhuria semina za Kiislamu za watu wazima maalumu ambazo ziliandaliwa na ama MSAUD, WARSHA, Munadhamat au IPC.

“Ni kutokana na shauku yake ya Uislamu aliamua kutokwenda shule ya Sekondari ya Pugu kusoma mchepuo wa sayansi PCB badala yake akajiunga na Ubungo Islamic High School kusoma EGM akiwa ni miongoni mwa wanafunzi walioanzisha A Level kwa shule hiyo ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Mohmmed Kassim kwa kushirikiana na Mwalimu Said Nsigarila na Sheikh Omar Msangi, iliyopo jijini Dar es Salaam,” ameeleza.

Akikariri maneno yake ya mwisho akiwa katika Zahanati ya Wakorea Magomeni siku ya jumamosi mwishoni mwa mwezi uliopita, Mwalimu huyo anasema Iddy alieleza mambo kadhaa yakiashiria kuiaga dunia muda si mrefu.

“Brother umenitoa mbali, nilikuwa nacheza Disco toto, ni wewe uliyenitoa huko, umenifunza dini yangu, Brother umenitoa mbali, nimekumbwa na Kadari kubwa”, Mwalimu huyo alimkariri marehemu Iddy akimsikia kutamka hayo akimuashiria yeye baada ya kufika kumjulia hali hospitalini hapo.

Kiongozi mwingine wa Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda amehimiza kumuomba Allah (S.W) Amrehemu, na kuwapa uwezo waliobakia nyuma kuendeleza pale alipoishia.

Prof. Hamza Njozi aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha waislamu Morogoro (MUM), na Mwenyekiti wa bodi ya Islamic Propagation Center (IPC), ambayo marehemu aliwahi kufanya kazi kama mwalimu wa moja ya shule za taasisi hiyo, na msanifu kurasa katika vitabu vya maarifa ya Kiislamu, amemsifu kuwa hakuchoka kutumikia Dini yake.

Dkt. Khalid aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi ya Daa’wa ya Munadhamat ambayo marehemu Iddi Kikong’ona alikuwa mfanyakazi wake hadi umauti unamkuta, naye amesifu utumishi wake wa kupigiwa mfano.

Ust. Sadiki Gogo na Ust. Ramadhan Sanze wanamuelezea Marehemu Iddi Kikong’ona kuwa katika uhai wake amewahi kushiriki harakati nyingi za maendeleo ya jamii yake ikiwa ni pamoja na programu ya kutoa elimu ya ziada katika ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Kiislamu, harakati za kuendeleza taasisi za Kiislamu, na harakati za kuandika na kusanifu tovuti, magazeti, na vitabu vya Kiislamu, na nyinginezo kadhaa.

Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema, ulingo wa harakati za kupigania haki na maendeleo ya Uislamu na waislamu utakuwa umemtendea haki marehemu Idi Kikong’ona si tu kwa kundeleza mema aliyoyaacha, bali pia kutazama namna ya kukiendeleza kizazi chake (watoto wake) kitaaluma, ili wasihisi pengo la kihuduma baada ya kuondokewa na mzazi wao.

Mwalimu Iddi Suleiman Kikong’ona atakumbukwa na wengi aliofanya nao kazi kama mwanaharakati aliyejitenga na majukwaa ya hadhara, bali alikuwa mpiganaji wa chini kwa chini aliyefanya Daa’wa kikamilifu hadi Muumba wake alipomchukua.

Tunamuomba Allah (S.W) Amrehemu. Sote ni wa Mwenyezi Mungu (S.W) na sote kwake tutarejea.


BURIANI KIKO
NA MAMA NASR SADIKI GOGO

Nilimfahamu marhum Bro. Idd S.Kikong'ona tokea 1996 kupitia gazeti la An-nnur akiandika mashairi na makala zake zilizokwenda kwa jina la "Kipondo wa Changarawe.’’ Nami pia nikiandika baadhi ya makala kwenye An-Nuur.

Nilikuja kukutana nae mnamo mwaka 2000, tulikutanishwa na Bro Sadiki Gogo  ambaye nilifahamiana nae mapema 1998 nikiwa Kidato cha Pili pale Kisutu Girls Secondary School, akinitambulisha kuwa ni ndugu na rafiki yake. Huku Bro Kiko siku zote akiona fakhari kumtambulisha Bro.Gogo kama mwanafunzi wake.

Kupitia kwao nikaweza kujiimarisha kitaaluma na kida'wah kwa kujiunga na elimu ya Kiislam kwa posta, vitabu na machapisho mbalimbali hasa ya akina Harun Yayha, Maududi, Sayyid Qutb, Ahmed Deedat n.k

Bro. Kiko ametuachia mengi ya kujifunza kutoka katika umri wake mchache hapa duniani, siku zote akijitahidi kuakisi mafunzo ya Qur'an na Sunnah katika maisha ya kila siku.

👉Bro Kiko alidhihirisha imani yake ya hali ya juu katika maisha yake, na alipigania anachoamini kwa hoja za kumshawishi kila mmoja. Katika mazungumzo yetu mara nyingi ukizuka mjadala namna ya kutekeleza jambo akituambia kuwa "Dini sio ngumu kiasi hicho" kwa fikra hii aliandika kitabu "Dini Imerahisishwa".

👉Bro Kiko aliamini katika elimu, nyakati zote ukimkuta ana kitabu au chapisho mkononi. Alikuwa chachu kielimu kwa vijana wengi nje na ndani ya familia yake. Nyumbani kwake hapakukauka vijana akiwasomesha na kuwalea kimaadili na kifikra.

👉Bro Kiko alikuwa mkarimu na bashasha kwa kila mtu. Alimsaidia aliyemjua na asiyemjua huku akitukumbusha mara nyingi kuwa "vyote mlivyonavyo vitakwisha itabaki jaza ya mola wako tu (An-Nahl: 96) na kuwa iko siku mtu atataka arudi duniani sio kuswali bali kutoa sadaqa tu kwa ule ukubwa wa malipo atakayoona baada ya mauti. Alijenga urafiki na watoto popote alipokwenda akiwapa zawadi, kuwapiga picha, vichekesho, akiwaelekeza namna nzuri ya kusoma Qur'an na kufanya hesabu, akiwaburudisha kwa katuni kutoka kwenye computer yake. Daima akisisitiza kuwa watoto amana Allah katupa tuwalee vyema.

👉Bro Kiko aliipenda kazi yake, alichapa kazi usiku na mchana akikariri usemi wake "Tutapumzika kaburini"! Hata gari yake aliigeuza ofisi akipenda kuendeshwa huku akiweka meza ndogo akiendelea na kazi zake akiwa safarini. Siku za mwisho za uhai wake pamoja na ugonjwa kumzidi kiasi cha kutoweza kukaa tena alikuwa akiomba  tulete computer yake kitandani pembeni yake japo aiguse tu.

👉Bro Kiko alikuwa mvumilivu na subra ya hali ya juu mno. Hakupenda migogoro na alikuwa tayari kwa gharama yoyote kusuluhisha penye mgogoro nje na ndani ya familia. Siku zote akituusia subra na uvumilivu katika kuamiliana na watu.

👉Ni ngumu kueleza yote kutoka  maisha ya Bro Kiko, itoshe tu kuwa ibra kwetu sote.
Buriani Kiko. Tulikupenda sana nawe ulitupenda sana. Pale uliposisitiza tusikuache na tuwaangalie watoto kumbe ulikuwa ukituaga!

Buriani IDD SULEIMAN KIKONG'ONA.....kaka, rafiki, mwalimu, mshairi, mwanafikra, mwanadaa'wah na msanifu mahiri.

