Showing posts with label makala. Show all posts
Showing posts with label makala. Show all posts

Monday 30 April 2018


WAISLAMU wachache wa Mwakaleli, mkoani Mbeya wameanza harakati za ujenzi wa msikiti huku wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wenyeji katika mji huo.

Msikiti huo unajengwa katika Kijiji cha Mpunguti Kata Luteba Kitongoji cha Kamasulu mpakani mwa Kata ya Luteba na Kandeta, bonde la Mwakaleli katika Wilaya mpya ya Busokelo, Mkoani Mbeya.

Mwandishi wa habari hizi, akiwa hapo Mwakaleli, alibaini kuwa katika wilaya hiyo mpya ya Busokelo, iliyogawanywa kutoka katika Wilaya ya Rungwe, haina msikiti hata mmoja na huo ndio msikiti wa kwanza kujengwa katika ardhi hiyo ya Mwakaleli.

Baadhi ya wenyeji wameeleza kuwa Mwakaleli, ina jumla ya kata nne ambazo ni Isange, Mpombo, Kandete, Luteba, ambapo sasa Waislamu wachache kutoka katika kata hizo watalazimika kutumia msikiti huo pindi utakapo kamilika.

Akielezea harakati hizo za ujenzi wa msikiti huo Bw. Majid Adam Mpangoji, ambae ni mwakakilishi wa Jumuiya ya Waislamu Mwakaleli, katika Wilaya ya Busokelo, alisema wameanza ujenzi wa msikiti chini ya Jumuiya hiyo katika hali ya upinzani mkali baada ya wenyeji kubaini kuwa wanajenga Msikiti.

“Awali tulipata upinzani mkubwa kutoka kwa wenyeji baada ya kubaini kuwa katika eneo hilo unajengwa msikiti kwa ajili ya Waislamu hii ni kutokana na kuamini na kuelewa tofauti kuhusu Uislamu na kutokuwepo kwa msikiti kwa miaka yote katika ukanda huu kwa ujumla, ukilinganisha na wingi wa Makanisa, hivyo kuona kama wanawekewa kitu kigeni katika mji wao.”

Amesema Bw. Majid. Akifafanua zaidi, alisema ilifikia hatua hata viongozi wa kitongoji kilipo kiwanja cha msikiti huo kuungana na wakazi kupinga kujengwa msikiti katika eneo hilo lakini akasema baada ya mvutano mkubwa walishinda kwa hoja na kuanza ujenzi wa msikiti huo.

 Alisema, harakati za kuhakikisha unapatikana msikiti katika ardhi hiyo zinafanywa na jumuiya hiyo ambayo mpaka sasa ina mwaka mmoja na nusu tangu kuundwa kwake ambayo ina mchanganyiko wa Waislamu wageni na wenyeji.

Bw. Majid, ambae ni mmoja wa Waislamu wageni na aliyechachu ya harakati hizo, amesema mpaka sasa Jumiya hiyo imefanya harakati za kununua ardhi kupitia michango ya Waislamu hao wachache waliopo hapo.

“Katika azima ya kupata msikiti changamoto kubwa tuliyokutana nayo hapa Mwakaleli ni kupata eneo (ardhi) wengi hawakuwa tayari kuuza ardhi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti lakini pia ilikuwa shida na ngumu kukutana kwa pamoja kama Waislamu na kujadili kuhusu umuhimu wa kuwa na msikiti katika mji wetu.” Amesema Bw. Majid.

Lakini alisema, zilifanyika juhudi za makusudi kwa kumpitia Muislamu mmoja mmoja na kuwaelimisha na baadae waliona kweli, upo umuhimu wa kutafuta eneo na kujenga msikiti ili na wao wawe na sehemu maalum ya kuabudia na kuwa na kituo cha kufanyia shughuli zao za kiibada kama wanavyofanya wenzao Wakristo.

Alisema, juhudi hizo zilizaa matunda baada ya kuungwa mkono na Waislamu wachache wenyeji na kuweza kufanikisha kuanza harakati hizo na kuweza kufikia hatua hiyo huku malengo zaidi yakiwa kujenga kituo kikubwa, huku msikiti huo ukiwa ni hatua za awali kwani ni matarajio yake baada ya kukamilika utakusanya Waislamu na kupanga mipango mingine zaidi.

Alisema, katika ukanda huo wa Mwakaleli na pengine Wilaya nzima ya Busokelo, hakuna msikiti na kwa Waislamu wachache waliopo hapo (Mwakaleli) ama huswalia majumbani mwao au hujumuika na Wanafunzi wa Kiislamu wa Shule ya Sekondari Mwakaleli, kuswali haswa swala ya Ijumaa, Shuleni hapo.

“Shule hiyo imetoa chumba kimoja kwa ajili ya matumizi ya msikiti kwa wanafunzi wa Kiislamu (wanaotoka mikoani) waliopo katika shule hiyo kwa ajili ya kufanya ibada zao hivyo na sisi Waislamu wa nje ya shule huungana nao kufanya ibada zetu hapo na haswa Ijumaa wenyeji tunaungana na wanafunzi wa Kiislamu pale sekondari kwa ajili swala ya Ijumaa, hata hivyo ni chumba ambacho hakina hadhi ya kuwa msikiti lakini kwa kuwa ni dharura, hamna namna ibada inafanyika hivyo hivyo.” Amesema Bw. Majid.

Aidha, Bw. Majid, alisema Jumuiya yao ina malengo mengi na kwa sasa ni kuhakikisha msikiti huo unasimama na kuanza kufanyiwa ibada kisha hatua itakayofata ni kuanzisha madrasa na shule ya awali. Bw. Majid, alisema mpaka sasa ana mwaka wa tano tangu aingie katika mji huo na kubaini kuwa hali ya Uislamu ipo chini na hakuna harakati zozote za kuuhisha Uislamu kwani karibia wenyeji wote ni Wakristo. Waislamu ni wachache mno.

Hata hivyo, Bw. Majid, alisema ujio wa watumishi katika idara tofauti tofauti za serikali kutoka katika mikoa mbalimbali na kupangiwa majukumu katika mji huo ndio kumepeleka hamasa ya kupatikana kwa msikiti huo.

Alisema, ujenzi huo wa msikiti mpya upo katika hatua ya msingi kutokana na michango na nguvu za Waislamu hao wachache waliopo hata hivyo akasema wanaomba kuungwa mkono katika juhudi hizo kutoka kwa Waislamu popote walipo. “Mahitaji ni mengi lakini vifaa kama matofali, Nondo na siment vinahitajika kwa haraka ili kuwezesha msikiti kwenda kwa kasi.” Amesema Bw. Majid.