TUNAMUOMBA ALLAH (S.W) amghufirie mapungufu yake, alitie nuru kaburi lake na kumruzuku Jannatul Firdaus.
Amiin
Mwapwani d/o Mohammed
(Mama Nasr Sadiki Gogo)

Sunday 11 February 2018


IDDI SULEYMAN KIKONG'ONA (A.K.A BRO. KIKO)



Assalaam alaykum warahmatullaah wabarakaatuh,

Nami nitabaaruk tanzia ya Bro. Kikong'ona....  Innaa lillaahi wa innaa ilayhi raajiuun! Mioyo inahuzunika na macho yanatoa machozi, hatusemi ila lile ambalo Mwenyezi Mungu analiridhia...

Bro. Iddi Kikong'ona ametangulia mbele ya haki... Brother kwa kweli alikuwa na ataendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa anayetaka miongoni mwa vijana wa Kiislamu, nimemjua Brother Kiko pale Ubungo Islamic, tukiwa wanafunzi wa Ualimu wa sekondari yeye akiwa mtaalamu wa graphic designing na typesetting ya Vitabu vya Islamic Knowledge ambavyo leo tunavitumia...

Brother alikuwa ni Mwanafikra, mpevu na makini sana... kila tukikutana lazima akuache na jambo la kuishughulisha akili yako juu ya Dini yako na nafasi yako km kijana...

Alhamdulillaah, nilimpenda sana na alikuwa akinipenda sana, nakumbuka ndiye mtu wa mwanzo kunipa seti ya DVD za "2 weeks Da'awah Program" za Sheikh Khalid Yasin na kwazo Vijana wengi wa Ubungo Islamic wa wakati huo walikuwa wakiitana "Akhy..." na "Daa'e..." ikiwa ni reflection ya mafunzo yatokanayo na DVD hizo.

Brother Kiko, alikuwa ni mchapakazi, kabisa alimuigiza Sayyiq Qutb, Abul Alaa Maududi, Prof. Maalik kupitia maandishi yao (ambapo muda mwingi utamkuta na kitabu mkononi) na Mwalimu na Mzazi wetu Kida'awah Sheikh Mohamed Qasim.

Al akhy Iddi Kikong'ona alikuwa akipenda mambo yaende bila kuleta nyudhuru... wakati akiendelea na typesetting anaprint baadhi ya kurasa na kuja darasani kutugawia... "Masheikh... au "wanazuoni" km alivyopenda kutuita... "hebu pitieni hizi kurasa kuzihakiki" na vitabu vya shule ya msingi utakuta jina "Mujtaba" kwa kweli ni jina la mwanae... sisi tukisaidiana nae kutunga maswali ya mazoezi na kuyahakiki ubora wake...

Hata baada ya Kuondoka Ubungo Islamic na kwenda Munadhwamat bado Iddi Kikong'ona alikuwa ni kiongozi wetu ktk harakati za kushape bongo za vijana wa Kiislamu.

Kifo cha Bro. Kiko, kiwe chachu ya kuongeza juhudi katika medani ya Da'awah hasa kwa sie vijana wa Kiislamu.

Twamuomba Allaah aikubali juhudi yake, amlipe pepo ya Firdaws na ampe kauli thaabit. Twamuomba Allaah nasi atujaalie mwisho mwema, Aamiyn.

Al Akhy Iddi Kikong'ona, pumzika kwa Amani, umeifanyia kazi kauli ya sheikh Mohammed Qasim, kwamba hapa Duniani hakuna kupumzika, tutapumzika Barzakh... Allaahu Kareem, pumzika Kaka... innaa lillaahi wa innaa ilayhi raajiuun.

Mwl. Abu Sumayyah Salah

Saturday 10 February 2018

Idd Suleyman Kikong'ona

Amani iwe juu yenu.

Hakika wiki hii imekuwa ya majonzi na maumivu makali ndani ya moyo wangu, ni wiki ambayo itakuwa ngumu kufutika ndani ya kumbukumbu za maisha yangu. Nafsi imekumbwa na mitikisiko mikubwa mitatu ndani ya wiki moja. Hii ni misiba iliyogonga moyo wangu. Maarifa yangu ujuzi wangu wa kusarifu kurasa nami leo mmenifahamu kama Graphic Designer mnayeniita mahiri na kunivika tuzo mbalimbali. Maarifa na Ujuzi ambao umejengwa na kusimamishwa na nguzo kuu mbili.

Leo nguzo yangu kuu moja imedondonka. Ni Idd Suleyman Kikong'ona ametangulia barzak. Sasa yupo mbele ya haki. Punde tunamzika hapa Morogoro baada ya mshuko wa Swala ya Alasiri.

Huyu ni miongoni mwa magwiji wachache wa fani ya Graphics mwenye upekee wa hali ya juu kuwahi kutokea ktk kitanga hiki cha taifa hili la Tanzania. Hakika tumeondokewa na mtu muhimu kabisa.

Ingawa najihisi kama nipo kwenye shimo lenye giza nene huku moyo wangu unalia, mwili wanitetema na nafsi haitaki kuamini, lakini ndiyo mipango ya Mola mlezi.
Nimelikubali nimelipokea,

Nakuomba ewe Mola umlaze mahala pema peponi, Ndugu yangu, kaka yangu, rafiki yangu, Mwalimu wangu IDD SULEYMAN KIKONG'ONA.

Aamin.
Innaalillah'i Wainnaa Ilayh'i Raajiu'n.

Ismael Abdoulkarym.
10/ Februari /2018

Monday 5 February 2018


TAAZIA
KOMREDI KINGUNGE NGOMBALE MWIRU
(1932 – 2018)


Sasa ni miaka mingi imepita lakini nakumbuka kama vile ilikuwa jana. Nimemfahamu Balozi Juma Mwapachu mwaka wa 1967 nyumbani kwa ‘’class mate,’’ wangu Edward Makwaia, mtoto wa Chief Kidaha Makwaia wa Siha. Siku hiyo Edward tukizoea kumwita Ted alitualika marafiki zake nyumbani kwao Upanga yalipokuwa Makao Makuu ya Red Cross kwenye tafrija ya kuzaliwa kwake. Siku hiyo ndipo nilipojuana na Juma Mwapachu na nikawa nimepata kaka na akanisaidia mengi sana katika ulimwengu wa kusoma na kutafuta elimu. Mwaka ule Kaka Juma kama wengi wadogo zake tulivyozoea kumwita alikuwa yuko nyumbani baada ya kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwa wanafunzi kugoma kwenda National Service. Kuanzia siku ile hadi sasa karibu nusu karne kila ninapokutana na Kaka Juma mazungumzo yetu yatajikita katika masuala ya kusoma na siasa hasa historia ya siasa katika Tanganyika chini ya ukoloni wa Waingereza.

Siku moja Juma Mwapachu akaniambia kuwa baba yake katika maktaba yake Tanga alikuwa na nakala ya kitabu cha Karl Max, ‘’Das Kapital,’’ toleo la mwaka wa 1924 na maktaba hii imehifadhiwa na mama yao kama alivyoiacha mwenyewe marehemu Hamza Mwapachu. Kitabu hiki kwa mara ya kwanza kimechapwa mwaka wa 1867. Nikamuuliza, ‘’Kwani Mzee alikuwa Mkomunisti?’’ ‘’Baba alikuwa, ‘’Leftist,’’ jibu lilikuja. Lazima nikiri kuwa Juma Mwapachu katika miaka ile ya utoto wangu alikuwa ananitia darasani. Mwanafunzi wa sekondari unamweleza kuhusu Karl Marx na ‘’Das Kapital,’’ kisha unamweleza ‘’concept,’’ za ‘’left’’ na ‘’right...’’ Haya yalikuwa nje ya dunia niliyokuwa naifahamu. Mwaka wa 1967 ndiyo ulikuwa mwaka wa Azimio la Arusha na moja katika masomo tuliyokuwa tunafundishwa ilikuwa somo la siasa na kwa hakika walimu walijitahidi kutueleza ubaya wa ‘’Mabepari,’’ na ‘’Wanyonyaji.’’ Hapa ndipo nilipotaka tupafikie ili tumpate Komaredi Ngombale Mwiru. Sikupata kujua kuwa Azimio la Arusha liliandikwa na Ngombale Mwiru hadi baada ya kusoma taazia ya Mh. Zito Kabwe. Miaka yote toka niko shule nikijua ile ni kalamu ya Mwalimu Nyerere. Ngombale Mwiru si tu aliandika Azimio la Arusha bali aliandika na Mwongozo wa TANU wa 1971 na Muongozo wa CCM wa 1981. Nyaraka hizi tunaambiwa ndizo zilikuwa dira ya kuongoza Tanzania wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kila kitu kina chanzo chake. Tuangalie ni wakati gani siasa za mrengo wa wa kushoto zilibisha hodi kwanza katika African Association miaka ya 1930 na kisha katika chama cha TANU kilipoasisiwa 1954. Kabla ya Vita Kuu ya Pili na baadae ukipitia gazeti la Zuhra chini ya mhariri wake Mashado Plantan utakuta makala nyingi za kuisifia Urusi ambayo ndiyo dola iliyokuwa hasimu mkubwa wa Waingereza na Wamarekani na washirika wao. Katika miaka ya 1950 Gamal Abdul Nasser alipoanzisha Radio Free Africa, Cairo ili isaidie ukombozi wa makoloni ya Afrika, radio hii ilipata wasikilizaji wengi Tanganyika khasa kwa kuwa mtangazaji katika idhaa ile alikuwa Ahmed Rashad Ali kijana maarufu kutoka Zanzibar na mchezaji mpira wa sifa, kiasi ikawa watu wakisema tumsikilize Ahmed Rashad badala ya kusema tusikilize Sauti ya Cairo. Sauti ya Cairo ilipiga propagamda kubwa dhidi ya wakoloni ambao Rashad aliwapa jina la ‘’Majibwa Meupe,’’ yaani, ‘’Mbwa Weupe.’’

Katika siku za mwanzo za vita baridi kufuatia kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili kulikuwapo katika Tanganyika mwamko mpya wa kuipenda Urusi kama taifa linalotetea wanyonge. Mashado Plantan ndiye aliyekuwa akiongoza kampeni ya kuwafahamisha Watanganyika siasa na misimamo ya Urusi kuhusu makoloni kupitia gazeti lake ‘’Zuhra.’’ Mashado katika tahariri na makala zake aliitukuza Urusi bila kifani. Mashado alikuwa msikilizaji maarufu wa matangazo ya Ahmed Rashad kutoka Cairo akiushambulia, ‘’Ubeberu na Vibaraka wake.’’ Ilikuwa kutoka kituo hiki cha redio ndipo Mashado alipata baadhi ya tahariri na makala zake. Lakini ukweli ni kuwa Tanganyika kabla ya Vita Kuu ya Pili (1938 – 1945) tayari ilishakuwa na viongozi waliokuwa na siasa za mrengo wa kushoto kama Erika Fiah mhariri wa gazeti la ‘’Kwetu.’’ Fiah hakuishia katika kuandika fikra hizi katika gazeti lake bali alijaribu hata kuwakusanya wakulima na wafanyakazi dhidi ya serikali ya Waingereza bila ya mafanikio.

James Suss au Abdullah Chuma akiwa na jeneza la David Livingstone

Katika uongozi wa TAA kulikuwa na Steven Mhando ambaye Waingereza wakimchukulia kuwa ni Mkomunisti. Steven Mhando yeye alikuwa kalitua jicho lake akiwa kama mwalimu Government School Kitchwele, kwa wanafuzni wake akijaribu kuwafunza kuhusu ubaya wa wakoloni. Steven Mhando akiwaita Waingereza, ‘’wezi wa fadhila,’’ akitoa mfano wa Susi na Chuma, Waafrika wawili waliobeba mwili wa David Livingstone kutoka Northern Rhodesia kijiji cha Ilala alikokufa 1873 hadi kwao Uingereza. Mhando akiwaambia wanafunzi wake kuwa juu ya wao kufanyiwa hisani hii kubwa na Susi na Chuma wanapowataja katika vitabu vyao vya historia watu hawa wanatajwa kama, ‘’watumishi,’’ wa Livingstone badala ya kuwapa heshima kuwa wale walikuwa rafiki zake. Mwalimu Steven Mhando akawa anaendelea kwa kuwauliza wanafunzi wake ni mfanyakazi gani atabeba maiti kichwani akitembea kwa miguu kwenye mvua na jua kutoka kijiji Northern Rhodesia kuileta hadi Bagamoyo?

Maneno haya yaliwafikia wenyewe Waingereza na hayakuwafurahisha. Mwandishi wa taazia hii ameona picha kubwa ya James Susi na Abdullah Chuma katika Makumbusho ya David Livingstone, Blantyre Glasgow Scotland, wakiwa na jeneza la Livingstone kwenye meli wakati wa safari kupeleka maiti ya Livingstone Uingereza. Ukiangalia nyuma utaona kuwa hisia za siasa za siasa za mrengo wa kushoto zilianza kujipenyeza kuanzia miaka ya 1930 zikianza na akina Erika Fiah kufikia miaka ya mwanzoni 1930 na mwaka wa 1950 zilipokelewa na akina Mwalimu Steven Mhando. Lakini hizi zilikuwa ni hisia tu katika nyoyo za baadhi ya wazalendo wa nyakati zile. Kwa upande wao Waingereza walikuwa na hofu kubwa kwa kuenea kwa fikra hizi za Kikomunisti na serikali ikishirikiana na wamishionari waliokuwa ndiyo wamehodhi elimu kwa ajili ya kuwa na shule nyingi Tanganyika, walijitahidi sana kuwakinga wanafunzi ambao kwao ndiyo kilikuwa kizazi cha kesho na fikra hizi za Marx wakijitahidi na wao kueneza propaganda kueleza ‘’uovu,’’ wa Ukomunisti hasa katika kupinga kuwepo kwa Mungu.

Waafrika waliokuwa na msimamo mkali kama huo hawakuvumiliwa hata kidogo. Father Van Ostroom akiandika katika Kiongozi Gazeti Katoliki, mwaka wa 1950, alipatapo kutoa onyo kwa kusema, ‘’Upumbavu wa mwanadamu unathibitisha kuwa hauna kikomo. Urusi na utawala wake wa kikomunisti bila tone lolote la shaka ni adui wa mwanadamu asiyeweza kusuluhishwa naye.’’ Huu ndio ulikuwa msimamo wa Kanisa na serikali kuhusu Ukomunisti. Katika hali kama hii vipi Ngombale Mwiru aliyekuwa mfuasi wa Kanisa Katoliki angeweza kusalimika katika mfumo huu kwani yeye alianza kuonyesha fikra za kupinga dini na kuwepo kwa Mungu mapema sana akiwa mwanafunzi wa darasa la sita.

Tuangalie hali ilikuwa katika TAA. Taarifa ya TAA kwa wanachama wake mwaka wa 1951, katibu ta TAA Abdulwahid Sykes anawaonya wanachama juu ya hatari za Ukomunisti. Abdu Sykes akitahadharisha kuhusu madhara ya Ukomunisti katika siasa za Tanganyika. Wakati huo baadhi ya viongozi wa TAA walikuwa tayari wakifahamika kwa misimamo mikali. Miongoni mwao alikuwa Steven Mhando na Hamza Mwapachu na baadae Zuberi Mtemvu akaingia katika orodha ile. Wakati huo Mwapachu alikuwa akiandika katika ‘’The Sentinel,’’ jarida la Fabian Society lililokuwa likichapishwa London. Siku Juma Mwapachu alipokuwa akanieleza uhusiano wa baba yake na Fabian Society, aliponambia kuwa Fabians wao walikuwa, ‘’Left of the left, ‘’ katika siasa za Uingereza. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kuwasikia hawa Fabians. Sasa TANU ilipokuja kuundwa na viongozi kama hawa, vipi kijana mdogo mwenye fikra kali kama Ngombale Mwiru aliweza vipi kuenea vizuri na uongozi huu? Halikadhalika vipi Komredi Ngombale aliweza kuelewanana Mwalimu Nyerere, mtu aliyekuwa na mapenzi makubwa na Ukristo na kanisa lake katika Tanganyika huru?