Kwa upande wake, Bw. Singolile Ngolako Mwakisenjele, aliye mzaliwa wa Kandete Mwakaleli, alisema wenyeji wa mji huo wanashuhudia msikiti wa kwanza kujengwa katika ardhi ya Mwakaleli tokea enzi za mababu zao.

 Bw. Mwakisenjele, alisema pamoja na kuwa wana fahamu kuwa dini zipo nyingi ikiwemo Uislamu, lakini baada ya Waislamu wachache waliopo hapo kwa sasa kuanza harakati za ujenzi wenyeji walistuka maana wamezoea kuona makanisa ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali na si misikiti.

Bw. Mwakisenjele, anasema tokea utoto wake na sasa ni mtu mzima akiwa katika ukanda huo alimjua Muislamu mmoja tu ambaye alikuwa ni maarufu kwa jina la Alwatan Mwafisi, hata hivyo nae aliupata Uislamu baada ya kwenda Mikoa ya Pwani.

Baadae, akasema aliingia Muislamu mwingine aliyekuwa akiitwa Majid, hivyo na kufanya mji kuwa na Waislamu wawili kwa miaka mingi hata hivyo pamoja na uwepo wao hapakuwa na fikra kuwa kutakuja kuwa na msikiti katika Mji huo.

“Lakini miaka inavyozidi kwenda na serikali kusambaza watumishi na wengine kupangiwa katika mji huo wa Mwakaleli, katika Taasisi za Serikali swa uchache wakaanza kuingia Waislamu japo sio wengi.

“Lakini kwa uchache wao huo na kukosekana kwa msikiti kila mmoja anaabudia nyumbani kwake, lakini naona kwa sasa wameamua kuunda Jumuiya yao ya Kiislamu na kuamua kujenga Miskiti kwa ajili ya kufanya ibada zao.” Amesema Bw. Mwakisenjele.

Bw. Mwakisenjele, alisema yeye haoni tatizo la ujenzi wa msikiti huo kwa sababu anaamini ni sehemu ya maendeleo na kwamba Serikali haina Dini ila wananchi wake ndio wana dini hivyo akasema si haki kuwapinga Waislamu kuwa na msikiti kwani ni haki yao ya msingi kikatiba katika haki za kuabudu.

Thursday 19 April 2018


Shajara ya Mwana Mzizima
Sheikh Yahya Hussein: ‘Mjawiid’, Mnajimu, Tabibu na Mtabiri Bingwa Africa Mashariki 
Sehemu ya Kwanza

Na Alhaji Abdallah Tambaza

Sheikh Yahya Hussein
Raia Mwema 20 - 22 April 2018

NIANZE kwa kuwashukuru wale wote waliofanya mawasiliano na mimi baada ya kusoma zile makala nne zilizopita kuhusu kuvunjika kwa EAC ya zamani na athari zake kwa nchi wanachama. Nimefarajika sana na nasema ahsanteni sana.

Jumatatu ya leo, Shajara inamwangazia Mwana Mzizima mwengine aliyeaga dunia takriban miaka 7 iliyopita, na ambaye ametoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Sheikh Yahya Hussein Juma Karanda, aliyefariki dunia mnamo Mei 20,2011 alikuwa na maarifa na akili nyingi mno, hivyo akawa gwiji na bingwa kwenye tasnia mbalimbali alizozipitia katika uhai wake. Sheikh Yahya alikuwa mjawiid (msomaji Qurani maarufu duniani wa kiwango cha kimataifa); mwanasiasa aliyepigania uhuru wa taifa letu; gwiji wa utabiri wa kutumia nyota; tabibu wa kutumia vitu vya asili na  pia alikuwa mwalimu wa madrassa na shule pia.


Kulia Sheikh Hussein Juma na Sheikh Hassan Juma

Babake Sheikh Yahya, alikuwa Mzee Hassan Juma, lakini Sheikh Yahya yeye alikuwa akitumia jina la babake mdogo Sheikh Hussein Juma, ambaye ndiye aliyemlea na kumwongoza kwingi kwenye safari yake ndefu ya maisha hapa duniani.

Habari zinasema, familia hii ya kina Sheikh Yahya na baba zake, ilihamia hapa Mzizima miaka mingi nyuma, wakitokea Bagamoyo ambako walikuwa wakifundisha watu elimu ya dini ya Kiislamu. Kutokana na umahiri na uhodari wao katika ufundishaji, watu wa Mzizima wakati huo - kwenye karne ya 18 hivi - akiwemo Mzee Mussa Pazi na Mzee Abeid Mwinyikondo Uweje - waliwaendea na kuwaomba wahamie hapa ambako kulikuwa na uhaba mkubwa wa walimu wa madrassa wa kiwango kile.

Walikubali na wakaanzisha madrassa iliyojulikana kama Al-Hassnain Muslim School pale Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo na ikawa madrassa ya mwanzo jijini iliyokuwa ikitoa elimu hiyo na ile ya ‘kisekula’ huku wanafunzi wakiwa wamekaa juu ya madawati. Madrassa hiyo ilikuwa imesomesha vijana wengi wa hapa jijini wakati huo, ambao walipojiunga na shule zile za serikali walikuwa wakishika namba za juu madarasani.

Mzee Ibrahim Abeid Uweje, akinisimulia habari za Al-Hassnain, anasema yeye na kaka zake Abdulkheir na Abubakar, walisoma hapo na alishuhudia hata mchezo wa mpira wa miguu ukifundishwa pale chuoni wakati huo.

“Pale Al-Hassnain tulikuwa tunafundishwa mpaka kucheza mpira, na hayati Sheikh Yahya ndiye aliyekuwa kocha na ndiye aliyenifanya mimi niwe golikipa,” alisema Mzee Uweje.

Madrassa nyingine ambazo zikitoa wachezaji mpira mahiri wakati ule ni pamoja na ile ya Maalim Mzinga & Sons, ambapo walimu wake watatu walikuwa wakicheza mpira wa kiwango kikubwa - Maalim Abbas Mzinga alikuwa mchezaji wa timu ya Tanganyika iliyochukua Gossage Cup 49; Maalim Mambo Mzinga akichezea Sunderland (Simba sasa); Juma Mzinga aliyechezea Yanga; Mwlimu Tumu Ramadhani (kocha New Style na baadaye Yanga katika miaka ya 1960s na hayati Juma Mzee aliyekuwa mchezaji na mwalimu wa klabu ya Sunderland. Hapa pia elimu ya kisekula ilikuwa ikitolewa. Mwandishi huyu alipata elimu ya dini ya Kiislamu chuoni hapo.