Ngombale Mwiru anaeleza kuwa alikuwa Ally Sykes ndiye aliyemuingiza TANU mwaka wa 1954 walipokuwa pamoja katika uongozi wa Tanganyika African Government Servant Association (TAGSA), Ally Sykes akiwa katibu. Ally Sykes ndiye aliyempa Ngombale Mwiru kadi za TANU atafute wanachama. Bila shaka Ngombale Mwiru katika uongozi wa TAGSA alikuwa kajikuta katikati ya ‘’petty bourgeoisie,’’ akina Sykes; ’’aristocrats,’’ na ‘’landed aristocracy; ’’Chief Thomas Marealle, ‘’the intelligentsia’’ Hamza Mwapachu, Dr. Wilbard Mwanjsi na Dr. Michael Lugazia hawa baadhi yao wakiwa pia mstari wa mbele katika TANU.  Lakini ndani ya TANU kulikuwa na Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadiri lililokuwa na wajumbe Waislam watupu wenye ushawishi mkubwa katika siasa za nyakati zile. Vipi Komrade Ngombale aliweza akaogolea na mchanganyiko huu? Hanishangazi kuwa wakati kwangu mimi nimekuta mengi katika utafiti ushahidi wa uhusiano mzuri kati ya viongozi wa TANU na Fabian Society, lakini sijapatapo kuona popote kama Komrade Ngombale Mwiru aliwahi kuwa na uhusiano na chama hiki.

Ingawa Ngombale Mwiru alikuwa mdogo kwa umri lakini kwa ule msimamo wake wa kuchukua msimamo toka mwanzo yeye tayari alikuwa keshavuka ‘’Rubicon,’’ siku nyingi tena kwa mbali sana na hakubadilika hadi kufa kwake. Ndani ya TANU Ally Sykes alikuwa na mawasilaino na Menahem Bargil, Katibu Mkuu wa International Union of Socialist Youth iliyokuwa Vienna akijaribu kutafuta nafasi za masomo kwa vijana wanaharakati halikadhalika akiwasiliana na Asia Socialist Conference Anti-Colonial Bureau ambayo ikifahamika kwa siasa za mrengo wa kushoto. Hata hivyo ushawishi wa siasa hizi za mrengo wa kushoto hazikuwa na athari kubwa katika siasa za Tanganyika. Hadi sasa wanahistoria hawajaweza kueleza ni kwa kiasi gani uhusiano huu ulikuja kuweka misingi ya siasa ya Ujamaa pale Mwalimu Nyerere alipoamua kubadilisha mwelekeo wa Tanzania kupitia Azimio la Arusha ambalo alama za vidole za Ngombale Mwiru katika waraka ule zinaonekana kote. Ningependa kuhitimisha taazia hii kwa mambo machache ya hisani, yaani wema ninayoyafahamu ambayo Komarade Kingunge Ngombale Mwiru amewafanyia Waislam ingawa wengine hawajui wa kuwa mkono wake haukuonekana.   

Katika matatizo makubwa yalioukumba utawala wa Rais Benjamin Mkapa ni kushambuliwa kwa Msikti wa Mwembechai na vyombo vya usalama mwaka wa 1998 na yaliofuatia baada ya shambulizi lile. Kilichofuata ni  kukamatwa kwa masheikh na kuwekwa rumande na kufungwa kwa Msikiti wa Mwembechai. Yaliyotokea Mwembechai yalikuwa hayajapatapo kutokea toka uhuru mwaka wa 1961. Haikupatapo hata siku moja Waislam kuingia barabarani kupambana na askari chini ya nembo ya Uislam. Rais Mwinyi na yeye utawala wake ulikumbwa na kuvunjwa kwa mabucha ya nguruwe. Jambo hili Rais Mwinyi alipata kwa faragha kueleza kuwa lilimhuzunisha kupita kiasi. Lakini baya zaidi kadhia hizi zote zilivyokuwa zinashughulikiwa ilijengeka dhana kuwa taasisi ya urais yenyewe ilikuwa haina usemi wala haiwezi kufanya lolote kuzuia vurugu zile na watendaji wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo walikuwa wanafanya maamuzi dhidi ya Waislam wapendavyo. Nguvu kubwa pasi na sababu ilikuwa inatumika dhidi ya Waislam kwa ujumla na hii ilizusha taharuki kubwa sana.


Chuki Athumani

Kulikuwa na kisa cha mtoto mdogo wa shule ya msingi Chuki Athumani mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Al Haramain yeye siku ya mapambano ya askari na Waislam pale Mwembechai alikuwa anatoka shule na akapigwa risasi na askari. Chuki kama ilivyokuwa kwa wote waliojeruhiwa katika ghasia zile walipelekwa hospitali ya Muhimbili na wakafungwa pingu katika vitanda vyao na hawakupatiwa matibabu. Picha ya mtoto Chuki katika kurasa za mbele za gazeti la An Nuur akiwa amelazwa na pingu hospitali akiwa kapooza mwili mzima lilikata maini ya akina mama wengi. Taarifa na tahariri za gazeti la An Nuur zilifikirisha wengi. Suali kubwa likiwa, nchi yetu imefikaje hapa na nani kaifikisha hapo?   Ngombale Mwiru alipata taarifa hizi kuwa majeruhi wa Mwembechai wako hospitali lakini hawapati huduma stahiki na wako chini ya ulinzi wa askari wa magereza na wamefungwa pingu vitandani hali ni wagonjwa. Komredi Ngombale Mwiru alikwenda hospitali na alimtembelea mtoto Chuki Athumani na kumkuta kweli kapooza na ana pingu mikononi. Siku ya pili mtoto Chuki alifunguliwa pingu pamoja na wenzake wote.

Tukio lingine ni jinsi Komredi Ngombale Mwiru alivyozuia serikali isilifungie gazeti la An Nuur kutokana na makala iliyoandika iliyokuwa imemshambulia kiongozi wa juu wa serikali. Mhariri wa An Nuur alipewa taarifa afike Maelezo kupokea barua ya kufungiwa gazeti kwa miezi mitatu. Mhariri na mpashaji wangu habari walikwenda hadi Dodoma kumfuata Ngombale Mwiru wakati huo Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa. Ilikuwa Jumapili lakini yeye alikuwa kazini. Ngombale Mwiru akamfanyia dhihaka mpashaji wangu aliyefuatana na Mhariri wa An Nuur akamwambia, ‘’Leo Jumapili lakini mimi sifungwi na dini hivyo niko kazini.’’ Mpashaji wangu kwa namna yake ni ‘’free thinker,’’ kama Ngombale Mwiru na hawakuwa wakijuana kwa muda mrefu lakini siku walipopata kujuana huko nyuma na kuzungumza, mapenzi yalijengeka baina yao kila mmoja akiusudu kichwa cha mwenzke. Kuanzia siku ile wakawa wanaitana, ‘’Komredi.’’ Ngombale Mwiru alimsikiliza komredi mwenzake wa kuchovya. Mapashaji wangu tayari alikuwa keshamsoma Ngombale Mwiru katika mazungumzo yao siku za nyuma wakiwa Dar es Salaam na alijua amweleze nini wapate kuelewana. ‘’Komradi Waislam walipokuwa hawana gazeti walikuwa wanamwaga makaratisi misikitini kueleza hisia zao na kama ujuavyo makaratasi ya ‘’protest,’’ tena kutoka jamii kubwa kama hii yetu athari yake ni kubwa. Serikali ikilifungia gazeti letu patakuwa na ombwe na vijana watarudi msituni na kuanza kumwaga makaratasi kuisema serikali na hili halitakuwa na maslahi si kwenu serikali wala kwetu sisi Waislam.’’ Mpashaji wangu akanambia. Ngombale Mwiru akamjibu kwa kumwambia kuwa yeye siku nyingi alishatoka Habari hana sauti tena kule. Hawa makomredi wawili wakaagana na safari ya kurudi Dar es Salaam ikaanza. Jumatatu asubuhi na mapema Mhariri wa An Nuur akafika Maelezo kumuona mkurugenzi ili apokee barua yake ya kufungia gazeti. Mkurugenzi wa Maelezo akamwambia hakuna kitu kama hicho aondoke kwa amani akaendelee na shughuli zake za kujenga taifa. Haikuwa tabu kwa Mhariri wa gazeti lile kujua kuwa Komredi Ngombale Mwiru kwa busara zake alikuwa kanyanyua mkono wake kusaidia gazeti la Waislam lisifungwe. Komrade Ngombale alikuwa msomaji wa An Nuur na akiwekewa nakala mbili kila Ijumaa katika duka moja la Muhindi.