Madrassa nyingine zilizokuwa mahiri wakati huo ni ile ya Sherrif Hussein Badawwy, pale sokoni, Kisutu, ambapo ilikuwa ikiongoza katika fani ya tajwiid, lakini pia kwa mchezo wa mpira. Mwalimu wake mkuu Sherrif Hussein Badawwy, ndiye aliyeasisi klabu mashuhuri ya mpira ya Cosmopolitan, ambayo yeye mwenyewe alikuwa mchezaji na kocha. Klabu hiyo ndiyo iliyokuwa ikitwaa makombe kwenye miaka hiyo ya 50 na 60.


Shariff Hussein Badawy
Kote huko kwenye madrassa hizo kulifundishwa pia elimu ya kisekula ‘Kizungu’, ambapo watoto waliotokea humo kujiunga na shule za kawaida walikuwa wakipata alama za juu sana kutokana na misingi ya awali waliyowekewa. Si kweli hata kidogo, kama ilivyozoeleka kusemwa, kwamba Waislamu hawakuitilia maanani elimu ya kisekula. 

Sheikh Yahya Hussein yeye alipata elimu ya msingi pale Mchikichini na, ile ya kati, pale Kitchwele African Boys Middle School, hapa jijini. Alikuwa ni mwanafunzi aliyeongoza kwa kila jambo darasani, hasa somo la Kingereza na hisabati, na hivyo kumfanya awe na kiburi cha aina fulani. Habari zinasema, siku moja alikosana na mwalimu wake wa Kiingereza (Mr. Monday) darasani, kwa kumwambia kwamba alikuwa hawafundishi vizuri somo hilo maana alikuwa akiwabaniabania hivi.

Ule ukawa ni utovu wa nidhamu na kijana Yahya akafukuzwa shule mara moja. Yahya alipenda sana kuzungumza ‘kimombo’ na habari zinasema, kwake ilikuwa jambo dogo kufunga safari kila siku kwenda sehemu za mbali na kwao, ili kumfuata rafiki yake yeyote azungumze naye Kiingereza tu, ili roho yake iridhike.

Baada ya kufukuzwa shule, alibakia pale madrassani kwao na akawa akisaidiana na wazee wake kufundisha dini ya Kiislamu. Babake Mzee Hussein, akiwa mtu mashuhuri jijini, hakukata tamaa; alikwenda kumbembelezea ili arudishwe tena kuendelea na masomo yake pale shuleni Kitchwele.

Alikubaliwa kurudi na kipindi kile kikawa ni karibu na mitihani kwa ajili ya uteuzi wa kujiunga na Tabora School, kwani pale Kitchwele, wakati huo mwisho ilikuwa ni darasa la 10 tu. Sasa, pamoja na kwamba hakuhudhuria masomo kwa miezi 6, kijana Yahya alifaulu kwa alama za juu na kuwapiku wenziwe wote.

Walimu walipigwa na butwaa; wakasema haiwezekani labda pengine anatumia ‘ndumba na tunguri’ (uchawi). Matokeo yalipotoka yakawa vilevile kama mwanzo na njia ikawa nyeupe kwake sasa kwenda Tabora School. Hakwenda! Ule ulikuwa utawala wa kikoloni, pakafanyika ‘figisufigisu’ akakatwa jina lake. 

Babake hakuchoka; akampeleka Zanzibar kujiunga na Zanzibar Muslim Accademy. Hapa akaonekana hana vigezo vya kujiunga na taasisi ile iliyosheheni walimu bobezi kutoka Chuo Kikuu cha Al-azhar Sherrif cha Cairo, Misri. Akaondoka zake akaenda mjini Zanzibar akawa anasoma Qurani Sauti ya Unguja pale wakati inapofungua matangazo yake jioni.

Usomaji wa Sheikh Yahya katika fani ya tajwiid ulikuwa wa hali ya juu sana. Mudir (mkuu) wa chuo pale Muslim Accademy, siku moja katika pitapita zake akaisikia Qurani ikisomwa redioni na mtu ambaye hakupatapo kumsikia.

Siku ya pili akauliza pale chuoni ni nani yule aliyekuwa akisoma Qurani redioni jana yake? Akajibiwa kwamba yule alikuwa ni yule kijana aliyetaka kujiunga na chuo chake akamkataa. Mudir wa Muslim Academy Sheikh Mohammed Addahani, akaamrisha haraka atafutwe aje ajiunge na chuo.
 Yahya akawa yuko hapo kwa miaka kadhaa, na siku moja akazusha tafrani nyengine tena. Hapa akamlaumu Sheikh Addahani kuwa anapendelea katika utoaji wake maksi, kwani huwa anawapendelea wanafunzi fulani fulani na kuwapa alama za juu. Mudir hakuvumilia, Yahya akafukuzwa chuo.

Aliondoka akatimkia nchi za Kiarabu. Kipaji chake cha kusoma Qurani kikampatia umaarufu na akaweza kufanyiwa hafla kubwa pale Continental Hotel, Cairo, akasoma mbele ya makari, yaani wasomaji wakubwa wakubwa akina kama Abdulbasit, Mahmud na nduguye Mohammed Al-Minshawi na Sheikh Mustapha Ismail. Tukio lile likawa mubashara ‘live’ kwenye Redio ya Cairo. Kwa wale wasomaji waliomjua Sheikh Yahya watapata picha ni kitu gani alikifanya siku hiyo. Habari zinasema kuna msomaji mmoja mkubwa alipangwa asome baada ya Sheikh Yahya, alitoweka mwenyewe pale ukumbini na alipotafutwa haikujulikana kaenda wapi! Kajua hatofua dafu tena mbele ya Yahya Hussein.

Aliondoka hapo akaenda Malaysia ambako alikaribishwa na kula chakula na Waziri Mkuu wa siku hizo Tunku Abdulrahman ambaye pia alimsomea Qurani ndani ya Jumba la Serikali.


Sheikh Yahya Hussein na King Hussein wa Jordan miaka ya 1950s

Mjini Amman, Jordan alikaribishwa na King Hussein kwenye Kasri ya Mfalme akala naye ‘dinner’ na baadaye kumsomea Qur’an tukufu mfalme ambayo aliliwazika kwelikweli.

Alikaribishwa pia na King Hassan wa Morocco, ambako pia alipata wasaa wa kula na mfalme na kusoma kwenye Kasri ya Mfalme. Msomaji kuwa na mazungumzo ya aina yeyote na wafalme wale wa Kiarabu siyo jambo dogo kwa mtu kutoka katika vijiinchi vidogo hivi kama Tanganyika.

Alijitengenezea jina na kupatiwa, ‘’schorlaships,’’ nyingi sana kuwasaidia Watanganyika wengine kwenda kusoma katika nchi hizo. Watoto kadhaa walinufaika na ‘’schorlaships’’ za kupitia kwa Sheikh Yahya. Kama ilivyo kawaida, nabii huwa hakubaliki nchini mwao, lakini aliyekuwa Rais wa Kenya hayati Jomo Kenyatta, alimteua Sheikh Yahya kuwa mwakilishi wake binafsi kwa nchi za Kiarabu kutokana na kule kuwa  na uwezo wa kukutana na wafalme wale wakati  wowote. Akawa sasa yuko kule Mombasa na Nairobi akiwa katibu katika East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Hapa napo alitoa mchango mkubwa katika kupeleka vijana masomoni nchi za Uarabuni.

Alirejea nyumbani na kutembelea Zanzibar wakati Abeid Karume akiwa kiongozi baada ya Mapinduzi. Sheikh Yahya alikamatwa na kuwekwa jela kwa sababu alikuwa mara nyingi akionekana anazungumza na watu wenye asili ya Kiarabu. Serikali ya Mapinduzi ikahisi labda anataka kufanya ubaya.

Akiwa kifungoni kule Unguja, alikutana na mfungwa mwengine Mwarabu kutoka Yemen. Huyu alikuwa mjuzi wa fani ya utabiri na mambo ya uganga. Mwarabu yule alimpenda Sheikh Yahya kwa kuwa alikuwa anawaliwaza wafungwa wenziwe kwa kuwasomea Qur’an mle jela. Aliamua kumfundisha fani ya unajimu na tiba. Siku moja yule Mwarabu aliwaaga wenzake mle jela na akaondoka hivi hivi na mlango ukiwa umefungwa! Yakawa maajabu makubwa kwa askari na wafungwa pia.

Hazikupita siku, Sheikh Yahya naye kwa kutumia fani ile mpya, akajitabiria kwamba siku fulani atatoka mle jela na kuwa huru. Ikawa kama vile ghafla, wanasiasa pale Unguja wakaanza kuhoji kwa nini mtu yule kutoka Tanzania Bara, awe amefungwa kule Zanzibar badala ya kwao. Sijui paliongelewa nini, lakini ndege ikatumwa kwenda kumbeba kule Zanzibar, akakabidhiwa kwa Julius Nyerere na baada ya siku chache akawa yuko huru mitaani Dar es Salaam.

Hapo akaanza kazi yake mpya ya kuwa mtabiri akawa anatabiri matokeo ya mechi za mipira, ndondi, ajali, vifo vya watu mashuhuri, kuanguka kwa ndege na kuzama kwa meli, pamoja na vita duniani kote. Alitabiri pia matokeo ya chaguzi mbalimbali za kisiasa duniani na kuweza kumtaja nani atakayeibuka mshindi kwenye vinyang’anyiro hivyo.

Hapa kwetu alipata kutabiri kwamba Mzee Mkapa, wakati ule akiwa anamaliza muda wake uongozini, ataongezewa muda wa kuongoza, na ikatokea kuwa kweli maana palitokea kifo cha Mgombea Mwenza wa kiti cha urais kupitia Chadema na hivyo uchaguzi ukaahirishwa.

Mambo aliyoyatabiri na kutokea yako mengi kurasa za gazeti hazitoshi kuyaorodhesha. Kuna wakati aliitabiria timu ya mpira wa miguu ya Kenya kwamba ingeibuka kidedea kwenye mashindano ya Kombe la Challenge yaliyokuwa yakifanyika Tanzania. Kenya na Uganda waliingia fainali za mashindano hayo. Sheikh Yahya aliitabiria Kenya ushindi na aliweza kutaja wachezaji watakaong’ara siku hiyo na magoli yatapatikana kutoka kwa mchezaji namba ngapi na dakika ipi.


Sheikh Yahya Hussein na Jomo Kenyatta akimpa Rais Kenyatta
zawadi ya fimbo Nairobi miaka ya 1970

Kwa tukio hilo, serikali ya Kenya ilimletea ndege maalumu kwenda Nairobi kwenye sherehe za ushindi na huo ukawa tena ndio mwanzo wa yeye kuhamia huko moja kwa moja; akafikia kuwa mtu tajiri sana kutokana na kazi zake za unajimu na utabiri, wateja wake wakubwa wakiwa ni viongozi wa serikali ya Kenya.

Alikuwa na ofisi kubwa sana pale Moi Avenue Nairobi na alimiliki fahari ya jumba kule Kileleshwa (mfano labda wa Masaki hapa Dar es Salaam), nje kidogo ya jiji la Nairobi. Magari aliyokuwa akiendesha yakawa ni yale ya kisasa kabisa yanayouzwa bei ‘mbaya’ na suti zake zikawa zile za ‘designers’ wakubwa kutoka New York, Paris na Italy.

Sheikh Yahya vilevile alikuwa mtu wa mwanzo kabisa katika Afrika Mashariki, kutoa utabiri wa nyota magazetini, unaojulikana kama ‘horoscope’ au ‘nyota zenu’; kwani kabla yake magazeti kote Afrika Mashariki yalitegemea habari hizo kutoka magazeti ya Uingereza na Marekani.

Wakati wa kudai uhuru hapa nchini, Sheikh Yahya alijihusisha na siasa za vyama na alipata kuwa mpinzani mkubwa wa chama cha TANU na Mwalimu Nyerere akiwaita Nyerere na wenzake kama waropokaji na wapayukaji wasiojua A na B.

Alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Kabila wa Congo- DRC, Mfalme Mswati wa Swaziland (aliyempa uraia wa heshima wa nchi yake), Rais Daniel Arap Moi wa Kenya; na watu wengi wengine mashuhuri duniani.