Ngombale Mwiru na Kitwana Kondo

Mwisho na hili ndilo kubwa sana ni msaada wa Komrade Ngombale Mwiru katika serikali kuwapatia Waislam majengo ya TANESCO Morogoro wafungue Chuo Kikuu. Marehemu Kitwana Kondo alikuwa heshi kumshukuru Komrade Ngombale Mwiru kila alipokuwa anakizungumza chuo hiki. Waswahili wanasema, ‘’Damu nzito kuliko maji.’’ Kadri itakavyokuwa Komrade Ngombale Mwiru ni Mswahili wa Kilwa Kipatimu na haiwezekani kuwa asiijue vizuri historia ya Vita Vya Maji Maji na historia za wale waliotoa roho zao katika vita ile kupambana na ukoloni wa Wajerumani. Ngombale Mwiru alikuwa anayajua matatizo ya msuguano uliokuwapo katika nchi yetu katika masuala ya dini. Komrade Ngombale Mwiru alikuwapo toka siku ya kwanza TANU inampandisja katika jukwaa Mwalimu Nyerere katika viwanja vya Mnazi Mmoja kupaza sauti kudai uhuru wa Tanganyika. Komrade Ngombale Mwiru kayaona yote toka siku ya kwanza umoja wa wananchi chini ya TANU ulivyokuwa na nguvu na Mungu akamjalia umri mrefu wa pia na kuona taratibu umoja ukimeguka kidogo kidogo na mabadiko yaliyokuja baada ya uhuru kupatikana. Kwake yeye mkinzano dhidi wa dhulma ya aina yeyote katika jamii ndiyo yalikuwa maisha yake. Akili yake haikuwa na tabu ya kuiona dhulma inapojitokeza. Ukweli huu ndiyo uliomsukuma Komrade Ngombale Mwiru asimame pamoja na Waislam katika wakati wao wa shida. Misaada hii aliyotoa kuwasaidia Waislam inasema mengi kumweleza Mzee Ngombale Mwiru.

Nahitimisha taazia hii kwa kusema kuwa Komredi Ngombale Mwiru amekufa katuachia muujiza mkubwa usio na kifani. Komredi Ngombale Mwiru ambae Balozi Juma Mwapachu alimwita Susilov jina la ‘’ideologue,’’ wa Soviet Union Communist Party, Mpanga Mikakati wa TANU na CCM kutangazwa kuwa akiwa katika siku zake za mwisho duniani katika kitanda chake cha umauti amempokea Bwana Yesu Kristo na kurejeshwa kundini hakika huu ni muujiza katika miujiza na ni mapinduzi katika mapinduzi yatakayozungumzwa kwa miaka mingi sana baada ya kizazi hiki chetu chote kutoweka. Hakuna mtu aliyetegemea kuwa Komredi Ngombale Mwiru atasindikizwa safari yake ya mwisho akiwa Mkristo na akiimbiwa pambio.


Saturday 3 February 2018

BURIANI KOMREDI KINGUNGE MSOMI WA TANU ULIYELISOMESHA TAIFA
KIZAZI KILICHOANDALIWA KUONGOZA NCHI YETU



Nilikutana na Mzee Kingunge Ngombale - Mwiru Bungeni mwaka 2005, mimi nikiwa Mbunge wa kuchaguliwa kutoka Kigoma Kaskazini na yeye akiwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais. Tulipoanza Bunge la 9 Mzee wetu huyu ambaye sasa ametangulia mbele ya haki alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano ya Jamii na Siasa. Baadaye alipumzishwa na kuendelea kuwa Mbunge wa kawaida.

Sikuwa na ukaribu naye, japo tulikuwa tuna ukaribu kifikra, kwa maana ya itikadi ya Ujamaa. Sikuwa nakunywa naye kahawa kama ilivyokuwa kwa Mzee Prof. Philemon Sarungi au Marehemu Jackson Makweta. Lakini tulikuwa tunasalimiana kwa bashasha na akipenda ukorofi wangu Bungeni.  Baadaye nilijifunza kuwa naye alikuwa mkorofi sana enzi za ujana wake.

Siku moja mwaka 2009 kulikuwa na mzozo Bungeni kuhusu mjadala wa Mahakama ya Kadhi. Wabunge Waislam wakiongozwa na Mohamed Misanga wakiitaka na Wabunge Wakristo wakiongozwa na Godfrey Zambi wakiipinga. Lugha zilizokuwa zikitumika zilikuwa za mgawanyiko mno na Bunge lilikuwa mubashara kwenye runinga. Nikaogopa sana namna viongozi wanaongea lugha za kugawa wananchi kidini. Nikasimama kuongea. Nikafoka sana kuhusu lugha tunazotumia kujenga hoja bila kujali madhara yake kwa raia wetu. Pia nikawalaumu Wabunge wakongwe kwa kukaa kimya bila kukemea. Mjadala ukabadilika na kuwa wa staha.

Tulipotoka nje ya Bunge nikakutana na Ezekiel Kamwaga, mwandishi wa habari ambaye enzi hizo hakuwa mwandamizi. Ezekiel akaniambia, “Nimemhoji Mzee Kingunge kuhusu lawama zako kwao. Ameniambia wewe umechelewa sana kuzaliwa. Ulipaswa kuzaliwa wakati wa Mwalimu Nyerere. Una maoni?” Nikamjibu Kamwaga kuwa wazee waliniudhi kukaa kwao kimya. Hata hivyo nimefarijika sana kuwa Mzee alikuwa ananisikiliza. Tangu siku hiyo kila nilipokutana na Mzee Kingunge nilikuwa nataniana naye kuhusu ‘intervention’ ile bungeni.

Nimekuwa na kawaida ya kuandika ‘’obituary,’’ (tanzia) kila mtu wa karibu yangu ama mtu ninayemheshimu anapofariki. Wakati mwengine huwa napata tabu sana kuandika kutokana na ukaribu ama uzito wa mtu mwenyewe. Tangu asubuhi jana nilipoletewa ujumbe wa simu kuwa Mzee Kingunge hatunaye nimekuwa natafakari kuwa naandika nini kuhusu jabali hili la siasa za nchi yetu? Naandika nini kuhusu kizazi cha dhahabu cha wanasiasa wazalendo wa nchi yetu? Naandika nini kuhusu ‘ideologue’ wetu huyu ambaye hajaweza kuzibwa nafasi yake na yeyote?