Mtoto wa kiume wa mnajimu huyu, Maalim Hassan Yahya Hussein amejikita kuendelea na fani ya unajimu na utabiri kama marehemu babake. Na kwenye usomaji wa Qurani kwa njia ya tajwiid, pamoja na kwamba ametoa mchango mkubwa kwa kufundisha vijana wengi wanaondeleza fani hiyo, lakini amemwacha kwa makusudi, Sheikh Mohammed Nassor, awe kiongozi wa Taasisi  ya Usomaji na Kuhifadhi Qurani Tanzania, ambayo aliianzisha kwa nguvu na juhudi zake binafsi.

Kwa hivyo basi, wakati tukiadhimisha kumbukizi zake, ni vyema basi tukamuenzi na kumkumbuka mwanamajumui huyu aliyeipenda na kuitangaza nchi yake kimataifa kupitia fani na ujuzi aliojaaliwa na Mungu.

Simu:0715 808 864
atambaza@yahoo.com

Wednesday 11 April 2018


Mwanachama mwandamizi wa Saigon Sheikh Aziz Salim akiagana na Dr. Mohamed
Ali Shein aliyehudhuria kisomo cha kumrehemu Dr. Omari Ali Juma kilichofanyika
Club ya Saigon Mtaa wa Narung'ombe na Livingstone 2001

Marehemu Habib Mwamba mwanachama mlezi akiwa amesimama
pamoja na mtoto wa marehemu Dr. Omari Alli Juma kulia kwake na 

kushootoni Alhad Chuma. baada ya kusomwa dua ya kumrehemu


[9:57 PM, 4/11/2018] Boi Juma: Sheikh Aziz Salim, hizi picha mbili ni kumbukumbu nzuri sana kwa wana Saigon.


Picha ya Kwanza
Dr. Mohamed Alli Shen Wakati huo akiwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya watu wa Tanzania akiagana na wanachama wa Saigon walioshiriki katika khitma iliosomwa ya kumrehemu Dr. Omari Alli Juma aliekua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanzania hapa klabu ya Saigon. 

Wanaomsindikiza Dr. Shen ni Marehemu Ibrahimu Khamis Chuwa Mwenyekiti wa Senet wa klabu ya Saigon na huyo anae agana nae ni Aziz Salim.
Picha y Pili
[10:10 PM, 4/11/2018] Boi Juma: Picha ya pili ni marehemu Habib Mwamba mwanachama mlezi akiwa amesimama pamoja na watoto wa marehemu Dr. Omari Alli Juma baada ya kusomwa dua ya kumrehemu hapa klabu ya Saigon,


Kifo cha Dr. Omari Alli Juma alikufa ghafla Mola amlaze mahala pema pia awasamehe makosa yao Ibrahim Chuwa na Habibu Mwamba Aamin...

Saturday 24 March 2018

Khoja FC
Khoja Football Club ni timu ya soka ya watoto wa madras wanaoishi Mtaa wa Khoja Magomeni Mapipa na wanasoma katika vyuo tofauti vinavyozunguka Masjid Nur. 

Umti wao wastani haujazidi miaka 13 na wote ni wanafunzi wa shule za msingi. 
Timu hii ina wachezaji waliohifadhi kuanzia juzuu moja hadi nne Mashaallah.

Khoja Street FC


Picha hii nimewapiga vijana wangu wa Khoja Streert FC mchana huu walikuwa wanafanya mazoezi mtaani na mpira wao wa makaratasi. Huwaambia kuwa mimi katika umri wao nikicheza mpira wenyewe ''gozi,'' tukijaza upepo kwa AK Nanji Tandamti na Sikukukuu. 

Sasa kweli kwa matayarisho haya nchi hii itapanda chati katika soka? 
Lakini hawa vijana usiwaone hivi. 

Wako hapo waliokunywa juzuu moja hadi nne...

Friday 2 March 2018

Sheikh Mohamed Issa
Sala ya Eid Mnazi Mmoja Dar es Salaam


DUNIA imeingia tena katika simanzi baada ya kudhihirika kwamba wasichana 110 ambao ni watoto wa shule, wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria.

Wasichana hao walitekwa nyara Februari 19 mwaka huu, baada ya wanamgambo wa kundi hilo kuvamia shule yao katika mji wa Dapchi ulioko kaskazini-mashariki mwa Jimbo la Yobe.

Kutokana na hali hiyo, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari anasema hilo ni “janga la kitaifa”, ameomba radhi kwa familia za wasichana hao na kuahidi vikosi vya serikali kuwasaka watekaji hao.
Tukio hilo limekumbusha yale yaliyotokea katika shule ya wasichana ya Chibok mwaka 2014 na kusababisha huzuni na hasira kwa wazazi wa wasichana hao.

Dapchi, ambayo iko umbali wa kilometa 275 kaskazini-magharibi mwa Chibok, ilivamiwa na Boko Haram na kusababisha wanafunzi na walimu wa Shule ya Sayansi na Ufundi ya Wasichana inayomilikiwa na serikali kukimbilia katika vichaka vinavyozunguka shule hiyo.

Wakazi wa Dapchi wanasema baadaye vikosi vya serikali ya Nigeria vilianza kupambana na waasi hao ambao baadaye walikimbia.

Mamlaka awali zilikana madai kwamba kulikuwa na wasichana waliotekwa nyara, zikisema kuwa walikuwa wamejificha dhidi ya wanamgambo hao. Hata hivyo, baadaye walikiri kwamba wasichana 110 walikuwa hawajulikani walipo baada ya uvamizi huo.

Wanagambo wa Boko Haram wamekuwa wakipambana katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo yenye Waislamu wengi, wakidai kwamba wanataka eneo hilo liendeshwe kwa sharia za Kiislamu.
Ni takribani miaka minne sasa imepita tangu kundi hilo liteke nyara wasichana 276 wa Chibok na kupeleka kilio dunia nzima na hivyo kuanza kwa kampeni iliyoitwa’BringBackOurGirls (rejesheni wasichana wetu)’.

Hadi leo serikali ya Nigeria imeshindwa kutambua wasichana zaidi 100 waliotekwa walipo.
Tangu kundi hilo la Boko Haram liibuke kupitia mgongo wa dini limesababisha mauaji ya maelfu ya Wanigeria.

Boko Haram wanapigania dini?

Je, ni kweli wanachopigania Boko Haram ni dini? Je, Uislamu unaruhusu yanayofanywa na kundi hilo?

Mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, Shehe Mohamed Issa, aliulizwa maswali hayo na mwandishi wa makala haya na kujibu kama ifuatavyo:

“Boko Haram na makundi mengine yanayojitambulisha kwamba yanapigania Uislamu kama Al-qaeda, Islamic State (IS) na Al Shababu, wanatumia Uislamu kama ngazi tu ya kufanikisha mambo yao, lakini ukweli ni kwamba wanachokifanya kinapingana kabisa na mafundisho sahihi ya Uislamu.”

Shehe Issa anasema hayo ni makundi ya waasi kama waasi wengine na Uislamu unatumiwa tu kama ngazi kwa ajili ya kupata wafuasi au kuungwa na mkono na Waislamu ambao hawajui vyema misingi ya dini yao.

“Heri hata makundi mengine yanapambana na maadui zao, lakini hawa wanateka waislamu wenzao… Wanateka wasichana ambao pia ni Waislamu wenzao… Hakuna Uislamu wa aina hiyo,” anasema.

Anasema alisikia pia wanawaoa wasichana hawa, jambo ambalo ni la ajabu kwa sababu ndoa ya Kiislamu inakuwa halali pale kunapokuwa na ruhusa ya mzazi wa msichana.

Anasema Uislamu unakataza kuua nafsi isiyo na hatia bila kujali mhusika ana dini gani na hivyo huwezi kupiga bomu sokoni na kisha ukadai kwamba unapigana vita kwa njia ya Mwenyezi Mungu, maarufu kama jihadi.

Anazidi kufafanua kwamba, Uislamu pia unasema: “Hakuna kulazimishana katika dini…” (Al-Qur’an 2:256).

Shehe Abdulqadir al-Ahdal, Rais wa Taasisi ya al-Hikma ya Dar es Salaam, amekuwa akisema kwamba mapambano mengi yanayofanywa na makundi ya kigaidi kama IS hayana sifa ya kupigana kwa njia ya Mwenyezi Mungu (jihadi).

Anasema Waislamu kupigana jihadi ni mpaka kwanza wachokozwe na wawe katika mazingira ambayo wanazuiwa kutekeleza ibada zao, jambo ambalo halipo kwenye makundi yanayodai kwamba yapigana jihadi.

Kadhalika, anasema hata pale Waislamu wanapolazimika kupigana vita, ni marufuku kuwapiga watu wasio vitani, watoto, wanawake, kupiga nyumba za ibada kama makanisa, kuua wanyama na hata kukata miti holela.

Nini kifanyike kukomesha makundi haya?

Shehe Mohamed Issa anasema ili dunia iepukane na makundi hatari kama haya ni Waislamu kujifunza dini yao na wale wasio Waislamu kuacha kuyaita makundi haya kuwa ya ‘Kiislamu’ au mujahidina (wanaopigana kwa njia ya Mwenyezi Mungu).

“Baadhi ya vijana wa Kiislamu hukutana na mafundisho yaliyokwishapotoshwa. Ni vyema vijana wasomeshwe kwa mashehe wenye itikadi na mafundisho sahihi ya dini yao,” anasema Shehe Issa.
Lingine la kufanya anasema ni vijana wa Kiislamu kusoma pia elimu ya dunia ili kuijua kwa uhakika dunia yao.

“Ipo shida kwa baadhi ya vijana wa Kiislamu kutokuwa na elimu sahihi kuhusu mazingira yao na hivyo huwa na upeo mdogo kuhusu dunia,” anasema.

Anashauri pia serikali mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania kuwa na sera zitakazowanyanyua wananchi, hususani vijana kiuchumi.

“Vijana wengi wanadanganywa kwamba wakijiunga na hawa magaidi watapata manufaa ya kiuchumi; watapata pesa, watapatawake, watahudumiwa vyema na mambo kama hayo,” anasema.

Nafasi ya taasisi za dini

Kwa mujibu wa Shehe Issa, mbali na madhara yanayosababishwa na makundi haya, lakini pia yanaupaka Uislamu picha mbaya.

“Katika muktadha huo, ninashauri taasisi za Kiislamu kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kufanya kampeni maalumu ili umma ufahamu kwamba kinachofanywa na makundi haya hakina asili katika dini ya Kiislamu,” anasema.

Anasema kwa vile Tanzania haiku kisiwani, kama haifanyi kampeni za nguvu za kupeleka elimu sahihi kwa wananchi, siku moja vijana wa Kitanzania wanaweza kurubuniwa kujiunga na makundi haya hatari kwa mgongo wa dini.

Anasema kampeni ya kuufumbua macho umma inaweza pia kufanywa kupitia hotuba mbalimbali zinazotolewa misikitini na kwenye majukwaa mengine au kwenye makongamano na warsha.

Anasema nchi zinazosumbuliwa na magaidi zinaweza pia kuwa na kampeni kama iliyofanyika hivi karibuni nchini Uingereza iliyopewa jina la “Ujue Msikiti Wangu” (Know my Mosque).

Anasema katika kampeni hiyo, mtu yeyote alikuwa anakaribishwa kuuliza swali lolote kuhusu Uislamu na kwamba imesaidia sana kuwafanya watu kuijua vyema dini hiyo dhidi ya mambo yasiyohusu Uislamu, baadhi yakienezwa kipropaganda na watu wanaouchukia Uislamu.

Dk Zakir Naik katika kitabu chake ‘Maswali Yanayoulizwa kuhusu Uislamu na Wasio Waislamu’, anasema kwamba kutokana na propaganda au mitazamo isiyo sahihi juu ya Uislamu kujirudiarudia, imefikia hatua ya watu kudhani kwamba Uislamu ndivyo ulivyo.

Anasema wale wanaoziamini propaganda hizi kutokana na kutopata usahihi wa mambo, huwafanya wauangalie pia Uislamu vibaya na hivyo anahimiza Waislamu kuwa na kampeni kama hiyo ya ''Ujue Msikiti Wangu.''

Dk Naik anasema propaganda zinazotokana na mtazamo kwamba Waislamu ni watu wa siasa kali au magaidi, zimesababisha wakati mwingine Waislamu kubaguliwa, kutengwa au hata kufanyiwa fujo.