Ni kama vile mtu anayetaka kuandika kuhusu maisha ya Komredi Marcelino Dos Santos wa FRELIMO. Ni kazi ngumu zaidi kwa sisi ambao hatukuwa na ukaribu mkubwa sana na mzee huyu. Hata hivyo, nimeona lazima nimuage Komredi Kingunge kwa namna ninayoweza, nayo ni kueleza kizazi cha sasa ni nani Kingunge Ngombale Mwiru, na ni kwa nini nchi yetu ilikuwa na raia huyu?

Maisha ya Komredi Kingunge ni taswira ya historia ya chama kilichotukomboa kutoka makucha ya ukoloni mkongwe. Mwaka 1957 ilikuwa dhahiri kwa chama cha TANU kuwa punde tu, miaka michache mbele, uhuru wa Tanganyika ungepatikana, hamasa ya wananchi ilikuwa juu mno, na uungwaji mkono wa TANU ulikuwa mkubwa nchi nzima. Katika wakati husika viongozi wenye maono wa TANU wakaamua kuliandaa taifa na kukiandaa chama chao kuendesha nchi.

Changamoto kubwa katika wakati husika ilikuwa ni rasilimali watu, wasomi wachache wa Kiafrika ambao pia walikuwa viongozi wa TANU hawakutosha kushika nafasi zote muhimu za kuliongoza taifa. Hivyo haja ya kusomesha wasomi wa Kitanganyika kwa ajili ya kusaidia kuliongoza taifa mara baada ya uhuru ikaibuka. Rais wa 19 wa Liberia, ndugu William Vacanarat Shadrach Tubman na chama chake cha True Whig Party (TWP) wakawa kimbilio la TANU, Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere, akiomba nafasi za masomo ya elimu ya juu (skolashipu) kwaajili ya vijana wa Tanganyika.

Komredi Kingunge alikuwa mtu wa tano kupata skolashipu hizo, mwaka 1958. Awali, mwaka 1957, Mzee Muharram Macatta Mwinyimtwana na Balozi Paul Malyago Rupia walikuwa ndio kundi la kwanza la wanafunzi kupata skolashipu za kwenda kusoma elimu ya juu kupitia Chama cha Ukombozi cha TANU, katika Chuo Kikuu cha Cuttington, Suacoco, Maili 120 Kaskazini ya mji mkuu wa Liberia, Monrovia. Muharram na Paul walikuwa watoto wa wafadhili wa chama cha TANU, Mzee Macatta Mwinyimtwana wa Ngamiani Tanga, na Mzee Paul Rupia wa Misheni Kota Ilala, Dar es Salaam.

Kundi la pili lilihusisha wanafunzi watatu, ambao pia walikuwa ni wafanyakazi wa kujitolea katika makao makuu ya TANU, hao ni Komredi Kingunge, Mzee Ghysla Mapunda, aliyekuwa waziri wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja Shaaban Nyelwa Kissenge, ambao wao walikwenda masomoni mwaka 1958.

Kundi la tatu lilikuwa kubwa zaidi, likihusisha idadi ya watu zaidi ya kumi, lilikwenda masomoni mwaka 1959. Kundi hili likiwahusisha ndugu Amani Samuel Mshote, Dakta John Peter Kasiga, ndugu Martin Kayuza, Chifu Nhindilo Humbi Ziota, Dkt Kassim Guluri, ndugu Charles Buzuka, Dkt William Kimweri Madundo, Dkt Mbaga, ndugu Joshua Mpogolo, ndugu Mjabuzi, pamoja na ndugu Edmund Luganga. Hivyo kufanya jumla ya watu wote waliopelekwa masomoni na TANU kufikia 16, katika kipindi kifupi cha kati ya mwaka 1957 - 1961. Wote hawa kwa nyakati tofauti tofauti walishika dhamana mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Jambo hili la TANU kuandaa vijana wa kuendesha nchi ni historia muhimu ya taifa letu, inajenga msingi wa namna vyama vya siasa vya wakati wa ukombozi vilivyojikita katika ujenzi wa nchi. Kwa Zanzibar, chama cha Umma Party nacho kilifanya jambo hili la kuwaandaa vijana, kwa kuwatafutia mafunzo kutoka sehemu mbalimbali, ulimwenguni, kuanzia Cuba, Ujerumani, USSR mpaka Misri. Hivyo vijana wa kizazi cha awali cha Tanzania, kina Komredi Kingunge na Dkt Salim Ahmed Salim, walipikwa na kuandaliwa vyema kuja kuliongoza taifa na vyama vyao, jambo ambalo vyama vya siasa vya sasa havifanyi kabisa.

Taswira kuu ya Mzee Kingunge ni kuwa alikuwa ni tanuri la kupika fikra zilizozaa sera na maamuzi ya nchi yetu. Ramani ya Maendeleo ya nchi yetu Tanzania, kwa miongo mitatu ya mwanzoni ilichorwa kwa kutumia nyaraka tatu; Azimio la Arusha, Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 na Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981. Nimechungulia nyaraka zangu ili kusoma muhtasari wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU ya Januari, 1967 iliyopitisha Azimio, na sikuona jina la Komredi Kingunge. Mkutano huu ndio uliiweka nchi yetu kwenye ramani ya nchi za kijamaa. Mzee Kingunge hakuwamo kwenye ule mkutano wa Arusha. Hata hivyo huwezi kuzungumzia utekelezaji wa azimio hilo bila kutaja miongozo niliyotaja hapo juu ambayo aliindika yeye. Kwa hiyo miaka minne mara tu baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha unaanza kumwona gwiji la itikadi “The Ideologue” Kingunge Ngombale Mwiru.

Juzi niliona taarifa kutoka Davos, Uswizi, ambapo mkutano wa mabepari wa dunia hufanyika. Taarifa ile ilisema Tanzania ndio nchi inayoongoza Afrika kwa kuwa na uchumi jumuifu (inclusive economy). Kwa watu wa fikra fupi walikimbilia kusambaza habari hizi bila kuzipa muktadha wake stahili. Muktadha wake ni Azimio la Arusha la 1967. Hili ndio lilikataa unyonyaji na kujenga uchumi usio na matabaka (inequality).

Katika kitabu kilichopewa jina ‘Miongozo Miwili: Kupaa na Kutunguliwa kwa Azimio la Arusha’ (https://www.udsm.ac.tz/sites/default/files/Miongozo_bk.pdf), kilichochapishwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kingunge anaeleza kwa ufasaha namna Mwongozo wa 1971 ulivyobuniwa na kutekelezwa.
Nanukuu:

 “Mwongozo wa TANU wa 1971 ulitolewa na kutangazwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU ya dharura mwanzoni mwa mwezi wa Februari, Dar es Salaam. Mwezi wa Januari mwaka 1971 Jeshi la Uganda chini ya Iddi Amin Dada, liliangusha serikali ya Rais Milton Obote na kutwaa madaraka. Kufika Agosti kitendo cha uchokozi kisicho cha kawaida kilitokea, kikosi cha Jeshi la Iddi Amin kilikivamia kikosi cha doria cha polisi wa Tanzania mpakani Mutukula na kumteka nyara Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na kumtoroshea Uganda”.
[Kamanda huyu aliyeuwawa hatimaye aliitwa Hans Pope, baba mzazi wa huyu Hans Pope wa Simba Sports Club inayoifunga funga Yanga kila wakikutana].

“Kitendo hiki cha uhasama kutoka kwa nchi jirani kilihitaji kupatiwa jibu la haraka na la kimkakati. Ndipo nilipoitwa Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais, Ndugu Rashid Mfaume Kawawa, ambaye nilimkuta na Meja Hashim Iddi Mbita (wakati ule Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU). Ndugu Kawawa alinieleza kwa kifupi kuwa Mwalimu alimwagiza aniarifu kuwa ameamua mimi niongoze timu ya viongozi wa vijana kadhaa wa TYL (TANU Youth League) kwenda Mkoa wa Ziwa Magharibi kufanya kazi ya kuhamasisha wananchi kisiasa na kiulinzi na usalama ili waweze kukabiliana ipasavyo na chokochoko zozote zile kutoka nchi jirani.

Pamoja na kukubali jukumu nililopewa na kuahidi kuanza maandalizi mara moja, nilitoa rai kwa Makamu wa Pili wa Rais kwamba kwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi kutoka Uganda ni sehemu tu ya tishio kwa taifa, maana kuna tishio kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Kusini, la majeshi ya Wareno, na uhasama wa Wareno, pamoja na wa dola za Afrika ya Kusini na Rhodesia (sasa Zimbabwe) ingekuwa busara kuitisha kikao cha NEC kutafakari juu ya ulinzi na usalama wa Taifa. Ndugu Kawawa alikubaliana na pendekezo langu na palepale aliondoka akifuatana na ndugu Hashim Mbita, kwenda kuonana na Mwalimu Ikulu. Walirejea baada ya nusu saa na kunitaarifu kuwa Mwalimu amekubali pendekezo nililolitoa na tayari ameagiza NEC iitishwe kwa dharura.”

Mwisho wa kunukuu.

Komredi Kingunge sio tu alipokea kazi na kuitekeleza kwa utii, bali pia alishauri kuipanua na kuipa baraka ya vikao vya Chama. Hebu fikiria, unaitwa na Kawawa unapewa kazi aliyoagizwa na Nyerere halafu wewe mpewa kazi unashauri kwanza nini kifanyike. Sio tu ni ujasiri bali ni kujiamini kulikopita kiasi cha kawaida. Hebu fikiria leo unaitwa na Rais kupewa kazi halafu unajifanya kujua, Eti itisha Halmashauri Kuu kwanza, thubutu. Kingunge ni darasa tosha la wanasiasa wa sasa.

Kwa taarifa tu kwa Vijana ni kwamba moja ya zao lililodumu la mwongozo wa mwaka 1971 ni Jeshi la Mgambo. Ilipotokea vita dhidi ya nduli Idi Amini, wanamgambo walioandaliwa kutokana na mwongozo wa mwaka 1971 walipigana bega kwa bega na wanajeshi wengine na kumshinda adui. Ukiona mwanamgambo popote ni alama ya fikra za Mzee Kingunge tunayemzika siku ya jumatatu ya Februari 5, 2017 siku ambayo kilizaliwa chama ambacho yeye ni miongoni mwa waasisi wake. Kwa hakika nchi yetu inaweza kumuenzi mzee wetu huyu kwa kuanzisha Kingunge Brigade ndani ya Jeshi la Mgambo ili vizazi na vizazi wajue wazo hili lilitoka kwa nani.

Kingunge Ngombale Mwiru na Kitwana Selemani Kondo

Lakini pia mwongozo wa mwaka 1971 ulisisitiza sana suala la maendeleo ya watu. Jambo ambalo ni mwafaka wakati huu kuliko wakati mwengine wowote ule katika nchi yetu. Mwongozo ulisema:

 “Kwa hiyo katika kufikiria maendeleo ya taifa letu na katika kupanga mipango ya maendeleo wakati wote mkazo mkubwa uwekwe kwenye maendeleo ya WATU na sio ya vitu... [W]atu wenyewe lazima washiriki katika kufikiria, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo yao.”

Hii ni kauli inayoishi na kudumu milele. Hupimi maendeleo ya taifa kwa madaraja, ndege, wala njia za reli, bali kwa namna ambavyo watu wa taifa hilo wameelimika na kuwa na afya tele inayowpa uwezo wa kuzalisha mali na kuongeza utajiri wa nchi.

Dhana hii ya ‘Maendeleo ya Watu’ Mzee Kingunge aliiamini mpaka mwisho wa uhai wake. Nakumbuka wakati wa mijadala ya Bunge Maalumu la Katiba aliamsha mjadala mzito juu ya jambo hilo, na aliandika eneo maalumu la Uchumi ili kutoa ‘Dira ya namna Uchumi wa Taifa letu unapaswa kuwa.’ Eneo hili limewekwa kama sehemu ya tatu ya Katiba Pendekezwa, likijikita katika kuelezea namna dola inavyopaswa kuwa wakala wa ukombozi wa wananchi.

Miaka 10 baadaye mwongozo wa mwaka 1981 ulitangazwa, ambao pia ni zao la fikra za Komredi Kingunge. Katika kitabu cha Miongozo Miwili hilo pia limeelezwa vizuri na Kingunge mwenyewe. Nanukuu:

 “Mwongozo wa 1981, kama ulivyokuwa mwongozo wa TANU wa 1971, ulikuwa ni mwendelezo wa fikra na matarajio ya Ujamaa na Kujitegemea uliotangazwa na Azimio la Arusha. Mwongozo huu ni matokeo ya mila iliyokuwa imejengwa ndani ya Chama ya kutumia vikao vikuu vyake, hususan NEC, kujadili na kuchambua masuala mazito ya nchi, ya siasa, uchumi na jamii, na kuyatolea maelekezo ya kisera, kiufafanuzi na kiutekelezaji.

Wakati Mwongozo wa TANU wa 1971 ulijielekeza kwenye mapambano dhidi ya Ukoloni, Ukoloni-Mamboleo na Ubeberu ili kufanikisha Ukombozi wa Afrika na wa Mwafrika na kuweka mkakati wa ulinzi na usalama wa umma ili nchi iwe na uwezo wa kukabiliana na uvamizi wowote kutoka kwa ubeberu au na vibaraka vyake, Mwongozo wa 1981 umejikita katika kufanya uchambuzi kosoa wa kina na mpana juu ya hali ya kisiasa na kiuchumi iliyokuwepo nchini, hali ya maendeleo ya demokrasia nchini na ndani ya chama, n.k., na kutoa mapendekezo ya kuimarisha na kupanua demokrasia katika Chama na nchi.”

Mwisho wa kunukuu.

Jambo kubwa tunalojifunza hapa ni Chama cha siasa kuwa chombo cha mijadala na maamuzi ya watu badala ya kuwa chombo cha kupitisha amri za wakubwa. Kwamba chama kinaweza kufanya uchambuzi kosoa ili kujikosoa. Na kwamba vikao vikuu vya chama vinapaswa kuwa na ajenda ya kudumu ya kujadili hali ya uchumi na siasa ya nchi. Sisi ACT Wazalendo tuliiga jambo hili, ndio maana katika kila kikao kikuu cha chama chetu, ni lazima tujadili hali ya nchi (Kiuchumi na Kisiasa) na kutoa taarifa ya mwingozo wa kisera kwa chama.

Jambo hilo ni muhimu sana, hasa katika zama za sasa ambapo hata kukosoa ni dhambi, na vikao vya vyama hukaa kwa dakika masaa machache sana kupokea amri tu za wakuu wa vyama hivyo. Kwa vyovyote vile vyama vya namna hiyo vinahesabu siku zake. Ni vema kutumia siku za kuomboleza kifo cha Komredi Kingunge kujitafakari kama tunafuata misingi ya mwongozo wa mwaka 1981 kuhusu uchambuzi kosoa ili kujenga msingi madhubuti wa ujenzi wa vyama vyetu vya siasa, pamoja na kupanua demokrasia nchini.

Mzee Kingunge ametuachia usia kwenye andiko lake nililonukuu sana kwenye makala haya. Mwenyewe ameziita changamoto na ninaomba niziweke kama alivyoziweka yeye:

- Unapoisoma miongozo hii miwili, wa TANU wa 1971 na wa 1981, huwezi kukosa kubaini kuwa fikra, nadharia na tafakuri kubwa zilitumika katika utunzi wake. Haya ni matokeo ya viongozi wa chama wanapokaa pamoja na kufikiri pamoja. Hii ni aina mojawapo ya uhai wa chama iliyo muhimu sana kwa uhai wa jumla wa chama cha siasa.