Chanzo Habari Leo, Febuari 28, 2018.
Hamisi Kibari

Thursday 1 March 2018


Mwandishi katika video hii anaanza kuzungumza katika dakika ya 40:40

Hii ni simulizi ya mkasa wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ilipodhaniwa kalishwa chakula kilichotiwa sumu kwa nia ya kutaka kukatisha maisha yake nyumbani kwa Abdulwahid Sykes Mtaa wa Stanley na Sikukuu katika miaka ya kati 1950 baada ya Mwalimu kutoka UNO safari ya kwanza 1955
Bi. Mruguru bint Mussa
Mama yake Abdulwahid Sykes

Bi. Nyang'ombe Mugaya
Mama yake Baba wa Taifa
Kushoto Bi. Mwamvua bint Mashu (Mama Daisy), wa tatu
Bi. Titi Mohamed akifuatiwa na Bi. Zainab mke wa Tewa
Said Tewa

Kushoto Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona

Thursday 22 February 2018


Kushoto Mwandishi wa Riwaya Mohamed H. Magora na Mohamed Said

Mohamed Magora ni mwanangu nimemuona akiwa mtoto akitambaa wakati nikienda kwao kwa baba yake kwa kazi za uandishi. Nikikaa katika varanda ya kwao na baba yake, Mohamed  mtoto mchanga akitambaa kwenye busati siku hizo kitoto kidogo kabisa. Sikutegemea kuwa iko siku Mohamed na mimi tutakutana uso kwa uso tena katika taaluma niipendayo ambayo na yeye pia kaipenda nayo ni uandishi. Lakini Mohamed kanishinda kwa kuwa mwenzangu, somo yangu yeye ni mtunzi wa riwaya zenye kusisimua sana tena zilizojaa mapenzi kitu kilicho aziz katika umri wa ujana kama huo wake.

''Baba nataka ukisome kitabu changu, baba kasema nikuletee.'' Mohamed huyo ananiambia baada ya kufika kwangu na baada ya mamkuzi.

Nimepigwa na butwaa kwani hata miaka miwili haijapita bwana mdogo huyu alikuwa kanipa kitabu chake cha kwanza, ''Masha Johari ya Kale,'' mara karejea tena kwangu na kitabu kingine. Ikanipitikia kuwa Mohamed si mwandishi wa kawaida na sioni kingine mbele yake ila In Shaa Allah mafanikio makubwa kwake katika uandishi.

Mohamed ni kijana hodari na fikra zake kazielekeza vizuri katika jamii anayoishi. Kalamu yake imelenga kwanza kwa vijana wenzake kueleza hali zao halisi katika ulimwengu huu wa usasa na kisha akageuza shingo upande wa pili kuwangalia wazazi wa vijana hawa jinsi wanavyohangaika katika kuwaelewa na kuwaelekeza watoto wao na pia kuelewa mazingira yanayowakabili. Kwa hakika ukimsoma Mohamed unapata picha ya mgongano wa nyakati, tabia, mwelekeo na mategemeo ya pande zote mbili ya watoto hawa wa kizazi kipya na wazee wao waliogubikwa na historia ya kale huku wakivutwa na mambo ya dunia hii ya leo. Mohamed anawasihi wazee wajaribu kuangalia mwelekeo wa dunia ya leo na changamoto zake.

Mwandishi Mohamed mwenyewe ana Kiswahili kizuri cha kuvutia unapomsikia akizungumza na halikadhalika ujuzi huu unaakisiwa katika kalamu yake. Mohamed katika kitabu hicho hapo juu anasema katika moja ya kurasa, ''...ajabu ya mbalamwezi kuanikia muhogo...'' Usemi  huu umenigusa pasipo kiasi kwani juu ya uzee wangu na umri wangu katika uandishi sijapatapo kusikia maneno haya na mimi  si mtu wa kucheza ngoma na mzigo kichwani katika dunia hii ya uandishi. Mzigo nimeutua uko chini. Naandika nikiwa sina hofu ya kuubwaga mzigo wangu.

Nashawishika kuuweka hapa utangulizi wa kitabu hiki, ''Chuo Kikuu ''Shaurimoyo,'' ili sote tufaidi kama mwenyewe mwandishi alivyoandika:

''Chuo Kikuu Shaurimoyo,’’ ni kitabu kinachosawiri uhalisia wa maisha ya wanafunzi wa Chuo Kikuu.

Ngazi ya elimu ya chuo kikuu huhesabiwa kuwa na dhima ya kufanya maandao ya maisha ya wanafunzi. Wanachuo hujifunza taaluma mahsusi walizochagua kwa hiari zao ili wazitumikie katika kuendesha maisha yao. Hujifunza maisha ya uhuru na kujitegemea, hujifunza namna ya kutangamana na wanajamii, hukuza ndoto zao za maisha na hivyo kuwa na kiu ya kujistawisha. Mambo yote hayo ni muhimu sana katika kujenga msingi wa kuta za ustawi kama yataendewa kwa nidhamu, uvumilivu, juhudi na maarifa.

Njia ya kuelekea katika kilele cha fanaka haipo tambarare wanachuo hukumbana na changamoto mbalimbali za kijamii zinazosogeza karibu hatari ya kudamirika kwa mustakabali wao. Changamoto za kimaadili hupelekea wanachuo kuathiriana na kujikuta wapo katika shimo la maangamivu kwa kuzama katika matendo yanayopambanulika kuwa ni haramu kama ulevi, kamari, na mambo mengine yanayokwamisha mafanikio.

Kitabu hiki ni cha kusomwa na wakubwa na wadogo kwani wote kwa namna moja au nyingine wameguswa sana humo ndani na naamini katika wasomaji wako ambao watakuja kusema, ‘’Ala, kumbe mambo ndivyo yalivyo?’




Saturday 17 February 2018


Ndugu Msomaji,

Fuatilia hapa In Sha Allah tutajitahidi kuweka mambo yanayosibu nchi yetu toka tupate uhuru mwaka 1961...

Ninaandika kitabu kuhusu siasa za Tanzania na jinsi dini inavyotawala hisia za watawala walio madarakani. Katika sura moja ninaeleza namna Jakaya Mrisho Kikwete alivyoweza kufanya kampeni kwa miaka kumi na hatimae akaweza kuchaguliwa kuwa rais...lakini haikuwa kazi nyepesi kwa mara ya kwanza 1995 alipojaribu juhudi zake zilipata upinzani wa chinichini..

Nakuwekea hapa msomaji yale niliyoandika katika mswada wangu.

Nia ni kuangalia ni kweli Mwalimu Nyerere aliacha taifa lisilo na udini, lenye mshikamano wa kweli na umoja?:

''But before the conference Kikwete went on record to complain that the secretary of the party Dr. Lawrence Mtazama Gama, a Catholic, and hailing from the south like Mkapa was undermining his campaign on religious grounds.  

Nyerere who had earlier and eloquently promised him that he would take care of religious sentiments for Kikwete, was suddenly dead silent.

For a time it seemed as if the party was to engulf into a religious crisis involving its own top leadership. Religion was a sensitive issue and CCM had always maintained that the party did not discriminate its members on religious grounds.

The conflict between Kikwete and Gama was an embarrassment to the party.  In a strange turn of reconciliation effort CCM issued a statement that Gama had apologised to Kikwete. 

It is a pity that Kikwete did not reveal what religious issue became the source of conflict that the party had Gama to apologise.

The thought of Gama apologising to Kikwete was a humiliation to Gama not only because of his seniority but because of other factors...''

Hii ndiyo hali ilikuwapo wakati Kikwete na Mkapa wanaelekea Dodoma kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM itakaochagua mgombea wa CCM.

Hapa Khalfan Mrisho Kikwete, Muislam alikuwa anakwenda kupambana na Benjamin William Mkapa Mkatoliki mfuasi wa kanisa lenye nguvu kupita kiasi Tanzania...

Fatilia ukarasa huu kwa mengine In Sha Allah...

''Mkapa was forced to pick his campaign committee from people outside the inner circle of the party. 

Two newspapers publishers were in his committee Damian Ruhinda and Jenerali Ulimwengu. 

The special NEC Conference convened to elect one CCM member to stand for presidential candidate elected Jakaya Mrisho Kikwete in the first round with Mkapa coming close second and Msuya was last.

But since he had not commanded an absolute majority voting had to be repeated.

There was tension in the conference hall as CCM delegates voted to choose between Kikwete and Mkapa.

Christians were heard to whisper to each other that they should not again allow a Muslim to govern the country, never again they whispered to each other.

And when Mkapa won hymns were sung.''

Huu ndiyo ukweli wa siasa za Tanzania... dini haichezi mbali.

Lakini ili ndugu mfuatiliaji upate picha halisi ya nini kilikuwa kinafanyika nyuma ya pazia itabidi nimlete mgombea mwingine aliyekuwa mwanachama wa CCM...

Prof. Kighoma Abdallah Ali Malima...

''The difference between Prof. Malima and Kikwete was that, while Kikwete really believed that he was a serious candidate for NyerereProf. Malima knew Kikwete was thrown into the race by the Christian lobby to block him.

The rule of the game was to play a Muslim against a Muslim. But Kikwete was too naive to understand that.

His background had not prepared him to understand the intricacies of the politics of Tanzania as it relates to dealing with Islam and Muslims.

If he had taken some time to think long and hard he would have realised that if experienced people like Malecela, Msuya and Kolimba were not seen as fit to rule the country despite of their long service to the country which span more than three decades how possible could he supersede them and be a better candidate than those old guards?''

Marehemu Malima alikuwa akihadithia mkasa huu wa mkutano wa Dodoma wa kuwafanyia usaili wagombea hakika akinitoa machozi kwa kucheka.

Si kama yale aliyokuwa anahadithia yanachekesha hivyo bali kwa vile mtu unavyoweza kushangaa inakuwaje watu wazima wakachezewa vile na Nyerere na wao wasijijue kama wanachezewa. 

Malima alikuwa akinichekesha pale alipokuwa anasema yeye alipoingia kuhojiwa kamkuta Nyerere yuko ubavuni kwa Mwinyi utadhani wamekaa kiti kimoja.

Ilikuwa lazima Kikwete aletwe kugombea vinginevyo wagombea wote wangekuwa Wakristo ukimtoa marehemu Prof. Malima. Hali ingelikuwa vile ingekuwa lazima Prof. Malima wamchague ama sivyo Waislam wangelikuwa hawamo katika mbio za kwenda Ikulu.

Sasa Nyerere hakuweza kucheza na shilingi chooni. 

Prof. Malima na Mkapa washindane...hakuweza kutabiri matokeo kwani Prof. Malima akipendeza sana kwa umma wa Waislam...sababu za kupendeza huko ni kuwa Prof. Malima allijtolea kuiasa serikali kuwa kuna ubaguzi wa kidini dhidi ya Waislam nchini petu.

Turudi mwanzo tulikoanzia...

Rais Kikwete anasema, ''Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano...'' (Mwananchi Ijumaa, Aprili 18, 2014).

Hiyo hapo juu ni picha ya ya nchi yenye amani na mshikamano?

Jibu utakuwanalo wewe msomaji.

Waislam bila kificho wametembea nchi nzima kuwaeleza wananchi kuwa Tanzania inaendeshwa na Mfumo Kristo na Waislam wanabaguliwa toka uhuru upatikane. Kwa kauli hiyo hapo juu ya Rais Kikwete ni kuwa kapuuza kilio cha Waislam.

Kwake yeye hakuna dhulma na Waislam ni waongo kwani wao na Wakristo wote wana fursa sawa. Kanisa linatumia vyombo vya ulinzi kama jeshi lake binafsi. Waislam wanapigwa ndani ya misikiti na kufunguliwa kesi za kubambika.

Kovu la Mwembechai la mwaka 1998 bado halijapona. Waislam wamesingiziwa kuwa ni magaidi na askari wemeingia katika vijiji vyao kuwapiga na kuwaua na misikiti yao kuchomwa moto.

Haya yametokea Kilindi na jambo la kusikitisha vyombo vyote vya habari vimekataa kuandika habari hizi.

Binafsi nimezungumza na vyombo vya habari vya kimataifa na kuwapa picha za video kuonyesha unyama waliofanyiwa Waislam.

Wamekiri kuwa hakika dhulma imetendeka lakini hakuna hata chombo kimoja kilichokuwa na ujasiri wa kufanya kitu.

Majuma mawili yaliyopita Masasi Waislam wameingiliwa msikitini baada ya sala ya Ijumaa na kupigwa kwa kusingiziwa ati wamemtukana Yesu.

Baada ya kipigo hicho wamfunguliwa kesi ya uchochezi. Swali la kujiuliza ni hili kwa nini Waislam hawapelekwi mahakamani ila sisi ni kupigwa kisha ndiyo tunafikishwa mbele ya vyombo vya sheria?

Ndugu msomaji hii ndiyo amani aliyotuachia chembelecho Rais KikweteMzee Nyerere? Hili ndilo taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano? 

Rais Kikwete kipi kinamfanya ajifanye kuwa haujui ukweli?