- Je, mila hii iliyokuwa imejengeka huko nyuma CCM ya sasa inaiendeleza? Je Vyama vingine vya siasa nchini vinajaribu kujenga tabia ya viongozi wake kuketi pamoja na kufikiri pamoja na kuchambua pamoja hali ya nchi yetu na namna vitakavyozikabili changamoto mbalimbali?

- Huu umaskini wetu wa sasa wa falsafa unaotuathiri vibaya unatokana na nini?

Mzee Kingunge alikuwa mtu mwenye kusimamia anayoyaamini, amefariki dunia akiwa ameondoka katika Chama chake alichoshiriki kukiasisi. Tunaambiwa kuwa hakujiunga na chama kingine cha siasa, ingawa alitoa msaada kwa chama kilichokuwa kinapingana na chama chake. Hili laweza kubakia kuwa jambo la mjadala mkali katika miaka inayokuja. Inawezekana mjadala huo ukafunika kabisa mchango wake kwenye ujenzi wa taifa letu. Hatuwezi kukwepa hilo kuwa mjadala Lakini tunaweza kukwepa kulikuza na kulifanya lifunike mambo makubwa aliyoyafanya kwa nchi yetu.

Sina hakika kama Komredi Kingunge aliandika kitabu kuhusu maisha yake. Hii ni changamoto kubwa kwa Viongozi wetu wengi. Hawapendi kuandika na hivyo kuondoka duniani na MAARIFA yao bila kuyarithisha kwa vizazi vya mbele yao. Kuna mambo mengi ambayo vizazi vingependa kujifunza kutoka kwa watu kama Kingunge Ngombale Mwiru lakini kwa sababu hatuandiki, basi vizazi vinaikosa hiyo fursa.

Kwa mfano, miaka ya 1970 Komredi Kingunge alikuwa ni Mkuu wa Mkoa, Katibu wa TANU wa Mkoa, na hivyo kuwa pia mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aligombana na Mzee Kawawa kuhusu kwenda kinyume na msimamo wa Serikali Bungeni ilhali yeye ni Mkuu wa Mkoa wa Serikali hiyo hiyo, kwa jambo la Serikali ambalo yeye hakukubaliana nalo. Mwalimu Nyerere alimfukuza kazi Kingunge.

Habari hii haijaweza kuelezwa kwa namna ambayo itakaa kwenye vichwa vya Vijana kama funzo la kuwa na msimamo. Mzee Kingunge hakujali cheo chake, alisimamia kile alichokiamini bila kujali cheo chake. Alifukuzwa kazi Lakini baadaye alirudi, na kuwa mjumbe wa kamati iliyoandika katiba ya kuunganisha vyama vya ASP na TANU. Aliheshimiwa kwa msimamo wake. Jambo hili hulioni kwa wanasiasa wa sasa. Limefanywa kuwa gumu zaidi pia kutokana na uongozi wa sasa pia ambao ni wa kiimla na hauruhusu mawazo pinga.

Tabia ya kuwa msimamo Kingunge ameiishi maisha yake yote, tangu chuo kikuu kule Liberia. Katika kundi la wanafunzi wale 16, ni kuwa ni kundi la kwanza tu, wazee wetu Muharram Mwinyimtwana tu na Paul Rupia, ndio waliomaliza masomo yao mwaka 1960, wanafunzi 13 waliobaki chini ya Uongozi wa Komredi Kingunge walifukuzwa chuo wakitetea uonevu dhidi ya wanafunzi wenzao, jambo lililozusha vurugu kubwa hapo Chuo Kikuu cha Cuttington, na hivyo wanafunzi hao kuhamishiwa Dakar, Senegal, na kisha kuendelea na masomo katika nchi za USSR.

Ningefurahi kusoma visa vyote hivi kutoka kwenye kitabu cha Komredi Kingunge mwenyewe. Natarajia kuwa ameacha mahala hazina ya maandiko ya historia hii muhimu kwa taifa, na kuwa watafiti na wanazuoni wataweza kuiweka hazina hiyo kwenye kitabu. Kwa hakika nchi yetu imepoteza Jabali la Siasa. Profesa Issa Shivji amejitahidi kumweka wazi Mzee Kingunge kwenye maongezi yao yaliyochapishwa kwenye jarida la Nyerere Chair miaka tisa iliyopita. Maongezi haya (https://issabinmariam.files.wordpress.com/2018/02/mazungumzo-kati-ya-ngombalemwiru-na-issa-shivji-2009.pdf ) yanatosha kuanzia kuandika kitabu cha Kingunge. 

Nawasihi watu wote msome maongezi yale. Yamesheheni historia ya nchi yetu ndani ya historia ya Mzee Ngombale.

Buriani Mzee Kingunge Ngombale - Mwiru. Ulisomeshwa na TANU nawe ukalisomesha Taifa. Uliandaliwa kuongoza Taifa letu, umetuongoza vema.
Pumzika kwa Amani Komredi.

Pichani ni wanafunzi wa TANU wakiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cuttington, Dkt. Watts (katikati aliyebeba mtoto) pamoja na mkewe. Komredi Kingunge ni wa watano kutoka kulia, waliosimama, akiwa pembeni ya Dkt. Watts. Picha hii ilipigwa 1959, na ni kwa hisani ya Mzee Muharram M. Mwinyimtwana (wa nne kutoka kushoto, waliosimama, mwenye tai).

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Februari 3, 2018

Friday 2 February 2018


TAAZIA: COMRADE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU
NA JUMA VOLTER MWAPACHU

Kaitan Maurus Ngombsle

Leo alfajiri nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha ndugu yetu Kingunge Ngombale Mwiru. Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake ambayo ni wiki chache tu tarehe 4 Januari, kilifiwa na mama yao, Peras Ngombale Mwiru, mke wa Ngombale Mwiru.

Tanzania nzima bila kujali misimamo ya siasa haina budi kuwa na majonzi mazito kwa kuondokewa na Comrade Ngombale Mwiru. Alikuwa shujaa wa siasa tangu TANU hadi kifo chake.

Nilimfahamu kwa karibu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Youth League, Chuo Kikuu, Dar-es-Salaam kwa kipindi 1967/68. Yeye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa TANU Youth League, Makao Makuu. Joseph Nyerere alikuwa Katibu Mkuu na Moses Nnauye alikuwa Katibu Mkuu Msaidizi.

Nilibahatika nami kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU Youth League. Tangu kipindi hicho Ngombale ananiona Comrade. Hata siku ile ya sala ya kumuaga mama Peras pale St Peters Church aliponiona akitoa smile kubwa alinipa mkono akiniita 'Comrade.’

Mwaka 1991 Ngombale alichaguliwa na CCM kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kupendekeza Sera na Mwelekeo wa Chama na nchi katika miaka ya 90. Mimi, Iddi Simba na Reginald Mengi tuliteuliwa kuwa wanakamati. Report yetu iliyokubaliwa kwa kishindo na Mkutano Mkuu wa CCM hapo 1992 baada ya kuwasilishwa na Ngombale kwa fasaha kubwa ndiyo iliyojenga misingi ya mageuzi ya uchumi nchini.

Wakati wa kazi hiyo Ngombale akawa karibu sana nami akitambua kwamba nilikuwa pia mjumbe wa Tume ya Nyalali kuhusu Chama Kimoja au tuingie kwenye Vyama Vingi. Comrade Ngombale alikuwa rafiki wa karibu sana wa Professor Ahmed Mohiddin, Mkenya aliyependwa sana na Mwalimu Nyerere kutokana na maandiko yake kuhusu ujamaa.
Mohiddin ana undugu na familia ya mke wangu. Sote tuliyokuwa karibu ya Ngombale tulimuita Susilov kutokana na kuwa 'ideologue' wa TANU na CCM.

Susilov alikuwa ideologue wa Soviet Union Communist Party. 

Tanzania imempoteza jabari wa siasa. Kwangu nimempoteza Mwalimu na rafiki. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
Amin.